Published By Said Al Habsy  Madhumuni ya kila nguo inayo valiwa na muislamu iwe ni kwa ajili ya kutii amri ya Mola, kusitiri uchi, na pia iwe ni pambo kwake.
Hakika kuwa na stara ni dalili ya kuwa na haya, na haya ndio tabia ya asili ya mwenendo wa maumbile ya mwanaadamu, ambayo inamtofautisha na mnyama, nayo ndio tabia ya dini ya Kiisilamu. Kasema Ibn Abbas R.A.A, “Kasema Mtume S.A.W., “
إِنَّ لِكُلِّ دِينٍ خُلُقًا وَإِنَّ خُلُقَ الْإِسْلامِ الْحَيَاءُ.
Maana yake, “Kila dini ina tabia, na tabia ya dini ya Kiislamu ni kuwa na haya.” Yaani tabia ya muislamu ni kujiheshimu na kuwa na haya kwa yale yaliyokatazwa, na haya ni katika iman, na iman iko peponi. Kasema Jabir bin Zaid R.A..A. “Kasema Mtume S.A.W., “
الْحَيَاءُ مِنَ الإِيمَانِ، وَالإِيمَانُ فِي الْجَنَّةِ.
Maana yake, “Haya ni katika imani na imani iko peponi.” Na haya na imani ni vitu viwili ambavyo vimefungamana pamoja, unapokikuta kimoja basi na cha pili kiko pale, na kinapokosekana kimoja basi na cha pili pia hakiko pale. Kasema Abdullah bin Umar R.A.A., "Kasema Mtume S.A.W., “
الحياء و الإيمان قرنا جميعاً فإذا رفع أحدهما رفع الآخر.
Maana yake, “Haya na imani vimefungamana ikiwa moja itatoka basi nyingine itafuata.” Yaani asiye na haya pia hana imani.
Maswala ya nguo za stara ni muhimu sana kwa Waislamu, na ni moja ya alama ya ucha Mungu. Kasema Abi Adhiina Al Sadafi, “Kasema Mtume S.A.W., “
خير نسائكم الودود الولود المواتية المواسية إذا اتقين الله وشر نسائكم المتبرجات المتخيلات وهن المنافقات لا يدخل الجنة منهن إلا مثل الغراب الأعصم.
Maana yake, “Alie bora katika wanawake wenu ni yule mwenye upendo, uzazi, utiifu, uvumilivu na kuridhika, ikiwa watamcha Mwenyezi Mungu. Na wale wasio kuwa bora wa wanawake wenu ni wale wanao onyesha mapambo ya miili yao wenye kunyata na kujivuna, nao hao ni wanafiki. Hawataingia peponi katika wao, ila kama kunguru mwenye mdomo mwekundu.”
Hadithi zinazozungumzia maswala haya ni nyingi, na wanavyuoni wanatukumbusha daima na kutusisitizia kuhusu jambo hili. Lakini mawaidha na makumbusho hayo hayachukuliwi maanani na walio wengi miongoni mwetu, kila siku tunapiga hatua ya kujipambua, na kuwafuata watu walio pewa vitabu kabla yetu kwa kila jambo lao, ikiwa ni pamajo na mavazi yao. Na hii inatokea kama alivyo tubashiria Mtume S.A.W. kasema Abi Said R.A.A. kasema, “Kasema Mtume S.A.W., “
لَتَتَّبِعُنَّ سَنَنَ مَنْ قَبْلَكُمْ شِبْرًا بِشِبْرٍ وَذِرَاعًا بِذِرَاعٍ حَتَّى لَوْ سَلَكُوا جُحْرَ ضَبٍّ لَسَلَكْتُمُوهُ قُلْنَا يَا رَسُولَ اللَّهِ الْيَهُودَ وَالنَّصَارَى قَالَ فَمَنْ.
Maana yake, “Mtafuata mwendo wa wale waliyokuwa kabla yenu shubiri kwa shubiri, na dhiraa kwa dhiraa, (yaani kidogo kidogo halafu haraka haraka), hata kama wakiingia katika tundu la kenge basi mtawafuata (na mtaingia).” Wakasema, “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, Mayahudi na Manasara. Akasema, “Nani wengineo?”. Tunamuomba Mola aturudishe katika dini yetu ya haki mrudisho mzuri na tuwe wenye kusikia na kutii.
Mafanikio sahihi hayapatikani isipokuwa tu kwa kufuata amri za Mola Mtukufu na ndio inakuwa sababu ya kuepukana na adhabu kali ya jahanam na kuingizwa peponi. Kasema Abu Huraira R.A.A., “Kasema Mtume S.A.W., “
كل أُمتي يدخلون الجنة إلا من أبى فقالوا يا رسول الله من يأبى قال من أطاعني دخل الجنة و من عصاني فقد أبى.
Maana yake, “Umma wangu wote wataingia peponi isipokuwa wale watakaokataa. Wakasema, “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. nani atakayekataa (kuingia peponi).” Akajibu, “Yule atakaye nitii ataingia peponi, na yule atakayeniasi ndiye aliyekataa.”
|