Ibadhi.com
Mada Mpya

MAIMAMU

Imam Abu Saidi Mohammad bin Said Al-Kudami Allah amrehemu: "Na yoyote katika watu akiacha njia ya haki -ikiwa ni Imamu au mwengine yoyote- hakumdhuru chochote yule aliyethibiti juu ya haki, hata kama huyo aliyethibiti juu ya njia ya haki -ambayo imesihi kwake kuwa ndiyo haki katika makubaliano- ni mmoja na kuendelea, hata kama ni kijakazi mmilikiwa, ikiwa peke yake ndiye aliyethibiti katika njia ya haki, basi yeye ndiye atakayekua hoja juu ya watu wote wa Ardhini.

Na kila atakayekwenda kinyume na njia ya aliyethibiti juu ya haki ambayo imefikiwa na makubaliano kuwa ndiyo haki, huyo atakuwa yuko katika moja ya hali mbili:

1. Ima ni mwenye madai, basi madai yake hayatakubaliwa isipokuwa kwa haki, wala haifai kwake kupigana kwa sababu ya madai yake.

2. Ima atakua ni mwenye kujitosa katika mambo ambayo anayaitakidi uharamu wake, hapo atakuwa amejitia kiburi huyo, amejishindia bila ya njia ya haki."

[Al-Istiqamah 2/40]

Imam Hilali bin Attiyah Al-Khurasani (134 Hijiria)

Alikuwa ni kiongozi wa kijeshi na msemaji mahiri, asili yake ni Khurasani kisha akahamia Basra Iraqi, ametajwa na Shammakhi katika tabaka ya Imamu Rabii bin Habib (r.a) naye alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi wa Imam Abu Ubaidah Muslim bin Abi Karimah (r.a).

Imamu Hilali bin Attiyah alikuwa kabla katika madhehebu ya Sufriyah kisha Allah mtukufu akamneemesha kwa uongofu, basi wanahaki walimtaka arejee katika mji wake na awarejeshe katika haki wale waliomkubalia hapo kabla katika ulinganiaji wake wa Itikadi ya Sufriyah, basi alirejea na akafanya aliyoamrishwa na wanahaki, na hapo akawa pamoja nao katika Walaayah.

Imamu Hilali bin Attiyah (r.a) aliunganyika na watu wa Oman na akawa Waziri wa Imamu Julandaa bin Massoud (r.a) na nguzo kati ya nguzo za Dola yake adilifu, naye ndiye aliyeongoza jeshi la Imamu Julandaa akiwa pamoja na Yahya bin Nujaihi (r.a) kwa kupigana na Mkhawariji Sheibani Imamu wa Sufriyah, basi ushindi ukawa wao na udhalilifu wa kushindwa ukawa kwa Sheibani Al-Khajirii.

Pia Imamu Hilali bin Attiyah (r.a) alikuwa ni mmoja wa washauri wa Imamu Julandaa (r.a) kuhusiana na jambo la Khaazim bin Khuzaimah Jemeradi wa Saffaah Mfalme wa dola ya Kiaabbas wakati huo; kwani Khaazim aliwakatalia isipokuwa kuhutubia na utiifu, basi alikataa Imamu Julandaa na waliokuwa pamoja naye kumpa aliyotaka, na hapo vikazuka vita baina yao, basi Khaazim alitumia hadaa na ujanja mpaka akaua jeshi lote la Imamu Julandaa bin Massoud (r.a) na hakubakia isipokuwa Imam Julandaa na Hilali bin Attiyah tu, basi Imamu Julandaa akamuambia Hilali: Ingia vitani ewe Hilali. Naye akajibu: Wewe ni kiongozi wangu tangulia mbele yangu na lako kwangu sitobakia baada yako, basi Imamu Julandaa akatangulia naye akapigana mpaka akauliwa, kisha akatangulia Hilali bin Attiyah akiwa na ngao yake ya vita, basi wanajeshi wa Khaazim wakawa wanashangaa kwa uhodari wake nao hawakumjua kisha wakamjua ni nani, wakasema: Hilali bin Attiyah, basi walimfanyia njama mpaka wakamuua Allah amrehemu. yalikuwa hayo mwaka 134 Hijiria.

Allah awakubali Mashahidi hao wa haki Imamu Julandaa bin Massoud Al-Julandanii (r.a) na Hilali bin Attiyah Al-Khurasani (r.a) na waliopata shahada pamoja nao.

IMAMU RABII BIN HABIB AL-BASRIY AL-FARAHIDIY (R.A)

Imamu Rabiu bin Habib Al-Basri R.A anafahamika katika safu za Kiibadhi kwamba ni Abu Amru Al-Rabiu bin Habib Al-Basriy Al-Farahidiy, naye ni Imamu wa tatu wa Kiibadhi katika marejeo ya Kielimu, Imamu Rabii R.A kazaliwa Oman kati ya mwaka wa 75 mpaka 80 Hijiriya, kisha akahama na kuhamia Iraq katika mji wa Al-Basra na akaishi huko muda mwingi wa maisha yake ya kutafuta elimu na kusoma, kisha akarejea Oman mwishoni mwa maisha yake, na akahitimisha maisha yake katika nchi yake ya asili alipozaliwa ndani ya Oman, alifariki kati ya mwaka 171 na 180 Hijiria na aliongoza sala ya kusalia jeneza lake Imam Mussa bin Abi Jabir Al-Azkawi (r.a) na kaburi lake ni maarufu liko katika wilaya ya Liwa Oman.

Imamu huyu katajwa na Maulamaa wengi wa Kiibadhi na wasiokuwa wa Kiibadhi, pia katajwa na watangulizi katika fani ya Hadithi ambao ni wajuzi wa wapokezi na wasimulizi.

REJEA ZA KIIBADHI ZILIZOMTAJA IMAMU RABII BIN HABIIB (R.A):

Kwa hakika Imamu Rabii (r.a) ni maarufu sana katika safu za Ibadhi, basi hakuna kitabu kilichoandikwa na mwanachuoni wa Kiibadhi na kikazungumzia suala la Hadithi na Athari za Maimamu ila hutajwa Imamu huyu mwenye hadhi kubwa katika safu zao, kuanzia vitabu vya karne ya pili Hijiria hadi zama zetu hizi.

Basi Imamu Rabii bin Habib ametajwa katika vitabu mashuhuri hususan:

 1. KITABU "AL-SIYAR WAL-JAWABAATI" CHA MJUMUIKO WA MAULAMAA KUANZIA KARNE YA PILI HADI YA NNE.
 2. KITABU "AL-MUDAWWANA" CHA ABI GHAANIM AL-KHURASANIY. KILICHOANDIKWA MWANZO WA KARNE YA TATU.
 3. KITABU "AL-JAAMIU" CHA IBNU JAAFAR. KARNE YA TATU.
 4. KITABU "AL-JAAMIU" CHA ABU AL-HAWARIY KARNE YA TATU.
 5. KITABU "AL-MU'UTABAR" CHA IMAMU ABU SAID AL-KUDAMIY KARNE YA NNE.
 6. KITABU "AL-JAAMIU" CHA IBNU BARAKA. KARNE YA NNE.
 7. KITABU "AL-JAAMIU" CHA ABU AL-HASAN AL-BISYAWIY. KARNE YA NNE
 8. KITABU "BAYANU AL-SHAR'IY" CHA SHEIKH MUHAMMAD BIN IBRAHIM AL-KINDIY. KARNE YA TANO
 9. KITABU "AL-MUSANNAF" CHA SHEIKH AHMAD BIN ABDALLAH AL-KINDIY. KARNE YA SITA.
 10. KITABU "TABAQAATU AL-MASHAAYKH. CHA SHEIKH AL-DARJINIY. KARNE YA SABA.
 11. KITABU "AL-JAWAAHIRU AL-MUNTAQAA" CHA AL-BARAADIY. KARNE YA NANE.
 12. KITABU "AL-SIYAR" CHA Al-SHAMMAKHIY ALIEFARIKI MWAKA 928H.

Hivi ni vitabu ambavyo ametajwa ndani yake Al-Imam Al-Rabi'u bin Habib R.A kwa uwazi kabisa na kumzingatia kuwa ni Imamu wa tatu wa Madhehebu ya Kiibadhi, utakuta hapo kwamba Imamu huyu katajwa tangu karne ya pili na ya tatu na zilizofatia.

MASHEKHE WA AL-IMAMU AL-RABIU BIN HABIB (R.A):

Miongoni mwa masheik wa Al-Imamu Al-Rabiu bin Habib ni:

 1. Abu Ubayda Muslim bin Abi Karima Al-Tamimiy (R.A)
 2. Dhimam bin Saaib Al-Umaniy (R.A)
 3. Abu Nuh Saleh Al-Dahhan (R.A)

ATHARI ZA AL-IMAMU AL-RABIU BIN HABIB (R.A):

 1. Al-Musnad Al-Sahihi (المسند الصحيح)
 2. Kitabu "Aatharu Al-Rabii" (كتاب آثار الربيع)

Huu ni mukhtasari mfupi sana kutoka kwa Maibadhi kuhusu Imamu Al-Rabiu bin Habib.

REJEA ZISIZOKUWA ZA KIIBADHI :

Tufahamu kuwa hakuna ulazima wa kutajwa Maimamu wetu katika vitabu vya Maulamaa wa madhehebu nyengine yoyote, na bila shaka kila watu wana haki zaidi na watu watu wao; kwa hiyo shahada ya Maibadhi kutoka vitabuni mwao na kupitia Maulamaa wao ndiyo ya kutegemewa kwa kuwajua Maulamaa wao na Maimamu wa Kiibadhi, basi kuleta kwetu uthibitisho wa Imamu Rabii bin Habib Al-Basriy (r.a) kutoka katika vitabu vya wasiokuwa Ibadhi hususan Masunni ni kwa njia ya kuituliza nafsi ya mwenye shaka kwa wale wanaoona ulazima wa kutajwa Maimamu katika vitabu vyao, basi elewa kwamba miongoni mwa waliomtaja Imamu Rabii bin Habib R.A ni:

MAIMAMU WA KISUNNI:

1. Imamu Al-Bukhari:

Katika kitabu chake "Al-TAARIKHU AL-KABIIR" juzuu ya tatu ukurasa wa mia mbili na sabiini na saba (J.3 UK. 277):

ربيع بن حبيب : سمع الحسن وابن سيرين روى عن موسى البصري

((Rabi'u bin Habib: Kasikia kutoka kwa Al-Hassan na Ibnu Siirin, kapokea kutoka kwa Musa Al-Basariy)).

2. Ibnu Hibban:

Katika katika kitabu "AL-THIQAAT" (J. 6 UK. 299) amesema kwamba:

الربيع بن حبيب يروي عن الحسن وابن سيرين ، روى عن موسى بن إسماعيل

((Al-Rabi'u bin Habib kapokea kutoka kwa Al-Hassan na Ibnu Siirin, na kapokea kutoka kwa Musa bin Ismail)).

3. Ibnu Shaahiin:

Kasema katika kitabu chake "TAARIKHU ASMAAI AL-THIQAAT"  kwamba: "Na Al-Rabiu bin Habib vile vile ni Al-Bisriy, kapokea kutoka kwa Al-Hassan na Ibnu Siirin, naye ni Thiqa.

4. Yahya bin Ma'iin:

Katika kitabu chake "Al-Taarikh" kamtaja katika sehemu kadha wa kadha.

5. Ahmad bin Hambal:

Katika kitabu chake "AL-'ILAL WA MA'ARIFATUL AL-RIJAAL" (chapa ya Al-Maktabatu Al-Islaamiyatu chapa ya mwanzo 1408H-1988)

Anasema Abdallah mtoto wa Imamu Ahmad katika (J. 2 UK. 56 No. 1538) kwamba: Nimemsikia anasema: Ilikuwa anatujia mtu kutoka Basra anaitwa Al-Haytham bin AbdulGhaffar Al-Taaiy anatusimulia rai ya Qatada kutoka kwa Hammam, nakutoka kwa mtu anaeitwa Al-Rabiu bin Habib aliepokea kutoka kwa Dhummam kutoka kwa Jabir bin Zayd na kutoka kwa Rajaa bin Abi Salma….

Zingatia maneno haya:

 1. Alikuwa anatujia mtu kutoka Basra
 2. Anasimulia kutoka kwa mtu anaeitwa Al-Rabiu bin Habib aliepokea kutoka kwa Dhimam kutoka kwa Jabir bin Zayd.

Na andiko hili vile vile limo katika "TAARIKHU BAGHDAD" (J. 14 UK. 55) ila yeye huko kasema Hammam badala ya Dhimam, na bila shaka hili ni kosa (Tas-hiif) la uchanganyaji wa jina ambalo limethibiti usahihi wake katika maneno ya Ahmad bin Hambal, ama Jabir bin Zayd Abu Al-Sha'athaa R.A ni Imamu muasisi wa madhehebu ya Kiibadhi, ama Dhimam yeye ni Dhimam ibn Saaib Al-Umaniy naye ni Ibadhi vile vile.

6. Yahya bin Ma'iin

Kamtaja katika "AL-TAARIKH" chapa ya (DAARUL QALAM BEYRUT KWA RIWAYA YA AL-DUURIY) kamtaja katika sehemu mbili:

 1. Kamtaja katika (J. 2 UK. 157 NO. 3940)
 2. Kamtaja katika (J. 2 UK. 268 NO. 4723)

7. Al-Daulabiy

Kamtaja katika "Al-KUNA WA AL-ASMAA" (J. 2 UK. 74-75).

Na sisi tumetangulia kusema kwamba Dhimam ni katika Masheikh wa Imamu Al-Rabiu bin Habib.

Na kapokea Imamu Al-Rabiu bin Habib katika Musnad wake kutoka kwa Dhimam kutoka kwa Jabir bin Zayd Hadithi (no. 520) na kapokea kutoka kwake Hadithi mbili (no. 112 na 688) kupitia kwa Abu Ubayda Muslim.

Kwa hakika sisi hatujui aslan kuwepo kwa Al-Rabiu bin Habib aliyepokea kutoka kwa Dhammam bin Saaib ambaye ni muibadhi kutoka kwa Jabir bin Zayd ambaye ni muibadhi isipokuwa Imamu Rabii bin Habib ambaye ni Muibadhi.

Tufahamu kuwa katika jerea za Maimamu wa Kisunni wametawa Rabii bin Habib watatu, yaani jina hilo hilo kwa watu watatu tafauti nao ni:

1. Al-Rabiu bin Habib Abu Salma kutoka Al-Yamama:

Huyu kamataja Al-Bukhari katika "Al-Taarikh Al-Kabiir" na akamtaja Ibnu Hibban katika "Al-Thiqaat" na akamtaja Al-Dhahabi katika "Miizan Al-I'itidaal" na akamtaja Al-Maziyu katika "Tahdhiibu Al-Kamaal" na akamtaja Ibnu Hajar katika "Al-Tahdhiib" na katika "Al-Taqriib" naye ni Thiqa.

2. Al-Rabiu bin Habib Al-Kufi:

Huyu ni kaka wa Aaidh bin Habib ambao inasemwa kwamba wao ni katika Banu Al-Malaah.

Huyu kamtaja Al-Bukhari katika "Taarikh Al-Kabiir" na akamtaja Ibnu Hibban katika "Al-Majruuhiin" na akamtaja Al-Dhahabi katika "Al-Miizan" na akamtaja Al-Mazyu katika "Tahdhiibu Al-Kamaal" na akamtaja Ibnu Hajar katika "Al-Tahdhiib" na katika "Al-Taqriib" naye wametafautiana katika kukubalika kwake kihadithi.

3. Al-Rabiu bin Habib Al-Bisriy:

Huyu ndiye Imamu wetu mkusudiwa, na inatosha shahada ya Ibnu Ma'iin  katika kitabu chake "Al-Taarikh" anasema Ibnu Ma'iin katika Taarikh yake kwamba:

1. Al-Rabiu bin Habib vile vile ni Bisriy anapokea kutoka kwa Al-Hassan na Ibnu Siirin naye ni Thiqa. (J. 1 UK. 260 NO. 1711)

2. Al-Rabiu bin Habib ni Bisryi naye ni Thiqa. (J. 2 UK. 87 NO. 3406)

3. Al-Rabiu bin Habib ni Bisriy anahadithi kutoka kwa Al-Hassan na Ibnu Siirin, naye ni Thiqa. (J. 2 UK. 113. NO. 3593)

4. Al-Rabiu bin Habib ni Bisriy naye ni Thiqa. (J. 2 UK. 195 NO. 4206)

5. Al-Rabiu bin Habib ni Bisriy anapokea kutoka kwake Abu Daud na Affan, kama ilivyotangulia kauli ya Ibnu Shaahiin kuhusu yeye, naye ni Thiqa. (J. 2 UK. 263 NO.4697)

Wabillahi Taufiiq.

Asanteni sana.

Inaelezwa kuwa Imamu Mohammed bin Abdillahi Al-Khalili (r.a) siku moja alihudhuria kwa kusali sala ya Magharibi katika sehemu ya kusalia ndani ya ngome, basi akaamrisha ikimiwe sala, wakati sala inakimiwa mara Imam akanusa harufu ya moshi wa sigara, basi hapo hapo alimuambia mwenye kukimu sala: "Nyamaza" kisha akauliza: "Huu moshi unatokea wapi?" Hapo akaambiwa: Huyu ni mgeni aliye mgeni, naye ndiye mwenye kuvuta sigara. Akasema: Mleteni. Basi alipofika alimwambia: Hakika Waislamu wamekukirimu basi wakakukaribisha katika ngome yao, na wewe hukuwatunzia heshima yao na wala hukutunza heshima ya nafsi yako, hivi unamuasi Allah na wewe ni mwenye kufurahi?!!! Toka nje ya ngome wala hatukukubalii kubakia hapa".

Basi yule mtu akajitayarisha kuondoka asubuhi yake, na Imam akamkabidhi mtu wa kumtoa nje ya ngome, kisha ndio Imam akamrisha kukimiwa sala baada ya kuondosha uovu na makero ya uovu huo.

Ifahamike kuwa Imam Mohamed bin Abdillahi Al-Khalili (r.a) alikamata hatamu za uongozi wa kuiongoza Oman kwa nidhamu ya Uimamu katika mwaka wa 1338 Hijiria naye aliendelea katika Uongozi huo mpaka mwaka 1373 Hijiria amabo ni sawa na 1954 AD.

Pia ifahamike kuwa Wanaelimu wa Kiibadhi wamekubaliana katika uharamu wa kuvuta segereti tokea hapo mwanzo.

HII NI ORODHA YA MAIMAMU MAIBADHI WALIOPEWA BAIA YA UONGOZI NA WAKAHUKUMU, ORODHA HII INAKUSANYA MAIMAMU KUANZIA WA MWANZO MPAKA WA MWISHO BILA YA KUZINGATIA SEHEMU ALIYOHUKUMU, NA MAIMAMU WA KIIBADHI WALIHUKUMU KATIKA YEMEN NA OMAN NA AFRIKA YA KASKAZINI LAO (ALGERIA LIBYA NA TUNISIA).

 1. Twalibulhaqi Abdullahi bin Yahya Al-Kindi (r.a) (130 HJ).
 2. Julandaa bin Massoud Al-Julandanii (r.a) (132-134 HJ).
 3. Abu Alkhattab Al-Maafiri (135 - 144 HJ).
 4. Abdurahman bin Roustum Al-Faarisi (144 - 168 HJ).
 5. Abdulwahaab bin Abdurahman Al-Faarisi (168 - 188 HJ).
 6. Mohammad bin Abi Affan (177-179 HJ).
 7. Aflah bin Abdulwahaab bin Abdurahman Al-Farisi (188 - 238 HJ).
 8. Waarith bin Qaab Al-Kharousi (r.a) (179-192 HJ).
 9. Ghassaan bin Abdillahi Al-Yahmadi (r.a) (192-207 HJ).
 10. Abdulmalik bin Humaid Al-Alawi (r.a) (207-226 HJ).
 11. Muhanna bin Jeifar Al-Yahmadi (r.a) (226 - 237 HJ).
 12. Salt bin Malik Al-Kharousi (r.a) (237 - 272 HJ).
 13. Abubakar bin Aflah bin Abdulwahaab Al-Farisi (238 - 241 HJ).
 14. Muhammad bin Aflah bin Abdulwahaab (241 - 281 HJ).
 15. Rashid bin Nadhar Al-Yahmadi (r.a) (272-277 HJ).
 16. Azzan bin Tamim Al-Kharousi (r.a) (277-280 HJ).
 17. Abu hatim Youssuf bin Muhammad bin Aflah Al-Farisi (281 - 294 HJ).
 18. Alyaqdhaan bin Muhammad bin Aflah Al-farisi (294 - 296 HJ).
 19. Alhakam bin Mullaa.
 20. Salt bin Qaasim Al-kharousi.
 21. Azzan bin Huzbar.
 22. Abdullah bin Muhammad Al-Haddani.
 23. Alhawari bin Matraf Al-Haddani.
 24. Hassan bin Said Al-Sahtani.
 25. Muhammad bin Hassan Al-Azdi.
 26. Said bin Abdillahi Al-Ruhaili (320-328 HJ).
 27. Rashid bin Waliid Al-Kindi (328 - 342 HJ).
 28. Hafs bin Rashid (355 - 364 HJ).
 29. Rashid bin Said Al-Yahmadi (442 - 445 HJ).
 30. Alkhalil bin Shaadhan (445 - 447).
 31. Mohammad bin Malik bin Shaadhan.
 32. Rashid bin Aliy Al-Kharousi.
 33. Khambash bin Mohammad bin Hishaam.
 34. Mohammad bin Abi Ghassan.
 35. Mussa bin Abi Al-Maali Kahlab bin Mussa. (549 - 579 HJ).
 36. Mohammad bin Khambash bin Muhammad.
 37. Alhawari bin Malik (832-833 HJ).
 38. Malik bin Alhwari bin Malik.
 39. Abu Hassan bin Khamis bin Aamir (839 - 846 HJ).
 40. Omar bin Khattab Al-Kharousi (885 - 894 HJ).
 41. Muhammad bin Sulleiman Al-Mufarriji (894 + 896HJ).
 42. Omar Ashariif (895 HJ).
 43. Ahmad bin Omr Al-Rubkhi.
 44. Abu Hassan bin Abdisalam.
 45. Muhammad bin Ismail Al-Hadhiri (906 - 942 HJ).
 46. Omar bin Qassim Al-Fudhaili (965 - 967 HJ).
 47. Abdullah bin Muhammad Al-Qarn (967 - 968 HJ).
 48. Aamir bin Rashid bin Muhammad Al-kharousi.
 49. Nassir bin Murshid Al-Yaarubi (1034-1059 HJ).
 50. Sultan bin Seif bin Malik Al-Yaarubi (1059 - 1090 HJ).
 51. Balaarab bin Sultan bin Seif Al-Yaarubi (1090 - 1104 HJ).
 52. Seif bin Sultan bin Seif bin Malik Al-Yaarubi (1104 - 1123 HJ).
 53. Sultan bin Seif bin Sultan Al-Yaarubi (1123 - 1131 HJ.
 54. Muhannaa bin Sultan bin Majid Al-Yaarubi (1131 - 1133 HJ).
 55. Yaarub bin Balaarab bin Sultan Al-Yaarubi (1134 - 1135 HJ).
 56. Muhammad bin Nassir Al-Ghaafiri (1137 - 1140 HJ).
 57. Seif bin Sultan bin Seif bin Sultan bin Malik Al-Yaarubi (1140 - 1146 HJ) + (1151 - 1154 HJ).
 58. Balaarab bin Humair bin Sultan Al-Yaarubi (1146 - 1151 HJ) + (1157 - 1162 HJ).
 59. Sultan bin Murshid bin Adey Al-Yaarubi (1154 -1156 HJ).
 60. Ahmed bin Said Al-Busaidi (1162 - 1198 HJ).
 61. Said bin Ahmed bin Said Al-Busaidi (1198 1225 HJ).
 62. Salim bin Rashid Al-Kharousi
 63. Muhammad bin Abdillahi Al-Khalili.
 64. Ghalib bin Aliy Al-Hinai.

 

Alikua Abu Ubaidah (r.a) haipi umuhimu sana mizozo ya suala la Qadar, na alikua akisema: "Wallahi hamuna ndani yake kuoa mwenye mume, wala kulazimika na kuhajiri, wala kuhukumu kwa asiyoyateremsha Allah; kwani hakika yake ni uoni wameutokezesha watu baina yao, basi yoyote mwenye kukubali kuwa Allah amevijua vitu kabla ya kua kwake hivo vitu huyo tayari ameshakubaali Qadar."

 

"Hakika mbora wa waumini mbele ya Allah kicheo, kidaraja, na kiutangulizi ni aliye mbora zaidi katika kumuadhimisha yeye na Kitabu chake na Dini yake na makatazo yake, na Allah anawapa waumini kila mwenye daraja kwa daraja yake"

(Rasail Imam Jabir bin Zaid uk. 37)

Amesema Abu Sufiyan Mahboub bin Ruhail (r.a): "Na ambayo yamepokewa kwetu kutoka kwa Jabir bin Zaid -Rehma za Allah ziwe kwake-, kua yeye aliulizwa: Ni yapi yenye wasaa kwa watu ujinga wake? Basi alisema: ((Ni yale waliyoitakidi uharamu wake ikiwa tu hawajayafanya, au kumpenda aliyeyafanya, au kujitenga na wanaelimu iwapo watajitenga na aliyeyafanya, au kusimama kwa kutowapenda wala kutowachukia))

Amesema Mahboub (r.a): "Ufafanuzi wa aliyosema Jabir bin Zaid wakati alipoulizwa kuhusu yaliyokua na wasaa kwa watu ujinga wake naye akasema: ((Ni yale waliyoitakidi uharamu wake ikiwa tu hawajayafanya, au kumpenda aliyeyafanya, au kujitenga na wanaelimu iwapo watajitenga na aliyeyafanya, au kusimama kwa kutowapenda wala kutowachukia)) hayo ni kua lau mtu hakujua kama ulevi ni haramu wala nguruwe ni haramu na mfano wake miongoni mwa aliyoyaharamisha Allah na hali yeye ni mwenye kuyaramisha, basi huyo yumo katika wasaa wa hilo ikiwa hatoyajua hayo kama yaalivyo, ikiwa hakula nguruwe au hakunywa ulevi au akampenda mwenye kuyafanya hayo au akawachukia Maulamaa iwapo watachukia mwenye kuyafanya hayo, au akasimama kwa kutowapenda wala kuwachukia."

 

بسم الله الرحمن الرحيم

Shukurani zote ni kwa Allah mtukumu, na rehma na amani ziwe kwa Mtume wake Muhammad pamoja na kila aliyeongoka kwa uongofu wake kuanzia kwa masahaba wake na aali zake na waliofuatia kwa wema mpaka siku ya malipo.

Tujue kuwa Allah mtukufu kwa fadhila zake ameikamilisha neema yake ya Uislamu katika uhai wa Mtume wetu Muhammad (s.a.w), basi ilisimama hukumu yake ya kuhukumu jamii kwa sheria ya Allah katika uhai wa Mtume (s.a.w), na baada ya kufariki Mtume (s.a.w) Waumini walichagua viongozi walioongoza kiuadilifu mpaka mwaka wa 38 Hijiria, kisha baada ya hapo zikatanda fitna ambazo ziliathiri uongozaji moja kwa moja, na katika hali hiyo walipatikana watetezi wa haki waliohifadhi mafundisho na kuisoma hali ya jamii iliyokua ikijiri, kwa kuweka misingi madhubuti ya kuihifadhi dini ili isije ikaathirika na mapenyezo ya kimafundisho kutoka kwa maadui zake; kwani bila ya shaka mafundisho ndio muhimu zaidi katika risala ya uislamu.

Basi ilipatikana madrasa ya Imam Jabir bin Zaidi Al-Uzdi (r.a) naye ni mwanachuoni muomani aliyezaliwa katika kipindi cha utawala wa Omar bin Al-Khattabi (r.a) na kufariki mwisho wa karne ya mwanzo hijiria mwaka 96 Hijiria, mwanachuoni huyu alichukua elimu yake moja kwa moja kutoka kwa Masahaba wa Mtume wetu (s.a.w) Allah awe radhi nao, basi chuo chake kwa taufiqi ya Allah kiliweza kutoa maulamaa wenye ujuzi mzuri sana katika Dini, wafuasi wa chuo hichi ndio waliojulikana baadae kwa jina la Ibadhi.

Chuo hichi kiliweza kutoa viongozi bora walisimamisha utawala wa kiislamu kwa misingi ya Qur-ani na Sunna ya Mtume wetu Muhammad (s.a.w), na sisi hatujui kuwa katika tarehe ya Waislamu tokea kuangushwa utawala wa Imam Aliy (k.a.w) kuwa iliweza kusimama Dola kwa misingi ya Shuura na Uadili isipokua kaatika safu za Maibadhi peke yao, hatukatai kuwa alikuja Mtawala mmoja muadilifu katika Dola ya Bani Umayyah naye ni Omar bin Abdilaziz (r.a) ambaye alihukumu kipindi cha miaka miwili mwishoni mwa karne ya mwanzo.

Basi Maibadhi waliweza kufanyia kazi msingi wa Shuura kikamilifu na kuteua viongozi waadilifu katika sehemu walizokuwepo na kupata nguvu ndani yake, nazo ni sehemu tatu maarufu.

1. Yemen.

2. Oman.

3. Afrika Kaskazini.

Basi katika sehemu yetu hii tutakua na utambulisho wa Maimamu wa Kiibadhi waliohukumu.

Tunamuomba Allah atukubali na atupe taufiqi yake katika njia hii njema.

Asanteni sana.

بِسْمِ اللَّهِ ٱلرَّحْمَـٰنِ ٱلرَّحِيمِ

Shukurani zote ni kwa Allah mtukufu, na rehma na amani ziwe kwa Mtume wetu Muhammad na kila aliyeongoka kwa uongofu wake mpaka siku ya malipo.

Kwa hakika Madhehebu ya Ibadhi ni kongwe sana, na uhakika ulivyo hasa ni kuwa Madhehebu hii ndiyo asili waliyobakia ndani yake Waislamu kila ilipotokezea migawiko ya kugawika umma kimakundi, kwa hiyo Waislamu hao waliweza kujulikana kwa kubaguka na wengine walio waathiriwa wa fitna za kisiasa na fitna zilizopelekea migawiko, nao waliweza kubaguka kikamilifu katika mwaka wa 64 Hijiria, kwani ndio mwaka iliokusanya tukio la kumeguka Makhawariji katika safu zao, pia hali ya uislamu huo iliweza kupatikana katika zile sehemu ambazo Uislamu ulifika mapema zaidi nazo zikabakiaa bila ya kuathirika na mawimbi hayo ya fitna za kisiasa na uchafuzi wa dini yaliyosababisha kugawika waislamu na kuwa makundi tofauti, kwani sehemu hizo ziliweza kubakia katika asili ya Uislamu kama ulivyokuwa wakati wa Mtume (s.a.w), na miongoni wa sehemu hizo ni Oman ambayo ilikuwa na mamlaka kamili ya kujitawala wenyewe kabla ya Utume wa Mtume wetu Muhammad (s.a.w), nayo ni nchi iliyokubali Uislamu na kuusihi vizuri hata kabla ya Mji wa Makka; kwani Oman ilikubali Uislamu kikamilifu katika mwaka wa sita hijiria kabla ya ufunguzi wa Mji mtukufu wa Makka, na tahere imetuhifadhia kuwa mtu wa kwanza kuusihi uislamu katika watu wa Oman ni Sahaba Maazin bin Ghadhuuba Asamaaili (r.a) na uislamu uliweza kuenea ndani ya Oman kupitia kwake, hadi Mafalme wa wakati huo Abdi na Jaifar wana wa Junalndaa (r.a) walipofikiwa na barua ya Mtume (s.a.w) na kuukubali Uislamu na kwa hiyo taifa la Oman kikamilifu kuingia katika Uislamu bila ya vita wala nguvu.

Oman ndiyo nchi pekee iliyokuwa mbali na fitna zilizotokea katika kipindi cha Masahaba, basi Waislamu wa Oman waliendelea kujitawala kwa misingi ya Kiislamu safi kama ilivyokuwa wakati wa Mtume (s.a.w) na Abu Bakar na Omar na Othman, ama katika kipindi cha Imam Aliy bin Abi Twalib wao hawakuwa chini ya Utawala wake kutokana na umbali uliokuwepo na kushughulishwa kwake na fitna zilizotokea hadi kuuangusha utawala wake katika mwaka wa 38 Hijiria, na kuanza rasmi Utawala wa Kifalme wa Bani Umayyah kuanzia kwa Mfalme Muawiyah bin Abi Sufiyan, na kuanza rasmi kipindi cha Dola ya Bani Umayyah kilichodumu kwa miaka 92 ambacho ni maarufu katika udhalimu wake katika Jamii za waislamu kwani hakikutoa Mtawala Muadilifu isipokuwa Omar bin Abdilaziz (r.a) naye alihukumu kwa miaka miwili tu na kufa kwa kupewa sumu, Allah amridhie.

Katika kipindi cha Mfalme Abdulmalik bin Marwan Al-Umawiy (65 HJ - 86 HJ) Dola ya Kiumayyah iliamua kuiingiza Oman ndani ya mamlaka yake, basi ilimtumilia Gavana wake wa Iraq Hajjaj bin Youssuf Al-Thaqafi katika kulitimiza jukumu hilo; na katika kutafuta njama za kisiasa dhidi ya Oman ndio wakawaita kwa jina la Ibadhi, na kuwaingiza katika hukumu ya Ukhawariji ili kupata sababu ya kisiasa ya kuwapiga vita, walifanya hivyo kwa sababu Imam Abdullahi bin Ibadhi Al-Tamimi (r.a) alidhihiri katika Iraqi akiwa katika asili ya mafundisho ya Uislamu na kuwataka watu wausihi Uislamu kwa mafundisho yake, naye hakuacha kuwemo katika njia hiyo hadi kufikia kuwataka viongozi kuerejea atika Uadilifu wa Uislamu, na barua yake aliyomjibu Mfalme Abdulmalik bin Marwan Al-Umawiy imenukuliwa katika baadhi ya vitabu vya Kitarehe.

Jaribio la Ufalme wa Kiumayyah -ingawa baada ya mapigano ya muda- lilifanikiwa na kuweza kuichukuwa Oman, lakini utawala wao haukubakia muda mrefu ndani ya Oman; kwani Waislamu wa Oman waliweza kuunganisha safu zao upya na kusimamisha Utawala wao kwa msingi wa Shura wa Kiislamu kuanzai mwaka wa 132 Hijiria ambapo walimpa Baia (Ahadi ya Uongozi) Imam Julandaa bin Massoud Al Julandanii  (R. A).

Kutokana na hapa Wanaelimu na Maimamu wa Kiibadhi waliweza kupatikana mapema sana tokea kipindi cha Masahaba wa Mtume (s.a.w) mpaka hivi leo.

Anasema Sheikh Nassir bin Abi Nabahani (r.a): ((Na watu wa Omani katika wakati huo (wa fitina) walikuwa mbali na fitna hizo, wanamuabudu Allah mtukufu kwa yale waliyoyachukuwa katika Elimu kutoka kwa Nabii (s.a.w) katika zama zake, na kutoka kwa Masahaba baada yake katika zama za Abu bakari Siddiiq na Omar bin Khattaab, na hali yao ni kuwa hawajui Khawarij, wala Abdullahi bin Ibadhi, wala wengineo, na hawakuchukuwa kutoka kwa Abdullahi bin Ibadhi hata mas-ala moja, basi zilipowafikia khabari hizo, na khabari za Abdullahi bin Ibadhi waliyaweka yote hayo yaliyotokeza katika yale waliyokuwa nayo katika Elimu iliyotangulia kuwa kwao, basi wakakuta kuwa Haki inayokubaliana na hayo waliyokuwa nayo katika Haki ni yale aliyoyasema Abdullahi bin Ibadhi, basi walinasibishwa wao kwake yeye huyo, na sio kwa kuchukuwa Sheria kwake yeye huyo)) Rj: [Jamil bin Khamis Qaamus sharia shar-i. Jz 7 uk.311]

Basi sisi katika sehemu hii tutakuwa tunatoa taarifu za Maimamu wa Elimu biidhinillahi taalaa, na kuwaelezea Salafu wetu wema waliotutangulia.

Asante sana.

"Nakuusia kumcha Allah Mola Mkuu ambaye anayajua kwako usiyoyajua katika nafsi yako, na ambaye anayaona yaliyofichwa na dhamiri yako na kufanyiwa khiyana na macho yako na unayoyadhihirisha na unayoyaficha katika nafsi yako, na yeye yuko karibu yako kuliko mshipa wa shingo yako, basi muangalie Mola huyu ambaye yuko na wewe kwa daraja hiyo na uwe mwenye kumuogopa zaidi na mwenye kumcha yeye zaidi kuliko chengine chochote, na ujue kuwa wewe utakapomtii yeye utakua pamoja na (maridhio) yake katika nyumba yake pamoja na Manabii na Wasadikishaji na Mashahidi na ubora ulioje kuwa pamoja na hao, na ikiwa wewe utamuasi yeye basi atakuingiza motoni ambao muwako wake ni kwa watu na mawe"