Published By Said Al Habsy  Tumekwisha kuona kuwa Makureshi walifanya mkutano kwenye nyumba yao ya shauri siku ya Jumaamosi mwezi 25 Mfunguo tano, na wakapatana wakamwue Mtume (s.a.w.) usiku wa Ijumaa, mwezi mosi au mwezi pili Mfunguo sita. Na tumekwisha kuona vile vile kuwa Mtume (s.a.w.) alipewa habari hii, naye akamjuvya Sayyidna Abubakr na akaagana naye kuwa atampitia kadiri ya usiku wa saa nane ili wafuatane wende Madina.
Usiku ulipoingia barabara – na watu wakawa hawaonekani tena kupita njiani – wale vijana wa Kikureshi waliochaguliwa kumwua Mtume (s.a.w.) walikuja kwa umoja wao nyumbani kwa Mtume (s.a.w.) na wakaizunguka nyumba hiyo “darmadar”. Baada ya muda mdogo kupita tangu kuja kwao, baadhi yao waliparamia nyumba ile ili wapindukie kwa upande wa uani. Kiasi cha kutokeza nyuso zao tu mara walionekana na wanawake waliokuwemo nyumbani kwa Mtume (s.a.w.), na wakaanza kupiga kelele za khofu, walipoona kuwa wenye nyumba hawajalala bado, walishuka upesi wakajificha, wakingojea wayakinishe kuwa wote wamelala. Katika kungoja kwao kule mara Mungu aliwaletea usingizi mkubwa ukawachukua moja kwa moja.
Muda wote huu Mtume (s.a.w.) alikuwa yu macho, akingojea saa zake zitimie atoke. Hata zilipotimia alimwamsha Sayyidna Ali akamjuvya kuwa anaondoka, alipofika nje aliwakuta wale vijana wa Kikureshi wakukuu katika usingizi, wanaukoromea tu, Mtume (s.a.w.) akachukua ukofi mzima wa mchanga akawa anawanyunyizia nao na huku anasoma sura ya “Yasin” na huku anakwenda zake, alifika nyumbani kwa Sayyidna Abubakr akamkuta tayari anamgojea, wakashika njia wakenda zao.
Waliacha njia ya kaskazini ambayo walijua kuwa watafuatwa kwa njia hiyo, wakashika njia ya kusini mpaka kwenye Ghar Thaur, pango liliyopo kwenye jabali liliyoko kiasi ya meli 2 kusini ya Makka, walipofika pango hili Sayyidna Abubakr ndiye aliyeingia mbele ili kutazama kama hapana cha kudhuru, akaziba kila matundu yaliyokuwa wazi, tena ndipo alipomwambia Mtume (s.a.w.) aingie.
Huko Makka wale Makureshi wakaamka, wakajiona kuwa wana mchanga kichwani na mlango wa Mtume (s.a.w.) ulipofunguliwa wakamwona Sayyidna Ali tu ndani, hayupo Mtume (s.a.w.), pale pale Makureshi wakatawanyika njia zote kumtafuta. Lakini kwanza walikwenda nyumbani kwa Sayyidna Abubakr, wakamkuta Bibi Asmaa, Abu Jahl akamwuliza: “Kenda wapi baba yako?” Alipomwambia kuwa hajui kenda wapi alimzaba kofi la uso, hata vipuli vyake (ear rings) vikadondoka, na uso ukamwiva mwekunduu! Walivyokuwa hawakupata bado jawabu ya kuweza kuwaonyesha alipo Mtume (s.a.w.), walimkodi Bedui mmoja aliyekuwa hodari wa kufata nyayo za mwenye kutafutwa aliyekuwa akiitwa Abu Kurz Al Khuzai, wakatoka wote nyuma yake, wakikagua Makka yote, mwisho wake aliweza kutambua njia yake, wakaingia kuitafuta kwa hadhari kubwa hata wakapanda juu ya lile jabali ambalo ndani yake ndimo lilipokuwamo lile pango alilojificha Mtume (s.a.w.). Walipofika hapo juu yule mfuata njia akawambia: “Sasa alama ya njia yake imekatika lazima yumo ndani ya pango lile” akawaashiria kwenye pango lililokuwa kiasi cha futi 40 na walipo wao. Vijana vya Kikureshi walipotaka kuliparamia. Umayya bin Khalaf mmoja katika mabwana wakubwa wa Kikureshi, aliwapigia kelele za ukali, akawaambia: “Hamna akili nyinyi kama huyu tuliyepoteza pesa zote kwa kumkodi? Vipi mtu ataweza kupita katika pango lile pasi na kuharibu utando wa mabuibui wale waliotanda pango lote? Au vipi njiwa wataweza kukaa pale na kulalia mayai yao ikiwa pana mtu ndani ya pango lile? Wallahi! Mabuibui wamelitumia pango hili kwa kutandia kabla ya kuzaliwa yeye Muhammad. Hajui chochote mfuataji huyu” wakashika njia wakenda zao.
Mabuibui hawa na njiwa wale hawajakuwapo zamani, kama alivyodai Umayya, bali wote walikuja alfajiri ya siku ile, ili wapate kuwaziba macho Makureshi, wasimwone Mtume (s.a.w.) na Sayyidna Abubakr.
Walipokata tamaa kuwa hawataweza kumwona katika viunga vya Makka, Makureshi walizialikia kabila nyengine kuwa yoyote atakayemleta Nabii Muhammad (s.a.w.) ijapokuwa kesha kumwua atapata zawadi ya ngamia 100. Nabii Muhammad na Sayyidna Abubakr walisalia katika pango muda wa siku 3 – Ijumaa, Jumaamosi na Jumaapili – na kila usiku akiwajia Bibi Asmaa na chakula, Bwana Abdalla na habari zote za Makureshi, na Bwana Amir bin Fuhayra na mbuzi wake usiku na alfajiri, ili awakamie maziwa wanywe.
Usiku wa Jumaatatu ulipoingia barabara alikuja Bibi Asmaa na vyakula vya kuchukua njiani mpaka Madina, akaja Bwana Amir bin Fuhayra na ngamia wawili aliowanunua Sayyidna Abubakr kwa ajili ya kupanda yeye na Mtume (s.a.w.) – mmoja wake na mmoja wa Mtume (s.a.w.) – na akaja yule Bedui waliomkodi kuwapeleka Madina kwa njia za ndani ndani. Jina la bwana wa Kibedui huyo lilikuwa Bwana Abdalla bin Arkat, na vile vile alikuwa akiitwa Bwana Abdalla bin Uraykit.
Baada ya hapo walipanda ngamia wao wakashika njia wakenda zao Madina, na Bibi Asmaa akarejea Makka, katika wale ngamia wawili mmoja alipandwa na Sayyidna Abubakr, na nyuma yake yule Bwana Amir bin Fuhayra. Yule Bedui alimpanda ngamia wake mwenyewe, waliacha njia inayopitwa na misafara, wakashika njia ya pwani, hata siku ya Jumaatano mchana, wakafika mahala panapoitwa Qudayd, kwa muda wa siku mbili walikuwa hawakuonja maziwa ya mbuzi, kwa hivyo walikuwa wakiyatamani sana. Hapo Qudayd walimkuta Bibi mmoja amekaa kwenye hema yake. Bibi huyu alikuwa mashuhuri sana kwa ukarimu wake aliokuwa akiwafanyia kila waliokuwa wakimpitia kwenye hema hiyo na kwa kufanya biashara pia.
Mtume (s.a.w.) na wenziwe walishuka hapo, na wakamtolea salamu bibi huyu na wakamtaka awagawie maziwa kidogo au awauzie ili wakate hamu yao. Yule bibi alisikitika sana akawaambia: “Hapana chembe ya maziwa nyumbani kwetu leo, wala hapana mbuzi wa kukama hapa. Mbuzi wote wamekwenda machungani. Tena siku hizi ni za taabu kubwa, majani yamekuwa haba kwetu kwa ajili ya uchache wa mvua, kwa hivyo hatuwezi kupata maziwa ila machache tu ambayo hayatutoshi hata sisi wenyewe, seuze kusalia na kuwapa wapita njia. Tunasikitika kupita watu watukufu kama nyinyi, nasi tukawa hatuna cha kukupeni” Mtume (s.a.w.) alitupa jicho upenuni mwa hema ya yule bibi, akaona kibuzi kidogo king’onda kimesimama kinasinzia kwa ugonjwa. Akamwambia yule bibi: “Si yule mbuzi yupo upenuni pale? Kwanini hatukamii maziwa yake? sisi tutakupa pesa utakazo” Akamjibu: “Wanangu! Mimi sitaki kukukhinisheni maziwa, bure ningekupeni licha kuwa mtanipa pesa, lakini mbuzi yule mnayemwona ni king’onda na mwenye ukurutu tangu kichwani mpaka miguuni, na viwele vyake ni vikavu kuliko kiriba kikavu. Hatoi tone moja la maziwa, hawezi hata kuwafuata wenziwe machungani kwa ajili ya ung’onda wake. Mwendo wake ni wa ‘tata miguu mipya’ tu”. Mtume (s.a.w.) akamwambia: “Utanipa ruhusa nimkame nitazame bahati yangu?” Akamjibu: “Kama utaweza kupata kitu mkame”
Mtume (s.a.w.) akamvuta yule mbuzi akamtoa uwanjani, akavipapasa viwele vyake, na huku anapiga Bismillahi. Muda si muda viwele vilionekana vimejaa maziwa na vimevimba, huneni viwele vya mbuzi mwenye kuzaa karibuni, Mtume (s.a.w.) akachukua chombo akakama akakijaza maziwa tele, akampa bibi yule, bibi akanywa shiba yake. Akakama tena mara tatu, akawapa wale wenziwe aliokuwa nao, na bakuli la tano akanywa yeye mwenyewe. Baada ya hapo akakama bakuli la sita akamwachia yule bibi ili amwekee mumewe atakapokuja. Hapo tena wakashika njia wakenda zao, huku nyuma alikuja mume wa yule bibi, alipoona maziwa alistaajabu sana, akamwuliza mkewe: “Umepata wapi maziwa haya, wala hapana mbuzi anayetoa tone la maziwa?” Mkewe akamhadithia mambo yote yaliyopita siku ile tangu kuja kwa wale mpaka kuondoka kwao, na akamtajia sifa moja moja ya yule bwana aliyemkama mbuzi hata akapata maziwa hayo. Mumewe akamwambia: “Huyo ni mgomvi wa Makureshi tuliyesikia kuwa ametoka Makka. Ningekuwepo hapa nikayaona haya machoni mwangu, ningemwamini papo hapo na nikenda naye endako”. Pamenenwa kuwa bwana huyu na mkewe mwisho wao walikuja kwa Mtume (s.a.w.) Madina wakasilimu. Jina la bibi huyu lilikuwa Bibi Aatika na la mumewe ni Bwana Aktham.
Tumeona katika milango iliyopitwa kuwa Makureshi walitoa ilani kuwa watampa ngamia 100 yoyote atakayemkamata Nabii Muhammad (s.a.w.) akamleta kwao Makka, kwa hivyo kila shujaa alivaa barabara, akatoka kumfuata, kila mtu na mkuki na upinde na mshare, juu ya farasi wake, kila mmoja katika hawa anataka yeye awe na hishma hiyo ya kumkamata Mtume (s.a.w.), hata siku ya Jumaatano siku ya tatu toka kutoka pangoni, shujaa mmoja aliyekuwa akiitwa Suraqa alipata habari ya mahali alipo Nabii Muhammad. Akavalia pale pale akawafuata kwa kunyemelea mpaka akawaona hakuwahi kupiga shoti mbili tatu ila yule farasi wake aliteleza akaanguka. Baada ya kumwinua alitwaa vijiti vyake vya kupiga bao akapiga, vikamwonyesha kumkataza kuwatafuta, lakini alivikhalifu akamtoa shoti tena farasi wake. Pele pele akajikwaa tena, lakini akajizoazoa juu ya yule farsi akainuka. Bwana huyu akapiga bao lake mara ya pili, nalo likamkataza tena, lakini akalikhalifu akamtoa mbio farasi wake, hata alipokuwa karibu na kuwafikilia, miguu ya farasi wake ilitumbukia ndani ya ardhi akazuilika hawezi kuchopoka. Hapo akapiga makelele ya kutaka amani, na Mtume (s.a.w.) akampa, pale pale akachopoka akasimama pembezoni mwa Mtume (s.a.w.). Suraqa akamwambia Mtume (s.a.w.): “Mimi nina yakini kuwa jambo lako hili litatangaa, na litaenea Bara Arabu yote, basi nataka unipe barua yako ya amani ambayo nikimwonyesha mtu wako yoyote atanipa amani na atanisaidia, mimi nachukua ahadi kuwa sitamjulisha mtu yoyote habari yenu mpaka mfike mnakokwenda na nitampoteza kusudi anayetaka kukufatieni kwa njia hii” Mtume (s.a.w.) akaamrisha aandikiwe barua hiyo ya amani. Tena wao wakashika njia yao ya kwenda Madina na Suraqa akashika njia yake ya kurejea kwao.
Baada ya siku mbili tatu Suraqa alikutana na Abu Jahl. Alipomwuliza habari ya Mtume (s.a.w.), alimjibu kuwa yeye hajui. Lakini Abu Jahl alimshika sana na akamyakinishia kuwa yeye ana yakini kwamba Suraqa amemfuata Mtume (s.a.w.). Mwishowe Suraqa alimkiria haya na akamhadithia yote yaliyomfika farasi wake, na akamtaka yeye Abu Jahl asilimu pia kama alivyosilimu yeye, kwani Nabii Muhammad (s.a.w.) ni Mtume wa haki. Abu Jah alimjibu akamwambia: “Masikini roho yako! Ndiyo kwanza sasa unajua kwamba Muhammad ni Mtume wa haki? Mimi tangu zamani najua kuwa ni Mtume wa haki lakini sitaki kumfuata tu. Kwanini kila utukufu wawe nao Bani Hashim peke yao? Bani Hashim wametoa watukufu na sisi Bani Makhzum tukatoa. Wakatoa mashujaa na sisi tukatoa, na wakalisha tukalisha. Hata leo walipokuwa farasi wao na wetu wanagusana magoti kwa kukaribiana anatokea kwao Mtume (s.a.w.) aliyeletwa na Mungu! Wallahi sitamfata. Tutapata wapi sisi Mtume (s.a.w.) wa kumlinganisha na wao? Basi kwa hivyo sitamwamini tukapata kuwapa cheo hiki Bani Hashim peke yao”.
|