Published By Ust. Abu Muslim  SAFINA YA UONGOFU
“EWE MOLA WETU… WEWE NDIYE UTAHUKUMU WAJA WAKO KATIKA YALE WALIYOKUWA WAKITOFAUTIANA” TUONGOZE KATIKA YALE WALIOTAFAUTIANA WATU KATIKA HAKI, KWA IDHNI YAKO, HAKIKA WEWE UNAMUONGOZA UMTAKAYE KATIKA NJIA ILIYONYOOKA”
Ewe msomaji mwerevu:
Hakika kusihi kwa imani kunashikamana na kukamatana na itikadi iliyo sahihi, iliyothibiti, iliyo mbali na matamanio na mapenzi ya nafsi. Na ujue – ewe mwenye kutaka uongofu – kuwa itikadi ndiyo inaziongoza tabia na mwenendo, na ndiyo siri ya kuthibiti, basi ni bora kwa kila muislam akaitafuta haki katika itikadi, na asimfuate kila msemaji, akijidai yeye ndiye mwenye haki, hali ya kuwa hana fungu lolote katika haki, jitahidi kweli kweli kufikia uhakika, na kushikamana na njia ilo imara zaidi ili ufikie makusudio yako, ukiwa mbali na ushabiki mbaya wa kimadhehebu, na kufuata kwa upofu. Na uamini moja kwa moja kuwa HAKI NI MOJA TU, basi usifuate ispokuwa hiyo tu.
Na ujihadhari - ewe Muislam -, usije ukatekwa na maandishi ya kitabu utakachokisoma, kabla hujakipima kwa kipimo cha sharia na akili, ili uupate usawa wala usitie shaka. Hapa, tutakwenda pamoja katika mfululizo huu mwepesi, ulio wazi utakaokuwekea wazi hakika ya AHLUDAAWA WA ISTIQAAMA – IBADHI, madhehebu ambayo wanajulikanwa wafuasi wake kwa uchamungu na usafi, na ambao hawaogopi kwa ajili ya Allah mtukufu lawama za wenye kulaumu,wamezitoa nafsi zao katika njia ya Allah mtukufu, wakaieneza haki, wakahukumu kwa uadilifu kwa karne nyingi, wakishikimana na kitabu cha Allah mtukufu, wakifuata Sunnah ya Mtume – Rehma na amani ziwe juu yake – LAKINII...
Madhehebu yao ikasukiwa vitimbi, ili ionekanwe kwa ubaya katika njia yake, na mashambulizi mangapi yamefanywa ili kuizima nuru yake, na mangapi mazuri yake yamechanganywa na mabaya ya wenye matamanio na nia mbaya, na mpaka leo… bado yatupiwa tuhma batili kwa sababu ya baadhi ya watu kutodiriki uhakika wa mambo. Lakini haiwezekani ikazimika nuru itokayo katika Quran na sunnah, kisha ikabebwa na vidume viloshiba mapenzi ya Allah mtukufu na kuwa tayari kufa mashahidi katika kuifikisha nuru hiyo, HAIWEZEKANI NURU HIYO IKAZIMIKA AU KUJIFICHA.
Basi tuwe pamoja ewe msomaji –, tuvuke pamoja kwa SAFINA HII YA UONGOFU tukaikamate bendera ya haki, huu ni ulinganio kwako , kwako wewe peke yako unayesoma, achana na kufuata mkumbo sasa hivi, njoo tuifutilie njia ya haki ilonyooka, huu ni wajibu wa kila muumin mwenye akili,usiukimbie, amesema Allah mtukufu “ NA WALE WATAKAOJITAHIDI KWA AJILI YETU TUTAWAONGOZA NJIA YETU”.Basi jitahidi – Allah akuhifadhi – na ipe nafsi yako njia ya kuifuatilia njia ya haki na uhakika, upate malipo ya kujitahidi na kuipatia haki. Ishi kwa haki na katika haki, weka qur-an na sunna kuwa ni mizani yako, wachana na ushabiki na ufuatishaji mkumbo wa kimadhehebu, na jihadhari kung’ang’ania rai za watu ambao wanapatia na kukosea, hawatakufaa kitu kwa kuiacha kwako haki.
Ndugu yangu , Kunywa katika chemchemi hii safi, maji ya haki na uhakika, achana na michirizi ilochanganyika na kuchafuka, na yarudie sana kuyasoma haya ninayokuandikia, mpaka lichomoze jua la maarifa katika moyo wako, kwa muono na hoja za wazi katika itikadi yako, na elimu ya kweli kuhusu dini yako.Huu ni mfuatano wa makala kuhusu haki na hakika, nauweka mbele yako, upate kuyafaham mambo kwa kufuatana,…. Allah mtukufu akuongoze, na akuweke katika njia ya Haki na msimamo katika dini. |