Tumekwisha kuona kuwa Mtume (s.a.w.) hakupata kufanya jambo lolote katika mambo waliokuwa wakiyafanya makafiri, wala hakuwa akihudhuria sikukuu zao tangu kufahamu kwake. Alikuwa akipenda kukaa peke yake. kufanya haya kulikuwa kukimwonyesha raha kubwa kuliko kutoka mbele za watu akaona yale mambo yao mabaya aliyokuwa akiyachukia. Kila usiku ukicha naye alikuwa akizidi kuyachukia. Lakini alikuwa hajui la kufanya.
Hata alipotimia miaka 38 hakuweza tena kustahamili kuona zile ibada za masanamu na tabia mbovu walizokuwa nazo wenziwe, ilivyokuwa hana la kufanya katika kuyazuiya yale, alifanya shauri kuuacha mji wa Makka na kwenda maporini kukaa. Akapata pango zuri katika Jabal Hira kaskazini ya Makka, inapata meli 3 toka huko Makka. Akawa akikaa huko kwenye Jabal Hira kwa muda wa wiki nyingi, kisha hurejea Makka kuja kumtazama mkewe, wanawe na jamaa zake wengine, na vile vile kwa ajili ya kuchukua chakula kinapokuwa kimekwisha. Wakati mwengine akikaa siku nyingi sana huko maporini hata humpasa mkewe Bibi Khadija kwenda kumsikiliza na mara nyengine alikuwa akifuatana naye, pamoja na watoto wao mpaka maporini. Alidumu juu ya hali hii muda wa miaka miwili na kitu.
Hata siku moja – katika mwezi wa Ramadhani mwezi 17, Jumaatatu katika mwaka wa 40 unusu wa umri wake – Mtume (s.a.w.) alimuona mtu kamsimamia mbele yake bila ya kumuona wapi katokea, akamwambia: “Soma” Mtume (s.a.w.) akamjibu: “Mimi sijui kusoma kwani sijapata kujifundisha kusoma” akaja akamkamata akambana, akamwambia tena: “Soma” Mtume (s.a.w.) akamjibu jawabu yake ile ile, hata mara ya tatu akamwambia: “Soma – Iqraa Bismi Rabbik - ” akamsomea sura hiyo ya 96 mpaka kati yake, kisha Mtume (s.a.w.) akaisoma kama alivyosomewa. Hii ndiyo sura ya kwanza kushuka katika Qurani, ingawa haijawekwa mwanzo.
Mara yule mtu (Malaika) akaondoka machoni mwake – asimwone kenda wapi. Na Mtume (s.a.w.) naye akarejea kwake – khofu imemshika – . Alipofika nyumbani, Bibi Khadija alidhani ana homa, akamfunika maguo gubi gubi na akakaa mbele yake akimsikiliza anavyoweweseka. Hata homa ilipomwachia alimweleza Bibi Khadija yote yaliyomtokea, na Bibi Khadija akamtuliza moyo wake, akamyakinishia ya kuwa hapana lolote baya litakalomzukia. Mara Bibi huyu akaondoka akenda kwa jamaa yake – Bwana Waraqa bin Naufal – akampa habari yote iliyompata mumewe. Naye akamwamrisha amwite, na Mtume (s.a.w.) akenda akamweleza habari yake yote. Bwana Waraqa akamwambia: “Huyo ndiye Jibril aliyemshukia Nabii Mussa na Nabii Isa. Basi jibashirie kuwa wewe ni Mtume wa Umma huu!! Nami natamani kuwa hai nikuone unavyosimama kuwatengeneza jamaa zako, Inshaalla nitakuwa mkono wako wa kulia!” wakarejea kwao na khofu yote imemtoka. Baada ya kuazimia kuwa hatakwenda tena kule pangoni. Pale pale akaondoka akenda pangoni mwake ili aonane naye tena, ingawa alikaa huko muda mrefu. Siku ile ya kupata Utume inawafiki mwezi wa December 610.
Huyu Bwana Waraqa hakuwa akiabudu dini ya masanamu bali alikuwa akifata dini ya Kimasihi[1], alipokuwa akisoma vitabu vya dini hii aliona kwamba kutatokea Mtume mwengine ndiyo maana alipohadithiwa habari ile iliyompata Mtume (s.a.w.), mara moja akatambua kuwa huyo mtu aliyemjia Mtume (s.a.w.) ni Jibril ambaye hamjii mtu yoyote ila Mtume tu.
[1] - Kusema kwake Sheikh "Dini ya Kimasihi" haimaanishi kwamba Nabii Isa alikuja na dini isiyo ya Kiislamu; laa! Bali alikuja na Uislamu kama walivyokuja nao Mitume wengine kwani hii ndio dini pekee ya mbinguni, na lile linalofanywa na baadhi ya watu wengi hii leo hasa wa nchi za Kiarabu la kumwita mkristo kuwa ni Masihi ni kosa kubwa, kwa sababu Masihi ni sifa iliyotoka kwa Allah kwa kumsifu Mtume wake Nabii Isa, kwa hivyo hii si sifa ya mwenye kulielekea sanamu wakati wa Ibada na kumgawa Mungu sehemu tatu: Baba, mwana na roho mtakatifu. Kwani wale wamesifiwa na hali hawa wamelaaniwa.
|