Ibadhi.com

MAKALA ZETU

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Shukurani zote ni kwa Allah mtukufu, na rehma na amani ziwe kwa kipenzi chetu Mtume wa Allah Muhammad pamoja na wafuasi wake na masahaba wake mpaka siku ya malipo.

Asalamu alaykum wa rahmatullahi wa barakatuh.

Kwa hakika mvutano baina na haki na batili ndio hali inayowafikia waja katika ulimwengu huu, na katika kila zama na mitihani yake, na katika hayo ndio linapatikana lengo la uwepo wetu katika ulimwengu huu, amesema Allah mtukufu:

كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ ۗ وَنَبْلُوكُم بِالشَّرِّ وَالْخَيْرِ فِتْنَةً ۖ وَإِلَيْنَا تُرْجَعُونَ

((Kila nafsi itaonja mauti, na tunakujaribuni kwa shari na kheri kuwatahini, na kwetu sisi munarejeshwa.)) [Al-Anbiyaa 35].

Dini ya Uislamu imetimia tokea miaka 1429 iliyopita kama ilivoeleza Qurani tukufu, miaka yote hiyo Waislamu walifanyia kazi mafundisho yake, yako ambayo walikubaliana ndani yake na yako waliyotafautiana ndani yake, yaliyoingiwa na tafauti yalisababisha kupatikana madhehebu tafauti ili kudhibiti misimamo ya kila upande na wahusika wake katika kila zama, ni sawa katika Itikadi au Fiqhi au Siasa, na mapote yalizuka, ni hali isiyoweza kupingika wala kukatalika, na kila wahusika wa madhehebu walitokeza ndani yake wanavyuoni na watetezi, kwa mwenye kusoma kitabu cha Allah mtukufu anajua kuwa hiyo si hali ngeni; kwani imeelezwa kuwafikia waliopita kabla yetu.

Si tatizo kutafautiana, bali tatizo sugu ni kufanyiana uadui kwa sababu ya tafauti, kwa hiyo ni wajibu wa kila Muislamu kuheshimu tafauti iliyotokeza na inayotokeza na itayotokeza, kama ilivokua ni wajibu wa kila Muislamu kujiepusha na njia ya ubabe na uadui dhidi ya waliotafautiana naye kimadhehebu, na iwapo atajikuta kuwemo katika safu za fikra za kufanyia ubabe na uadui wengine kwa sababu ya kutafautiana kimadhehebu basi ajijue kuwa amekumbwa na maradhi mabaya yaliyoelezwa katika Quraani kuwapata waliopita kabla yetu, haraka sana airejee nafsi yake na ajue kuwa hapo alipo sipo; kwani yupo katika batili, kwa haya upendo utaenea, na jamii itaimarika, na umoja utapatikana, kwani mshikamano katika yenye makubaliano utaweza kuimarika, na heshima katika yaliyoingiwa na tafauti itaweza kupatikana, na kila wenye msimamo wataweza kueleza dalili zao katika jamii. Umoja kwamwe hauji kwa kulazimishana na kutetea wingi, kwani hakuna haki ya kuificha haki, na haki ni kwa dalili si kwa wingi.

Ibadhi kwa upande wetu ni tunda ya kujishika na haki kwa dalili katika kila lenye tafauti ndani yake, tunasema kwa wote: "Leteni dalili zenu ikiwa nyinyi ni wakweli mumepatia haki" tunajiongoza kwa Kitabu cha Allah na Sunna ya Mtume S.A.W. na yenye makubaliano ndani yake, hii ndiyo hali yetu tokea hapo mwanzo mpaka hivi leo.

Leo hii limekuja suala la funga ya siku ya arafa.

Jee! Kufunga siku ya arafa ni kwa kisimamo cha Mahujaji katika sehemu ya Arafa, au kwa Muandamo wa mwezi wa Dhul-Hijja (Mfunguo tatu)?

Kwa kweli inafahamika vizuri sana kuwa karne zote zilizopita Waislamu hawakua wakiijua siku ya arafa isipokua kwa kupitia muandamo wa mwezi wa Hija, na kuwa watu wa miji yote, kila mji waliijua siku hiyo ya arafa kupitia muandamo wa majira yao, na wanavyuoni wote waliijua siku ya kufunga arafah kuwa ni siku ya tisa ya mwezi wa Hijja (mfunguo tatu), kwa ufupi makubaliano ya wote ni kuwa siku ya arafa ni siku ya tisa ya mwezi wa Dhul-Hijja (mfunguo tatu), na kuwa siku hii ina ibada zinayoihusu, nazo ni mbili:

1. Ibada iliyofungamana na sehemu maalumu.

2. Ibada isiyofungamana na sehemu maalumu.

Zote ni ibada za siku ya arafa ambayo ni siku ya tisa ya mwezi wa Dhul-hijja.

Ama ibada iliyofungamana na sehemu maalumu hiyo ni ibada ya kusimama katika sehemu inayoitwa arafa iliyoko katika mji mtakatifu wa Makka, na ibada hii inawahusu Mahujaji peke yao nayo ni nguzo mama ya ibada ya Hijja.

Ama ibada isiyojifunga na sehemu maalumu hiyo ibada ni kufunga siku hii ya tisa ya mwezi wa Dhul-hijja nayo ndiyo inayojulikana kuwa ndiyo siku ya afara.

Kwa hiyo ni haki kuwa kila muislamu ajishike na majira ya mji wake katika kutekeleza ibada hii ya funga ya arafa kama vile anavyoanza mchana wake kwa aljfajiri ya mji wake na kumaliza kwa kuchwa jua katika magharibi ya mji wake basi vile vile afunge siku ya tisa kwa mujibu wa muandamo wa mji wake; kwa sababu hayo ndiyo majira aliyofungwa nayo katika ibada zake zote za wakati, kwa hakika sehemu iitwayo arafa ina majira yake nayo haindoki mpaka dunia itamalizika, kwa hiyo uhakika ni kuwa ibada ya siku ya arafa ni ya wakati wa majira ya sehemu ya mji husika na si kwa ibada ya Mahujaji mbayo pia imefungwa kwa majira ya mji wanaotekeleza ibada hiyo ndani yake, vipi Muislamu anakubali kuondoshwa katika asili na sababu ya ibada na kufungwa na jambo jengine?

Leo hii wamezuka watu na jambo jipya na geni, kwa hakika halikuwepo kwa miaka zaidi ya elfu moja iliyopita, watu hao hao utawasikia wakisema: Jichungeni sana na mambo mapya mapya, kwani kila jipya ni bidaa, na kila bidaa ni upotevu, na kila upotevu ni motoni".

Tunawambia: Ni yakini isiyokua na shaka yoyote kuwa Dini ya Uislamu imetimia tokea zama za Mtume S.A.W. na kuwa waislamu kwa miaka zaidi ya 1400 hawajui chengine katika ibada hizi isipokua kujifunga na tarehe ya muandamo kwa mujibu wa nyakati za majira yao tu, kama ilivokua hawasali wala hawafungi kwa mjira ya mji mtakatifu wa makka, basi vipi watafunga kwa ibada ya watu wa mji huo? Hakika ibada za walioko Makka zote zimefungwa kwa mujibu wa majira ya mji huo, kama ilivokua ibada zetu zote zimefungwa kwa majira ya miji yetu.

Mumepata wapi nyinyi sababu hiyo munayoidai hivi leo?

Vipi nyinyi leo munafanya kila pupa la kuwaondosha watu katika njia ya wema waliopita katika kila madhehebu na kuzua jambo jipya?

Ewe Allah hakika sisi tumeshabainisha.

Tunawatakia Waislamu wote siku kuu njema ya kheri na barka.

Amin.

 

NIDHAMU YA AZZABA

Nidhamu ya Azzaba ni badala ya nidhamu ya uimamu wa kiibadhi ambao husimamia uadilifu, Nidhamu ya Azzaba ndio huwakilisha dola hiyo ikisimamiwa na viongozi mahodari katika jamii husika kwa elimu na wema, na neon Azzaba katika lugha ya kiarabu limetokana na neon “Aazib” ambalo linatumika kwa aliyejiweka mbali na kitu, kama ambavyo linatumika kwa maana ya kutokuwepo.
Anasema mwanachuoni Aldarjeini: (( Azzaaba ni wingi, akiwa mmoja anaitwa Azzaabiy, neno hili linatumika kama alama ya kila aliyejilazimisha njia ya wema, kutafuta elimu, na kufuata njia ya watu wa kheri, akazihifadhi na kuzifanyia kazi, mambo yote hayo yakipatikana ndio huitwa mwenye kuwa nayo ataitwa Azzabiyy”
Hapana shaka umejua - ewe mwanafunzi wa ilmu – kuwa nidhamu ya uimam kwa maibadhi imesimama kwa mashauriano (Shura) sawa ikiwa wakati wa Difai au Dhuhuur, na Azzaba inasimama kwa Mashauriano (Shura) wakati wa Kitman na Sharai ( Kujitoa Muhanga).
Ametaja Sheikh Muhammed Atfeish kuwa : “Kuwepo kwa Azzaba ni la Lazima, kwa sababu kuamrisha mema na kukataza mabaya kunalazimika kwa kuwepo kwake” na wamekubaliana kuwa itakuwa ni lazima kama wanaliweza, na hilo limetolewa katika Qur an na Sunnah.
Jua ewe ndugu yangu – Allah mtukufu akuzidishie fahamu- kuwa kila nidhamu ya utawala ina namna yake ya kutawala, kwa hivyo hapana budi kuwepo misingi na mipango, kwa ajili hii Azzaba inatengenezeka baina ya wajumbe kumi (10) mpaka kumi na sita (16) kwa mujibu ukubwa wa mji huo, na hao wajumbe ni katika wachamungu, wema, mwenye elimu, na muaminfu. Watachagua baina yao Sheikh wa Azzaba ambaye ni mjuzi wao, na mwenye uwezo zaidi wa kusimamia, atahesabiwa kuwa ndiyo marejeo yao, msemaji wao, na amri yake inatekelezwa. Makao makuu ya Azzaba yatakuwa katika pembe miongoni mwa pembe za Msikiti, na haiwajuzii kujadili jambo lolote nje ya makao makuu yake rasmi.


Kwa kuwa Nidhamu hii ndiyo yenye jukumu la kusimamia mambo ya mji ule, kwa hivyo watakuwa na majukumu yatakayogawanywa kwa wajumbe wake, kama ifuatavyo:
1. SHEIKH WA AZZAABA: Mjuzi zaidi wa mji ule, anasifika kuwa na Shakhsiya kubwa, atasimamia Kutoa mawaidha, kufikisha matangazo ya Azzaaba kwa watu wote, naye ana amri kama ya mtawala muadilifu, na atabakia katika cheo chake maisha yake yote.
2. WASHAURI: Idadi yao ni wanne, watakuwa na Sheikh Daima katika vikao vyake, hatoamua jambo ispokuwa kwa kukubali kwao.
3. IMAMU: Mtu mmoja, amekalifishwa kuwasalisha watu kwa Jamaa, na Inajuzu kuwa ni mmoja wa washauri.
4. MSOMA ADHANA: mtu muaminifu, mchamungu, mwenye kujua nyakati.
5. WASIMAMIZI WA WAKFU: watachaguliwa wajumbe wawili, wenye hali ya katikati, sio matajiri wala mafaqiri, ili wasimamie na kuendeleza waqfu, wadhibiti vyenye kuingia na vyenye kutoka, na Bajeti ya Azzaba.
6. WALIMU: watachaguliwa wajumbe watatu au zaidi ya watatu kwa mujibu wa mahitaji ili wasimamie kuweka mpango wa Malezi na mafunzo na kuwasimamia wanafunzi.
7. HALI ZA MAITI: watachaguliwa wajumbe wanne au watano kwa ajili ya kusimamia haki za maiti na yote yahusuyo kuzika, kutekeleza wasiya na kugawa urithi.


 Khamis Yahya Khamis Alghammaw

07. NURU ING'AAYO-AZZAABA

Kila sifa njema ni za Allah mtukufu, mola wa walimwengu wote, Sala bora na salam tukufu ziwe juu ya mbora wa viumbe, Amma baad…Kwa hakika kuna pande tofauti zenye kuvutana na kugongana katika ulimwengu, ikiwemo kheri na shari, tangu kuumbwa kwa viumbe mpaka leo, basi inapoenea shari, ikawa kubwa hatari yake, Kheri hutokeza kutoka katika maficho yake, ili anga ijae nuru yenye kung’aa, na kama utafuatilia historia utaona kuwa kheri na shari daima zimo katika kuvutana, baada ya zama za Mtume –Sallallahu alayhi wasallam- na makhalifa wake waongofu fitna ilianza kudhihiri katika umma wa kiislamu hata ilikaribia nguzo zake kuporomoka kutokana na kuliwa sana na fitna hiyo, Lakini Allah mtukufu hakubali ispokuwa kuitimiza nuru yake, basi huwaleta waja wake waumini ili wahifadhi usalama wa jamii hiyo.

Ukiwaona wanachuoni wa dunia na matamanio wanaegemea katika safu za viongozi madhalimu na wakiwanyenyekea, jua huo ndio mwanzo wa kutoka katika njia sahihi, hapo wanachuoni wachamungu, wenye ikhlasi, husimama kushindana na fikra hizi zilizopotoka,  zinazowajia kwa sura tofauti. Hutetea uislamu kwa azma na kuendelea ili ubakie katika usafi wake katika hukmu zake za kisiasa na kidini, na huendelea kufundisha tabia na kuzilea nafsi zisiambukizwe maradhi mengine.Hivyo Natarajia kutoka kwako ndugu yangu – msomaji mpenzi- usome mistari hii kwa akili iliyofunguka, isiyo na ubishi au ususuavu wa namna yoyote, ili haki ipenye katika moyo wako bila kuzuiliwa na Kufuli  za matamanio.

Jua –ewe mwenye kutaka matukufu- kuwa tangu dola dhalimu ya kishia ya Faatimiyya iimalize dola adilifu ya kiibadhi ya Rustumiyya, basi njia ilibadilika vibaya sana kuelekea dhulma, matumizi ya nguvu, na uovu. Na Maibadhi walikuwa wanaona kuwa dola hii haisimamishi sharia ya Allah mtukufu wala haiifanyii kazi..baada ya kuzima moto wao wa jitihada ya kusimamisha dola adilifu, wanachuoni wa kiibadhi walifikiri njia ya kuweka nidhamu watakayopitia ili kuhifadhi hukmu za Allah mtukufu katika maeneo yao, na wapate kuupeleka ummah katika mwenendo sahihi pasina kutaka kusimamisha dola mpya au kushikana na dola dhalimu isiyotaka shura.

Waliweka nidhamu inayoendana na marhala ya SIRI ((kitman)), Nidhamu ya kimalezi inayohifadhi umoja wao, inayohifadhi madhehebu yao isije kumalizika, na ili ibaki madhehebu yao imesimama imara dhidi ya majaribio ya kuifanyia uadui.

Kwa ajili hiyo Maibadhi waliacha kufikiria mambo ya dola na wakaanza kuifikiria jamii mpaka alipokuja Mwanachuoni hodari Mvumbuzi Abu Abdillahi bin Bakri Alfurstai ambaye aliweka pembeni kufikiria mambo ya dola na kuanzisha nidhamu nyingine badala ya dola adilifu, ikakua fikra hiyo na kuwa NIDHAMU YA AZZAABA, akaiwekea nidhamu hiyo misingi na kanuni, na akawaita watu  katika nidhamu hiyo.

Ninavyodhani… utakuwa una maswali mengi unajiuliza . Ngoja nishirikiane nawe katika baadhi ya maswali hayo ili tufikie majibu yanayotakiwa: Ni nini nidhamu ya Azzaaba ? Ni zipi sharti zake?

Je ina cheo gani katika dola yenye kuhukumu? Ni ipi kazi yake ?Je ni kweli ilikuwa ni badala ya dola adilifu ?

Njoo nami katika njia hii kwa roho ya uchangamfu ili tupambanue mwenendo huu.

By Khamis Yahya Khamis Alghammawi


UIMAMU WA KUJITETEA –DIFAAI


MJUKUU: Ajabu iliyoje!, Ajabu iliyoje!,  ((Na katika watu yupo ambaye huiuza nafsi yake kwa kutaka radhi za Allah mtukufu; na Allah mtukufu ni Mpole kwa waja wake.)) Baqarah:207, Zimebakia aina mbili za Uimam, nina hamu sana ya kuzijua, niambie yanayohusiana na aina hizo ewe babu yangu.
BABU: Kwa hivyo unafuatilia vizuri ewe mjukuu wangu, basi endelea kujitahidi… Allah mtukufu akubariki.
Aina ya tatu: Ni Uimam wa Difai – Kujiitetea-, “Kikawaida Uimam huu hutokea baina ya Uimam wa siri na dhahiri, wanapokuwa maibadhi wapo katika uimam wa siri na wakakvamiwa na maadui hapo hutangaza hali ya kujitetea, na kujitetea ni katika mambo ya lazima kwa Maibadhi unapokosekana Uimam wa Dhahiri, watamchagua mmoja katika masheikh wao, mjuzi wa mambo ya vita, maarufu kwa ushujaa, ili awaongoze katika mapigano dhidi ya maadui, watamwita Imam wa Difai, mapigano yakimalizika na uimam wake utakuwa umemalizika”
MJUKUU: Hakika mimi nashangazwa na hikma iliyojaa katika fikra ya kisiasa ya Maibadhi, njia yao hii iliwezesha kubaki kwao karne nyingi.
BABU: Usifanye haraka ewe mjukuu wangu, imebakia aina ya mwisho ya uimamu nayo ndiyo aina muhimu zaidi, bali hilo ndio lengo wanaloliendea maibadhi zama zote za historia yao, nao ni UIMAM WA DHUHUR – Dhahiri – “ Maibadhi wanapofikia idadi yao nusu ya maadui kinguvu, mali na elimu, au muda wowote watakaoweza kumshinda adui yao  na kuwa juu yao, itakuwa imewawajibikia kusimamisha Uimamu wa dhahiri na kumchagua Imamu muadilifu, na kama hawakufanya watakuwa kama walioua dini ya Allah mtukufu, na wao Maibadhi  bila shaka wako mbali  na kuiua Itikadi ya kiislamu, ambayo wamepambana muda mrefu, na wamepigana katika njia ya kuihifadhi ibaki safi na iliyosalimika, kwa mujibu wa mafundisho ya Qur-an tukufu na Sunnah sahihi ya Mtume –Sallallahu alayhi wasallam-.
MJUKUU: Nizidishie ewe babu yangu, bado nina hamu ya kusikia mengi kuhusu fikra ya kisiasa kwa Maibadhi.
BABU: Haya yanakutosha ewe mwanangu, leo mazungumzo yamerefuka, kama unataka ziyada rejea katika maktaba ya kiibadhi, usome vitabu vifuatavyo:
1.    Alwuheibi, Musallam bin Salim: Alfikr al-aqadiyy indal ibadhiyyah hattaa nihaayatil qarni thanil hijry, chapa ya mwanzo, Maktabat Dhaamiri, Siib, 1427h/2006.
2.    Taalib, Mahdiyyu Haashim: Alharakatul Ibaadhiyyah fil Mashriqil Arabiyyi, chapa ya pili, Daarul hikmat, London 2003m.
3.    Muammar, Ally bin Yahya: Al-ibadhiyyah bainal firaqil Islaamiyyah inda kuttaabil maqaalaat fil qadiimi walhadiithi, jz 2, wizaaratu turaathil qawmiy wathaqaafah, Usultan wa Oman, 1406h/1986m.

Ndio nini “Azzaaba” ….. Njoo pamoja name makala ifuatayo:


By: Khamis Yahya Khamis Alghammawi Abu Muslim

UIMAM WA SHARAA (KUMUUZIA NAFSI ALLAH MTUKUFU)


MJUKUU: Ewe babu yangu hakika hii ni dalili ya usawa wa fikra ya kisiasa kwa Maibadhi; kwa kuwa wanazingatia hali inayowazunguka na hujiweka kwa namna itakavyowawezesha kueneza daawa yao na kuipa nguvu katika nafsi, ili waweze baada ya hayo kufikia marhala nyingine ya Dhuhuur.
BABU: Ahsante ewe mwanangu, mambo ni kama ulivyotaja, lakini ipo namna nyingine ya Uimam kabla ya kufikia marhala ya Dhuhuur nayo ni marhala ya “Uimam wa Sharaa”; uimam ambao kikawaida husimamishwa wakati wa kitmaan, pale ambapo baadhi ya wapiganaji, wanaume, waliobaleghe, wasiopungua arobaini huchagua kumuuzia Allah mtukufu  nafsi zao, basi wao hutoka dhidi ya hukmu za madhalimu, lakini wao huwa hawamlazimishi yoyote kujiunga nao, wajibu wao ni kutowatisha watu katika waislamu, wala wasiwapige vita mpaka wao wawapige vita. Hili ni jambo la kujitolea hakuna kulazimishwa na yoyote. Na wakichagua njia hii baadhi ya Maibadhi basi watachagua baina yao Imam, ataitwa “IMAAM SHURAA”, utawala wake utakuwa juu ya kundi hilo tu maadam wapo katika marhala hii, atawaongoza katika vita na kuyapanga mambo yao, watampa kiapo cha utiifu cha kupigana jihad na maadui kwa kutetea nafsi  na dini mpaka mauti au kupata ushindi. Na namna ya kuweka kiapo cha utiifu ni kama ifuatavyo:


Atatangulizwa mtu aliyechaguliwa kuwa Imam, hupewa mkono wa kulia kisha anaambiwa: “Hakika sisi tumekutanguliza uwe Imam juu ya nafsi zetu na waislamu, uhukumu kwa kitabu cha Allah mtukufu na Mtume wake –sallallahu alayh wasallam- utaamrisha mema, utakataza mabaya,  utaidhihirisha dini ya Allah mtukufu ambayo amewalazimisha waja wake kumuabudu, na utalingania katika dini na jihaad kwa kadri utakavyopata njia” Akisema: “Ndio” basi inakuwa kiapo chake kimewajibika, hapo atasimama mmoja mmoja katika kundi hilo nao watampa kiapo cha utiifu. Kisha Khatibu atatoa khutba baada ya hapo juu ya usahihi wa kiapo cha utiifu na kufungika kwake kisha atasema “ Hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki ispokuwa Allah mtukufu, hakuna hukmu ispokuwa ya Allah mtukufu, na hakuna hukmu kwa anayehukumu tofauti na alivyoteremsha Allaah mtukufu, na hakuna utiifu kwa mwenye kumuasi Allah mtukufu, Hakuna hukmu ispokuwa ya Allah mtukufu, kuuzuliwa na kufarikiana na maadui wa Allah mtukufu”


MJUKUU: kwa kuthibiti itikadi yao katika nafsi zao imekuwa rahisi kuzitoa muhanga nafsi zao katika njia ya Allah mtukufu kwa kuinusuru dini ya Allah mtukufu na kuisimamisha sharia yake.
BABU: Umesema kweli ewe mwanangu, Itikadi ikithibiti inakuwa rahisi kutoa muhanga kila kitu, kuzitoa nafsi katika njia ya Allah mtukufu ni moja ya muhanga mkubwa walioutoa maibadhi katika njia ya Allah mtukufu, na katika masharti ya Sharaa ni:
1.    “Haijuzu kwa Mashuraati – waliouza nafsi zao katika njia ya Allah mtukufu – kutumia Taqiyya ya kidini, vyovyote itakavyokuwa hali na matatizo, na kwa sababu yoyote itakayokuwa”
2.    “Haijuzu kwa atakayechagua njia hii kurudi nyumbani kwake ispokuwa kama kuna shida kubwa, na kukaa kwake kutabakia kwa muda, na katika hali hii yeye atazingatiwa ni mgeni pale na itamuwajibikia kusali kupunguza sala kama msafiri”
3.    “Haijuzu kwa watakaochagua njia hii kurudi nyuma na kuacha ispokuwa kama watakapofanikiwa kumshinda adui yao”
Je kuna masharti mengine, au kuna marhala nyingine…. Tukutane makala ijayo


By: Khamis Yahya Khamis Alghammawi (Abu Muslim)

Anasema الله ﷻ katika Qur-an;

{يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِنْ قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ}

Enyi mlio amini! Mmeandikiwa Saumu, kama waliyo andikiwa walio kuwa kabla yenu ili mpate kuchamngu.

-Sura Al-Baqarah, Ayah 183

MIONGONI MWA MAMBO MUHIMU YA KUYAFANYA NDANI YA MWEZI HUU AMBAO BADO TUPO KATIKA MADIKU YA AWALI KABISA NI PAMOJA NA.

KUWAKUMBUKA MAFUKARA, MASIKINI,WAJANE NA MAYATIMA.

Huenda wewe ukawa ni miongoni mwa watu ambao wametumia mali zao muda mrefu sana katika mambo ya maasi na pia ya upuuzi kitu ambacho bila shaka ni khasara kubwa kupoteza na kutumia mali katika maasi,  Sasa basi hii ni nafasi ya kipekee ya wewe kwanza kutubia juu ya hayo lakini pia kuwatazama wenye kustahiki kuwasaidia ambao ni pamoja na;

Masikini.
Mafakiri.
Wajane.
Mayatima.

Amali hii ni amali nzuri tena iiiyo bora kabisa khususan ndani ya mwezi huu wenye malipo makubwa mara dufu zaidi na zaidi.

Sifa ya kuwalisha na kuwasaidia hawa wenye kuhitaji ni miongoni mwa sifa za waja wa Allah waliyo wema kabisa.

Anasema الله ﷻ katika Qur-an;

{وَيُطْعِمُونَ الطَّعَامَ عَلَىٰ حُبِّهِ مِسْكِينًا وَيَتِيمًا وَأَسِيرًا ﴿٨﴾ إِنَّمَا نُطْعِمُكُمْ لِوَجْهِ اللَّـهِ لَا نُرِيدُ مِنكُمْ جَزَاءً وَلَا شُكُورًا ﴿٩﴾ إِنَّا نَخَافُ مِن رَّبِّنَا يَوْمًا عَبُوسًا قَمْطَرِيرًا ﴿١٠﴾}  

Na wanalisha chakula juu ya mapenzi yao (kwa hicho wanacholisha) masikini na mayatima na mateka. “Hakika sisi tunakulisheni kwa (ajili ya) Wajihi wa Allaah, hatutaki kwenu jazaa na wala shukurani. “Hakika sisi tunakhofu kwa Mola wetu siku inayokunjisha uso ngumu nzito

[Al-Insaan: 8-10]

NI VIZURI TUKUMBUKE KWAMBA: MIONGONI MWA HEKIMA PIA ZA KUFARADHISWA IBADA HII YA FUNGA ILI TUWEZE KUWAKUMBUKA WATU AMBAO HUPATA TABU NA DHIKI KUTOKANA NA NJAA WANAYO IPATA KWA KUKOSA CHAKULA,  BASI TUWAJALI NA KUWASAIDIA ILI TUPATE RADHI ZAKE ALLAH MTUKUFU.

Anasema الله ﷻ katika Qur-an;

{شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنْزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ فَمَنْ شَهِدَ مِنْكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ ۖ وَمَنْ كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۗ يُرِيدُ اللَّهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ وَلِتُكْمِلُوا الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُوا اللَّهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ}

Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur'ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi. Basi ataye kuwa mjini katika mwezi huu naafunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushukuru.

-Sura Al-Baqarah, Ayah 185

VIPI TUIPOKEE RAMADHANI?

*Kwanza kabisa hapana budi hadi sasa tumshukuru Allah kutuchagua kua hai tena wazima wa afya miongoni mwa aliyo wachagua na tumuombe aendelee kutupa uzima na siha hadi tutekeleze ibada ya funga na ibada zinginezo.

Nasema hayo kwa sababu naamini wapo ambao tulikua nao Ramadhani aliyopita miongoni mwa Baba zetu, Mama zetu, Dada zetu,  Kaka zetu na ndugu na jamaa wa karibu na leo hatupo nao tena, kifo kimewaondosha katika hii dunia na tumebakia sisi tukiwa hai tena wenye afya.

Haya ni mazingatio na mawaidha kwetu tuliyobakia hai,  tukae tukifahamu kwamba: hatuna dhamana na mauti,  kwani kifo hakina taarifa na hakijalishi nguvu za mtu,  cheo chake afya yake na hata mali zake na umasikini wake,  pia si uzee wala ujana wake,  bali kifo kipo kama ilivyokuja ndani ya qur an tukufu.

Anasema الله ﷻ katika Qur-an;

{وَمَا كَانَ لِنَفْسٍ أَنْ تَمُوتَ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّهِ كِتَابًا مُؤَجَّلًا ۗ وَمَنْ يُرِدْ ثَوَابَ الدُّنْيَا نُؤْتِهِ مِنْهَا وَمَنْ يُرِدْ ثَوَابَ الْآخِرَةِ نُؤْتِهِ مِنْهَا ۚ وَسَنَجْزِي الشَّاكِرِينَ}

Na haiwezi nafsi kuwa ife ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu kama ilivyo andikwa ajali yake. Na mwenye kutaka malipo ya duniani tutampa; na mwenye kutaka malipo ya Akhera tutampa. Na tutawalipa wenye kushukuru.

-Sura Aal-E-Imran, Ayah 145

Basi kila mwenye akili na azingatiye na muda woote afanye juhudi katika ibada na azidishe zaidi na zaidi, wala isitokee mtu kufanya uvivu akitarajia kuja kufanya amali njema ramadhani ijayo,  kwani unaposali kipindi kimoja waambiwa uswali kama sala ya kuaga sala ambayo hadhanii mwenyekusali kama atakutananayo tena siku ingine,  sasa hali hii ya kipindo kimoja kwenda kingine,  vipi wewe ujipe matumaini ya kua hai mwaka mzima wakati wafahamu kua,  ulikua na jamaa zako maiti yamewafika ghafla tu na haupo nao tena duniani? Pia yafahamika kwamba: hakuna hata mmoja ambae amefunga ahadi na Allah mtukufu ya kujua siku yake ya kufa.

Pia tukumbuke kuwaombea wagonjwa waliyo sehemu mbalimbali huenda kwa dua zetu Allah akawapa shifaa nao wakatekeleza ibada ya funga pamoja nasi,  sisi pia tumuombe Allah aendelee kutupa siha na uzima ili tufikiwe na Mwezi wa Ramadhani tukiwa kamilifu na wenye uwezo wa kuhimili funga na ibada mbalimbali.

Anasema الله ﷻ katika Qur-an;

{يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّهَ حَقَّ تُقَاتِهِ وَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنْتُمْ مُسْلِمُونَ}

Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu kama ipasavyo kumcha; wala msife ila nanyi ni Waislamu.

-Sura Aal-E-Imran, Ayah 102

VIPI TUIPOKEE RAMADHANI?
Ikiwa ni siku chache mno zimebakia kuelekea katika mwezi mtukufu, mwezi wa rehma, mwezi wa maghfira na mwezi wa kuachwa mbali na moto wa Jahannama, mwezi mtukufu wa RAMADHANI ni vyema muislamu aingie katika mwezi huu mtukufu akiwa amekwisha elewa na amefanya maandalizi, huku akijua nini anatakiwa akifanye ili kujivunia zawadi ya TAQWA aliyoiahidi Allah mtukufu ndani ya kitabu chake kitukufu (QURAN).*

*Utukufu wa mwezi huu na utukufu wa ibada iliyofungamana na mwezi huu, Bwana Mtume (SAW) anasema:


عنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ:
"كُلُّ عَمَلِ ابْنِ آدَمَ يُضَاعَفُ الْحَسَنَةُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا إِلَى سَبْعمِائَة ضِعْفٍ قَالَ اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ إِلَّا الصَّوْمَ فَإِنَّهُ لِي وَأَنَا أَجْزِي بِهِ يَدَعُ شَهْوَتَهُ وَطَعَامَهُ مِنْ أَجْلِي لِلصَّائِمِ فَرْحَتَانِ فَرْحَةٌ عِنْدَ فِطْرِهِ وَفَرْحَةٌ عِنْدَ لِقَاءِ رَبِّهِ وَلَخُلُوفُ فِيهِ أَطْيَبُ عِنْدَ اللَّهِ مِنْ رِيحِ الْمِسْكِ"
(مسلم)

Imepokewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu): amesema,

Amesema mjumbe wa Mwenyezi Mungu (ﷺ) ((Kila amali njema ya mwanaadamu inalipwa mara kumi na inaongezewa thawabu kutoka kumi hadi mia saba, na Allaah mtukufu Anasema: Isipokuwa Swawm, kwani hiyo ni kwa ajili Yangu na Mimi Ndiye Nitakayemlipa.  Ameacha matamanio yake na chakula chake kwa ajili Yangu. Kwa aliyefunga swawm atapata furaha mbili; furaha anapofuturu na furaha atakapoonana na Mola wake, harufu inayotoka kinywani mwa aliyefunga ni nzuri mbele ya Allaah kuliko harufu ya misk))

BAADHI YA MAMBO MUHIMU YA KUFANYA.

Panapo uhai tukifikiwa na mwezi huo tukiwa wazima wenye Afya njema,  basi tuupokee mwezi huo kwa kusoma sana Qur an,  kwa kufanya dhikri kwa wingi,  kusimama qiyamu za usiku kwa ajili ya ibada za usiku, tutowe sadaka kwa wingi kwa ajili ya masikini, mayatima na hata mafaqiri na wajane, kwani ni mwezi ambao malipo ya mja ndani ya mwezi huo hua maradufu zaidi na zaidi. Basi juu ya hayo.

Anasema الله ﷻ katika Qur-an;

{وَفِي ذَٰلِكَ فَلْيَتَنَافَسِ الْمُتَنَافِسُونَ}

Na katika hayo washindanie wenye kushindana.

-Sura Al-Mutaffifin, Ayah 26

*Watu wengi huonekana kushindana kwa ajili ya dunia na sio kwa ajili ya akhera.  Mfano leo mtu akinunua gari,  basi mungine atafanya juu chini anunuwe gari la kifahari zaidi kuliko mwenzake,  mtu akijenga nyumba,  basi mungine atataka kujenga jumba la kifakhari zaidi kuliko mwezake,  wakati haya yoote si chochote wala si lolote.*

Anasema الله ﷻ katika Qur-an;

{اعْلَمُوا أَنَّمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا لَعِبٌ وَلَهْوٌ وَزِينَةٌ وَتَفَاخُرٌ بَيْنَكُمْ وَتَكَاثُرٌ فِي الْأَمْوَالِ وَالْأَوْلَادِ ۖ كَمَثَلِ غَيْثٍ أَعْجَبَ الْكُفَّارَ نَبَاتُهُ ثُمَّ يَهِيجُ فَتَرَاهُ مُصْفَرًّا ثُمَّ يَكُونُ حُطَامًا ۖ وَفِي الْآخِرَةِ عَذَابٌ شَدِيدٌ وَمَغْفِرَةٌ مِنَ اللَّهِ وَرِضْوَانٌ ۚ وَمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا إِلَّا مَتَاعُ الْغُرُورِ}

Jueni ya kwamba maisha ya dunia ni mchezo, na pumbao, na pambo, na kujifakhirisha baina yenu na kushindana kwa wingi wa mali na watoto. Mfano wake ni kama mvua ambayo huwafurahisha wakulima mimea yake, kisha hunyauka ukayaona yamepiga manjano kisha yakawa mabua. Na akhera kuna adhabu kali na maghfira kutoka kwa Mwenyezi Mungu na radhi. Na maisha ya dunia si chochote ila ni starehe ya udanganyifu.

-Sura Al-Hadid, Ayah 20

Anasema الله ﷻ katika Qur-an;

{شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنْزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ فَمَنْ شَهِدَ مِنْكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ ۖ وَمَنْ كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۗ يُرِيدُ اللَّهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ وَلِتُكْمِلُوا الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُوا اللَّهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ}

Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur'ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi. Basi ataye kuwa katika mji katika mwezi huu na afunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushukuru.

-Sura Al-Baqarah, Ayah 185

*NAAM NDUGU WAPENDWA KATIKA IMANI,  TUNAENDELEA KUELEZEA MAMBO MUHIMU MIONGONI MWA MAMBO AMBAYO TUNA PASWA KUYASHIKA KATIKA MWEZI HUU WA RAMADHANI,  MWEZI ULIYOBARIKIWA,  KATIKA MAMBO MUHIMU NI PAMOJA NA.

4 - QIYAAMUL-LAYL (KISIMAMO CHA  USIKU)

Bila shaka visimamo katika sala za usiku zinafaida nyingi sana,  hasa ukizingatia mtu ambae atasimama ndani ya mwezi ambao fadhila na malipo yake huwa makubwa zaidi.

Visimamo katika sala za usiku humkurubisha zaidi mja kwa Mola wake mlezi, pia humuweka kua katika daraja la waja wema wa Allah ambao amewaelezea ndani ya Qur an tukufu.

Anasema الله ﷻ katika Qur-an;

{وَالَّذِينَ يَبِيتُونَ لِرَبِّهِمْ سُجَّدًا وَقِيَامًا}

Na wale wanao kesha kwa ajili ya Mola wao Mlezi kwa kusujudu na kusimama.

-Sura Al-Furqan, Ayah 64

Lakini pamoja na hayo yoote;

Mtume (ﷺ) anasema:

(من قام رمضان إيماناً واحتساباً، غفر له ما تقدم من ذنبه)
أخرجه البخاري ومسلم

Atakayesimama [kwa Swalah ya usiku] kwa iymaan na kutaraji malipo, ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)

Basi tusiwe wavivu juu ya kusimama katika sala za usiku,  wala tusipumbazwe na michezo mbalimbali katina simu, TV zetu, maana zama hizi wapo watu kazi yao ni kushinda au kukesha katika mitandao wakifuatilia tamthilia na mambo ya kipuuzi yasiyo na faida tena yenye khasara.

Kwa hakika huko ni kupoteza muda na wakati kiasi ambacho tutakuja jua thamani ya wakati katika kipindi ambacho kujua kwetu hakutokua na faida kabisa bali tutabakia na majuto yasiyo na manufaa.

TUKITHIRISHE SANA KUSIMAMA USIKU KWA AJILI YA IBADA ILI TUWE KARIBU ZAIDI NA ALLAH MTUKUFU WALA TUSIFANYE UVIVU JUU YA AMALI NA NAFASI HII AMBAYO HUENDA NDIO IKAWA YA MWISHO.

Anasema الله ﷻ katika Qur-an;

{شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنْزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ فَمَنْ شَهِدَ مِنْكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ ۖ وَمَنْ كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۗ يُرِيدُ اللَّهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ وَلِتُكْمِلُوا الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُوا اللَّهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ}

Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur'ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi. Basi ataye kuwa katika mji katika mwezi huu naafunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushukuru.

-Sura Al-Baqarah, Ayah 185

LEO TENA BI IDHINLLA TUNAANGALIA JAMBO LA TATU (3) KATIKA MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIWA NDANI YA MWEZI WA RAMADHANI AMBAO NI MWEZI UNAOTUHITAJIA KUJIFUNGA SAWASAWA KWA KUFANYA KILA YALIYO YA KHERI,  JAMBO HILO NI.

3 - KUKITHIRISHA KUSOMA QUR-AAN.

Kwa nini kukithirisha kuisoma Qur an?  Kwa sababu Mwezi wa Ramadhaan ni mwezi wa Qur-an, ni mwezi ambao   ndani yake ndio hasa kimeteremshwa kitabu huki kitukufu (Qur-aan),

Anasema الله ﷻ katika Qur-an;

{شَهْرُرَمَضَانَ الَّذِيَ أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَى وَالْفُرْقَان}

Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe Hidaaya kwa watu na hoja bayana za Hidaaya na Al-Furqaan (Upambanuzi).

[Al-Baqarah: 185]

Ni vyema kwa kila  muislamu kuzidisha jitihada zake katika kukisoma  kitabu hiki kitukufu (Qur-aan) angalau kila muislamu aweze kukihitimisha japo mara moja katika mwezi huu. Bila shaka kabisa kwa zama hizi watu wengi wameshuulishwa na dunia na hasa kiasi ambacho laiti leo tungezikamata na kushinda nazo kama ambavyo tunazishika simu zetu na kushinda nazo tukisoma mambo mbalimbali, kwa hakika dunia na miji yetu ingejaa baraka tele.

Lakini kwa kweli Qur an tumeitelekeza sana ila tu kwa wachache sana miongoni mwetu,  sasa angalau basi ndani ya mwezi wa Qur an tukithirishe kuisoma kwa kuizingatia huenda ikapatikana kheri tukaikamata na kusoma hata baada ya Ramadhan.

Aidha hali ya kuisoma Qur an,  ndiyo iliyokua desturi ya maswahaba waongofu kushindana katika kukisoma kitabu cha Allah Mtukufu 'Uthmaan bin 'Affaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa akihitimisha Qur-aan kila siku moja yani kwa siku juzuu 30, kadhalika na maswahaba wengine ambao walikua wakishindana na kuoneana wivu juu ya usomaji wa Qur an khususan ndani ya mwezi wa Ramadhan.

MWEZI WA RAMADHAN SIO MWEZI WA KUVUMBUWA KILA AINA YA MICHEZO NA KUPOTEZA MUDA,  BALI NI MWEZI WA KUCHUMA KWA KUKITHIRISHA KUISOMA QUR AN AMBAYO MALIPO YAKE YATAKUA MARA DUFU ZAIDI NA ZAIDI NA ZAIDI.


Anasema الله ﷻ katika Qur-an;

{يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّهَ حَقَّ تُقَاتِهِ وَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنْتُمْ مُسْلِمُونَ}

Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu kama ipasavyo kumcha; wala msife ila nanyi ni Waislamu.

-Sura Aal-E-Imran, Ayah 102

NAAM NDUGU ZANGU KATIKA IMANI,  TUNAENDELEA NA SILSILA YA DARSA YETU YA SAUMU YAKO DHAMANA YAKO,  NA LEO KWA UWEZO WAKE ALLAH TUNAANGALIA JAMBO LA PILI MIONGONI MWA MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIWA AMBALO NI.....

2 - IKHLASWI.

Ikhlasw ni kitendo cha kumkabidhi Allah Mtukufu amali zako huku ukitaraji malipo kutoka kwake yeye peke yake. Hujumuisha kufunga Swawm kwa iymaan na matarajio kwa yale aliyo yaahidi Allah mtukufu.

 قال صلى الله عليه وسلم:
(( من صام رمضان إيماناً و احتساباً غفر له ما تقدم من ذنبه )) 
أخرجه البخاري ومسلم.

Amesema Mtume ﷺ
 ((Atakayefunga Ramadhaan kwa iymaan na kutaraji malipo ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia ))
 
Hii yamaanisha kwamba: kila amali ambayo haipo au mja haifanyi kwa kutaka radhi za Allah na malipo aliyo yaahidi,  basi amali hii haitokubalika wala haitomfaa mja hata kama atadumu nayo hadi mwisho wa uhai wake, yani ukifanya amali ili watu wakuone au wakusifie basi wewe utakua ni miongoni mwa watu wenye khasara kubwa kabisa.

Au ikiwa muisilamu atafanya amali njema kwa mazoea tu na hana matarajio kutokana na amali zake akatambua kwamba Allah Mtukufu atamlipa ndio ile (Kitarajia malipo)  kadhalika huyu anakua bado hajafanya amali zake kwa ikhlasw na hazitoweza kumfaa kabisa.

HIVYO BASI,  HAPANA BUDI TUZITAKASE AMALI ZETU KWA KUZIFANYA KWA AJILI YA KUTARAJIA MALIPO KWA ALLAH NA KUTAKA RADHI ZAKE ILI TUSIJIKUTE KUA NI WENYE KHASARA SIKU YA MALIPO.