Baba yake Mtume (s.a.w.) amezaliwa mwaka wa 545 A.D. alikua ni mtoto wa kumi 10. katika ndugu 12 wanaume. Ama ndugu zake wote wanaume na wanawake ni 14. Yeye alikua ni baba mmoja mama mmoja na Bwana Abu Talib, baba yake Sayyidna Ali (Khalifa wa nne), lakini Bwana Abu Talib alikua mkubwa kuliko yeye kwa miaka mitano. Alipotimia miaka 24 na kitu, baba yake Bwana Abdul Muttalib, alimposea Mwana Amina bint Wahab – alikua miaka 24 – . Wakaingia nyumbani awali ya mwezi wa Rajab, Agost 570, A. D. Mwezi ule ule bibi huyu alishika mimba ya Mtume (s.a.w.).
Hata ulipokua msafara mdogo wa Kikureshi unatoka kwenda Sham kufanya biashara, baba yake Bwana Abdul Muttalib, alimuamrisha atoke pamoja nao akafanye baadhi ya biashara, ili wapate pesa za kufanyia karamu wakati atakapozaliwa huyo mtoto, kwani mtoto huyo atakua ndiye mtoto wake wa kwanza, kifungua mlango wake. Akenda mpaka Sham na akafanya biashara yake kama alivyoamrishwa na baba yake. Hata wakati wa kurejea, alipofika Madina, alishikwa na homa ya malaria – Madina ilikua mashuhuri kwa homa ya malaria – Akakaa kwa wajomba wa baba yake, Bani Najjar. Kwani tumekwisha kuona kuwa mama yake Bwana Abdul Muttalib ni mwanamke wa Kimadina. Akaugua kwa muda wa mwezi mzima, kisha akafa katika Mfunguo nne. Akazikwa huko huko Madina katika nyumba ya jamaa yake aliyekua akiugulia kwake siku zote. Alipokufa alikua ni kijana wa miaka 25 na kitu.
Wakati huo alipokufa baba yake, Mtume (s.a.w.) alikua mtoto wa matumboni wa miezi minane – Kama wenye Tarehe[1] wengine wanavyothibitisha, si mtoto wa matumboni wa miezi miwili kama alivyo sema mwenye Maulidi ya Barzanji na wengine –. Mwana Amina alichukuliwa na Bwana Abu Talib, shemeji yake, akakaa eda nyumbani kwake. Baada ya mwezi na kitu akamzaa Mtume (s.a.w.) nyumbani kwa Bwana Abu Talib, katika mtaa unaoitwa Suqu Al-layl, mtaa wa Bani Hashim.
Alizaliwa alfajiri ya Jumatatu mwezi 12 Mfunguo Sita katika mwaka walioazimia Mahabushia kuuteka mji wa Makka – baada ya kua Yaman yote imo chini ya mikono yao – . Lakini Mwenye-ezi-Mungu aliwaletea ndui, yakaangamia majeshi yao kwa muda mdogo, wakapukutika kama kuku. – Hivi ndivyo alivyosema Askalany katika Al-Bukhary, na ndiyo kauli aliyoitilia nguvu Sheikh Muhammad Abdoo katika tafsiri yake –. Na siku hii ya kuzaliwa kwake inawafiki mwezi 20 April 571. Kama alivyo hakikisha haya mwanachuoni mkubwa wa Misr – Mahmoud Basha Al-Falaky –. Na siku hii ya kuzaliwa kwake palitokea ajabu kubwa, kama tunazozisikia vitabuni, kwani yeye ni Mtume, na kila Mtume ana miujiza yake.Wala si uhodari kwa mtu kukanusha kila asilolijua na lisiloingia katika akili yake. Bali uhodari ni kujitahidi kufahamu. Ikiwa mtu hakuiona “Television” wala haiwezi kuingia katika akili yake ndio atasema ni “Uongo, hapana kitu cha namna hiyo!” Basi na akatae vingi visivyoweza kuingia katika akili yake fupi.
Pale pale alfajiri alipokwisha kuzaliwa Mtume (s.a.w.), alikwenda kuitwa babu yake kuja kumuona mjukuu wake, Babu huyu alifurahi sana, na akamfunikafunika maguo mjukuu wake, akajikongoja naye mpaka kwenye Al-Kaaba. Akafungua mlango, akaingia naye ndani akasimama anamuombea dua kwa mashairi mazuri ya kiarabu aliyotunga mwenyewe wakati ule ule. kisha akarejea naye, na jua bado halijachomoza.
Hata siku ya saba au ya nane alifanya karamu kubwa, na akampa mjukuu wake jina la Muhammad, yaani mwenye kushukuriwa kwa vitendo vyake vizuri. Jamaa zake walipomuuliza sababu ya kumwita jina hili, aliwajibu ya kuwa anamtarajia afikilie cheo hicho cha kushukuriwa na kila mtu. Jina hili kabisa halikua likitumika katika nchi ya Bara Arabu. Hata ilipokua karibu atadhihiri Mtume (s.a.w.). Mapadiri wa Kinasara na Makohani wa Kiyahudi waliokua wakikaa Bara Arabu walikua wakiwatahayarisha majirani zao wa kiarabu waliokua wakiabudu masanamu, Wakiwaambia: “Karibu ataletwa Mtume katika nchi hii yenu, abatilishe hii ibada yenu mbovu ya masanamu” Walipoambiwa hivi wale waarabu waliwauliza nini litakua jina la Mtume huyo, wakawajibu kuwa jina lake litakua Muhammad. Kwa hivyo kila mwenye kusadiki hayo alimwita mwanawe Muhammad. Lakini hayakusikilizana[2] majina haya ila kwa baadhi ya waarabu waliokua wakikaa Sham tu na Najran (Yaman) ambako Mapadri wengi wa kinasara wakikaa, na vilevile katika Madina ambayo ilikua nusu ya wakaazi wake ni Mayahudi. Hata lilipoanza kutangaa jina la Mtume wetu (s.a.w.), waliokuwa wamekwisha kuitwa kwa jina hili ni watu kidogo tu Bara Arabu nzima.
|