Home UJUWE UISLAMU

UJUWE UISLAMU

1. TUUJUWE UISLAMU

UTANGULIZI

Baada ya kumshukuru Allah na kumtakia rehema na amani Mtume wake Muhammad, pamoja na watu wake na kila mwenye kufuata uongofu wake mapaka siku ya mwisho.

Tunakuletea kijitabu hiki katika ubainisho mwepesi wa kuweza kuuelezea  Uislamu kwa undani kabisa; ili aweze kufaidika kwa yaliyomo ndani yake aliyekuwa Muislamu na asiyekua Muislamu.

Ama kwa asiyekuwa Muislamu basi huenda ubainisho huu ukawa ni sababu ya kuongoka kwake; kwa kuwaunamuonesha njia sahihi ya kumfikisha yeye katika radhi za Mola wake aliyeumba kila kitu.

Kwa hakika Uislamu ndio njia sahihi katika mfumo wa maisha bora yenye malengo makuu kabisa, na malengo hayo ni kuwemo katika maridhio ya muumba mtukufu na kunufaika katika maisha ya milele, basi faidika kwa yaliyomo humu, ambayo ni uhakika usiokuwa na shaka.

بِسْمِ اللَّهِ ٱلرَّحْمَـٰنِ ٱلرَّحِيمِ

Uislamu: Ni dini aliyoiridhia Allah, na maana yake ni “Kujisalimisha mja kwa Allah kwa kufuata sheria yake”.

Allah: Ni jina la aliyeumba kila kitu -hata sehemu na wakati-, hajafanana na chochote, habadiliki, ni mkamilifu wa Dhati kwa kila sifa, hahitaji, hana mwanzo, wala hatuwezi kumfikiri wala kumuona, na yeye haonekani kabisa.

Muislamu: Ni yule aliyejisalimisha kwa Allah kwa kukubali kufuata sheria yake. Mtu atakuwa Muislamu kwa kushuhudia mambo matatu:

 1. Kuwa hakuna wa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah.
 2. Kuwa Muhammad ﷺni Mtume wa Allah.
 3. Kuwa aliyokuja nayo Muhammad ﷺni haki inayotoka kwa Allah.

NGUZO ZA UISLAMU: 

Nguzo za Uislamu kwa ujumla ni tano, nazo ni Shahada, Sala, Zaka, Funga, na Hija.

 1. Shahada: Ni lile neno la Ahadi ya kuingia katika dini ya Uislamu nalo ni: “Ninashuhudia kuwa hakuna wa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah, na ninashudia kuwa Muhammadﷺ ni Mtume wa Allah, na nimekubali kuwa aliyokuja nayo Muhammadﷺ ni haki inayotoka kwa Allah.
 2. Sala:Ni ibada maalumu inayolazimika kuitekeleza kila siku mara tano, iliyokusanya takbira, kusoma Qur-ani, kurukuu, kusujudu, tasbihi na salamu.
 3. Zaka: Ni fungu maalumu linalotolewa na Matajiri katika mali zao, kila mwaka mara moja kwa ajili ya kupewa makundi maalumu ya watu ambayo ni mafakiri, masikini, kuunganisha nyoyo, wenye kuikusanya, wapita njia, waliozidiwa na madeni, ukombozi wa watumwa na njia ya Allah.
 4. Funga:Ni kule kujizuia kutokana na kula, kunywa, kuingiliana kindoa, na kila kosa kubwa, kuanzia kuchomoza kwa Alfajiri mpaka kuzama kwa jua wakati wa Magharibi kwa nia ya kufanya ibada, ndani ya mwezi mzima wa Ramadhani, nao ni mwezi wa tisa kwa mujibu wa kalenda ya Kiislamu.
 5. Hija: Ni ibada maalumu ya kuitembelea Al-kaaba, na sehemu takatifu zilizoko Hijaz katika mji wa Makka katika mwezi maalumu wa Hija.

 

MISAMIATI MUHIMU KATIKA UISLAMU:

Sheria: Ni yale mafunzo yaliyo toka kwa Allah, aliyokuja nayo Mtume miongoni mwa Mitume wake.

Mtume: Ni mtu aliyepewa sheria aifikishe kutoka kwa Allah, muda wake humalizika kwa kuja Mtume mwengine baada yake, na kila watu wanalazimika kufuata sheria ya Mtume wao.

Muhammad: Ni Mtume wa mwisho katika Mitume ya Allah. Na yeye amefuta sheria za waliopita kabla yake: Nuuh, Ibrahim, Mussa, Daudi, Sulaiman, Issa mwana wa Maryam, n.w. Wala hakuna Mtume mwengine baada yake.

Qur-ani: Ni kitabu alichopewa Mtume Muhammadﷺ, kilichokusanya sheria ya Allah, nacho ni dalili ya Utume wake, na hakuna kitabu kilichokuwa na mfano wake. Allah amechukuwa ahadi ya kukihifadhi, basi kimehifadhiwa kwa lugha yake, muandiko wake, pamoja na visomo vyake kizazi kwa kizazi, nacho ni msingi wa mwanzo wa sheria katika Uislamu.

Sunna: Ni yale mambo yaliyo sihi kupatikana kwake kutoka kwa Mtume (ﷺ) sawa yakiwa ni maneno, vitendo au maridhio kwa yaliyofanywa, nayo Sunna ni msingi wa pili wa sheria katika Uislamu.

Ijmaa: Ni yale makubaliano ya Wanazuoni wa Kiislamu katika hukumu ya kitu iliofichika hukumu yake, bila ya kwenda kinyume na yaliyomo katika Qur-ani na Sunna sahihi. Ijmaa ni msingi wa tatu katika misingi ya sheria katika Uislamu.

HUKUMU ZA SHERIA YA KIISALMU:

Katika Uislamu kuna hukumu tano; jambo lolote halitoki nje ya hukumu hizo tano, nazo zinathibiti kwa hiyo misingi ya sheria ya Uislamu iliyo tangulia kutajwa, nazo ni Wajibu, Haramu, Man-duubu, Mak-ruuhu, na Mubaah.

 1. Wajibu:Ni hukumu inayojuilisha kulazimika kukifanya kitu, anayelifanya jambo la Wajibu anapata thawabu, na anayeliwacha anapata kosa la dhambi kubwa; mfano wa Wajibu ni kama vilekuwatii wazee, kusali, kufunga, na kuhiji.
 2. Haramu:Ni hukumu inayojuilisha kulazimika kukiacha kitu, anaelifanya jambo la Haramu atapata kosa la dhambi kubwa, na atakaewacha atapata thawabu; mfano wa Haramu ni kama vilekuzini, kulewa, na kuvuta Sigereti.
 3. Man-duub:Ni hukumu inayojulisha kupendelewa kukifanya kitu, anayelifanya jambo la Man-duub atapata thawabu, na atakayeliwacha hana kosa; mfano wa Man-duub ni kama vile,kuandikiana wenye kudaiana walio waaminifu.
 4. Mak-ruuhu:Ni hukumu inayojulisha kuchukizwa kukifanya kitu, anayeliwacha jambo la Mak-ruuhu atapata thawabu, na atakayelifanya hana kosa; mfano wa Mak-ruuhu ni kama vile,kukaa na mwenye kutuhumiwa katika Dini.
 5. Mubaah: Ni hukumu inayojuilisha kuwa kinachokusudiwa hakimo katika moja ya hukumu yoyote ile miongoni mwa hizo zilizopita; kama vile, mtukujichagulia chakula anachotaka miongoni mwa vilivyo vyahalali. Mja katika Mubaah analipwa kwa mujibu wa nia yake.

NGUZO ZA IMANI:

Imani ina nguzo sita ambazo haiwezi kutimia isipokua kwa nguzo hizo, nazo ni: kumuamini Allah, Malaika wake, vitabu vyake, Mitume yake, siku ya mwisho, na kadari (hukumu) ya Allah katika matokeo yote.

 1. Allah:Ni jina la yule aliyeumba kila kitu, asiyekuwa na mwanzo wala mwisho, kuwepo kwake ni kwa lazima, na yeye ni mkamilifu wa dhati.
 2. Malaika:Ni viumbe wa Allah wasio muasi, wasioacha kufanya ibada, wenye kufanya kila amri wanayoamrishwa, hatuwezi kuwaona, wako wanaoandika na kushuhudia yote wanayoyafanya waja wa Allah, na wao wameumbwa kwa nuru.
 3. Vitabu: Ni maandiko maalumu aliyoyajaalia Allah kuwa ni mkusanyo wa sheria za Mitume; ikiwemo Zaburi aliyo teremshiwa Mtume Daudi, Taurati aliyo teremshiwa Mtume Mussa, Injili aliyo teremshiwa Mtume Issa na Qur-ani aliyo teremshiwa Mtume Muhammad (ﷺ). Na vitabu hivyo hakuna kilichobakia katika asili yake bila ya kubadilishwa isipokuwa Qur-ani peke yake.
 4. Mitume:Ni wale watu aliowateuwa Allah kuwa ndio njia ya kufikisha sheria zake kwa waja wake, wao wamehifadhiwa kutokana na makosa makubwa, wanapata ufunuo utokao kwa Allah, na wao ni hoja juu ya waja. Mitume ni wengi sana, miongoni mwao ni Nuuh, Huud, Swaleh, Ibrahim, Is-haka, Is-mail, Yaaqub, Yuusuf, Yuunus, Luut, Id-ris, Daud, Suleiman, Mussa, Yahya, Issa, na wa mwisho wao ni Muhammad (ﷺ), na kila Mtume humalizika mudawake kwa kuja Mtume wa mbele yake.
 5. Siku ya mwisho: Ni ile siku ya malipo, ukubwa wake ni sawa na mika 50,000 ya hapa Duniani, watasimama watu wote kwa ajili ya kulipwa kila mmoja kwa imani yake na matendo yake, aliyekuwa mwema kwa kuifuata sheria ya Mtume wake aliyepelekwa katika zama zake; huyo atalipwa makazi mema katika Pepo yenye kudumu, atapata humo kila analolitamani; na aliyekuwa muovu kwa kumuasi Allah na Mtume wake, na yeye hakutubia, huyo atakuwa katika adhabu yenye kudumu ya Motoni, kwa mujibu wa makosa yake. Allah atuepushe nao (Amin).
 6. Kadari:Ni yale makadirio ya mambo yote yatakayotokezea katika viumbe tokea kuanza kuumba, nayo ni siri ya Allah mtukufu, sisi ni juu yetu kujitahidi kwa kufuata sheria ya Allah, na huku tunaamini kuwa hakuna linalotokezea isipokuwa Allah ametaka litokeze ikiwa ni zuri au baya; kwa sababu Allah haasiwi kwa kushindwa, wala haadhibu kwa kudhulumu, na yanayowapata waja ni kwa mavuno ya utiifu au kuasi kwao, au hua ni mtihani wa Allah kwa waja wake.

 

AINA ZA WATU:

Watu wapo aina tatu: Muumini, Mnafiki na Mshirikina, mtu yeyote atakuwa ni mmoja katika ya hawa; ima atakuwa ni  Muislamu au Mshirikina, na atakuwa ima ni Muumini au Mkafiri.

 1. Muumini:Ni yule aliyeikubali sheria ya Allah na ikamuhukumu katika maisha yake katika fikra, maneno na matendo yake.
 2. Mnafiki: Ni yule aliyeikubali sheria ya Allah lakini yumo katika kumuasi Allah kwa kosa kubwa katika fikra, au maneno, au vitendo vyake, mpaka atubie kwa Allah. Na huyo anafahamika kama ni Mnafiki wa kiutendaji, na anahisabika kua ni miongoni mwa Waislamu, na atatimiziwa haki zote zinazo wajibishwa na kuingia katika Uislamu. Pia yupo Mnafiki wa kiitikadi, huyo ni yule anayejidhihirisha kua ni Muislamu lakini kumbe ameficha ukafiri ndani ya nafsi yake. Na huyo hahisabiki kua ni miongoni mwa Waislamu.
 3. Mshirikina:Ni yule anaye muabudu asiyekuwa Allah, au kumshirikisha Allah na kitu chengine katika ibada, au kumkataa, au kupinga hukumu iliyomo katika sheria ya Allah inayojulikana katika Uislamu kwa yakini, na kwa makubaliano.

UKAFIRI:

Ukafiri ni kumuasi Allah kwa kosa kubwa lolote, nao umegawika vigao viwili: ukafiri wa kinafiki na ukafiri wa kishirikina.

      1.Ukafiri wa Kinafiki:

Ni kule kumuasi Allah kwa kosa kubwa lisilokuwa la ushirikina, na mwenye kuwa na sifa hiyo atapata haki zote za Waislamu isipokuwa Walayah.

Walayah: Ni kumpenda mtu kwa ajili ya kumtii kwake Allah, kwa kumsaidia, kumpenda, kumnusuru, kumridhia pamoja na kumuombea dua ya kumtakia rehema.

    2.Ukafiri wa kishirikina: 

Ni kule kumuasi Allah kwa kosa la ushirikina, na mwenye kosa hilo hana haki yoyote ya Kiislamu, na haki yake ni Baraa-a.

Baraa-a: Ni kinyume cha Walayah, nayo inalazimika kwa kila mwenye sifa ya ukafiri, kwa sababu kila kafiri ni adui wa sheria ya Allah, basi laana ya Allah inakuwa juu yake mpaka atubie kwa Mola wake.

MEZANI SIKU YA MALIPO: 

Kila mja yatapimwa matendo yake siku ya malipo, ima mezani zake zitakuwa nzito au zitakuwa nyepesi.

       1.Mezani nzito: 

Mezani za mja zitakuwa nzito kwa kukubaliwa mema yake hata kama ni jema moja, na atalipwa kwa hilo jema lake, na kuongezewa na Allah mtukufu, na yeye atakuwa katika makazi mema katika Pepo bila ya kuadhibiwa katika Moto, na Allah anayakubali matendo mema ya Waumini wachamungu.

       2.Mezani nyepesi:

Mezani za mja zitakuwa nyepesi kwa kukataliwa matendo yake, kwa sababu ya maasi yake makubwa, ikiwa hakutubia kwayo, kwa sababu Allah hasamehe kwa aliyeendelea na Dhambi kubwa mpaka yanapomfika mauti husema: “Ninatubia hivi sasa”, na Allah hawaridhii watu waovu; basi mtu huyo atakuwa katika adhabu ya Motoni kwa mujibu wa makosa yake, na yeye humo atabakia milele bila ya kukosekana au kutoka.

 

BAADHI YA MISAMIATI YA UISLAMU

Shafaa: Ni uwombezi wa Mtume (ﷺ) katika siku ya malipo, nao wataupata waja wema aliowaridhia Allah tu, kwa kukubaliwa toba zao, na kupandishwa daraja zao, na kuondolewa kwa mazito ya siku hiyo juu yao, kutokana na yale makosa ambayo walitubia kwayo; wala hakuna Shafaa kwa waovu madhalimu wa nafsi zao, ambao hawakutubia kutokana namaasi yao makubwa waliyoyafanya, kwani Allah haridhii watu waovu.

Jihadi: Ni kule kujitahidi kwa kila njia ya kuiweza nafsi katika kuyahama maovu, na kuiendesha nafsi hiyo kwa mujibu wa sheria ya Allah, na kuilinda dini kutokana na njama za maadui, na kuiendeleza dini kwa njia mbali mbali; kama vilekuisomesha, kuitangaza, kushikamana nayo katika raha na shida, wepesi na uzito, tena bila ya khofu, wala aibu, wala haya, pamoja na kuzuia uadui dhidi ya Waislamu.

Hijrah: Ni ile safari ya kuhama kwa Mtume Muhammad (ﷺ) kutoka mji wa Makka kwenda mji wa Madina, na ndipo ilipoanza Tarekhe ya Uislamu ndani ya sheria ya Mtume Muhammad kwa makubaliano ya Maswahaba (r.a).

Sahaba: Ni kila aliyekutana na Mtume -katika uhai wake- hali ya kuwa yeye ni Muislamu na akafa katika hali hiyo.

Shetani: Ni kila mwenye kumuasi Allah kwa makosa makubwa na kufanya kila juhudi za kuwapoteza wengine na kuwaingiza katika kufuru.

Ibilisi: Ni shetani wa mwanzo, naye ni katika majini, aliifanyia kiburi amri moja tu -ya kumsujudia Adamu-, basi akalaaniwa na kufukuzwa, kwani alikataa kutubia, lakini alichukuwa ahadi ya kukipoteza kizazi cha Adamu.

Jini: Ni kiumbe alichokiumba Allah kutokana na Moto, hatuwezi kukiona, na wao wanazaliana, na wanaishi, wako Waislamu kati yao, na wako wasiokuwa Waislamu.

Maamrisho: Kumtakasa Allah kutokana na kufanana na viumbe, au viumbe kufanana na Allah. Kukubali kuwa Muhammad (ﷺ) ni Mtume wa Allah. Kusimamisha Sala katika wakati wake. Kutoa Zaka, nayo ni 2.5% kila mwaka baada ya kutimiza kiwango cha 85g za Dhahabu au 595g za Fedha, pia kuna Zaka ya wanyama kwa wafugaji wa wanyama wa miguu minne, na Zaka ya mazao ya nafaka za kula kwa wakulima, nayo hutolewaasilimia 10% kwa asiotilia maji kwa nguvu yake, na 05% kwa wanaotilia maji kwa nguvu zao. Kufunga mwezi wa Ramadhani. Kuhiji na Kufanya Umra kwa mwenye uwezo. Wasia kwa Jamaa wasiorithi. Kuwafanyia wema wazazi wawili, jamaa, jirani, masikini, rafiki, mpita njia na mgeni. Kutia jando kwa mwanamme. Kuoga Baada ya Hedhi na Nifasi kwa mwanamke. Usafi. Kuoga janaba baada ya kuingiliana au kutokwa na maji ya uzazi. Udhu kabla ya Sala. Kukata kucha kila wiki. Kunyoa sehemu za siri kila mwezi. Kuacha ndevu. Kupunguza masharubu. Kuamrisha mema na kukataza mabaya. Kutaka idhini ya kuingia katika Nyumba. Kutoa salamu. Kurejesha salamu, heshima kwa wakubwa. Kuwarehemu wadogo. Ukweli katika maneno na ahadi. Uaminifu. Kutafuta riziki ya halali. Kuondosha maudhi. Kutafuta elimu. Kuhifadhi utupu. Kukwepusha jicho kwa kutoangalia ya haramu. Kuvaa kwa kuyasitiri aliyoamrisha Allah yasitiriwe -kwa mwanamme kutoka kitovu mpaka magoti, kwa mwanamke ni mwili mzima isipokuwa uso na viganja-. Sadaka. Kutubia. Kusamehe. Kusimamisha ushahidi kwa wakaribu na wambali. Kuoa kwa asiyeweza kujizuia. Kushuhudisha mashahidi wawili waadilifu katika kumrejea mke. Kumtunza yatima na mali yake. Kutembelea mgonjwa. Kumkosha maiti wa Kiislamu, kumsalia na kumzika. Mirathi kama alivyogawa Allah katika Qur-ani. Kusimamisha uadilifu kwa mwenye uwezo. Kuwahudumia wake na watoto. Kuwahifadhi wazazi na kuwatii.Kumpenda mwenye kumtii Allah na Mtume wake. Kuwatii viongozi waumini waadilifu. Kujifunga na Wanazuoni waumini. Kuamini kua Allah hailazimishi nafsi yeyote nje ya uwezo wake, na yeye anawapenda wenye kutubia na wenye kujitakasa na makosa na uchafu.

Makatazo: Kumshirikisha Allah kwa kumfanyia msawa katika sifa, ibada na sheria (amri na makatazo). Kuvunja udugu. Kulewa. Kuzini, nako ni kumuingilia mwanamke bila ya ndoa. Ndoa ya walioziniana.Kulawiti, nako ni kuingilia katika utupu wa nyuma. Kusagana, nako ni kupitisha matamanio ya kuingiliana baina ya mwanamke kwa mwanamke. Kuikaribia zinaa, nako ni kuingia katika kila kinachopelekea kuzini, kama vilemuziki, kuangalia, kukonyeza, kugusa, kufikiri, kujitoa matamanio kwa kujichezea. Kuiba. Kiapo cha uongo. Kusengenya, nako ni kumsema mwenzio kwa asiyoyapenda. Kufitinisha, nako ni kuchukuwa na kupeleka maneno kwa kusababisha ugomvi na chuki. Uwongo. Khiyana. Kujisemea bila ya elimu. Kuwaudhi wazazi. Kuasi amri ya kiongozi muadilifu. Kula maiti, nguruwe, damu, najisi, uchafu, punda, kilichochinjwa bila ya kutajwa Allah juu yake, na kila chenye meno ya ncha katika wanyama, na chenye kuwinda kwa makucha katika ndege. Kujiua. Kuidhuru nafsi. Kutoa au kupokea rushwa, nako ni kutoa pato maalumu lenye hadhi ikiwa ni pesa au cheo kwa ajili ya kupata haki isiyokuwa na haki ya kuipata. Khadaa. Shahada ya Uongo. Kudhulumu. Kuua nafsi bila ya haki. Kuua watoto. Kumkaripia masikini. Kuishi na zaidi ya wake wanne. Kiburi, nako ni kuidharau haki, na kujiona mbele ya watu. Kutembea kwa maringo. Kudanganya katika vipimo. Uhasidi, nao ni kutamani kuondoka neema ya mwenzako. Kutembea uchi. Kuvaa mwili wako hasa kwa mwanamke. Kujifananiza na jinsi nyengine; mwanamke kujifananiza na wanaume kitabia, kimavazi, kimaumbile, na mwanamme kujifananiza na mwanamke katika hayo; kama kuvaa dhahabu au hariri. Kujibadilisha kimaumbile, kama kunyoa nyusi, kuunganisha nywele, kuchonga meno, kupaka nyeusi kwa kuficha mvi. Kula riba, nayo ni ongezo kwa mujibu wa wakati katika jinsi ya kitu. Kamari, nayo ni pato linalopatikana kwa kukusanya vya wengi kisha akapewa mwenye kuangukiwa na kura, na ndio wakaipa jina la bahati nasibu (Nipate au nikupate). Uadui. Kusaidia katika dhambi na uadui. Kumpenda mwenye kumuasi Allah na Mtume wake. Na Allah anawapenda wenye kutubia na kujitakasa.

Neema: Kila alilotupa Allah katika uhai huu ni neema kwetu sisi waja wake, basi ni wajibu wetu sisi waja kumshukuru Allah katika neema zake zote.

Kushukuru: Ni kule kuzitumia neema za Allah katika yale anayo yaridhia Allah.Mja atapata barka na nyongeza katika maisha yake iwapo atashukuru; hata ikiwa ni baya kwa kusubiri, kwani huo ni mtihani.

 

TAHADHARI: 

Watu wengi wamepotea kwa sababu nne:- Kukipa kiumbe sifa ya Muumba, kumpa Muumba sifa ya kiumbe, kuitakidi usamehevu bila ya toba, na ubadilishaji wa majina ya kisheria katika vitu. Na huu wote ni upotevu katika sifa za Muumba na katika kufuata mapendwa ya moyo. Allah ametakasika na kila upungufu, na kuhitaji, na kwenda kinyume na aliyoahidi kwa Mitume yake (s.a.w); atuepushe Allah na udhalimu wa kufuata mapendwa ya moyo (Amin).

 • Kukipa kiumbe sifa ya Muumba:Hawa ni wale waliopotea kwa kujifanyia Mungu katika viumbe, ima watu katika mitume, wafalme, waja wema, miti, milima, makaburi, masanamu, n.v. wao wanaviomba na kuviabudu, wanavipa uwezo wa aliyeumba kuwa navyo vinadhuru na kufaa, vina amri na katazo, vinalipa na kuadhibu, ni vya tangu havina mwanzo n.m.
 • Kumpa Muumba sifa za Viumbe:Hawa ni wale walioitakidi kuwa Muumba anahitaji vitu vyengine katika ufalme wake, wakaitakidi kuwa yeye ana sehemu, sura, na viungo vyote isipokuwa uchi na ndevu, anashuka na kupanda, wako waliosema yeye ni kama sisi, na wengine wakajificha kwa neno lao: “Yeye sio kama sisi, lakini hayo anayo kiuhakika, na uhakika wake anaujua yeye mwenyewe”.
 • Ubadilishaji wa majina ya Kisheria katika vitu: Hili linapatikana katika kutoa majina yenye kupendeza kwa vitu vilivyoharamishwa, namajina yenye kuchukiza kwa vitu vilivyohalalisha na kuamrishwa, basi hili linazalisha upotevu katika kuhukumu, kwa mfano: Uzinifu unaitwa mapenzi. Ulevi unaitwa kiburudisha roho. Kamari inaitwa bahati na sibu. Kukamata dini kunaitwa kupitwa na wakati. Kuoa kunaitwa kujifunga pingu za maisha. Kutembea uchi kunaitwa kwenda na wakati, na mafano wa hayo yako mengi tujihadhari, ambayo yanaleta upotevu katika fikra.

Zingatia kuwa: Sifa za Allah ni maana za kuzingatia ukamilifu wa Allah, na sio kitu chengine kilicho nje ya uhakika wake, kwa sababu yeye ni mkwasi hategemei wala hahitaji. Basi ametakasika na kila sifa inayolazimisha kupatikana chengine ndio nayo ipatikane kama vilemkono, mguu, macho, masikio, pua, kuwepo katika sehemu fulani n.k, kwa sababu yeye yupo kabla ya kuwepo kitu chochote, na yeye hahitaji kitu, sifa zake za Dhati ni yeye mwenyewe, anajua kwa Dhati yake, anaweza kwa Dhati yake, anasikia kwa Dhati yake, kwa maana Dhati yake imekamilika haihitajii kitu chengine katika kusifika. Uhai wake ni wakidhati, usikuvu wake ni wakidhati, uoni wake ni wakidhati, elimu yake ni yakidhati, uwezo wake ni wakidhati, na namna hivi.

 • Kuitakidi usamehevu bila ya toba:Mayahudi na Manasara walisema kuwa Pepo ni kwa ajili yao tu, na kuwa wao hata kama wataadhibiwa basi ni kwa muda mdogo wa siku chache tu, kisha watasamehewa na kwenda Peponi, haya anayaeleza Allah katika kitabu chake, na kueka wazi kuwa ndio yaliyowapeleka katika kudharau mafundisho ya Allah, na kuyageuza ili yakubaliane na mapendwa ya mioyo yao, na kuiharibu dini kwa kujichukulia pato la kidunia, kisha wao wakidai kuwawatasamehewa tu. Basi tujue kuwa haya ndio Maradhi mabaya kabisa kwa waliopita, na ujihadhari yasije yakapata nafasi katika fikra zako, ukidhani kuwa na wewe maadamu ni Muislamu basi utafika Peponi tu, hata kama utaadhibiwa basi ni kwa muda tu, ukawa huna tofauti na hao waliopita kabla yetu isipokuwa majina tu, na ujue kuwa Allah ameiandaa Pepo kwa ajili ya waja wake walio wachamungu,waumini waliowema, na kuwa Allah ameandaa adhabu ya Moto kwa ajili ya waja wake wote waovu wenye kumuasi, ambao wameondoka na hawakutubia, basi na wewe ukiwa umo katika kosa kubwa, na hutubii ujijue kuwa Pepo ni haramu juu yako, na wala hutokosekana katika Moto milele; basi tujiandae na sio kujipa matamanio tu, tukawa kama hao waliopita.

 

MAMBO YANAYO HIFADHIWA NA UISALAMU

Uislamu unahifadhi mambo matano ya lazima katika uhai, nayo nidini, akili, nafsi, heshima na mali.

1.Dini: Inahakikisha utulivu wenye malengo ya kuridhiwa na Mola wako -aliyeumba kila kitu- katika maisha yako, basi ni lazima kuilinda dini kwa nafsi, mali, fikra, malezi na wakati.

2.Akili:Ni haramu katika uislamu kila linaloharibu akili, kama mfano waulevi, bali ni lazima kujilinda na kila linaloharibu akili, na kuihifadhi kwa kuikuza.

3.Nafsi: Nayo ni mwili, ni haramu kufanya yanayosababisha kuiangamiza nafsi bila ya haki, kama vile kijiua, kuua, kuvuta Sigereti. Hivyo, ni lazima kuuhifadhi mwili kiafya kwa kula chakula bora, na kufanya usafi.

4.Heshima:Kila linaloharibu heshima ya Muislamu ni haramu, kama matusi, uzinifu, kutembea uchi. Hivyo, ni lazima kulinda heshima zetu kwa malezi bora ya Kiislamu, na kukaa mbali na kila linalovunja na kuhatarisha heshima zetu.

5.Mali:ya Muisalmu ni haramu isipokuwa kwa kuridhika mwenyewe, na katika anayoridhia Allah Mtukufu; ama wizi, dhulma, rushwa, riba, kamari, shahada za uongo vyote hivi ni haramu.

Ndugu yangu, huu ndio Uislamu kama ulivyo katika kitabu cha Allah Qur-ani, na mafundisho sahihi yanayotoka kwa Mtume Muhammad (ﷺ), na yasiyodhurika na mwenye kwenda kinyume nayo, au kuyawacha, na kila moja katika haya lina ushahidi wa kutosha katika kitabu cha Allah.

QURANI TUKUFU