Kila Salaa ya faridha ina wakati wake maalum wa kuisali. Haijuzu kabisa kuisali Salaa yoyote ile ya faridha kabla au baada ya wakati wake, ila kwa sababu maalum zinazo kubaliwa kisheria ambazo tutazitaja ikifika sehemu yake akipenda Mola Mtukufu. Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat AN-Nisaai aya ya 103, “ ﴿فأَقِيمُواْ اْلصَّلاةَ إِنَّ الصَّلاةَ كَانَت عَلَى المُؤمِنِينَ كِتَاباً مَّوقُوتاً﴾. Maana yake, “Basi simamisheni Salaa. Kwa hakika Salaa kwa Waislamu ni faridha iliyowekewa nyakati mahsusi.” Kasema Mola Mtukufu katika Suratil Baqara aya ya 238, “ ﴿حَـفِظُواْ عَلَى الصَّلَوتِ وَ الصَّلاةِ الوُسطَى وَقُومُواْ للهِ قَانِتِينَ﴾. Maana yake, “Angalieni sana Salaa (zote kuzisali, khasa jamaa) na (khasa) ile Salaa ya kati na kati. Na simameni kwa unyenyekevu katika kumwabudu Mwenyezi Mungu.” Nyakati za Salaa zilifafanuliwa kwetu na Mtume S.A.W. Kasema Ibn Abbas R.A.A., "Kasema Mtume S.A.W., [1]“ أَمَّنِي جِبْرِيلُ عَلَيْهِ السَّلام عِنْدَ الْبَيْتِ مَرَّتَيْنِ فَصَلَّى بِيَ الظُّهْرَ حِينَ زَالَتْ الشَّمْسُ وَكَانَتْ قَدْرَ الشِّرَاكِ وَصَلَّى بِيَ الْعَصْرَ حِينَ كَانَ ظِلُّهُ مِثْلَهُ وَصَلَّى بِيَ يَعْنِي الْمَغْرِبَ حِينَ أَفْطَرَ الصَّائِمُ وَصَلَّى بِيَ الْعِشَاءَ حِينَ غَابَ الشَّفَقُ وَصَلَّى بِيَ الْفَجْرَ حِينَ حَرُمَ الطَّعَامُ وَالشَّرَابُ عَلَى الصَّائِمِ فَلَمَّا كَانَ الْغَدُ صَلَّى بِيَ الظُّهْرَ حِينَ كَانَ ظِلُّهُ مِثْلَهُ وَصَلَّى بِي الْعَصْرَ حِينَ كَانَ ظِلُّهُ مِثْلَيْهِ وَصَلَّى بِيَ الْمَغْرِبَ حِينَ أَفْطَرَ الصَّائِمُ وَصَلَّى بِيَ الْعِشَاءَ إِلَى ثُلُثِ اللَّيْلِ وَصَلَّى بِيَ الْفَجْرَ فَأَسْفَرَ ثُمَّ الْتَفَتَ إِلَيَّ فَقَالَ يَا مُحَمَّدُ هَذَا وَقْتُ الْأَنْبِيَاءِ مِنْ قَبْلِكَ وَالْوَقْتُ مَا بَيْنَ هَذَيْنِ الْوَقْتَيْنِ Maana yake, “Jibril A.S. aliniongoza katika Salaa kwenye Al Kaaba mara mbili, aliniongoza katika Salaa ya adhuhuri wakati jua lilipopinduka, na ilikuwa kama mfano wa kigwe cha malapa[2]. Na aliniongoza katika Salaa ya Al`aasir wakati ambapo kivuli kilikuwa sawa sawa na kitu chenyewe. Na aliniongoza katika Salaa ya Magharibi wakati wa kufuturu aliyefunga. Na aliniongoza katika Salaa ya Isha wakati yalipo potea mawingu mekundu. Na aliniongoza katika Salaa ya Alfajiri wakati ambapo inakatazwa kula na kunywa aliyefunga. Na ilipokuwa siku ya pili aliniongoza katika Salaa ya Adhuhuri wakati kitu ni sawa sawa na kivuli chake. Na aliniongoza katika Salaa ya Al`aasiri wakati ambapo urefu wa kivuli ni mara mbili kuliko kitu chenyewe. Na aliniongoza katika Salaa ya Magharibi wakati wa kufuturu aliyefunga. Na aliniongoza katika ya Salaa ya Isha ilipofika thuluthi moja ya usiku. Na aliniongoza katika Salaa ya alfajiri wakati ilipotoka weupe (yalipoingia mapambazuko kabla ya kuchomoza jua). Halafu akanigeukia akaniambia Ewe Muhamad huu ndio wakati wa Salaa wa Mitume kabla yako pamoja na wakati uliobaina ya nyakati hizi”.
|