DUA NA UMUHIMU WAKE.Ni mwenendo wa maisha wa mwanadamu kupitikiwa na hali inayochukiza yenye kuleta msiba, huzuni au machungu, ambayo humtatanisha na kumfanya kukata tamaa, na yote haya ni majaribio kutoka kwa Mola Mtukufu ili kutimiza lengo halisi la kuumbwa kwa mwanaadamu na kuletwa hapa ulimwenguni. *Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Al Insan aya ya 1 na aya ya 2, " ﴿هَلْ أَتَى عَلَى الْإِنْسَانِ حِينٌ مِنَ الدَّهْرِ لَمْ يَكُنْ شَيْئًا مَذْكُورًا﴾ ﴿إِنَّا خَلَقْنَا الْإِنْسَانَ مِنْ نُطْفَةٍ أَمْشَاجٍ نَبْتَلِيهِ فَجَعَلْنَاهُ سَمِيعًا بَصِيرًا﴾. Maana yake, "Hakika kilimpitia binaadamu kipindi katika zama ambacho kwamba hakuwa kitu kinacho tajwa. Hakika Sisi tumemuumba mtu kutokana na mbegu ya uhai iliyo changanyika[1], tumfanyie mtihani. Kwa hivyo tukamfanya mwenye kusikia, mwenye kuona"[2]. *Pia Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat al Mulk aya ya 2, " ﴿الَّذِي خَلَقَ الْمَوْتَ وَالْحَيَاةَ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا وَهُوَ الْعَزِيزُ الْغَفُورُ﴾. Maana yake, "Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi. Na Yeye ni Mwenye nguvu na Mwenye msamaha.
*Pia Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Suratil Baqara aya ya 155, " ﴿وَلَنَبْلُوَنَّكُمْ بِشَيْءٍ مِنَ الْخَوْفِ وَالْجُوعِ وَنَقْصٍ مِنَ الْأَمْوَالِ وَالْأَنْفُسِ وَالثَّمَرَاتِ وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ﴾. Maana yake, "Hapana shaka tutakujaribuni kwa chembe ya khofu, na njaa, na upungufu wa mali na watu na matunda.
*Pia Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Suratul Muh`ammad aya ya 31, " ﴿وَلَنَبْلُوَنَّكُمْ حَتَّى نَعْلَمَ الْمُجَاهِدِينَ مِنْكُمْ وَالصَّابِرِينَ وَنَبْلُوَ أَخْبَارَكُمْ﴾. Maana yake, “Na bila ya shaka tutakujaribuni[3] mpaka tuwadhihirishe wafanyao jihad[4] katika nyinyi na wanao subiri. Nasi tutazifanyia mtihani khabari zenu.[5]
*Kutoka kwa Abu Huraira R.A.A kasema Mtume S.A.W.,[6] " مَا يَزَالُ الْبَلَاءُ بِالْمُؤْمِنِ وَالْمُؤْمِنَةِ فِي نَفْسِهِ وَوَلَدِهِ وَمَالِهِ حَتَّى يَلْقَى اللَّهَ وَمَا عَلَيْهِ خَطِيئَةٌ. Maana yake, "Muisilamu ataendelea kupata balaa (mitihani) katika nafsi yake, na mtoto wake, na mali yake mpaka akutane na Mwenyezi Mungu hali ya kuwa hana dhambi".
*Kutoka kwa Anas bin Malik R.A.A kasema, “Kasema Mtume S.A.W., [7]" عِظَمُ الْجَزَاءِ مَعَ عِظَمِ الْبَلَاءِ وَإِنَّ اللَّهَ إِذَا أَحَبَّ قَوْمًا ابْتَلَاهُمْ فَمَنْ رَضِيَ فَلَهُ الرِّضَا وَمَنْ سَخِطَ فَلَهُ السُّخْطُ. Maana yake, "Hakika thawabu kubwa ni pamoja na balaa kubwa. Na Mwenyezi Mungu anapowatakia watu kheri anawapa mitihani, atakaeridhika basi anazo radhi za Mwenyezi Mungu, na atakae chukia anapata hasira". Na ni kawaida ya mwanaadamu akijaribiwa huhaha huku na kule akitafuta ufumbuzi na faraja, na ikiwa yeye yatamshinda basi huanza kuomba msaada, na hapana shaka ataomba msaada kwa yule mwenye nguvu na uwezo kuliko yeye. Na mbora wa kuombwa msaada ni Mola Mtukufu ambae ndie mmiliki mkuu anaepanga na kupangua. Rehema Zake zimekizunguka kila kitu, Nae ni Mkarimu, Mwenye huruma kuliko mama kwa mwanawe, Nae ni mwenye kusikia na kuona, na mwenye kujibu dua ya aliedhulumiwa, na asie dhulumiwa. Msamehevu kwa kila mwenye kutubia, mlango wake uko wazi. Hapana nguvu wala uwezo isipokuwa wake Yeye, ni Muweza na Muwezesha.
*Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Naml aya ya 62, " ﴿أَمَّنْ يُجِيبُ الْمُضْطَرَّ إِذَا دَعَاهُ وَيَكْشِفُ السُّوءَ وَيَجْعَلُكُمْ خُلَفَاءَ الْأَرْضِ﴾. Maana yake, "Au nani yule anaye mjibu mwenye shida pale anapo mwomba, na akaiondoa dhiki, na akakufanyeni warithi wa ardhi?”. DUA NA NYIRADI.Mtume Muhammad S.A.W. wakati wa utume wake amewafundisha Masahaba zake aina tofauti za nyiradi, maombezi na istigh`fara, hivyo basi inapendeza mtu kukamatana nazo, kwani yeye ni kiongozi na mwalimu wetu, naye kwetu ni mfano bora wa kufuatwa. Na kwa kumfuata Mtume S.A.W. mtu anapata ujira mkubwa. Naye alikuwa hasemi kwa matamanio yake, kila alichosema, au kutenda kilikusudiwa kuwa kielelezo kwetu nacho kimetoka kwa Mola Mtukufu.
Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat ANNajm aya ya 3 na aya ya 4," ﴿وَمَا يَنطِقُ عَنِ الهَوَى} {إِن هُوَ إِلاَّ وَحيٌ يُوحَى﴾. Maana yake, "Na wala hasemi kwa matamanio yake. Hayakuwa haya (anayosema) ila ni Wahyi (ufunuo), uliyofunuliwa (kwake)". Pia Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu Surat Al-Ahzab aya ya 21," ﴿لَقَد كَانَ لَكُم فِى رَسُولِ اللَّهِ أُسوَةٌ حَسَنَةٌ لِمَن كَانَ يَرجُوا اللَّهَ وَاليَومَ الأَخِرَ وَذَكَرَ اللَّه كَثِيراً﴾. Maana yake, "Bila shaka mfano ulio mwema (ruwaza nzuri) ni kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu[8], kwa mwenye kumwogopa Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, na kumtaja Mwenyezi Mungu sana."
Pia Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat al Imran aya ya 31, “ ﴿قُلْ إِنْ كُنْتُمْ تُحِبُّونَ اللَّهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ وَاللَّهُ غَفُورٌ رَحِيمٌ﴾. Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Mwenyezi Mungu basi nifuateni mimi, Mwenyezi Mungu atakupendeni na atakufutieni madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta madhambi na Mwenye kurehemu”[9].
Pia Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat al Ara`af aya ya 158, “ ﴿قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنِّي رَسُولُ اللَّهِ إِلَيْكُمْ جَمِيعًا الَّذِي لَهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ لَا إِلَهَ إِلَّا هُوَ يُحْيِي وَيُمِيتُ فَآمِنُوا بِاللَّهِ وَرَسُولِهِ النَّبِيِّ الْأُمِّيِّ الَّذِي يُؤْمِنُ بِاللَّهِ وَكَلِمَاتِهِ وَاتَّبِعُوهُ لَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ﴾. Maana yake, "Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni Mtume kwenu nyinyi nyote, niliye tumwa na Mwenyezi Mungu Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Hapana mungu ila Yeye anaye huisha na anaye fisha. Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake asiyejua kusoma na kuandika, ambaye anamuamini Mwenyezi Mungu na maneno yake. Na mfuateni yeye ili mpate kuongoka”. Na Mtume S.A.W. kwetu alikuwa kama mzazi, anayewafundisha watoto wake. Kutoka kwa Abu Huraira R.A.A. kasema, “Kasema Mtume S.A.W.,[10] “ أَنَا لَكُمْ مِثْلُ الْوَالِدِ أُعَلِّمُكُمْ أَمْرَ دِينِكُمْ. Maana yake, "Mimi kwenu ni kama mzazi nawafundisha kuhusu mambo ya dini yenu”. [1] Maji ya uzazi ya mwanamume na mwanamke. [2] Tukampa hisia za kusikia na kuona ili kusudi azitumie kwa kutii au kutokutii. [3] Kwa amri na makatazo. [4]Yaani wanaojitahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu: Juhudi zilizokusudiwa ni za muumini wa Kiisilamu kuishi kama jinsi vile imani ya dini yake inavyomuamrisha yaani kufanya yote aliyoamrishwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mtume Wake S.A.W. na kujiepusha na yote yale yaliyokatazwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mtume Wake S.A.W; kufanya juhudi ya kuuboresha umma wa Kiisilamu; na inaweza kuwa vita takatifu ya kulazimishiwa ya kujihami na kuihami dini na wala sio vita ya kuvamia au kuharibu au kuua bila sababu. [5] Ili kujua utiifu na unyenyekevu wenu. [6] Ttirmidhiy 8/418 (2323). [7] Ibn Maajah 12/38 (4021). [8] Kumuiga na kumfanya kigezo cha muongozo. [9] Kasema Ibn Kathiir: "Aya hii ni msingi mkubwa wa kumfuata Mtume S.A.W. katika kauli, matendo na hali zake. Kwa ajili hiyo Mwenyezi Mungu Mtukufu amewaamuru wanaadamu wamuige Mtume S.A.W. wakati wa siku ya Ahzaab kwa kusubiri, kulinda, juhudi na kusubiria faraja kutoka Kwake. [10] Al Rabi`u 1/50 (80). Mfano wa Hadithi hii imetolewa pia na Ibn Maajah 1/374 (309), An-Nassai`y 1/77 (40), Ahmad 15/105 (7064), Ahmed Hambal 2/247 (7363). |