Published By Said Al Habsy  Wamekhitilafiana wanavyuoni hukumu ya adhana na iqama katika Salaa za jamaa. Kauli mashuhuri na yenye nguvu kwa wanavyuoni wetu Mwenyezi Mungu awe radhi nao, ni kuwa adhana na Iqama ni fardhi ala-kifaya. Wameegemeza rai yao hiyo kutokana na mwenendo wa Mtume S.A.W. na kutoka katika kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kasema Mwenyezi Mtukufu katika Surat Al-Maida aya ya 58, “
﴿وَإِذَا نَادَيْتُمْ إِلَى الصَّلاَةِ﴾.
Maana yake, “Na mnapo adhinia Salaa”. Pia Kasema Mwenyezi Mtukufu katika Surat Al-Jumua aya ya 9, “
﴿يأَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ إِذَا نُودِيَ لِلصَّلاَةِ مِن يَوْمِ الْجُمُعَةِ﴾.
Maana yake, “Enyi mlio amini! Ikiadhiniwa Salaa siku ya Ijumaa”. Kasema Abi Said Al Khudhry R.A.A., “Kasema Mtume S.A.W., “
إِذَا سَمِعْتُمُ النِّدَاءَ فَقُولُوا مِثْلَ مَا يَقُولُ الْمُؤَذِّنُ.
Maana yake, “Mtakaposikia adhana semeni kama asemavyo muadhini” Pia kasema Malik R.A.A, "Kasema Mtume S.A.W., “
فَإِذَا حَضَرَتْ الصَّلاةُ فَلْيُؤَذِّنْ لَكُمْ أَحَدُكُمْ.
Maana yake, “Ikifika wakati wa Salaa basi aadhini mmoja wenu.” Toka ilipoanza kutamkwa adhana Mtume S.A.W. hakuiacha adhana na wala iqama wakati wa Salaa akiwa nyumbani au akisafiri.
IV. Hukumu ya adhana na Iqama kwa wanawake.
Adhana na iqama ni kwa ajili ya wanaume tu, wanawake wao hawana adhana wala iqama. Kasema Ibn Umar R.A.A., “Kasema Mtume S.A.W, “
ليس على النساء أذان ولا اقامة.
Maana yake, “Wanawake hawana adhana wala iqama.” Na huu ndio msimamo wa mwanachuoni wetu maarufu Sheikh Ahmed al Khalil.
|