Published By Said Al Habsy  Maibadhi wanaonelea kuwa, kitabu cha Musnad Ar-Rabi’i bin Habib, kuwa ni kitabu sahihi kabisa miongoni mwa vitabu vya hadithi, kufuatana na jinsi vile ulivyo mlolongo wa wapokeaji wa Hadithi zake, kwani nyingi ya Hadithi zake katika kitabu hichi zimesimuliwa na Imam Ar-Rabi’i, kutoka kwa Shekhe wake (Abu Ubaydah), kutoka kwa Jabir bin Zayd, kutoka kwa mmoja katika Maswahaba wa Mtume (S.A.W.). Ingawa ziko ndani ya Musnad baadhi ya Hadithi zilizosimuliwa na Abu Ubaydah, kutoka kwa wasimuliaji wengine, mbali na Jabir, lakini hadithi zake ni chache.
Wametaja wanavyuoni wa Hadithi kuwa daraja ya Hadithi Sahihi zinatofautiana kama ifuatavyo: Daraja ya Hadithi ya kwanza ni Hadithi ile yenye mlolongo wa wasimuliaji watatu, kumfikia Mtume S.A.W. kama mfano vile mlolongo wa Hadithi zilizotokana na Azzuhriy, kutokana na Salim bin Abdillah bin Umar, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Mtume (S.A.W.). Na pia ya mlolongo wa Ibrahim An-Nakhaiy, kutoka kwa Alqamah, kutoka kwa Ibn Masoud, kutoka kwa Mtume (S.A.W.). Na mlolongo wa Malik, kutoka kwa Nafii’, kutoka kwa Ibn Umar, kutoka kwa Mtume S.A.W. Hadithi za milolongo ya aina hiyo zinahesabiwa na wanavyuoni, na mabingwa wa Hadithi, kuwa ni za daraja ya kwanza, sababu milolongo (sanadi yake) hii ni mifupi, na wasimuliaji wake ni mashuhuri kwa kuhifadhi, na kudhibiti, na wamekamilika kwa ukweli, na amana. Na ikiwa tutazifuatilia na kuzichunguza Hadithi alizozisimulia Ar-Rabi’i katika mlango wa mwanzo, na wa pili katika Musnad yake, tunaona aghlabu ya hadithi zake zina mlolongo wa wasimuliaji watatu, na wasimulizi wake ni katika watu wa kutegemewa kabisa, na wenye uwezo wa juu wa kuhifadhi, na watu wenye kutegemewa kwa ukweli, na amana. Na hadithi zenye mlolongo wa watu watatu katika Musnad alizozisimulia Imam Ar-Rabi’i aghalabu yake zimetokana na Abu Ubaydah, kutoka kwa Jabir, kutoka kwa mmoja katika Maswahaba, kutoka kwa Mtume (S.A.W.). Kwa hiyo Maibadhi wanaona kuwa Hadithi zilizokuwamo katika juzuu ya kwanza, na ya pili ndani ya Musnad, ni miongoni mwa Hadithi zilizo kuwa sahihi, ambazo hazina shaka kuwa zimetokana na Mtume (S.A.W.).
Hadithi zilizokuwa katika Musnad zenye mlolongo wa wahadiathiaji watatu, waliokuwa mashuhuri, na wenye kutegemewa, na wenye uwezo mkubwa wa kuhifadhi, pia zipo katika katika vitabu vya Sunan vingine. Japokuwa hatuoni kuwa kitabu hiki kutajwa miongoni mwa vitabu vya Hadithi, na wale walioshughulikia elimu ya Hadithi. Na hata kuna baadhi ya wanavyuoni wa Hadithi hawakupata kusikia kabisa kuhusu kitabu hiki. Na jumla ya wanavyuoni wa Kiislamu ambao wanashughulikia kufuatia hali za wasimuliaji wa Hadithi, na wakawafuatilia kwa ajili ya kuzikanusha, au kuzithibitisha hadithi, wamepuuzia, au wameghafilika kumtaja Ar-Rabi’i bin Habib katika vitabu vyao vinavyofafanua elimu ya hadithi, kwa kuzikubali, au kuzikataa. Isipokuwa aliyoandika Yahya bin Mui’n katika kitabu chake kinachoitwa "Tariikh” yeye kasema, "Ar-Rabi’i bin Habib ni mtu wa kutegemewa kufuatana na jinsi alivyosimuliwa na Al-Hasan na Ibn Sirin”. Na baadhi ya wanavyuoni wengine waliomtaja ni wanafunzi wa Hadithi kama Imam Ahmad na Bukhary.
Wameulizwa baadhi ya wanavyuoni mashuhuri wa Hadithi wa sasa, lakini wamesema hawamfahamu Ar-Rabi’i na Musnad yake. Ingawa kauli hii inasikitisha kwa jinsi vile inatokana na wanavyuoni waliobobea wanaoshughulikia mambo ya Hadithi, baadhi yao wamesameheka, kwani hawakuwa na fursa ya kupitia, na kuifahamu fikra ya Kiibadhi Na hii inaweza kuwa sababu ya kuficha historia, au mambo yanayohusiana na siasa. Na ukichunguza sana, utaona habari zimefichwa kwa ajili ya siasa, na historia, kwa karibu miaka 1000, na ikawa ndio sababu kubwa ya kuwarejesha nyuma wataalamu, na watafiti wa Hadithi kuijua fikra ya Kiibadhi. Ilivyo hakika inatuwajibikia kueleza hapa kuwa Maibadhi wenyewe hawakuchukua hima ya kutosha, katika kutangaza dhehebu hili, na fikra zake, toka awali hadi hivi leo. Isipokuwa katika hii miaka ya karibuni tunaona baadhi ya vitabu vya Kiibadhi vimechapishwa na wizara ya mila na mambo ya kale katika Oman.
Na juu ya vitabu hivyo kuchapishwa, na kusambazwa bado tunaona kuwa wengi miongoni mwa watafiti, na wamaizi (wasomi), na wanavyuoni wa kisasa, wenye kuyajua madhehebu ya Kiibadhi, na historia yake, na fikra zake, na mwelekeo wao katika imani ya dini: kwa kukusudia, au bila kukusudia wanabeza, na kuwazushia uongo, na kuficha habari zote za ukweli zinazohusiana na dhehebu la Kiibadhi, bali wengine huwatoa katika Uislamu kabisa. Na wanapoulizwa hujibu katika njia ambazo hazina ushahidi, zisizofuata misingi ya kielimu, na hatujui sababu ya jambo hili kutokea wakati wetu huu, ambao tunatarajia kuwepo uaminifu wa kielimu, na majadaliano ya kielimu, yenye misingi iliyo sawa, ambayo haiegemei, wala kuvutia upande mmoja, majadiliano yaliyo na uwazi wa kifikra, na kiakili. |