Published By Said Al Habsy  Watu walioadhibiwa sana kwa ajili ya dini yao ni hawa:-
1. Sayyidna Abubakr: Mara tu Mtume (s.a.w.) alipodhihirisha kwa watu Utume wake, Sayyidna Abubakr alikwenda msikitini akatoa khutba juu ya Uislamu. Hakushtukia ila watu wote waliokuwa hapo wanampiga, baada ya kuanguka chini, aliinuka Utba bin Rabia akampiga kwa viatu mpaka akazimia, hakupata fahamu ila walipokuja jamaa zake wakamchukua kitikiti mpaka kwake, akasalia ndani baadhi ya siku, hawezi hata kujinyanyua kitandani.
2. Bwana Bilal: Alikuwa mtumwa wa Umayya bin Khalaf, – Adui mkubwa wa Waislamu – Huyu Umayya alikuwa akimfunga kamba za mikono na miguu na ya shingo, na akiwambia watoto wamburure njiani kama wadudu chungu wanavyoburura nyuki aliyekufa, mara nyingi alikuwa akimshindisha na akimlaza na njaa, kisha humchukua siku ya pili yenye jua kali, akenda naye akamlaza chali, utupu juu ya mchanga wa moto, na akamwekea jiwe la moto juu ya kifua chake, na akamwambia “Utasalia vivi hivi mpaka ufe au uache dini ya Muhammad” Bwana Bilal alikuwa hasemi ila “Ahad Ahad” yaani “Naabudu Mungu mmoja tu wa haki” akawa anataabishwa vivyo hivyo mpaka akakombolewa na Sayyidna Abubakr kwa kumbadilisha na mtumwa wa kikafiri pamoja na mkewe na mtoto wake na pamoja na pesa nyingi juu yake.
3. Bwana Abu Fukayha: Alikuwa akitaabishwa na mtoto wa Umayya kwa namna ile ile ambayo Umayya akimtaabisha Bwana Bilal.
4. Bibi Zinira: Abu Jahl alikuwa akikiunguza chuma motoni kisha akimgandamiza nacho machoni mpaka akawa pofu.
5. Bwana Khabbab: Alikuwa mtumwa wa mwanamke katili kweli kweli, alikuwa akinyolewa nywele kisha akichomwa kwa bapa la chuma chenye moto juu ya kichwa, akawa madonda matupu kichwani.
6-8. Ammar bin Yasir na Baba yake na Ndugu yake: Walikuwa wakibabuliwa kwa majani ya mtende kila siku, hata wakajaa madonda mwili mzima, na 2 katika hawa wakafa, akasalia Bwana Ammar tu.
9. Mama yake Bwana Ammar: Alifungwa baina ya ngamia wawili – mguu mmoja huku na wa pili huku – tena wakaendeshwa mbio njia mbali mbali, na huyu mwanamke akachanika pande mbili.
10. Bwana Amir bin Fuhayra: Aliadhibiwa hata akarukwa na akili.
11. Bibi Lubayna: Sayyidna Umar – kabla ya kusilimu kwake – alikuwa akimpiga bakora wee hata mpaka achoke mwenyewe.
Wapo wengi wasiokuwa hawa, na wengine waliteswa kwa mateso ambayo hayafai kutajwa kitabuni.
|