Tumekwisha kuona ya kuwa Mtume (s.a.w.) aliandika mkataba na Makureshi wasipigane kwa muda wa miaka 10, na vile vile ya kuwa kila mmoja katika wao wasipigane na muitifaki wa mwenziwe. Bani Khuzaa wakawa waitifaki wa Waislamu, na Bani Bakr wakawa waitifaki wa Makureshi.
Baada ya miaka miwili kutimia vilitokea vita baina ya hawa Bani Khuzaa na Bani Bakr. Sababu yake ni hii:- Siku moja kijana wa Bani Bakr alikaa mahali na wenziwe, akawa anakwimba nyimbo za kumtukana Mtume (s.a.w.), na wenziwe wa Kibani Bakr wanacheka, pale pale alitokea kijana wa Kibani Khuzaa akawakuta katika kutukana kwao huko. Kijana huyu akamkataza mwimbaji asiendelee na nyimbo zake hizi za ufidhuli, yule mwimbaji asikubali, bali alimtolea utovu wa adabu mkubwa. Kijana huyu wa Kibani Khuzaa akahamaki, akampiga yule mwimbaji kichwani kwa mkia wa ngamia, kichwa kikapasuka akawa anatoka damu.
Pale pale vikaanguka vita baina ya Bani Khuzaa na Bani Bakr. Baada ya kupigana kwa muda mrefu walitokea mabwana wakubwa wakapatanisha na vita vikanyamaza. Lakini wale Bani Bakr walikubali sulhu ile kwa ncha ya ulimi tu, kwani waliondoka wakubwa wao wakaenda kwa mabwana wa Kikureshi wawaazime silaha, na wawape baadhi ya mashujaa wao wachanganyike nao katika kuwashambulia Bani Khuzaa usiku – bila kuwa na mshindo wowote – Makureshi wakawapa silaha na wakawachagulia wakali katika mashujaa wao wakawapa. Miongoni mwa mashujaa hao ni mabwana hawa:-
Mabwana hawa walijificha kwa Bani Bakr, mpaka usiku wakatoka pamoja nao wakawashambulia Bani Khuzaa kwa ghafla wakawaua watu 23, na wakachukua baadhi ya mali. Bani Khuzaa walikwenda mbio na wake zao na watoto wao mpaka kwenye msikiti wa Makka wakajitia, hapo ndipo walipopata salama.
Asubuhi ilipopambazuka tu alitoka Shairi na mkubwa wa Bani Khuzaa – Bwana Amr bin Salim – pamoja na mabwana wengine 40, wa Kikhuzaa mpaka Madina kwa Mtume (s.a.w.). Akaingia msikitini, akamkuta Mtume (s.a.w.) kakaa na Masahaba wake, akatoa salamu, kisha akasimama akamsemesha Mtume (s.a.w.) kwa mashairi haya.
Rabi ninafikilisha ** Kwa Nabii Muhamadi Kureshi wamepitisha ** Jeuri kubwa ya hadi. Watu wengi wamefisha ** Na mali wamefisidi. Basi tunakukumbusha ** Ahadi tulopeana.
Metwingilia ghafula ** Usiku bila habari. Hawajatupa muhula ** Nasi tukawa tayari. Tukawa hatuna hila ** Ila tulidahadari. Basi tunakukumbusha ** Ahadi tulopeana. . Bwana habari ni hizi ** Bani Khuzaa twalia. Twapukutika machozi ** Kwa yaliyo tufikia. Nawe ndiye mwokozi ** Tumekuja kukwambia. Basi tunakukumbusha ** Ahadi tulopeana.
Mtume (s.a.w.) akawajibu: “Mtanusuriwa, Amr! Mtanusuriwa, Amr!” Pale pale Mtume (s.a.w.) akaamrisha iandaliwe Jihadi kwenda kupigwa Makureshi waliowaua watu 23 katika waitifaki wa Mtume (s.a.w.). Pale pale akawapelekea wajumbe wakubwa wa kabila nyengine za Kiarabu zilizokuwa zimesilimu, ili na wao walete majeshi yao wachanganyike na Muhajir na Ansar. Haukupita muda mrefu ila majeshi ya kabila hizo yalianza kumiminika Madina. Kabila zenyewe ni hizi:-
1. Bani Aslam 2. Bani Ghifar 3. Bani Muzayna. 4. Bani Juhayna. 5. Bani Asad. 6. Bani Sulaym. 7. Bani Kaab.
Hata asubuhi ya Ijumaa mwezi 10 Ramadhan mwaka 8 A.H (January 630.) Mtume (s.a.w.) alitoka kwenda kuipiga Makka na jeshi la watu 10,000. miongoni mwa hao Muhajir walikua 700 na Ansar 4,000 na 5,300 ni katika hayo majeshi ya kabila za Kiarabu zilizokuja kumsaidia Mtume (s.a.w.).
Mtume (s.a.w.) aliyagawa majeshi haya sehemu 4, na kila sehemu ilikuwa na mkubwa wake. Amir jeshi wa Kiansar alikuwa Bwana Saad bin Ubada. Amir wa Kimuhajir alikuwa Bwana Zubeyr bin Al Awwam. Yale majeshi ya Waislamu wengine yaligawika sehemu mbili – sehemu moja ikawa chini ya Bwana Abu Ubayda, sehemu ya pili chini ya Bwana Khalid bin Al Walid .
Njiani Mtume (s.a.w.) alikutana na baadhi ya Makureshi waliokuwa wanahama Makka wanakuja Madina kusilimu. Miongoni mwa hao ni ndugu yake – Bwana Abu Sufyan bin Harith bin Abdul Muttalib – Bwana huyu alikuwa akimtukana mno Mtume (s.a.w.) na Uislamu kwa mashairi yake ya usafihi, lakini Mtume (s.a.w.) akamsamehe yote aliyoyafanya, kwani Uislamu unafuta kila dhambi zilizotangulia[1]. Na miongoni mwa aliyokutana nao ni shemeji yake, na mtoto wa shangazi lake – Bwana Abdalla bin Abi Umayya –. Alikuwa ni ndugu wa Bibi Ummu Salama Hind bint Abi Umayya, ambaye alikuwa katika jeshi hili la kwenda kupiga Makka. Bibi huyu alimwombea sana ndugu yake huyu hata Mtume (s.a.w.) akamwelea radhi.
Bwana huyu alikuwa akimuudhi sana Mtume (s.a.w.) kwa kumtaka – kufundisha watu wengine – wamtake namna kwa namna za miujiza. Miongoni mwa mambo aliyowafundisha watu wamtake Mtume (s.a.w.) ni haya yaliyotajwa katika Sura ya Subhana tangu Aya ya 90 mpaka 93:
{Walisema hatutakuamini mpaka utuchimbulie katika ardhi (yetu hii) chemchem (yenye maji mengi)} (Aya ya 90).
{Au ujipatishie (sasa hivi) bustani ya mitende na mizabibu, uchimbue ndani yake mito kuichimbua }[2] (Aya ya 91).
{Au utuangushie mbingu – kama ulivyodai –vipande vipande, au umlete Mungu na Malaika makundi kwa makundi} (Aya ya 92).
{Au ujipatishie (sasa hivi) nyumba ya dhahabu (tupu) au upande mbinguni, wala hatutasadiki kupanda kwako mpaka utushushie – na huku tunakuona unavyoshuka – daftari (yenye shahada ya Mungu na Malaika wake ya kuwa wewe ni Mtume (s.a.w.) }[3] (Aya ya 93).
Mwisho kabisa alikutana na baba yake mdogo, Bwana Abbas bin Adil Muttalib pamoja na watu wa nyumbani kwake wote. Mtume (s.a.w.) akawaamrisha wanawake na watoto wende Madina na akamchukua baba yake mdogo na kila aliyekuwa mtu mzima, akenda nao Makka.
Hata wakati wa Laasiri walipofika mtaa wa Batn Mar. Mtume (s.a.w.) aliwamrisha wajenge mahema mengi wapumzike hapo usiku kucha. Masahaba wakafanya kama walivyoamrishwa na Mtume (s.a.w.). Hata usiku ulipoingia aliwaamrisha wawashe mioto (nyoto) ili kuwaonyesha Makureshi kuwa wao ni wengi. Bwana Abbas alifanya hofu kubwa na huzuni kubwa juu ya Makureshi kwa kuona jeshi kubwa lile limezatiti barabara. Mshipa wa Kikureshi ukampiga. Akamfikiri rafiki yake Ubu Sufyan bin Harb, na mabwana wengine wa Kikureshi. Mara akamwambia Mtume (s.a.w.): “Ya Rasulallah Makureshi jamaa zako. Jeshi hili likiwavamia litawamaliza wote, hawatakuwapo tena Makureshi. Nakuomba unipe ruhusa nende Makka usiku huu huu nikamchukue mkubw wao, Abu Sufyan ili aje afanye sulhu kabla hamjawashambulia kwa jeshi hili” Mtume (s.a.w.) akampa ruhusa na akampa nyumbu wake mwenyewe aliyekuwa kampanda ampande.
Bwana Abbasa hakuwahi kufika Makka mara alikutana na Abu Sufyan na bwana mwengine aliyekuwa akiitwa Bwana Hakim bin Hizam bin Khuwaylid – mtoto wa kaka yake Bibi Khadija – Bwana Abbas aliwaambia kubwa na dogo la jeshi la Mtume (s.a.w.), na wao wakaona shauri nzuri hiyo ya kusilimu kabla ya kupigana. Mabwana hawa wakafuatana na Bwana Abbas mpaka kwa Mtume (s.a.w.). Mtume (s.a.w.) akamwamrisha Bwana Abbas akalale nao mpaka asubuhi. Asubuhi akaja nao mpaka kwa Mtume (s.a.w.). Mtume (s.a.w.) akamwambia Abu Sufyan: “Ee Abu Sufyan! Bado tu hukwisha kutambua ya kuwa miungu yenu si ya haki?” Akajibu: “Nimekwishajua kwani wangekuwa miungu kweli wengetusaidia leo kumshinda Mungu wako wa haki” Akamwambia tena: “Bado huyakinishi ya kuwa mimi ni Mtume?” Akamwambia: “Ama hili nina shaka nalo bado lakini sasa na tuseme habari ya kusalimu amri kwanza” Mtume (s.a.w.) akamwambia: “Nenda Makka ukanadi kwamba wakati litakapoingia jeshi letu kila atakayekuwa nyumbani kwako au nyumbani kwa Hakim bin Hizam kasalimika, na kila atayeingia nyumbani kwake akafunga mlango kasalimika, na kila atakayekwenda kukaa kwenye msikiti mkubwa wa Makka naye kasalimika pia” Abu Sufyan na Hakim wakaondoka na utumwa huu wakenda zao Makka kuwapasha habari watu wao. Watu wa Makka wakadawaa, wasijue la kufanya, kweli imedhihiri uongo umejitenga.
Hata asubuhi ya Jumaatatu mwezi 20 Ramadhan, Mtume (s.a.w.) aliamrisha jeshi lake liondoke liingie mji wa Makka. Lakini aliwafahamisha majamadari wote barabara ya kuwa wasifanye mapigano yoyote bali waingie kwa salama – pasipo kumfinya hata mtu ukucha wala kuchukua chake – Akamwamrisha jamadari Khalid aingie kwa upande wa Kusini kwa njia inayoitwa Kudaa, na jamadari Saad aingie kwa upande wa Magharibi, na jamadari Abu Ubayda aingie kwa upande wa Mashariki, na yeye na Muhajir na jamadari wao Zubeyr wakaingia kwa upande wa Kaskazini kwa njia inayoitwa Kadaa. Majeshi haya yakaingia mpaka kwenye msikiti wa Makka, pasina jambo lolote kutokea. Lakini Bwana Khalid bin Al Walid alikutana na jeshi la vijana wa Kikureshi waliokataa kusalimu amri. Wakalipinga jeshi lake lisiingie. Basi kwa hivyo wakatiana mikononi. Haikupatikana njia ila walipoua Makureshi 23, na waliosalimu amri wakakimbia.
Mtume (s.a.w.) aliingia mji wa Makka naye yupo juu ya ngamia, na nyuma yake kampandisha mtoto wa huru wake – Bwana Osama bin Zayd bin Haritha – akatufu juu ya ngamia wake yule, na watu wanamfuata. Alipokwisha aliingia yeye na watu wake katika kuyavunja masanamu yaliyokuwa juu ya nje ya Al Kaaba.
Baadaye Mtume (s.a.w.) alimtuma Sahaba mmoja aliyekuwa akiitwa Bwana Uthman bin Talha ende kwa mama yake akachukue ufunguo wa Al Kaaba, kwani ufunguo ulikuwa ukishikwa na watu wa ukoo wao – Ukoo wa Bani Abdid Dar – Bwana huyu alimrai mno mama yake hata akakubali kuutoa kwa salama, kwani mzee huyu alikuwa hakusilimu bado. Ulipoletwa ufunguo, Mtume (s.a.w.) alifungua akaingia ndani ya Al Kaaba akasali rakaa mbili halafu akatoka nje, akasimama juu ya kizingiti cha chini cha Al Kaaba, akahutubu kubainisha amri na makatazo ya dini ya Kiislamu. Kisha akasema: “Enyi Makureshi! Mungu amekwisha kukuondosheeni jeuri za kijinga na kujitapa kwa ajili ya nasaba. Watu wote wanatokana na Adam. Na Adam kaumbwa kwa udongo. Hana fadhila Mwarabu juu ya kuwa Mwarabu wala mwekundu juu ya mweusi, wala mweupe juu ya mwekundu” Kisha akasoma Aya hii ya 13 ya Sura ya 49 (Suratul Hujurat).
{Enyi watu! Hakika sisi tumekuumbeni (nyote) kwa mwanamke na mwanamume na tumekujaalieni mapote[4] (mbali mbali) na kabila (mbali mbali) ili mjuane (tu), (lakini) mtukufu wenu kwa Mungu ni yule anayemcha Mungu zaidi}[5] (Aya ya 13)
Kisha akasema: “Enyi Makureshi, mnaonaje? Mnadhani nitakufanyeni nini leo” Suhayl akajibi: “Tunasema kheri na tunadhani kheri. Wewe ni ndugu mtukufu na mtoto wa ndugu mtukufu” Mtume (s.a.w.) akasema: “Mimi nasema kama alivyosema ndugu yangu Nabii Yusuf: ‘Hapana kulaumiwa leo. Mungu atakughufirieni[6], Inshaallah’ haya nendeni zenu kafanyeni mambo yenu”.
Baada ya kumaliza Mtume (s.a.w.) hutuba yake, Sayyidna Abubakr akenda akamleta baba yake mbele ya Mtume (s.a.w.) ili aje kusilimu naye, Mtume (s.a.w.) akamwambia Sayyidna Abubakr: “Yanini kumtaabisha? Lau ungalinambia kabla ningalikwenda mimi nyumbani kwake” Bwana huyo alikuwa mzee sana wakati huo, kila unywele uliokuwa juu ya mwili wake ulikuwa mweupe. Alipokwisha kusilimu Bwana huyu, Mtume (s.a.w.) alimwita Bwana Uthman bin Abi Talha aliyeleta ufunguo kutoka kwa mama yake. akatwa ule ufunguo wa Al Kaaba akampa akamwambia: “Utwaeni enyi Bani Abdid Dar ufunguo wenu na ukae kwenu, kina Bani Abdid Dar”. Basi mpaka leo hii ufunguo wa Al Kaaba unashikwa na Bani Abdid Dar kama ulivyokuwa kabla ya Uislamu.
Baadaye Mtume (s.a.w.) alikwenda kuwatolea hutba wanawake waliokuwa wamekusanyika mahali pamoja wanamngojea. Mkubwa wa wanawake wote wa Makka wakati huo alikuwa Bibi Hind bint Utba – mke wa bwana mkubwa wa Kikureshi Bwana Abu Sufyan na mama wa Bwana Muawiya bin Abi Sufyan – Bibi huyu alikuwa amejifunika gubi gubi ili asijulikane na Mtume (s.a.w.), kwani alikuwa kafanya mambo mengi mabaya juu ya Waislamu. Moja katika hayo ni kule kumpasua tumbo ami yake – Sayyidna Hamza – na akalitafuna ini lake, kisha akamkata vipande vipande. Mtume (s.a.w.) alianza hutba yake akasema hivi: “Enyi wanawake mliokusanyika hapa. Msiabudu Waungu wengine tena ila Mungu mmoja wa haki” Bibi Hind akajibu: “Hatuna shughuli nao, kwani lau wangekuwa wanafaa kitu wangetufaa leo” Mtume (s.a.w.) akaendelea: “Wala msiibe” Bibi Hind akauliza: “unaonaje? Mwanamke akiwa mumewe bakhili hampi cha kumtosha, ana dhambi akimuibia kidogo? Mtume (s.a.w.) akamjibu la[7]” Kisha akaendelea: “Wala msizini” Bibi Hind akadakiza akasema: “Tangu lini mwanamke muungwana kuzini? Wewe unatukataza tusiyoyafanya”. Mtume (s.a.w.) akaendelea: “Wala msiue watoto wenu”. Bibi Hind akasema: “Lau tungalikuwa tunawaua ungaliwapata wapi wewe kuwaua katika vita vyetu baina yako na sisi?”[8] Mtume (s.a.w.) alipoona mno tena wala hamjui nani alimwambia: “Wewe ni Hind nin?” Bibi Hind akajibu: “Ndiye mimi” Mtume (s.a.w.) akamwambia: “Tumekusamehe yote uliyotufanyia zamani. Yaliyopita yamepita”. Bibi Hind akainuka akasema: “Wallahi! Nimehudhuria hapa, na hapana mtu yoyote ninayemchukia mno ulimwenguni, na ninaye mtakia kila baa imfikie kuliko wewe. Na sasa naondoka hapa, na hapana ninayempenda mno na kumtakia kheri imfike kuliko wewe”.[9] Mtume (s.a.w.) akajibu: “Na kila siku yatazidi mapenzi yako kwetu”. Baada ya hutuba yake hii, wanawake walitawanyika wakenda majumbani mwao.
Mtume (s.a.w.) akaamrisha kujengewa hema zake katika mtaa wa Hajun, hema moja ilikuwa ya mkewe. Bibi Hind bint Umayya na nyengine ya mkewe Bibi Maymuna bint Al Harith, akakaa mahali hapo muda wa siku 18. baadae akaondoka yeye na majeshi yake wakenda zao. Kwa muda huu aliokuwako Makka, kila siku alikuwa akitoa vikosi vya watu kwenda miji iliyokuwa karibu na Makka ili kuvunja masanamu yaliyokuwako huko.
Alipoazimia kuondoka alimchagua awe Liwali wa Makka kijana mdogo mzalendo wa Kibani Umayya alikuwa kasilimu siku zile zile na ambaye alikuwa kijana wa miaka 18 tu. Kijana huyu alikuwa akiitwa Bwana Attab bin Asid bin Abil As bin Umayya, mshahara aliyoahidiwa kupewa na Mtume (s.a.w.) ni dirham 354 kila mwaka, yani dirham moja kila siku (takriban senti 60)[10]. Na akamwacha kijana mmoja wa Kiansar ambaye alikuwa akipata miaka 26 tu ndiye awafundishe dini watu wote waliokuwako Makka. Bwana huyu ingawa alikuwa kijana mdogo, lakini alikuwa hodari mno ajabu, na alikuwa akipendwa sana na Mtume (s.a.w.). Jina lake lilikuwa Bwana Muadh bin Jabal.
[1] - Allah anasema: {قُلْ لِلَّذِينَ كَفَرُوا إِنْ يَنتَهُوا يُغْفَرْ لَهُمْ مَا قَدْ سَلَفَ} (Wambie wale waliokufuru kama wataacha (yale mabaya waliokuwa nayo) watasamehewa yaliopita). Anfal Aya ya 38. Na Mtume (s.a.w.) anasema: "الإسلام جب لما سبق" (Uislamu unakata yote yaliopita). [2] - Na upasue ndani yake mito yenye kububujika (maji) } -[3] وَقَالُوا لَنْ نُؤْمِنَ لَكَ حَتَّى تَفْجُرَ لَنَا مِنْ الأَرْضِ يَنْبُوعاً (90) أَوْ تَكُونَ لَكَ جَنَّةٌ مِنْ نَخِيلٍ وَعِنَبٍ فَتُفَجِّرَ الأَنهَارَ خِلالَهَا تَفْجِيراً (91) أَوْ تُسْقِطَ السَّمَاءَ كَمَا زَعَمْتَ عَلَيْنَا كِسَفاً أَوْ تَأْتِيَ بِاللَّهِ وَالْمَلائِكَةِ قَبِيلاً (92) أَوْ يَكُونَ لَكَ بَيْتٌ مِنْ زُخْرُفٍ أَوْ تَرْقَى فِي السَّمَاءِ وَلَنْ نُؤْمِنَ لِرُقِيِّكَ حَتَّى تُنَزِّلَ عَلَيْنَا كِتَاباً نَقْرَؤُه قُلْ سُبْحَانَ رَبِّي هَلْ كُنتُ إِلاَّ بَشَراً رَسُولاً (93) { [4] - Mataifa. [5] } - يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُمْ مِنْ ذَكَرٍ وَأُنثَى وَجَعَلْنَاكُمْ شُعُوباً وَقَبَائِلَ لِتَعَارَفُوا إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِنْدَ اللَّهِ أَتْقَاكُمْ إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ { [6] - } قَالَ لا تَثْرِيبَ عَلَيْكُمُ الْيَوْمَ يَغْفِرُ اللَّهُ لَكُمْ ...........{ . (92) Surat Yusuf Aya [7]- Wamepokea Imam Bukhari na Muslim Riwaya isemayo: "عَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اللهُ عَنْهَا قَالَتْ: قَالَتْ هِنْدُ امْرَأَةُ أبِيْ سُفْيَانَ لِلنَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: إنَّ أبَا سُفْيَانَ رَجُلٌ شَحِيْحٌ وَلَيْسَ يُعْطِيْنِيْ مَا يَكْفِيْنِيْ وَوَلَدِيْ إلاَّ مَا أَخَذْتُ مِنْهُ وَهُوَ لاَ يَعْلَمُ، قَالَ: خُذِيْ مَا يَكْفِيْكِ وَوَلَدكِ بِالْمَعْرُوْفِ" "Kutoka kwa Aysha (r.a) kasema: kasema Hind mke wa Abu Sufyan kumwambia Mtume (s.a.w): Hakika Abu Sufyan ni mwanamme bakhili, na wala hanipi chenye kunitosha mimi na mwanangu, isipokuwa kile ninachochukua kwake pasina yeye kujua, akasema (Mtume s.a.w): 'Chukua chenye kukutosha wewe na mwanao kwa wema (kadiri ya haja)". [8] - Bali yote alioyakataza Mtume (s.a.w.) hapa yalikuwa yakitendeka kama Qur-ani, Hadithi na historia zinavyonena kwa uwazi. [9] - Tazama jinsi tabia njema zinavyozaa matunda mazuri! [10] - Bila shaka hisabu hii ni kwa mujibu wa reti katika zama za Sheikh Abdallah Saleh Al–Farisi, ama kwa sasa ni tofauti na hivyo. Lakini Sheikh alipokuwa akizungumzia kuhusu "Kuja Madina watu wa Mtume (s.a.w.) na wa Sayyidna Abubakr" alisema kuwa "Dirham 500 ni kiasi cha shilingi 250". Kwa hivyo utakapotazama hesabu hii ya dirham 500 ambazo ni kiasi cha shilingi 250 utona kuwa dirham moja ni sawa na senti 50 (nusu shilingi), ambapo hapa katika hesabu hii ya dirham 354 kasema kuwa kila dirham ni sawa na senti 60. Kwa hivyo, kama hili si kosa la chapa, basi dhahir ni kuwa Sheikh kafanya makadirio tu (rough figure).
|