Published By Said Al Habsy  1. Kurz bin Jabir: Bwana mkubwa wa Kikureshi. Alikuja kwa siri yeye na baadhi ya wenzake mpaka kwenye viunga vya Madina wakawakamata ngamia, mbuzi na kondoo wote waliowakuta, wakakimbia nao mpaka Makka.
2. Abu Sufyan: Bwana mkubwa kabisa wa Kikureshi. Alikuja na watu 200 wa Kikureshi wakashuka kwenye viwanja vya Madina, wakatia moto mkubwa, wakawaua Masahaba wawili, na wakachukua kila wanyama waliowapata, nao ni ngamia 200.
3. Huyu huyu Abu Sufyan alimpeleka shujaa mkubwa Madina kwa siri ili amuuwe Mtume (s.a.w.), lakini hakupata nafasi hata chembe. Akakata tamaa akarejea.
4. Wakubwa wa Bani Lihyan, na wa Bani Adhl na wa Bani Qara, walikuja kwa Mtume (s.a.w.) wakataka awape baadhi ya Masahaba wende wakawafundishe dini, kwani wanatumai kuwa watu wao watasilimu. Mtume (s.a.w.) akawapa watu 6. Walipofika nao waliwageukia wakawatatiza makamba ili kwenda kuwauza Makka kwa Makureshi wapate kuwachinja wakate hamu yao. Wane katika hao walifanya ukaidi kwenda wakawaua papo hapo, na wawili walisalimu amri wakenda nao Makka wakawauza, na huko wakawaua na wakasulubiwa kwa shangwe kubwa.
5. Amr bin Malik: Bwana mkubwa kabisa wa Kibani Amr. Alisilimu akataka kwa Mtume (s.a.w.) ampe watu 70 kwenda kuyafundisha matumbo yote ya kabila yake kubwa dini hiyo ya Kiislamu. Mtume (s.a.w.) alifurahi, akachagua watu 70 mahodari kwa dini kwenda huko, mmoja katika 70 hao alikuwa Bwana Amr bin Fuhyra – yule mtumwa wa Sayyidna Abubakr amaye alikuwa akiwaletea maziwa pangoni – Huyu Bwana Amr bin Malik alisalia kwa Mtume (s.a.w.) na akawapa Masahaba hawa 70 barua wamfikishie mtoto wa ndugu yake Amr bin Tufayl bin Malik. Bwana huyu alipoipata barua hii hakuifuata hata chembe, bali aliamrisha matumbo matatu ya Kibani Sulaym yawaue watu hao wote, matumbo hayo yakawazunguka mara moja, yakawachinja kama kuku.
6. Uyayna bin Hisn: Mkubwa wa Bani Fazara wote. Alikuja na watu 40, juu ya farasi mpaka kwenye viunga vya Madina, wakachukua ngamia 40, wakamwua mlindaji na wakamchukua mkewe – Bibi Leyla – Walimchukua mwanamke huyu mpaka kwao Najd, wakamfanya mchungaji wanyama. Mwisho bibi huyu alipata nafasi akakimbia akaja zake kwa Mtume (s.a.w.) .
7. Watu wanane katika Bani Uql na Bani Urayna walikuja kwa Mtume (s.a.w.) wakajidai kusilimu, wakamwomba Mtume (s.a.w.) wakae huko huko Madina, Mtume (s.a.w.) akawapa ruhusa. Mwisho wakashikwa na ugonjwa wakadhoofika sana, Mtume (s.a.w.) akawaambia wende kwenye viunga vya Madina kwa mchungaji mmoja wa ngamia wa Zakaa. Alikuwa akiitwa Bwana Yasr, naye atakuwa akiwapa maziwa kunywa asubuhi na jioni mpaka wapate uzima warejee Madina. Wakenda huko na yule mchungaji akawapokea kwa uzuri, akawa anawafanyia kama alivyosema Mtume (s.a.w.). Lakini walipopata uzima kidogo tu walimkamata huyu mchungaji miguu na mikono, wakamtoboa macho yote mawili, wakamtoboatoboa ulimi wake kwa miba, na wakamkata viungo vyake vyengine visivyopendezwa kutajwa vitabuni. Baada ya haya wakawachukua ngamia wote hao wakenda nao kwao kwa jamaa zao. Kiunga hiki kilikuwa meli 6 toka mji wa Madina.
8. Habbar bin Aswad na Nafii bin Qays: Mabwana wakubwa wa Kikureshi. Walimchochachocha mikuki Bibi Zaynab bint Nabii Muhammad (s.a.w.) alipokuwa anahama kwenda Madina kwa baba yake, na wakamchochachocha ngamia aliyempanda pia, mpaka akafanya machachari akamwangusha huyu bibi, naye alikuwa na mimba, akaumia sana, akawa mgonjwa siku zote hata ndiyo ikawa sababu ya kufa kwake.
9. Shurahbil bin Amr: Jamaa yake Harith bin Abi Shamir Al Ghassany, Mfalme wa nchi ya Sham. Shurahbil huyu alimwua bure mjumbe wa Mtume (s.a.w.) aliyepewa barua kumletea huyo Mfalme wa Sham. Na mengi mengineyo ambayo yatachukua nafasi kubwa ukitaka kuyaandika. Lakini haya yaliyotajwa yanatosha kuyakinisha uhaki wa Waislamu katika kupigana na hao waliokuwa wakiwatesa kila walipokuwa wanakimbilia. |