Mtume (s.a.w.) alirejea Madina mwezi 20 Mfunguo tatu wa mwaka wa 10 A.H – 632. Lakini tangu kurejea kwake hakua na afya nzuri kama zamani, ila ugonjwa haukumtupa kitandani bado. Hata lilipokuchwa jua la kuamkia Jumaatano mwezi 29 Mfunguo tano, Mtume (s.a.w.) alitoka na mtumwa wake Abu Muwayhiba, wakenda wakazuru makaburi ya kiwanja cha Al Bakii akawatolea salamu waliozikwa huko na akawaombea dua. Khatimaye akarejea nyumbani kwake akamkuta Bibi Aysha anajida[1] kuwa kashikwa na kichwa barabara, na huku analia na kusema: “Ee kichwa changu wee!” Mtume (s.a.w.) akamwambia: “Anayestahiki kusema kichwa changu wee ni miye si wewe. Kwani mimi nitakufa kabla yako wewe. Lau ungekufa kabla yangu mimi. Wallahi! Ningekutengeneza mimi mwenyewe vizuri na ningekusalia kwa dua nyingi na nzuri nzuri”.
Mtume (s.a.w.) kuamka tu asubuhi aliamka na kichwa kikali na homa ndogo, kila siku ikipambazuka na homa ilikuwa ikizidi. Lakini vivyo hivyo alikuwa akijikaza kwenda msikitini kusali na kwenda kumtimizia ngono za kila mke katika wakeze tisa. Hata ugonjwa ulipomzidi sana aliwaomba wakeze wampe ruhusa augulie nyumbani kwa Bibi Aysha, nao waje kumwuguza huko huko. Mabibi hao wote walikubali shauri hiyo, wakahamia nyumbani kwa Bibi Aysha kumwuguza mume wao mtukufu. Nyumba hii ya Bibi Aysha ilikuwa karibu na Msikiti kuliko nyumba za wake wenziwe, ndio maana Mtume (s.a.w.) akaichagua, ili aweze kuhudhuria Msikitini na kusalisha mwenyewe kila kipindi. Navyo ndivyo alivyokuwa akifanya.
Lakini sala ya Isha ya kuamkia Ijumaa, mwezi 9 Mfunguo sita ilipoadia, akapelekewa Mtume (s.a.w.) mjumbe kwenda kumwita, alikutikana taabani, kwa hivyo aliamrisha aambiwe Sayyidna Abubakr akasalishe. Akafanya kama alivyoamrishwa, akawa yeye ndiye mwenye kusalisha mpaka kufa kwa Mtume (s.a.w.). Hata siku moja baada ya kusalisha Sayyidna Abubakr, Mtume (s.a.w.) alijikongoja – na huku kashikwa na watu wawili – akaja msikitini akapanda juu ya mimbar, akasema maneno haya: “Enyi watu! Pana mtu mmoja ambaye Mwenyezi Mungu amemkhiyarisha baina ya Dunia na Akhera, naye amechagua “Akhera”. Sayyidna Abubakr akafahamu madhumuni ya maneno haya ya Mtume (s.a.w.), kwa hivyo akalia akasema: “Tunakufidia kwa roho zetu, Yaa Rasula Llah!” Kisha Mtume (s.a.w.) akaendelea kusema: “Hakika mwenye neema kubwa juu yangu miongoni mwenu, kwa mali yake na nafsi yake, ni Abubakr” Kisha akasema: “Enyi Muhajir! Jiusieni kuwafanyia wema Ansar. Wao ndio vipenzi vyangu ambao tumekimbilia kwao, wakatufanyia kila ihsan. Walipeni mema kila watakaokufanyieni mema, na mwasamehe kila watakaokufanyieni mabaya” Baada ya haya Mtume (s.a.w.) akashuka akajikongoja mpaka kwake.
Tangu siku hiyo hakutoka tena kwani ugonjwa ulimzidi sana, ila alfajiri ya Jumaatatu mwezi 12 Mfunguo sita, alikuja msikitini akasali nao rakaa ya mwisho ya sala hiyo. Baada ya kumalizika rakaa yake ya pili, aliwakabili watu akasema: “Enyi watu! Moto unawangojea wabaya, na Pepo imeandaliwa wema. Zimekukabilini fitna za dini kubwa kubwa. Kila zikisha fitna zitafuatwa na nyenginezo. Wallahi! Hapana yoyote katika nyinyi anayenidai haki yake. Wallahi mimi sikuhalalisha ila kilichohalalishwa na Qurani, wala sikuharamisha ila kilichoharamishwa na Qurani” Kisha akakaa akazungumza nao mpaka kadiri ya saa moja au mbili ya mchana. Baadaye akawaaga akenda zake kwake, na kila aliyekuwepo hapo akenda kwenye jambo lake. Sayyidna Abubakr akamwaga Mtume (s.a.w.) ende shamba akamtazame mkewe, na Mtume (s.a.w.) akampa ruhusa, watu wote walifurahi wakaona ya kuwa Mtume (s.a.w.) kesha pona, sasa hivi atakamata kazi zake kama zamani.
Lakini baada ya kurejea kwake tu, alihisi nguvu zake zinamwacha upesi upesi. Akajitupa juu ya kitanda akazungukwa na wake zake na mwanawe Bibi Fatma, mara zikaonekana juu yake alama za ‘Sakratilmaut’ (kukata roho). Bibi Aysha akampakata juu ya mapaja yake, na wenziwe wote wakakizunguka kitanda cha Mtume (s.a.w.) na macho yao yanamiminika machozi njia mbili mbili. Karibu ya kitanda kilikuwapo kibakuli cha maji ambacho Mtume (s.a.w.) alikuwa akichovya ndani yake mkono wake, kisha akifuta kwa maji hayo uso wake, na huku anasema: “Enyi watu! Hakika kutoka roho kuna machungu makubwa” wakati huo aliingia mtu mmoja na msuwaki mkononi mwake. Mtume (s.a.w.) akaashiria apewe msuwaki huo. Bibi Aysha akamtafuniatafunia, kisha akampa, na Mtume (s.a.w.) akautia kinywani akawa anasuwakia kidogo kidogo.
Pale pale ule msuwaki ulimtoka mkononi, akaregea yu taabani! Akakodoka macho kutazama juu – huku anakata roho – na huku anasema: “Nakwenda kwa rafiki yangu Mtukufu, nakwenda kwa rafiki yangu Mtukufu” wanawake waliokuwako ndani jinsi walivyokiangua kilio hicho hata mji wote ulitikisika.
Muda si muda watu wote wakimbizana kuja nyumbani kwa Mtume (s.a.w.) mbio – nguo mikononi – Mtu wa mwanzo kufika alikuwa ni Baba yake mdogo, Bwana Abbas, kufika tu aliufunga mlango kwa ndani, akawaacha watu wote nje, kuingia ndani alimwona mwanawe anamaliza pumzi zake za mwisho, na pale pale akakata roho, Bwana Abbas akamfumba macho, akambana kinywa, akamnyoosha viungo, kisha akamgubika guo moja kwa moja tangu kichwani mpaka nyayoni.
Baadaye akatoka nje akawapa habari waliokuwapo hapo ya kuwa Mtume (s.a.w.) amefariki Dunia. Si msiba uliotokea siku hiyo! Si mtaharuki uliowazukia watu hao! Si huzuni isiyopata kuonekana mfano wake. Si kujigubika huko kulikojigubika mji wa Madina siku hiyo! Bwana Abdalla bin Unays – kusikia tu kwamba Mtume (s.a.w.) kafa – alianguka papo hapo chini – mkavu – amekwisha. Sayyidna Uthman na wengi wengineo iliwapooza miguu, wasiweze kuvuta hata hatua moja, wakapigwa na bumbuwazi kamili! Wengine walitokwa na fahamu, wakawa wanakwenda njiani mapepe! Hawajui watokako wala wendako, Sayyidna Umar akatafuta njia mpaka akaingia ndani kwa maiti. Akamfunua uso wake akaona Mzuri, una bashasha na kutoa nuru kama zamani. Furaha ilimrarulia nguo, akasema: “Wallahi! Hajafa. Uso huu si uso wa mtu aliyekufa. Waongo wakubwa wanaosema kuwa amekufa!” Kisha akatoka nje na upanga mkononi, na huku anasema: “Mtume (s.a.w.) hakufa. Yoyote atakayesema kuwa Mtume (s.a.w.) amekufa nitampiga kwa upanga huu. Wanafiki wakubwa nyi[2]! Mtume (s.a.w.) atakufa kabla dunia yote haijasilimu? Muhali huo!” watu walioko nje wakababaika, hawajui wafuate maneno ya Bwana Abbas aliyesema kuwa Mtume (s.a.w.) amekufa au maneno ya Sayyidna Umar, anayechaga kuwa hukufa, ila roho yake imekwenda mbinguni kisha itarejea.
Muda si muda alitokea Sayyidna Abubakr – pumzi mbili mbili – macho paani. Watu wakamzonga kwa vilio na masuali. Wanamuuliza yepi yaliyo kweli, maneno ya Bwana Abbas au maneno ya Sayyidna Umar, Sayyidna Abubakr akaingia ndani kwa maiti akamfunua uso akambusu, akasema: “Unanukia vizuri na unapendeza, kama katika uhai wako. Wallahi! Mimi nakiri ya kwamba umekufa. Mungu hatakuonjesha mauti mara mbili. Inakutosha taabu iliyokukuta katika kukata roho sasa hivi. Wallahi! Sisi tunashuhudia ya kwamba umetekeleza ujumbe, umeunasihi umma, na umesimama juu ya haki za Mungu na za wanaadamu, ukazitekeleza vilivyo. Amani ya Mungu na Rehema zake zikushukie asubuhi na jioni” Baada ya hapa alifululiza Msikitini, akapanda juu ya Mimbar akahutubu akasema: “Enyi watu! Kama palikuwa katika nyinyi ambaye akimwabudu Muhammad, basi Muhammad amekwisha kufa. (Naakatafute Munghu mwengine). Ama ambaye alikuwa akimwabudu Mungu, basi Mungu yu hai milele hafi. Mungu amesema katika Quran:
{Hakuwa Muhammad ila Mtume tu ambaye wamepita kabla yake yeye Mitume wengi. Basi atakapokufa au atakapouawa mtarejea katika ujinga? Basi yoyote atakayerejea katika ujinga wake hatamdhuru Mungu chochote}[3]
Baada ya kusikia maneno haya watu wote waliyakinisha – hata Sayyidna Umar pia – ya kuwa kweli Mtume (s.a.w.) amekufa. Basi hapo ndipo walipoingia kutafuta khalifa na kutengeneza shauri ya kuzika. Akachaguliwa Sayyidna Abubakr kuwa Khalifa, baada ya upinzani mkubwa uliokuwepo katika mkutano wa kuchagua, alipata sauti nyingi kuliko sauti alizopata Sayyidna Ali na kuliko alizopata Bwana Saad bin Ubada – bwana mkubwa wa Kiansar wote – Baadhi ya Ansar na Muhajir – wasiokuwa Bani Hashim – walimtaka Sayyidna Abubakr, ama Bani Hashim wote[4] na baadhi ya Ansar walimtaka Sayyidna Ali, na Ansar waliosalia walimtaka Bwana Saad bin Ubada[5]. Muda huu walipokuwa wanamchagua Khalifa, Sayyidna Ali na jamaa zake, walikuwa katika kazi ya kumwosha Mtume (s.a.w.)[6]. Mtume (s.a.w.) alipakatwa na Bwana Al Fadhil bin Abbas bin Abdul Muttalib, akaoshwa na Sayyidna Ali bin Abi Talib bin Abdul Muttalib, na aliyekuwa akitilia maji ni Bwana Abbas bin Abdul Muttalib. Ama mahuru wake Mtume (s.a.w.) wawili – Bwana Usama bin Zayd na Bwana Shakran – wao walikuwa wakiwasaidia. Baada ya kuoshwa lilichimbwa kaburi kuko huko chumbani alikokufia – chumba cha Bibi Aysha – na aliyesimama kutengeneza hilo kaburi na kulitilia mwanandani ni Bwana Abu Talha wa Kiansar. Baada ya hapa wakamvua nguo za kuoshea, wakamkafini kwa nguo tatu nyeupe za pamba, baada ya kufukizwa kwa udi vyema na kutiwa manukato vizuri. Kisha akalazwa juu ya kitanda kwenye ukingo wa kaburi, akafunikwa guo moja kwa moja. Baadaye wakapewa ruhusa watu kuingia kumwaga Mtume wao (s.a.w.). Yakawa makundi haya yanaingia na haya yanatoka, mchana kutwa wa Jumaatatu na mchana kutwa wa Jumaane na usiku kucha wa kuamkia Jumaatano. Hata karibu na alfajiri ya hii Jumaatano. Mtume (s.a.w.) alishushwa kaburini mwake, akazikwa kama wanavyozikwa Waislamu wote wengine. Walioshuka kaburini siku hiyo ni:-
Bwana Abbas, Sayyidna Ali. Na mabwana hawa wengine wajao:- Al Fadhil bin Abbas, Qutham bin Abbas na Shakran.
Mtume (s.a.w.) amekufa mchana wa Jumaatatu mwezi 12 Mfunguo sita mwaka 11 A.H – 8 June 632, na akazikwa karibu na alfajiri ya Jumaatano mwezi 14. Alipokufa ulikuwa umri wake ni miaka 63 barabara.
Hii dunia dania *** Haidumu na bashari. Akhi! Yakutosha haya *** Kutawafu Mukhtari. Watu walijililia *** Mwishowe wakasubiri. Ayyuhal Maghruri *** Ina khadaa dunia.
[1] - Dhahir ni kuwa neno "Anajida" ni kosa la spelingi la neno "Anajidai? Lakini ni dhahir pia kwamba Sheikh hawezi kutumia lugha hii dhidi ya Bibi Aysha kwamba alikuwa anajidai kuwa anaumwa na kichwa. Bali ni wazi kuwa neno "Anajida" Sheikh kalichukua katika riwaya yenyewe inayozungumzia kisa hiki ambapo ndani yake Bibi Aysha kasema: "وَأنا أجِدُ صُدَاعًا فِي ْرَأسِيْ" Wa Ana Ajidu Suda'an Fii Ra-asi (Nami nina maumivu ya kichwa). Tazama Ibn Majah Al-Sunan Hadithi na. 1465. Kwa hivyo, baada ya Sheikh kutumia maneno "Nina maumivu" katumia maneno "Anajida kuwa kashikwa na kichwa". Inaonesha neno "Anajida" ndio lile Ajidu lililo katika Hadithi. Wallahu A'alam.
[2] - Bwana mmoja wa huko kwetu Afrika Mashariki siku moja aliielezea sehemu hii ya kufa kwa Mtume (s.a.w.). Aliponukuu maneno hayo ya Sayyidna Umar, Bwana huyo alisema: “Umar anakusudia kwamba Ali na Abbas ni wanafiki”. Lakini kila mwenye akili anadiriki kwamba huku ni kutaka kukuzisha mambo tu: si jengine, kwani ukweli ni kuwa kifo cha Mtume (s.a.w.) kiliwafadhaisha wengi, nyoyo na nafsi zilibabaika, watu wasijue nini wanafanya; wasijue nini wanakisema: mtafaruku mkubwa ulikuwa katika nafsi za Masahaba kila mmoja kapigwa na bumbuwazi, kaduwaa, wakaanguka walioanguka, miili ikawapooza na wengine wakaiaga dunia papo hapo. Kwa hivyo, ikiwa imethibiti kuwa Sayyidna Umar alitamka neno hilo basi haikuwa kamwe akiitakidi kuwa Ali na Abbas ni wanafiki. Haashahu! Vipi aitakidi hivyo, halafu: 1) Papo hapo – baadae – akubali kuwa Mtume (s.a.w.) kafa? Hili linaonesha wazi kuwa hakuyasema hayo ila kwa kufadhaika: si kwa kuyaitakidi. 2) Vipi Umar amuone Ali kuwa ni mnafiki halafu amfanye mmoja wa watu sita wa kuchaguliwa kwa ukhalifa baada yake?! Bali tunaona kwamba mfazaiko wa aina hii pia tunaona kwamba ulimkumba hata Bibi Fatma, kama alivyosimulia Imam Bukhari kwamba alipozikwa Mtume (s.a.w) alisema Fatma: “Vipi zimekupelekeeni nafsi zenu hata mukaufukia mwili wa Mjumbe wa Allah katika dongo?” Lakini ukiwa unamchukia Bibi Fatma na ukataka kupotoa ukweli na kukuzisha jambo hili unaweza kusema kuwa: “Mtizameni huyu Fatuma! Hivyo yeye hajui kuwa hivi ndivyo Uislamu ulivyofundisha?! Hivyo hajui huyu Fatuma kwamba Allah kasema: (Katika hii ardhi tumekuumbeni na humo tutakurudisheni na kutoka humo tutakutoeni mara nyengine??!!) (Taha - 55). Au hajui kuwa Allah kasema: (Je hatukuifanya ardhi kuwa ni yenye kukushanya (viumbe) * Vilivyohai na wafu) (Al-Mursalat 25-26). Je hajui kuwa kauli ya Allah isemayo : (Allah akamletea kunguru anayefukua ardhini ili amwonyeshe jinsi ya kuificha (kuizika) maiti ya nduguye) (Maida – 31); hajui yeye kuwa Aya hizi ni dalili ya mafundisho ya kuzikwa baada ya kufa? Je yeye hajui kuwa haya ni mafundisho aliyokuja nayo Mtume (s.a.w.)?!” Na unaweza kusema mengi kuliko haya ya kumfanya yeye kuwa hana analolijua na hali ya kuwa mambo hayakuwa hivyo, bali ni kule kufazaika kwake kwa kifo cha Baba yake Mpenzi, Rasulu Allah (s.a.w.). Na ndio maana baada ya Sayyidna Abu Bakr kuwasomea watu kauli ya Allah isemayo: (Na hakuwa Muhammad ila ni Mtume tu. Wamepita kabla yake Mitume (mingi) akifa au akiuawa ndio mtarudi nyuma kwa visigino vyenu (muwe makafiri) na atakayerudi nyuma kwa visigino vyake hatamdhuru Allah chochote. Na Allah atawalipa wanaoshukuru), kasema Ibnu Abbas kuwa: وَاللهِ لَكَأنَّ النَاسَ لَمْ يَعْلَمُوْا أنَّ اللهَ أنْزَلَ هَذِهِ الآيَةَ حَتَّى تَلاَهَا أبُوْ بَكر (Wallah kana kwamba watu walikuwa hawajui kuwa Allah kateremsha Aya hii ila baada ya kuisoma Abu Bakr).
[3] - }وَمَا مُحَمَّدٌ إِلاَّ رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِنْ قَبْلِهِ الرُّسُلُ أَفَإِيْن مَاتَ أَوْ قُتِلَ انْقَلَبْتُمْ عَلَى أَعْقَابِكُمْ وَمَنْ يَنْقَلِبْ عَلَى عَقِبَيْهِ فَلَنْ يَضُرَّ اللَّهَ شَيْئاً... (144) { [4] - Ni wazi kuwa watu bado walikuwa na ukabila, kama ilivyo kawaida ya Warabu wengi. Kwa nini iwe Bani Hashim wote wamtake 'Ali, Bani Hashim mwanzao na wamkatae Abu Bakr?! Ukabila na utabaka ndio yalilokuwa matatazo sugu kwa Waislamu hadi kupelekea kuundika madhehebu tafauti. Na tatizo hili bado linaendelea hadi leo: watu hawatazami Allah anasema nini wala nani anastahiki kuwa kiongozi, bali wanatazama watu wa makabila yao wanasema nini, kisha wanawatetea kwa hali yoyote wakiwa ni madhalimu au wakiwa ni wenye kudhulumiwa. Wa Allahu Al-Musta'an! [5] - Katika jambo hili la Ukhalifa kila mmoja alijiona kuwa yeye anastahiki zaidi kuliko mwengine. Muhajirina walijiona kuwa wao wanastahiki kuliko Ansari na Ansari vivyo hivyo. Na katika haya kuna dalili tosha kuwa Mtume (s.a.w.) hakuusia kuwa ukhalifa baada yake uwe wa Sayyidna Ali wala wa mwengine, ingawa aliashiria – kwa mujibu wa riwaya sahihi ya Bukhari – kuwa Abu Bakr ndiye atayeshika ukhalifa na baada yake ni 'Umar, lakini hio haikuwa amri. Na kwa sababu hii, ndio maana utaona kuwa kila mmoja alikuwa na watu waliompendelea kuwa Khalifa pasina kutoa andiko lolote kutoka kwa Mtume (s.a.w.) kuwa fulani ndiye aliyechaguliwa na Mtume (s.a.w.) kuwa Khalifa baada yake, bali hoja zote zilikuwa kwa misingi ya ukabila na ukaraba (ujamaa na Mtume s.a.w.) na kufadhilishana baina yao. Na ndiyo maana utaona katika kuchaguliwa Sayyidna Uthman kuwa Khalifa alisema Miqdad kuwa: "أتُبَايِعُوْنَ رَجُلاً لَمْ يَشْهَدْ بَدْرًا؟!" “Hivyo munamchagua mtu ambaye hakuhudhuria (vita vya ) Badr?!” Kwa hivyo, yeye aliona kuwa Sayyidna Uthman hafai kwa sababu hakuhudhuria vita vya Badr: si kwa sababu hakuusiwa. Na haya aliyasema katika kumpigia kampeni rafiki yake kipenzi Sayyidna Ali. Na kilichosahihi ni kuwa Sayyidna Ali mwenyewe juu ya kuwa alijiona kuwa kadhulumiwa – kama inavyodaiwa – lakini hakutoa hoja ya kuwa yeye kausiwa kuwa Khalifa baada ya Mtume (s.a.w.). Bali tunakuta riwaya inayosimuliwa na Wanavyuoni wa Kishia kwamba Sayyidna Ali na Abbas waliingia kwa Mtume (s.a.w.) wakati alipozidiwa wakamwambia: “Ewe Mjumbe wa Allah tuchagulie Khalifa akasema: “La mimi nahofia mukaja mukafarikiana kama walivyofarikiana Bani Israili kutokana na Harun, lakini Allah akijua kwamba nyoyoni kwenu kuna kheri basi atakuchagulieni” Sh. Ahmad Al Katib Tawatur Al Fikri Al Siyasy Al Shi’i uk. 19. Naye kanukuu Riwaya hii kutoka katika kitabu “Al- Shafi” cha Sharif Al Murtadha. Na lililowazi zaidi ya hilo na ambalo limekubaliwa na Uma mzima ni ile Sulhu baina ya Al-Imamu Al-Hasan bin Ali na Muawiya kwa sharti kwamba MU'AWIYA AKIFA UKHALIFA UWE KWA NJIA YA SHURA. Haya yote yanaonesha wazi kuwa Ahlu Al-Bayt wenyewe walikuwa wakiizingatia Shura kuwa ndio njia pekee ya kuteuliwa Khalifa wa Kiislamu, vyenginevyo Imam Hasan asingelisisitiza hivyo. Kwa hivyo, ni wazi kuwa Mtume (s.a.w.) hakuchagua Khalifa baada yake. Na utakapotizama msimamo waliokuwa nao Muhajirina na Ansar unazidi kuthibitisha hayo, kwani kukutana kwao na kumchagua Khalifa wa Uislamu kunapingana na kauli ya kuwa Mtume (s.a.w.) kausia. Na kwa hivyo, Ali mwenyewe kanena havi: “Kilichowajibu katika hukumu ya Allah na hukumu ya Uislamu kwa Waislamu, baada ya kufa Imamu wao au kuuliwa… wasifanye kitu wala wasizuwe jambo wala wasitangulize mkono wala mguu wala wasianze chochote kabla hawajajichagulia Imamu mwenye kujizuia (na machafu) mjuzi, mnyenyekevu mwenye maarifa ya hukumu na Suna” . Almajlisi Biharu Al Anwaar j. 8 uk. 555 chapa ya zamani. [6] - Walinganiaji wengi waliowapinzani wa Abu Bakr na 'Umar wanaipotoa mafuhumu sahihi ya sehemu hii kwa kusema: ‘Baada ya kufa Mtume (s.a.w.) tu wakakutana mabwana wakubwa huko kwenye Saqifa kwenda kugombania ukubwa na huku wakauwacha Mwili Mtukufu wa Bwana Mtume (s.a.w.) pasina kuujali, na hakuna aliyeshughulika naye isipokuwa Imam Ali na Abbas na Al Fadhil bin Abbas’. Yaani wanataka kuonesha kuwa hao waliokutana kwa ajili ya kumchagua Khalifa ni watu wenye uchu wa madaraka na vyeo, na walengwa hasa hapa ni Sayyidna Umar na Sayyidna Abu Bakr, kwani falsafa za aina hii zenye ushawishi katika ulinganiaji hutumika zaidi linapotokea jambo lenye kuwahusu wao. Lakini utakapotizima mafundisho ya Uislamu utaona kuwa walivyofanya Masahaba ndivyo hasa ilivyokuwa ikitakikana, kwani: 1) Wanaostahiki kuishughulikia maiti ni watu wa familia: si watu wa nje na hivyo ndivyo ilivyokuwa – Ali na Abbas na Al Fadhil bin Abbas ndio watu wa karibu zaidi kwa Mtume (s.a.w.) kidamu, kwa hivyo wao ndio wenye haki ya kumkosha. 2) Uislamu umefundisha kwamba atakapokufa tu kiongozi wao basi wakutane Waislamu na kumchagua mwengine pasina kuchelewa kama Sayyidna Ali alivyosema: “Kilichowajibu katika hukumu ya Allah na hukumu ya Uislamu kwa Waislamu, baada ya kufa Imamu wao au kuuliwa… wasifanye kitu wala wasizuwe jambo wala wasitangulize mkono wala mguu wala wasianze chochote kabla hawajajichagulia Imamu…”. Na hii ni riwaya ya Kishia. Sasa sijui ni kosa gani walilolifanya wale waliokimbilia katika Saqifa ikiwa hivi ndivyo inavyotakiwa.
|