Published By Said Al Habsy  Maisha ya dunia ni kama vile shamba na mtu atalipwa kufuatana na vitendo vyake, marejeo ya mwanadamu ni kesho akhera, na baraka ya uhai ni kutenda yale yenye manufaa kesho akhera. Salaa ndio kitendo cha kwanza ambacho mtu ataanza kuhisabiwa; ikiwa ataziharibu basi ameharibu kusudio la kuumbwa kwake, na vitendo vyake vyote kesho akhera vitakuwa havina thamani, na juhudi na wakati wake alioutumia duniani kwa kutenda alio tenda itakuwa haina thamani. Kasema Mwenyezi Mungu katika Surat AN-Nur aya ya 39, “
﴿وَالَّذِينَ كَفَرُواْ اأَعمَـلُهُم كَسَرَابِ بِقِيعَةٍ يَحسَبُهُ الظَّمئَانُ مَآءً حَتّى إِذَا جَآءَهُ لَم يَجِدهُ شَيئاً وَّوَجَدَ اللَّهَ عِندهُ فَوَفَّــهُ حِسَابَهُ وَاللهُ سَرِيعُ الحِسَابِ﴾.
Maana yake, “Na wale waliokufuru, vitendo vyao (wanavyoviona vizuri) ni kama mazigazi, (mangati sura ya maji) jangwani, mwenye kiu huyadhani ni maji, akiyaendea hayaoni chochote (na wao watakapoziendea amali zao siku ya Kiyama. Hawatopata chochote); Wamkute Mwenyezi Mungu hapo, awalipe hesabu yao sawa sawa; na Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhesabu.”
Pia kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Al-Furqan aya ya 23, “
﴿وَقَدِمنَآ إِلى مَا عَمِلُواْ مِن عَمَلٍ فَجَعَلنـهُ هَبَآءً مَّنثُورًا﴾.
Maana yake, “Na tutayaendea yale waliyoyatenda katika amali (zao walizofanya japo nzuri, maadamu walikuwa wanakanusha Uislamu); Tuzifanye kama mavumbi yaliyotapanywa, (yaliyotawanyika).” Yaani vitendo vyao vitakuwa havina thamani yoyote ile.
Baadhi ya watu wanafikiria vipi mtu aliefadhiliwa mambo duniani ambayo kwa nadharia yao ni mambo mazuri na thamani, kama vile watoto, mali, madaraka na kadhalika, atakuwa hana baraka. Fikra hizo sio sahihi kwani utulivu na furaha havitokani na vitu hivyo na inawezekana vikawa ndio sababu ya adhabu na mashaka yake duniani na kesho akhera. Wanasema waswahili, "Kitanda usicholalia hujui kunguni zake". Kasema Mola Mtukufu katika Surat AT-Tawba aya 55, “
﴿فَلاَ تُعجِبكَ اَموَلُهُم وَلآ اَولـدُهُم إِنَّمَا يُرِيدُ الله لِيُعَذِّبَهُم بِهَا فِى الحَيوةِ الدُّنيَا وَ تَزهَقَ أَنفُسُهُم وَ هُم كـفِرُونَ﴾.
Maana yake, “Yasikufurahishe mali yao wala watoto wao. Anataka Mwenyezi Mungu awaadhibu kwa hayo katika maisha ya dunia, na zitoke roho zao, na hali ya kuwa ni makafiri.” Pia Mola Mtukufu ametuhadharisha na vitu hivyo kuwa vinaweza kuwa ndio sababu ya kutusahaulisha na ibada na akaonya kwa kupata hasara na adhabu kali kwa atakaefanya hivyo. Kasema Mola Mtukufu katika Surat Al-Munaafiqun aya ya 9, “
﴿ياَيُّهَا الَّذِينَ ءَامَنُواْ لاَ تُلهِكُم اَموَلُكُم وَلآ أَولـدُكُم عَن ذِكْرِ اللهِ وَ مَن يَفعَل ذلِكَ فَأُ لَـئِكَ هُمُ الخسِرُونَ﴾.
Maana yake, “Enyi Mlioamini! Yasikusahaulisheni mali yenu na wala watoto wenu kumkumbuka Mwenyezi Mungu; Na wafanyao hayo, hao ndio wenye kukhasirika.” (Na wafasiri wa Qur`aani wamesema, “Kumkumbuka Mwenyezi Mungu katika aya hii inamaanisha Salaa tano za faridha za kila siku. Kwa hali hiyo ikiwa mtu itamshughulisha biashara yake, au shughuli yake yoyote ile, au watoto wake, mpaka ashindwe kusali kwa wakati wake basi atakuwa, ni miongoni wa wenye kupata hasara.) |