Kasema Bibi Aisha R.A.A.H.,[1]" أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ كَانَ يَنْفُثُ عَلَى نَفْسِهِ فِي الْمَرَضِ الَّذِي مَاتَ فِيهِ بِالْمُعَوِّذَاتِ فَلَمَّا ثَقُلَ كُنْتُ أَنْفِثُ عَلَيْهِ بِهِنَّ وَأَمْسَحُ بِيَدِ نَفْسِهِ لِبَرَكَتِهَا فَسَأَلْتُ الزُّهْرِيَّ كَيْفَ يَنْفِثُ قَالَ كَانَ يَنْفِثُ عَلَى يَدَيْهِ ثُمَّ يَمْسَحُ بِهِمَا وَجْهَهُ. Maana yake, "Alikuwa Mtume S.A.W. akijizingua kwa kujipulizia mwenyewe kwa Mu`awwidhat alipokuwa na maradhi ambayo alikufa nayo. Yalipomzidia (maradhi) nilikuwa nikimzingua kwa kumpulizia nazo, na nilikuwa na upangusa (mwili wake) kwa mkono wangu kwa ajili ya kupata baraka zake". Akauliza Zuhri, "Vipi akijipulizia?" Akasema alikuwa anapulizia kwanza katika mikono yake halafu anaipangusia uso wake".
Katuhadithia Sufiani kutoka kwa Abdi Rabih bin Said kutoka kwa Amrata kutoka kwa Bibi Aisha R.A.A.H. kuwa, [2]"Ikiwa mtu atashitakia kwa maradhi yoyote yale, au ana uele[3] au ana jeraha, akasema (Sufiani), "(basi)Mtume S.A.W. ataweka kidole chake cha gumba hivi, na akaweka Sufiani vidole vyake ardhini halafu akaviinua huku akisema, “ بِسْمِ اللَّهِ تُرْبَةُ أَرْضِنَا بِرِيقَةِ بَعْضِنَا لِيُشْفَى بِهِ سَقِيمُنَا بِإِذْنِ رَبِّنَا. BismiLlahi turbatu ardhina biriiqati ba`adhinaa liyushfa bihi saqiimuna bi`idhini Rabbina. Maana yake, “Kwa jina la Mwenyezi Mungu (Bismillah) na vumbi vumbi ya udongo wa ardhi yetu pamoja na zinguo[4] ya baadhi yetu itakuwa sababu ya kuponesha maradhi yetu kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu".
Kutoka kwa Ibn Abbas R.A.A. kasema, “Kasema Mtume S.A.W., [5] "Atakaemzuru[6] yule ambaye bado wakati wa mauti haujafika, na akamzingua kwa kusema mara saba, " أَسْأَلُ اللَّهَ الْعَظِيمَ رَبَّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ أَنْ يَشْفِيَكَ. As`alu Llaha L`Adhiim, Rabba l`Arshi l`Adhiim an Yash`fiyaka. Maana yake, "Namuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mola wa kiti cha enzi, Akuponeshe". Mola atamponesha kutokana na yale maradhi”.
Kutoka kwa Bibi Aisha R.A.A.H. mke wa Mtume S.A.W. kasema, "Akiugua Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. Jibril alikuwa akimzingua (kumsomea ruqiya) akisema,[7] " بِسْمِ اللَّهِ يُبْرِيكَ وَمِنْ كُلِّ دَاءٍ يَشْفِيكَ وَمِنْ شَرِّ حَاسِدٍ إِذَا حَسَدَ وَشَرِّ كُلِّ ذِي عَيْنٍ. Bismillahi yubriika, wa min kulli daain yash`fiika, wa min sharri haasidin idha hasad, wa sharri kulli dhii aiyn. Maana yake, "Kwa jina la Mwenyezi Mungu Atakuponesha kila maradhi, na shari ya kila hasidi anapohusudu, na shari ya jicho baya".
Kutoka kwa Ibn Abbas R.A.A. kasema, "Mtume S.A.W. aliingia kwa bedui (alie kuwa anaumwa) kumjulia hali, (akaendelea akasema), na ilikuwa kawaida ya Mtume S.A.W. kila anapoingia kwa mgonjwa alikuwa akisema, [8]" لَا بَأْسَ طَهُورٌ إِنْ شَاءَ اللَّهُ. La ba`asa tahurun in sha Allah. Maana yake, "Hapana neno, ni tohara akipenda Allah[9] "Yule bedui akasema, "Kuhotarishwa?, Hapana hii ni homa inayochemka, au inayomsumbua mwanamume mkongwe, na itamsababishia mauti" Akasema Mtume S.A.W., "Basi neema ikiwa hivyo" |