Kuwa Na Shaka,Kusahau Na Kurudia Sala
KUWA NA SHAKA, KUSAHAU NA KURUDIA SALA: 1
Published By Said Al Habsy  Mstahiwa Sheikh, jamaa walisali fardhi ya adhuhuri, baada ya imamu kutoa salamu baadhi yao walisema: tumesali rakaa tatu tu, na wengine wakasema: bali tumesali rakaa nne, kisha wakakubaliana juu ya kurudia sala. Je inawalazimu kuirudia sala kwa kuwa na shaka tu?Haimlazimu kurudia mwenye kuwa na shaka na sala baada ya sala kumalizika, na akitaka mwenye shaka kujitoa wasiwasi kwa kurudia sala basi hilo linamkhusu yeye pasina wengine ambao hawakuwa na shaka, kwasababu mwenye kusali akiwa na yakini asiache yakini yake kwa ajili ya shaka ya mwengine. Na Allah anajua zaidi. |
KUWA NA SHAKA, KUSAHAU NA KURUDIA SALA: 2
Published By Said Al Habsy  Mstahiwa Sheikh, kukamilisha suali letu lilotangulia, je warudie sala kwa jamaa katika hali iliyotangulia au wairudie kila mmoja peke yake? Na nini hukumu iwapo wakati wa sala umepita?Haikatazwi kurudia sala kwa jamaa kwa kauli sahihi pakiwapo kinachowajibisha kurudiwa, na ni sawa iwapo hilo ni katika wakati wa sala au baada ya wakati, kwani hapana dalili ya kuzuiwa sala kurudiwa kwa jamaa, ingawa kumesemwa na baadhi ya maulama. Na Allah anajua zaidi. |
KUWA NA SHAKA, KUSAHAU NA KURUDIA SALA: 3
Published By Said Al Habsy  Mtu aliwasalisha jamaa sala ya alasiri, baada ya kumalizika sala jamaa hao walikhitalifiana, kuna kati yao waliosema tumesali rakaa nne na waliosema tumesali rakaa tano. Wale ambao walisema rakaa tano walimsabihia imamu lakini hakushughulika nao, bali aliendelea na sala yake mpaka akaimaliza, nini hukumu ya sala yao?Ikiwa imamu au mwenginewe hana wasiwasi kuwa hakuzidisha katika sala yake kuliko rakaa nne basi asishughulike na utiaji shaka wa wanotaka kumtia shaka katika sala yake. Halikadhalika iwapo ameingiwa shaka katika nafsi yake kukhusu ziada hii baada ya kutoka katika sala asishughulike na shaka hiyo. Na Allah anajua zaidi. |
KUWA NA SHAKA, KUSAHAU NA KURUDIA SALA: 4
Published By Said Al Habsy  Nini hukumu ya aliyesali fardhi ya isha na baada yake sunna ya witri, na wakati anasali witri ikamuingia shaka je alitoa salamu kumaliza fardhi ya isha au alisahau kutoa salamu, lakini aliendelea katika sala yake, je inamlazimu kuirudia?Mwenye kuwa na shaka kukhusu kutoa salamu baada ya kupapita mahala pa kutoa salamu hapana kitu juu yake, na vivo hivo mwenye kulipita tendo lo lote kati ya matendo ya sala hamlazimu kulirudia. Na Allah anajua zaidi. |
KUWA NA SHAKA, KUSAHAU NA KURUDIA SALA: 5
Published By Said Al Habsy  Mtu aliwasalisha jamaa sala ya alfajiri, kisha akenda safari nje ya mji wake akakuta kuwa katika nguo yake mlikuwa mna najsi, na hakurudi kwenye mji wake ila baada ya wiki, nini afanye kukhusu sala yake na sala yao?Inamlazimu alipe sala yake, kwasababu sala kwa nguo yenye najsi haisihi, na inampasa awape khabari jamaa waliosali nyuma yake akiweza, kisha mwenye kutaka kurudia sala yake kati yao atarudia na mwenye kutaka kuchukua rukhsa iliyopo atachukua. Na Allah anajua zaidi. |
KUWA NA SHAKA, KUSAHAU NA KURUDIA SALA: 6
Published By Said Al Habsy  Nini hukumu iwapo mtu anasali sala mojawapo ya rakaa nne, na wakati anasali akasahau na hakujua rakaa ngapi amesali, akataka kuirudia sala yake, je inamlazimu atoe salamu akitaka kutoka katika sala hii?Akisahau sala yake na hakujua rakaa ngapi amesali inampasa airudie upya, na haimlazimu kutoa salamu kwa vile sala yake imeharibika. Na Allah anajua zaidi. |
KUWA NA SHAKA, KUSAHAU NA KURUDIA SALA: 7
Published By Said Al Habsy  Mtu alisahau kusali sala ya alasiri na hakuikumbuka ila wakati anasali sala ya magharibi jamaa, je inamlazimu atoke katika sala yake pamoja na imamu ili alipe sala ya alasiri, au atimize sala yake na baadae alipe fardhi ya alasiri? Na akiilipa baada ya magharibi je inamlazimu arudie tena kuilipa katika wakati wa alasiri wa siku inayofuata?Kauli yenye nguvu atimize fardhi ya magharibi, akimaliza asali alasiri aliyoisahau, na haimwajibikii kurudia. Na Allah anajua zaidi. |
KUWA NA SHAKA, KUSAHAU NA KURUDIA SALA: 8
Published By Said Al Habsy  Nini hukumu ya aliyeisahau fardhi ya adhuhuri na hakuikumbuka ila na imamu anakimu kwa sala ya alasiri, nini afanye?Aliyesahau sala ya fardhi kisha akaikumbuka wakati sala nyengine imewadia inasaliwa jamaa inampasa asali ile aliyoisahau pahala ambapo sala yake haifungamani na sala ya imamu, kisha ajiunge na imamu katika sala iliyowadia. Na Allah anajua zaidi. |
KUWA NA SHAKA, KUSAHAU NA KURUDIA SALA: 9
Published By Said Al Habsy  Mtu amepata janaba, kisha akaamka akaoga na kusali alfajiri, kisha akalala msikitini mpaka jua likachomoza, alipoamka akakuta kadiri fulani ya manii kwenye paja lake, akawa ana shaka kama yalibaki kutokana na yale yaliyotangulia, je arudie sala yake?Inampasa arudie sala yake, ama kuoga bora akurudie ili kujitoa wasiwasi yasijekuwa manii hayo yametoka baada ya kuoga. Na Allah anajua zaidi. |
KUWA NA SHAKA, KUSAHAU NA KURUDIA SALA: 10
Published By Said Al Habsy  Mtu nguo yake imepata najsi na hakutanabahi ila baada ya kusalia nguo yake hiyo iliyonajisika sala tano, je inamlazimu azirudie sala hizo? Na ikiwa inamlazimu kuzirudia, je azirudie alipotanabahi au arudie kila sala kwa wakati wake katika siku inayofuata? Na je aanze kwa sala iliyowadia au kwa ambayo inarudiwa?Inamlazimu azirudie sala tano zote kwa mpangilio mara anapotanabahi. Na ikiwa wakati wa sala iliyowadia una nafasi basi aanze kwa sala zilizompita kama alivofanya Mtume –rehma za Allah na amani zimshukie- walipomzingira washirikina, alilipa adhuhuri, alasiri, na magharibi katika wakati wa isha. Na Allah anajua zaidi. |
KUWA NA SHAKA, KUSAHAU NA KURUDIA SALA: 11
Published By Said Al Habsy  Mtu alipata maradhi akawa hana fahamu kwa muda wa siku tatu, nini kinamlazimu kukhusu sala?Analazimika kuzilipa akipata fahamu. Na Allah anajua zaidi. |
KUWA NA SHAKA, KUSAHAU NA KURUDIA SALA: 12
Published By Said Al Habsy  Nini hukumu kukhusu mtu ambaye Allah amempa mtihani wa maradhi, na akabaki muda wa mwezi mzima hajui hadathi gani inamtokezea wala nini anasema, na hakuzisali sala tano, kisha Allah akumuafu maradhi yake na siha yake ikamrudia, nini kinamlazimu kwa sala zilizomfutu?Maulama wamekhitalifiana juu ya kughumiwa (kuzimia) je hukumu yake ni hukumu ya wazimu au ni maradhi tu? Walioona kughumiwa ni wazimu hawaoni kwa mwenye kughumiwa wajibu wa kulipa sala ambazo wakati wake wote alikuwa katika kughumiwa, isipokuwa tu akighumiwa na wakati wa sala umeshaingia, au akipata fahamu na wakati wa sala unaingia itamlazimu katika hali hizo mbili kuilipa sala hiyo. Na wanaoona kughumiwa ni maradhi wanamlazimisha kulipa sala zote zilizomfutu kwasababu ya kughumiwa, na kauli hii ndiyo ya hadhari zaidi na ndiyo ya wengi. Na hailazimu pamoja na hizo sala kafara yo yote au saumu, bali atatosheka na kulipa tu, sawa ikiwa atalipa sala moja wakati wa kila sala au atakusanya sala nyingi azilipe wakati mmoja. Na Allah anajua zaidi. |
KUWA NA SHAKA, KUSAHAU NA KURUDIA SALA: 13
Published By Said Al Habsy  Mstahiwa Sheikh, Allah amenikadiria ajali ya gari nikavunjika mbavu na kulazwa hospitali muda mrefu, na nilikuwa nikisali sala zote, isipokuwa mkojo ulikuwa ukiendelea kutoka bila kusita. Sasa, wa kushukuriwa ni Allah, nimepona maradhi hayo, na ninataka kugawa kwa mafakiri mchele iwe kafara kwa sala zilizoniharibikia, je hili linatosha au inanilazimu kuzirudia sala zile?Haikulazimu kurudia sala hizo wala kutoa kafara, kwasababu hukuwa na uwezo wa kuliko ulivofanya, na Allah Taala anasema:ﭽ ﮧ ﮨ ﮩ ﮪ ﭼ التغابن: ١٦{Basi mcheni Mwenyezi Mungu kama muwezavyo}Na anasema Subhana:ﭽ ﯗ ﯘ ﯙ ﯚ ﯛ ﯜ ﭼ البقرة: ٢٨٦{Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya iwezavyo}Na anasema:ﭽ ﮅ ﮆ ﮇ ﮈ ﮉ ﮊ ﮋ ﭼ الطلاق: ٧{Mwenyezi Mungu hamkalifishi mtu ila kwa kadiri ya alicho mpa}Na Mtume –rehma za Allah na amani zimshukie- anasema: "Ninapokuamrisheni kitu kifanyeni kadiri muwezavyo". Masahaba walikuwa wakisali na majeraha yao yakivuja damu. Hata hivo ukitaka kutoa sadaka kwa mafakiri ili kuziba kasoro ambayo hakuna takriban mtu anayesalimika nayo kwa hali yo yote ni vizuri kufanya hivo, na Allah atakupa ujira na kukulipa kheri. Na Allah anajua zaidi. |
KUWA NA SHAKA, KUSAHAU NA KURUDIA SALA: 14
Published By Said Al Habsy  Sheikh wetu alimu –Allah akuhifadhi-, nimekuta katika kitabu Jaami' cha Sheikh Abu Muhammad –Allah amrehemu- juz 1 uk 473 maneno yafuatayo: "Watu wamewafikiana juu ya kwamba mwenye kusali kwa kufuata sala ya imamu akiwa haijui hali yake kisha ikambainikia kuwa imamu huyo ni miongoni mwa aina za washirikina kwamba inamlazimu kurudia sala hiyo hata kama wakati umepita. Na nimekuta katika mapokeo ya waliotangulia kutoka kwa baadhi ya watu wetu kwamba bwana mmoja aliwasalisha watu wakiwa safarini kiasi mwaka kisha ikawabainikia kuwa alikuwa mshirikina, wanachuoni wa fiqhi wakawawajibishia kurudia sala walizosali nyuma yake." Mwisho wa kunukuu. Kumenitatiza Mstahiwa Sheikh kule kuwalazimisha kurudia sala, kwani wao walisali nyuma yake kwa mujibu wa hali iliyowadhihirikia, na hilo ndilo ambalo Allah Subhana Wataala ametutaka tumuabudie, na miongoni mwa misingi ya Sharia Tukufu ni kuwepesisha, na kwa kuwa kurudia sala ni usumbufu kwa mwenye hedhi Sharia imemsamehe, basi kwanini haisemwi hapa yaliyosemwa katika suala la mwenye hedhi? Naomba maelezo kwa Sheikh wangu pamoja na kutaja dalili na Allah akulipe.Sala nyuma ya mshirikina haisihi, na kwa hiyo wanachuoni wa fiqhi wamemlazimisha aliyesali nyuma ya imamu mshirikina akiwa hajui kuwa ni mshirikina kulipa sala yake hata kama aliendelea kufanya hivyo muda mrefu. Na hili ni jambo lililo wazi na bayana ; unaonaje lau kama mtu amesali mwaka mzima kwa nguo yenye najsi akiwa hajui kama ina najsi je haimlazimu kulipa sala hiyo ? Kisha suala hili halipimwi na suala la mwenye hedhi, kwani mwenye hedhi hana jukumu la kusali tangu awali, wakati huyu mwenye kusali angali ana jukumu la kusali kwasababu sala aliyoisali haikuwa kwa namna sahihi inayotakiwa kisharia, ingawa yeye hakulijua hilo wala halikumbainikia ila baadae. Kwa ajili hiyo kauli yenye nguvu imekuwa ni kuwajibika kulipa sala aliyosali nyuma ya imamu mshirikina yote. Na Allah anajua zaidi. |
KUWA NA SHAKA, KUSAHAU NA KURUDIA SALA: 15
Published By Said Al Habsy  Mtu aliacha sala mwanzoni mwa umri wake miaka kadha – hajui idadi yake – nini kinamlazimu ? Na vipi alipe sala alizozipoteza ?Inampasa aliyepoteza sala katika ujana wake au uzee wake akadirie idadi yake na azilipe, na achukue hadhari kwa kuongeza kiasi fulani katika makadirio hayo. Kisha kuna khilafu kukhusu kafara, na kwa kauli inayowajibisha imesemwa ni kafara tano, na imesemwa kafara moja, na imesemwa kila sala ni kafara moja. Na Allah anajua zaidi. |
KUWA NA SHAKA, KUSAHAU NA KURUDIA SALA: 16
Published By Said Al Habsy  Na amejibu pahala pengine : kauli ya wastani ni kwamba inamlazimu alipe sala alizopoteza, hata kama atalipa pamoja na kila sala ya fardhi sala moja iliyo mfano wake mpaka moyo wake uwe hauna wasiwasi kuwa amelipa sala zote zilizomfutu. Pia anaweza kulipa idadi kadha ya sala katika wakati mmoja, sawa ikiwa ni wakati wa sala au la, isipokuwa nyakati zilizokatazwa kusali ndani yake, na inamlazimu pamoja na hilo kafara tano kwa sala alizopoteza. Na Allah anajua zaidi. |
KUWA NA SHAKA, KUSAHAU NA KURUDIA SALA: 17
Published By Said Al Habsy  Na katika fatwa mfano wa hiyo kasema Mstahiwa Sheikh : Inamlazimu kwanza kutubu kisha kulipa sala ambazo anakadiria kuwa kazipoteza, na inamlazimu pamoja na hayo kafara tano kwa ajili ya hadhari, kila kafara moja kati ya hizo ni kumpa uhuru mtumwa au kufunga miezi miwili mfululizo au kulisha maskini sitini. Na Allah anajua zaidi. |
KUWA NA SHAKA, KUSAHAU NA KURUDIA SALA: 18
Published By Said Al Habsy  Mwenye kusali akiwa na shaka kukhusu takbira ya kuinuka je airudie ?Ikiwa kabla hajapita pahala pa kupiga takbira hiyo basi na apige takbira, vinginevyo asirejee kwasababu ya shaka, bali hata akiwa na hakika kuwa amesahau asirejee kwenye sunna – zikiwamo takbira za baina ya matendo ya sala – baada ya kupita mahala pake. Na Allah anajua zaidi. |