Tumekwisha kuona kuwa Mtume (s.a.w.) na Masahaba zake walitaabishwa sana katika mji wa Makka, hata ikawapasa katika mwaka wa 5 wa kuja Utume, kwenda nchi ya Mahabushia, na mwaka wa13 kwenda Madina, na mara hii Mtume (s.a.w.) alikuwa pamoja nao. Walitaabishwa kwa kudharauliwa, kwa kuudhiwa, kwa kudhulumiwa mali yao, kwa kupigwa na kwa adhabu nyingi nyinginezo, ambazo nyengine hazifai hata kutajwa hapa, walipokimbia kwenda Madina walikimbia wao tu na baadhi ya nguo zao na vitu vilivyokuwa vyepesi kuchukulika. Ama mali yao yote mengine waliyaacha kuko huko Makka, yakahoziwa na jamaa zao wasiokuwa Waislamu. Hata nyumba alizokuwa akikaa Mtume (s.a.w.) na watu wake pia ziliuzwa.
Walipokimbilia Madina walidhani kuwa watasalimika na mateso na jeuri za Makureshi, waishi maisha ya raha na utulivu, na waabudu Mungu kama wanavyotaka. Lakini wapi! Masahaba hawajakaa siku nyingi Madina ila asubuhi moja waliletewa habari kuwa jana usiku walikuja Makureshi kwenye viunga vya Madina na wamechukuwa kila wanyama waliokuwa huko. Hazikupita siku nyingi sana tena ila waliletewa habari asubuhi nyengine kuwa jeshi la Makureshi jengine lilikuja usiku kwenye viunga vya Madina na likakata mitende yote iliyokuwako huko, likachukuwa kila wanyama waliowapata baada ya kumchinja mchungaji wao na mwenziwe, na baadae wakakiwasha moto kiunga kizima.
Baada ya haya na mengineyo Waislamu walipewa ruhusa nao, kupigana kwa ajili ya kujikinga nafsi zao. Siku moja katika mwezi wa Ramadhan baada ya miezi 19 tangu Mtume (s.a.w.) kuhamia Madina, Mtume (s.a.w.) alipata habari kuwa kuna msafara wa mali mkubwa wa Kikureshi unakuja kutoka Sham, na hauna wa kuulinda ila watu 40 tu, na mkubwa wao ni Abu Sufyan, ambae ndiye aliyekuwa mkubwa siku waliyokuja kwenye viunga vya Madina na wakachukua wanyama na wakamwua mchungaji wao na mwenziwe. Mtume (s.a.w.) aliwahadithia habari hii Masahaba akawaambia: “Kama walivyotuzuilia kwenda Makka na wakatutesa kwa kila namna ya mateso basi na sisi tuwazuilie misafara yao na kupita kwenye mji wetu – Madina –” . Wakamfuata watu 313 – 83 katika Muhajir na waliosalia katika Ansar, wakaondoka Jumaatano mwezi 8 Ramadhan kuufuatia msafara huo. Hawakuwa na wanyama wa kupanda katika msafara wao ila ngamia 76 na farasi 2 tu, wakawa wanapokezana kupanda. Kila ngamia 1 alikuwa na watu wake makhsusi wa kupanda kwa zamu akishuka huyu apande huyu. Ngamia aliyepewa Mtume (s.a.w.) alikuwa apande kwa zamu baina yake na Sayyidna Ali na Bwana Marthad. Ngamia wa Sayyidna Abubakr alikuwa akimpanda kwa zamu baina yake, Sayyidna Umar na Bwana Abdur Rahman bin Auf.
Abu Sufyan kwa ile jeuri yake aliyowafanyia watu wa Madina – aliogopa sana alipokuwa anaikurubia Madina – akaweka majasusi kumsikilizia habari za watu wa Madina, majasusi wake wakamjia wakampa habari kuwa Mtume (s.a.w.) na Masahaba zake wameondoaka Madina ili kuwafuatia wao. Abu Sufyan aliogopa sana, akamkodi Bedui mmoja pale pale aliyehodari kwa kupanda ngamia, ili ende Makka akawete Makureshi waje wahami mali yao ambayo yalikuwa yanapata kiasi cha Paundi 20,000. Alimkodi huyu Bedui kwa Paund 14. Bedui huyu akatoka mbio mpaka Makka hasiti ila kwa dharura kubwa. Kufika tu Makka alipiga kelele juu ya jabali moja kubwa kuwapa habari hiyo Makureshi, Makuresi walifurahi kwani waliona ndio njia ya kwenda kumsaga Mtume (s.a.w.) na watu wake, wasimsaze[1] hata mmoja ili waondoshe kabisa dini aliyokuja nayo.
Kila Kureshi mtukufu alivaa nguo zake za chuma papo hapo, akatoka akasimama kwenye uwanja wa Al Kaaba anangoja wenzake. Hazijapita saa nyingi ila walikuwa wamekwisha kusimamisha jeshi la watu 1,000 na ngamia 700 na farasi 100! Watu 600 katika 1,000 hao walikuwa wamevaa nguo za chuma za vita. Hakusalia mtukufu yoyote katika Makureshi ila alivalia kwenda huko, ili apate hishma ya kumwua Nabii Muhammad (s.a.w.) na Masahaba zake.
Watu 12 katika hao Mabwana wakubwa wa Kikureshi walidhamini kulilisha bure jeshi hilo toka kutoka kwake mpaka kurejea. Waliona kuwa inahitajia kuchinja ngamia 10 kila siku. Miongoni mwa hao walaiodhamini kulilisha jeshi hili ni Bwana Abbas bin Abdul Muttalib – Baba yake mdogo Mtume (s.a.w.) – Utba bin Rabia – babu yake Bwana Muawiya kwa upande wa mama yake – Abu Jahl – Farauni wa Umma huu – na Hakym bin Hizam – mtoto wa ndugu yake Bibi Khadija - .
Hili jeshi la Kikureshi lilipokuwa likiondoka lilichukuwa wanawake wengi waimbaji na wachezaji ili waimbe na wacheze muda wa siku tatu baada ya kuwaua watu wa Nabii Muhammad (s.a.w.) wote na yeye mwenyewe pamoja, na kwa ajili ya kuwazidisha mori hao Makureshi watapokuwa wanapigana, ili wasipate kukimbia vita vitaposhika moto. Makureshi walikuwa na yakini kuwa watashinda, ndio maana wakatoka na shangwe hilo la wanawake.
Makureshi baada ya kuona jeshi lao limekamilika, waliondoka hao wanakwenda upande wa Madina – na bendera yao ya vita kaichukua Bwana Saib bin Yazid – babu wa nne wa Imam Shafi –, kwani alikuwa hakusilimu bado siku hiyo. Mambo yote hayo yaliyotokea Makka. Mtume (s.a.w.) na Masahaba zake hawakuwa na habari nayo wao wakijidhani kuwa wanakwenda kuwazuilia hao watu 40 waliokuwemo katika msafara, basi hawakuwa na habari kuwa Abu Sufyan amekwisha wasikia na amegeuza njia na amepeleka mjumbe kuweta watu wa Makka, na kuwa hao watu wa Makka wako njiani wanakuja kuwapiga kwa jeshi lililokubwa zaidi ya mara tatu kuliko lao. Hawakupata habari hii ila wako karibu na mtaa wa Badr. Pale pale Mtume (s.a.w.) aliwakusanya Masahaba zake akawataka shauri ya kufanya katika 2 haya:-
Wengi waliipenda shauri ya kuufata huo msafara, khalafu wakimbilie Madina wakastarehe, kwani walipoondoka Madina hawajaondoka kwa nia ya vita, kwa hivyo wao hawajavalia kivita. Lakini Mtume (s.a.w.) hakuwafiki rai hii. Aliona kuwa wakifuata msafara halafu jeshi la Makureshi litawafata huko huko, lichanganyike na watu wa msafara lizidi wingi wake. Na aliona vile vile Makureshi watakapokuwa wanapigana na mali yao yako mbele yao watazidi kupata ushujaa, wasikubali kukimbia upesi. Lakini juu ya hayo Masahaba wegine walishika rai yao ile ile. Pale pale aliondoa Sayyidna Abubakr akaitilia nguvu rai ya Mtume (s.a.w.). Kisha akainuka Sayyidna Umar akaitilia nguvu vile vile rai aliyoitoa Mtume (s.a.w.) na Sayyidna Abubakr. Baadae akaondoka Sahaba mmoja aliyekuwa akiitwa Bwana Miqdad akasema: “Ee Mtume wa Mwenyezi Mungu! Fanya shauri unayoiona sisi sote tuko pamoja nawe. Wallahi hatutasema kama walivyosema Mayahudi kumwambia Nabii Musa, ‘Nenda wewe na Mungu wako mkapigane, na sisi tutakaa hapa kukungojeni’ Lakini sisi Waislamu tutasema: ‘Nenda wewe na Malaika wa Mola wako mpigane na makafiri, na sisi tutakuwa mkono mmoja na nyinyi katika kupigana nao!’”. Mtume (s.a.w.) alifurahi sana na maneno yake na akamwombea dua. Lakini Mtume (s.a.w.) hakutoa amri yake vile vile, kwani alikuwa hataki kufanya jambo ila kwa radhi ya Masahaba zake wote, walio Muhajir na Ansar. Wote hawa watatu waliosema hapa ni Muhajir. Pale pale aliinuka Bwana mkubwa wa Kiansar – Bwana Saad bin Muadh – akamwambia Mtume (s.a.w.): “Ee Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Sisi sote tumekuamini, na tunakusadiki kuwa kila unalotwambia ni haki, basi fanya kama unavyoona wewe. Sisi tuko tayari kukufuata, hata lau ungelijitumbukiza ndani ya bahari ukawa uanaivuka kwa miguu tungevuka pamoja nawe, asingesalia yoyote”. Hapo Mtume (s.a.w.) ndipo alipowaamrisha waifuate njia wanayotokea Makureshi.
Waislamu wakenda mpaka kwenye mtaa wa Badr. Wakatua hapo penye visima vya maji. Ikawa maji yote ya mtaa ule wanayo wao. Tena Masahaba wakamjengea Mtume (s.a.w.) kiriri ambacho ataweza kuwamo humo aone vipi vita vinapiganwa, na aweze kuashiria kwa amri zake wakati wa vita. Hata wakati wa usiku Mtume (s.a.w.) akapanda kwenye kiriri yeye na Sayyidna Abubakr. Usiku kucha Mtume (s.a.w.) alisimama kusali na kuomba dua wapate kushinda. Akisujudu sijda ndefu ndefu huku anaomba dua.
Masahaba wengine walilala chini karibu na kiriri hiki. Hata asubuhi baada ya kusali wakaliona hilo jeshi la Makureshi linakuja, lakini limepungua baadhi ya watu wake. Mtume (s.a.w.) alisimama akaelekea kibla akamwomba Mungu akasema: “Hawa Makureshi wanakuja na mafarasi wao na jeuri yao, wanakuja ili waniangamize mimi na hawa watu wachache wanaokuabudu! Naomba unipe leo ile nusura uliyonambia kuwa utanipa”. Aidha aliomba dua nyenginezo, na Sayyidna Abubakr akiitikia “Amin”
Jeshi la Makureshi lilikuwa limepungua kidogo wakati huu, na sababu ya kupungua kwake ni: Abu Syfyan – alipojua njia anayopita Mtume (s.a.w.) na Masahaba zake – aligeuza njia nyengine na akasalimika na mali yote kamili. Alipoona hivi aliwapelekea mjumbe wakuu wa jeshi la Makureshi, kuwataka warejee na jeshi lao, kwani wo wametoka kuyahami mali yao ambayo yamekwisha kusalimika. Basi nini faida ya kupigana? Wakubwa wote wa kabila za Kikureshi hawajakubali shauri hii ya Abu Sufyan, wakakataa kurejea wakawa hao wanakwenda zao Badr. Mkubwa wa Bani Zuhra tu ndiye aliyekubali, akarejea yeye na watu wake wote, ndiyo maana ikawa wakati huu lile jeshi la Kikureshi limepungua kidogo. Ukoo wa Bani Zuhra ndio ukoo wa mama yake Mtume (s.a.w.), na vile vile ukoo wa Bani Adiy ulirejea – ukoo wa Sayyidna Umar – .
Makureshi walipokaribiana na Waislamu wakaona maji yao, walikuja mbio ili kuyateka wanywe, Masahaba wakataka kuwazuilia lakini Mtume (s.a.w.) aliwakataza. Baada ya kukabiliana hivi, mtoto wa ndugu yake Bibi Khadija anayeitwa Bwana Hakim bin Hizam, ambaye ni mmoja katika wale Makureshi waliodhamini kulisha jeshi lao, aliondoka akamwendea Utba bin Rabia, aliyekuwa mtukufu kuliko Makureshi wote waliokuwa Makka siku hizo. Akamwomba awatie maneno Makureshi warejee kwao wasipigane na Nabii Muhammad, kwani wote ni wenyewe kwa wenyewe. Utba akainuka akasema: “Enyi Makureshi! Na turejee tusipigane na Muhammad, kwani tukiwashinda tukawaua, hapana mmoja katika sisi atakayeweza kumnyanyulia jicho mwenzake kumtazama, kwani kila mmoja katika sisi atakuwa kamwua mtoto wa mwenziwe au baba yake au mjomba wake au bin ami yake, basi shauri yangu mie ni kurejea na kuwaachia Waarabu wengine wawaue. Na lawama yote ya kurejea leo nirejeshewe mimi. Semeni kuwa mimi ni mwoga, nimekurejesheni baada ya kuwa mko tayari kuwasagasaga” Pale pale akainuka Abu Jahal akawakataza Makureshi kufuata shauri ya Utba. Alisema: “Mwongo huyo anaogopa mwanawe tu aliyopo upande wa Muhammad asiuliwe. Haogopi watu wengine, haturejei popote baada ya kufika hapa. Tutawapiga sasa hivi tuwachinjechinje tufanye karamu tuimbe na tucheze hapa kwenye mtaa wa Badr muda wa siku tatu mpaka Waarabu wote wapate habari ya ushujaa wetu”.
Baada ya kuinuka huyu Abu Jahl na kuvunja ile rai ya Utba, watu wote walimfuata Abu Jahl, ikawa hapana chochote ila vita tu. Dasturi ya Waarabu walipokuwa wakipigana, kwanza hupigana mmoja mmoja. Hutoka mkubwa wa upande huu na wa upande huu wakapigana kwa panga, hata mmoja akimwua mwenziwe ndipo vita vinapoumana ikawa mpata mpatae. Ilivyokuwa hii ndio dasturi yao, basi alitoka kwenye jeshi la Makureshi Utba bin Rabia bin Abdi Shams bin Abd Manaf, na ndugu yake Shayba bin Rabia – na mwanawe – Walid bin Utba, wakasimama juu ya mafarasi wao mbele ya jeshi la Waislamu, kungoja mashujaa wa Kiislamu nao watoke kupigana nao, wakatoka vijana watatu wa Kiansar kukabiliana nao, lakini wale mabwana wakubwa wa Kikureshi walikataa kupigana nao wakasema: “Hutuwataki ila Makureshi wenzetu” wakampigia kelele Mtume (s.a.w.) ili awape Makureshi watatu wenye utukufu kama wao, Mtume (s.a.w.) akamtoa Bwana Ubeyda bin Harith bin Muttalib bin Abd Manaf, apigane na Utba, akamtoa Bwana Hamza bin Abdul Muttalib bin Hashim bin Abd Manaf, apigane na Shayba na akamtoa Sayyidna Ali bin Abi Talib bin Abdul Muttalib bin Hashim bin Abd Manaf, apigane na Walid bin Utba – mtoto mwenziwe –. Wote hawa watatu waliotoka upande wa Waislamu walikuwa jamaa zake Mtume (s.a.w.) khasa.
Bwana Hamza hakuchukua muda ila alimwua Shayba, vile vile Sayyidna Ali hakuchukua muda ila alimwua Walid. Ama Bwana Ubeyda na Utba panga zao zilikwenda sawa sawa, kila mmoja alimpiga mwenziwe dharba ya kumwua, Utba alimalizwa pale pale, na Bwana Ubeyda akafa njiani walipokuwa wakirejea kwao Madina. Makureshi – kuona wakubwa wao wamekufa mara moja – walivunjika moyo sana wakaona kuwa hiyo ni dalili mbaya kwa upande wao. Lakini waliinuka hivyo hivyo kupigana ijapokuwa wana khofu, wala hawakuwa wakipigana mmoja mmoja sasa, bali ilikuwa ovyo ovyo aliyekukabili ndiye wako.
Mtume (s.a.w.) baada ya kuwaambia maneno mazuri Masahaba, na baada ya kuwatia moyo alipanda juu ya kiriri chake, akakaa huko yeye na Sayyidna Abubakr, huku anaomba Mungu na Sayyuidna Abubakr anaitikia, kwenye mlango wa kile kiriri alisimama Bwana Saad bin Muadh pamoja na vijana wa Kiansar ili kuwazuilia maadui wasimfikilie Mtume (s.a.w.). Masahaba walipigana kwa ushujaa mkubwa sana na wakaua idadi kubwa ya Makureshi, ingawa wao Masahaba walikuwa kidogo mara tatu kuliko hao Makureshi. Hata wakati wa adhuhuri Mtume (s.a.w.) aliletewa Wahyi kuwa sasa hivi Masahaba watashinda, wawaendeshe mbio Makureshi, na akaamrishwa achukue gao la mchanga, alimwaiye lile jeshi la Makureshi, na huku anaomba dua. Mtume (s.a.w.) pale pale alichukua gao hilo akalisukumiza kwenye jeshi la makureshi, na huku akisema: “Nazidhalilike nyuso hizi Inshaallah”. Halikusalia jicho la yoyote katika wale ila liliingiwa na mchanga huo, likawa linawasha kama pilipili, kila mmoja asijijue ikawa anaania jicho lake tu, basi wakawaua kama vikuku, na wakawa wanakimbizana mbio kama vibuzi, na huku wanakamatwa na Waislamu na kufungwa kamba. Waliosalimika hawakusimama, walikwenda mbio mpaka kwao. Mwenyezi Mungu anasema katika Sura ya 8 (Suratul Anfal) Aya ya 17:
{Siye wewe uliyewamwaia (mchanga), wakati ulipowamwaia, lakini Menyezi Munghu ndiye aliyewamwaia}
Baada ya Makureshi kwenda zao Mtume (s.a.w.) aliwaamrisha Masahaba zake wahisabu mateka na wafu wa maadui zao, wakaona kuwa mateka walikuwa 70, na wafu 70. Ama katika Waislamu walikufa 14 tu – 6 katika Muhajir na 8 katika Ansar –. Walivyokuwa hawa maiti wa Makureshi ni wengi, na Masahaba wamechoka sana na itakuwa taabu juu yao kuchimba makaburi 70, Mtume (s.a.w.) aliamrisha wachukuliwe wote hao maiti 70 watiwe kwenye kisima kimoja, kisha kifukiwe. Mtume (s.a.w.) akasimama kutazama, na Masahaba wakawa wanawatia mmoja mmoja. Kila mmoja akitiwa Mtume (s.a.w.) akiwaambia Ansar: “Huyu ndiye fulani”. Kwani baadhi ya vijana wa Kiansar hawakuwa wakiwajua baadhi ya mabwana wa Kikureshi.
Huu ni muujiza kuwa watu 300 waliwashinda barabara watu wanaokaribia elfu, na wakawaulia watu 70 wao na wakawapokonya watu 70. Lakini ukisha kuisoma Aya ya 17 ya Sura ya 8 (Suratul Anfal), na ukajua maana yake, itakuondoke ajabu hiyo yote, Mungu anasema:
{Siyo nyinyi mliowaua, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaua}[2]
Baada ya kwisha kumalizwa kutiwa kisimani. Mtume (s.a.w.) alisimama kwenye ukingo wa kile kisima akawa anaweta mmoja mmoja kwa majina yao. Alikuwa akisema hivi: “Utba! Shayba! Walid bin Utba!” Na kadhalika “Mmekwisha yakinisha kuwa yale niliyokuwa nikikwambieni kuwa ni kweli? Ama sisi tumekwisha kuona kuwa ni kweli” Sayyidna Umar alimwambia Mtume (s.a.w.): “Unawasemesha maiti?” Mtume (s.a.w.) akamwambia: “Hamkuwa nyinyi mnasikia zaidi kuliko wao, wanasikia kila ninalowaambia lakini hawawezi kusema tu[3]”
Alipokwisha kusema maneno haya, Mtume (s.a.w.) aliletewa habari kuwa Bwana Abu Hudhayfa bin Utba amekaa kwa unyonge, na kuwa labda kwa ajili ya kusimangwa baba yake pamoja na wale maiti wengine wa Kikureshi waliosimangwa. Mtume (s.a.w.) akamwita Bwana Abu Hudhayfa akamwambia yale maneno aliyoyasikia. Bwana Abu Hudhayfa akamjibu akamwambia: “La! mimi sikukasirika kwa kusikia baba yangu na ndugu yangu na ami yangu wakisimangwa. Lakini nasikitika kumwona baba yangu kafa katika ukafiri. Nalikuwa nikidhani kuwa hapana katika wakubwa wa Kikureshi mwenye akili kuliko yeye, kwa hivyo nikitaraji kuwa mwisho wake lazima atasilimu, akili yake kubwa itamwonyesha ukweli wa dini ya Kiislamu na upotofu wa dini ya masanamu. Lakini leo nimekwisha kukata tamaa. Hasha! Mimi sitawaonea uchungu makafiri waliotufanya yale” Siku hiyo ya vita vya Badr Masahaba walisahau nasaba zao, ujamaa ulikuwa wa dini tu. Hata baadhi ya Masahaba walipigana na baba zao au ndugu zao au watoto wao, na wengine waliwaua khasa.
Baada ya haya Mtume (s.a.w.) na Masahaba zake wakaondoka kwenda Madina pamoja na mateka wao 70. Walipofika Madina Mtume (s.a.w.) aliwataka shauri Masahaba nini wafanye juu ya mateka hao, Sayyidna Abubakr akambwambia Mtume (s.a.w.): “Hawa ni ndugu zako na labda Mungu atawaongoa siku zizi hizi za karibu, basi mimi naona bora kuwatoza kila mmoja kikomboleo makhsusi, khalafu muwaache wende zao.” Sayyidna Umar akamwambia Mtume (s.a.w.): “Shauri iliyobora ni kuwachinja wote” Mwamrishe ami yako Hamza amchinje ndugu yake – Abbas bin Abdul Muttalib – umwambie ndugu yako Ali amchinje kaka yake – Aqil bin Abi Talib – na kila mtu umwamrishe amchinje jamaa yake”. Mtume (s.a.w.) akafuata shauri ya Sayyidna Abubakr, na akamwambia: “Wewe Abubakr unamshabihi Nabii Ibrahim na Nabii Isa katika upole wao, na wewe Umar unamshabihi Nabii Nuh na Nabii Musa katika ukali wao”.
Tena Mtume (s.a.w.) akamtajia kila mmoja katika mateka kiasi cha fedha zinazompasa kutoa ili aachiwe kwenda zake. Ama waliokuwa maskini na hawana cha kujikombolea – wakawa wanajua kuandika – kila mmoja alipewa watu 10 kuwafundisha kuandika, wakisha kujua wende zao, na wale ambao walikuwa maskini na wala hawajui kuandika Mtume (s.a.w.) aliwapa ruhusa vivi hivi wende zao.
Mtume (s.a.w.) alimwambia kila Sahaba anayejiweza amchukuwe mmoja katika hao mateka akakae naye kwake kwa kula na kunywa mpaka waje watu wake wamkomboe. Masahaba hawa waliwatazama vizuri wageni wao hata wenyewe wale mateka yakawajia mapenzi ya kuipenda dini hii ya Kiislamu, na siku zile zile wakaingia, miongoni mwao alikuwa Bwana Abbas bin Abdul Muttalib, Bwana Aqil bin Abi Talib, Bwana Saib bin Yazid, Bwana Shafi bin Saib, hawa wawili wa mwisho ni mababu wa Imam Shafi.
Katika mateka wa siku hiyo alikuweko mkwewe Mtume (s.a.w.) kwa mwanawe mkubwa Bibi Zaynab. Bwana huyu alimzuilia huyu Bibi Zaynab kumfuata baba yake kwenda Madina. Basi alipotekwa Mtume (s.a.w.) alimwambia: “Kikomboleo chako ni kumleta mwanangu. Basi umekubali kuchukua ahadi ya kwenda Makka ya kumleta mwanangu?” Yule bwana akatoa ahadi na Mtume (s.a.w.) akamwachia ende zake Makka. Alipofika huko alimfanyia safari nzuri mkewe na akampa mtu wa kufuatana naye mpaka Madina. Lakini njiani walipingwa na Makureshi. Wakamtaabisha yule bibi sana mpaka akaanguka juu ya ngamia aliyekuwa kampanda.
Makureshi walijizuilia siku nyingi na kuja kuwakomboa watu wao, kwa ajili wakiona udhalilifu kufanya hayo. Lakini khatimaye walikuja kuwakomboa. Waislamu walipata kiasi cha shillingi 10,000 katika vikombolea hivyo, wakazitumia katika kununulia silaha na kwa mambo mengine. Makureshi walivunjika sana kwa vita hivi na wakauchukia zaidi Uislamu, wakatia niya mwaka wa pili kuja na jeshi kubwa zaidi mara 3 kuliko hili, ili walipize kisasi. Kwa hivyo walimlazimisha kila tajiri katika matajiri wao atoe kitu kikubwa katika kutengeneza hivyo vita.
Tangu siku hii ndipo alipopata ukubwa Abu Sufyan – baba yake Bwana Muawiya – na wengineo waliokuwa wadogo zamani, kwani wakubwa wao wote waliuawa siku ya vita vya Badr. Hata Shairi wao mmoja aliwatukana hawa wakubwa wapya akasema hivi:-
Sasa mekuwa wakubwa * Ambao wasingekuwa Wamepata unasaba * Taadhima na murua Lau kuwa si misiba * Ya Badr kuingia Wasingeonja ukubwa * Licha kututawaliya.
Vita vya Badr vilipiganwa mwezi 17 Ramadhan 2 A.H. – January 624 –.
[1] - Wasimbakishe. [2] - { فَلَمْ تَقْتُلُوهُمْ وَلَكِنَّ اللَّهَ قَتَلَهُمْ} [3] - Baadhi ya watu huitumia Hadithi hii kwa kumpa mawaidha maiti wakati wa kuzikwa, na kwa hivyo utawaona wanamwambia maiti kuwa: “Ukiulizwa Mola wako nani, sema Allah; Mtume wako nani, sema Muhammad; Kitabu chako gani, sema Qur-an…” na mfano wa hayo. Lakini watu hawa hawakujikalifisha na kuitupia macho Qurani, kwani kama anavyosema Allah katika Surat Yasin Aya ya 70 kuwa Qur-an unaweza kumuonya kwayo yule aliyehai na akaonyeka: sio mfu. Basi ndipo akasema vile vile kumsikilizisha maiti mawaidha hakumfai kitu, pale aliposema katika Suratl Naml Aya ya 80 na Surat Rum Aya ya 52 kuwa: {إِنَّكَ لا تُسْمِعُ الْمَوْتَى... } (Kwa hakika huwezi kuwasikilizisha wafu (mwito wako)…). Na Aya 22 Surat Fatir isemayo: { وَمَا أَنْتَ بِمُسْمِعٍ مَنْ فِي الْقُبُورِ } (…Na wewe huwezi kuwasikilizisha waliomo makaburini). Ingawa Aya hizi si maandiko ya wazi katika maudhui hii, lakini ndani yake kuna dalili kwamba maiti hafaliwi tena na wito wowote ule, inayomfaa ni: amali yake ndio msingi, kisha dua za Waislamu, au sadakat jariya kama kaiwacha ikiwemo elimu inayowafaa watu. Na hivi ndivyo Mtume (s.a.w.) alivyofundisha.
|