Published By Said Al Habsy  Tunaomba utufafanulie kukhusu suala la kusoma "مَالِكِ" (Maaliki) katika kauli Yake Taala "مالِكِ يَوْمِ الدِّينِ" na kipi kati ya visomo viwili ni bora: kwa alifu (baada ya mimu) au bila alifu? Na nini dalili waliyoitegemea wenye kila kauli kati ya mbili hizo? Na ipi kauli yenye nguvu kwenu?
Jua kuwa mwenye kuchagua kisomo cho chote kati ya visomo saba mashuhuri vya Qur'ani akakisomea katika sala au nje ya sala hakatazwi hilo, wala hilo haliharibu kitu katika sala yake kutokana na umashuhuri wa visomo hivi na usahihi wa sanadi zake na kukubaliwa na Umma, isipokuwa aliye na rai ya peke yake na ambae kukhalifu kwake hakudhuru ijmai (makubaliano ya Umma). Kumeandikwa vitabu makhususi kwa visomo hivi kama alivofanya A'shaatibi katika utenzi wake, na idadi kadha ya wenye ilmu, akiwemo Imam Al Jazari, na wakavijumuisha na visomo hivo saba visomo vilivobaki kati ya visomo kumi mashuhuri. Kwa hiyo vilivozidi baada ya visomo saba, navyo ni visomo vya wasomaji watatu waliobakia kati ya wasomaji kumi mashuhuri, vina hukumu ile ile ya kwamba inajuzu kuvisoma katika sala na nje ya sala. Na katika ambayo hayana khilafu baina ya wenye ilmu kwamba visomo viwili vya "ملِكِ" (Maliki) na "مالِكِ" (Maaliki) katika sura ya Alfaatiha vimo katika visomo saba vilivopokewa kwa wingi wa uhakika, kwani kwa kuvuta kasoma 'Asim na Alkisaai kati ya wasomaji saba, pia Ya'qub na Khalaf –katika uchaguzi wake- miongoni mwa waliobaki kati ya wasomaji kumi. Waliobaki baada ya hao wamesoma kwa kuto kuvuta. Idadi kadha ya wanavyuoni wa hadithi na wa tafsiri wamekinasibisha kila kimoja kati ya visomo viwili hivi kwa idadi kadha ya masahaba na waliowafuatia, kama nilivoeleza katika kitabu "Jawaahir A'tafsiir" kwa ufafanuzi ambao hapa si mahala pake. Na ikiwa visomo viwili hivi vimepokewa kwa wingi wa uhakika hakuna haja ya kufadhilisha kimojawapo kwasababu kila kimoja kati ya viwili hivo ni kweli isiyowezekana kuwa uongo na ni sawa isiyowezekana kuwa kosa. Kwa ajili hiyo mimi nimeacha kuingia katika kukipa uzito kisomo kimojawapo kati ya viwili hivi – ingawa wamejitumbukiza katika bahari ya jambo hili idadi kadha ya maulama wahakiki – nami siwaoni ila wameshughulikia jambo ambalo halina faida ila kurefusha mjadala. Hapana neno tukitaja ufupisho wa maoni waliyofikia hali ya kuwa wamekhitalifiana katika hilo wakawa makundi mawili: kundi moja linaona bora kisomo cha "ملِكِ" (Maliki) bila alifu. Katika hawa ni Al-Mubarrid na Abu Ubaid kati ya maulama wa Lugha ya Kiarabu, na idadi kadha ya wanavyuoni wa tafsiri kama Ibnu Jarir, A'Zamakhshari, A'Sayyid Al-Jarjaani, Al-Qurtubi, Qutbu al-aimma, Imam Abu Nabhan, na A'Sayyid Rashiid Ridha. Na kundi la pili linaona bora kisomo cha "مالِكِ" (Maaliki) kwa alifu, akiwemo Abu Haatim, Ibnu Al'arabi, Ibnu Atiyya, A'Shawkaani, na Imam Muhammad Abduh.Kundi la mwanzo, wanaoona bora kisomo cha "ملِكِ" (Maliki) bila alifu wametoa hoja kwa yafuatayo:Kwamba kisomo cha "ملِكِ" (Maliki) ndicho kisomo cha watu wa Ardhi Mbili Tukufu (Makka na Madina) nao wanastahiki zaidi kufuatwa, kwani wao ndio wanaopaswa zaidi kuisoma Qur'ani katika hali ya ubichi na upya kama ilivyoteremshwa.Hoja hii ikapingwa kuwa kisomo cha watu wa Ardhi Mbili Tukufu si dalili ya ubora, kwasababu kama itakubaliwa kwamba watangulizi wao waliijua zaidi Qur'ani halikubaliki hilo katika zama za wasomaji mashuhuri. Kisha hapana tafauti baina ya upokezi wa kisomo cha Qur'ani na upokezi wa hadithi, wakati wataalamu wa hadithi na wengineo wamekubaliana kuwa Sahihi ya Al Bukhari inatangulizwa kuliko Muwatta' ya Malik ingawa Malik ni mwanachuoni wa Madina. Isitoshe, visomo vyote viwili vimepokewa kwa wingi kama ilivyotangulia, na baada ya mapokezi ya wingi unaoonesha uhakika hapaangaliwi asili za wapokezi.Na kauli ya baadhi yao: ni dhahiri kwamba watu wa Ardhi Mbili Tukufu hapo zamani na hivi sasa ni wajuzi mno wa Qur'ani na sheria, haikubaliki. Kwani ingalikuwa ni hivo mapokezi yao yangalitangulizwa kuliko mapokezi yote, na rai yao ingalikuwa aula kuzingatiwa pasina rai yo yote. Isitoshe, imetangulia kuoneshwa kwamba mapokezi waliyopokea wapokezi wa hadithi yakathibitishwa na wanavyuoni wa tafsiri yanaonesha kuwa kisomo cha "مالِكِ" (Maaliki) ndicho kisomo cha wengi kati ya Masahaba –radhi za Allah ziwashukie- bali kinanasibishwa na kumi wa mwanzo kati yao. Nimeeleza hilo kwa urefu katika kitabu "Jawaahir A'tafsiir".Kwamba kisomo cha "ملِكِ" (Maliki) kinapata nguvu kwa kauli Yake Taala -katika kuieleza Siku ya Malipo- ﭽ ﯸ ﯹ ﯺ ﭼ {Ni wa nani ufalme leo}.Hoja hii ikapingwa kwamba hilo linazuiwa na kauli Yake Subhana:ﭽ ﮪ ﮫ ﮬ ﮭ ﮮ ﮯ ﭼ {Siku ambayo nafsi haitamiliki kitu kwa ajili ya nafsi nyingine}, ambayo ni maelezo ya siku hiyo hiyo, na kukanusha umilikaji kwa mwenginewe kunamaanisha kuuthibitisha kwake Yeye Taala kwasababu muktadha wa maneno ni wa kubainisha utukufu Wake Taala, ambalo linatiliwa nguvu na kauli Yake baada ya hapo ﭽ ﮱ ﯓ ﯔ ﭼ {Na amri yote siku hiyo ni ya Mwenyezi Mungu}, kwani linalokusudiwa kwa neno 'amri' hapo ni jambo si maamrisho.Kwamba kisomo cha "مَلِكِ" (Maliki) kinakubaliana na kauli Yake Taala "مَلِكِ النَّاسِ" {Mfalme wa wanaadamu}, nayo imo katika sura A'naas ambayo ni mwisho wa Qur'ani kimpangilio.Hoja hii ikapingwa kwamba yaliyo katika sura A'naas yanatafautiana na yaliyo katika sura Alfaatiha, kwasababu kama ingalisomwa kule (katika sura A'naas) "مَالِكِ النَّاسِ" (Mmiliki wa wanaadamu) ingalijirudia maana yake katika kauli Yake "رَبِّ النَّاسِ" {Mola wa wanaadamu}. Ama hapa (katika Alfaatiha) hakuna urudiaji kwa vile yanasemwa pahala pengine.Kwamba mamlaka ya Mfalme (مَلِكِ) ni makubwa kuliko mamlaka ya Mmiliki (مَالِكِ).Hoja hii ikapingwa kwamba hilo halikubaliki, bali baina yao kuna ukubwa wa mamlaka kwa upande mmoja pasina mwengine. Linabainika hilo katika mfalme ambaye mamlaka yake yamejumuisha mji ambao una watu wengi na vitu vingi vilivomilikiwa, lakini mfalme huyu hamiliki kitu kati ya vitu hivo kwani yeye ni mfalme si mmiliki kwa vitu hivo, na wenye kuvimiliki ndio wanaovisarifu pasina yeye.Kwamba kwa kisomo cha "Maaliki" "مالِكِ" (yaani Mmiliki) panakuwa hapana budi kuwapo urudiaji wa namna fulani kwasababu "Maaliki" (yaani Mmiliki) lina maana ya "Rabbi" (yaani Mola).Hoja hii ikapingwa kwamba madai ya kuwepo urudiaji hayakubaliki, kwasababu kila moja kati ya sifa mbili hizi imeambatishwa na kile ambacho haijaambatishwa nacho sifa ya pili na kwa hiyo kila moja ikawa na maana yake pekee. Na hata kama yangekubalika madai hayo basi yangekuwapo pia kwa kisomo cha "Maliki" "مَلِكِ" (yaani Mfalme) kwa mujibu wa alivotaja Aljawhari vya kufasiri "Rabbi" kwa maana ya "Maliki" (yaani Mfalme), na miongoni mwa yanayotoa ushahidi juu ya maana hiyo ni kauli ya A'naabigha:تًخُبُّ إلى النُّعْمانِ حتى تَنالَهُ فِدًى لكَ مِنْ رَبٍّ تَلِيدِي وَطارِفِي"Wanakimbilia kwa Nuumani wapate kumfikiaKwako mfalme nichumacho na nirithicho ni fidia"Na kauli ya mwengine:وَكُنْتَ امْرَأً أَفْضَتْ إِلَيْكَ رَبابَتِي وَقَبْلَكَ رَبَّتْـنِي فَضِعْتُ رُبُوب"Umekuwa mtu ambaye kwako yangu yarejeaKablayo walinitawala wafalme nikapotea"Kwamba Allah Subhana ameielezea dhati Yake kwa ufalme akajisifu kwa sifa hiyo katika kauli Yake "مالِكُ المُلْكِ" "Maaliku-lmulk" (yaani Mmiliki wa ufalme), na "مَلِك" "Maliki" (yaani Mfalme) inatokana na "مُلْك" "mulk" (yaani ufalme), tafauti na "مالِك" "Maaliki" (yaani Mmiliki) ambayo inatokana na "مِلْك" "milk" (yaani umilikaji).Hoja hii ikapingwa kwamba kauli Yake Taala "مالِكُ المُلْكِ" "Maaliku-lmulk" (yaani Mmiliki wa ufalme) inamaanisha zaidi umilikaji kuliko ufalme, kwani kukhusishwa 'Mmiliki' na 'ufalme' kunaonesha kwamba 'Mmiliki' ina maana zaidi kuliko 'Mfalme' kwasababu ufalme unaingia katika umilikaji wa huyo Mmiliki.Watu wa upande wa pili, ambao ni wanaokipa uzito kisomo cha "مالِك" "Maaliki" wametoa hoja kwa yafuatayo:Kwamba katika kisomo cha "مالِك" "Maaliki" mna herufi iliyozidi, na kila herufi moja ina thawabu kumi katika kuisoma. Ametoa Al Bukhari katika kitabu chake 'Taarikh', pia A'Tirmidhi na Al Haakim –wakaisahihisha- kutoka kwa Ibnu Mas'ud –Allah amridhie- kwamba Mtume -rehma za Allah na amani zimshukie- kasema "Atakayesoma herufi moja ya Kitabu cha Allah ana thawabu moja, na kila thawabu moja hulipwa mara kumi …" Hadithi hii inaonesha kuwa kusoma "مالِك" "Maaliki" kuna thawabu nyingi zaidi.Kwamba Mmiliki ("مالِك" "Maalik") ana nguvu zaidi za kufanya atakavo katika anachomiliki kuliko Mfalme ("ملِك" "Maliki") katika ufalme wake, kwasababu Mfalme ni mwenye kuendesha mambo ya ujumla ya raia wake lakini hana uwezo wa kuingilia kitu kati ya mambo yao ya binafsi. Imam Muhammad Abduh kasema "mfano ambao tafauti hii inadhihiri ndani yake ni mtumwa anayemilikiwa katika nchi ya mfalme, hapana shaka kuwa mwenye kummiliki mtumwa huyo ndiye ambaye ana mamlaka ya mambo yote ya mtumwa huyo pasina mfalme."Kwamba mfalme ni mfalme wa raia, wakati mmiliki huyu ni mmiliki wa watumwa, na mtumwa hali yake ni duni kuliko raia, na kwa hiyo lazima utawala wa mmiliki juu ya mtumwa ni mkubwa kuliko utawala wa mfalme juu ya raia, na kwa hiyo lazima mmiliki atakuwa na hali ya juu kuliko mfalme.Kwamba raia wanaweza kujitoa katika uraia wa mfalme wao kwa hiari yao wenyewe, kwa kuhama utawala wa mfalme wao na kuhamia utawala mwengine na kuchukua uraia wa kisiasa mwengine, jambo ambalo haliwezekani kwa mtumwa, kwani mtumwa hawezi kujitoa katika kumilikiwa na anayemmiliki, na hili linaonesha kuwa utawala wa mmiliki juu ya mtumwa ni mkubwa kuliko utawala wa mfalme juu ya raia.Kwamba mtumwa anatakiwa kumhudumia anayemmiliki na hawezi kufanya atakavo bila ruhusa yake, wakati raia hawawajibiki kumhudumia mfalme, na hili ni dalili ya kwamba utiifu na unyenyekevu katika watumwa ni mkubwa kuliko katika raia.Kwamba mmiliki ana haki ya kumuuza mtumwa wake na kumuweka rehani tafauti na mfalme, ambaye hana haki ya kuwauza raia wake.Kwamba mmiliki anahusishwa na mtu na kisichokuwa mtu ikasemwa mmiliki wa watu na wanyama na miti na ardhi na vitu. Ama mfalme hahusishwi ila na watu, isipokuwa tu kwa njia ya mithali, na hii ni dalili ya wazi kuwa mmiliki ana madaraka na nguvu juu ya anachomiliki kuliko mfalme juu ya raia, kwani watu wana uhuru kufanya watakavo na wana hiari ambayo vitu vinginevo havinayo, achilia mbali kuzamia kwa maana kunakopatikana kutokana na ukamilifu wa umiliki.Baada ya hayo, sikudhanii kuwa kwa mtazamo mdogo na mazingatio machache itakufichikia nguvu ya hoja ambazo kimepewa nguvu kwazo kisomo cha "Maaliki" "مالِكِ" (yaani Mmiliki) kuliko hoja za kisomo kingine. Kwani umeshuhudia vipi hoja zile ambazo kimepewa nguvu kwazo kisomo cha "Maliki" "ملِكِ" (yaani Mfalme) zinavoporomoka mbele ya pingamizi zilizo elekezewa mpaka haikubaki hata moja iliyosalimika na kupingwa; wakati hoja hizi zimebaki imara hazijakaribiwa na pingamizi yo yote.Pamoja na hayo yote, mimi sioni haja ya utafiti wote huu kama nilivotangulia kutaja katika rai yangu, kwani visomo vyote viwili vimepokewa kwa wingi na ni sahihi kwa makubaliano ya wote, na wamesoma kwa kila kimoja kati ya visomo viwili hivo miongoni mwa wasomaji ambao visomo vyao kwa makubaliano ya wote ni sahihi na vinajuzu kusomwa katika sala. Hata hivyo, msomaji ye yote atakayeanza kusoma kwa kisomo kimojawapo kati ya visomo saba au kumi vilivokubalika atapaswa azingatie maneno ya kisomo hicho yote, na adumishe utamkwaji wake ili ayatimizie haki zake yanazostahiki. Atakayekuwa anasoma kwa kisomo cha Naafi' kwa mfano –kama inavofuatwa katika Watu wa Magharibi ya Kiarabu, iwe anafuata upokezi wa Warshi au wa Quuluun- basi katika haki yake ni kusoma "Maliki" "ملِكِ" bila kuvuta, na halikadhalika kama atasoma kwa kisomo cha Abu 'Amr au Ibnu 'Aamir au Hamza au Ibnu Kathir. Ama akiwa anasoma kwa kisomo cha 'Aasim kama inavofuatwa katika nchi za Mashariki –ikiwemo nchi yetu ya Oman- basi asome "Maaliki" "مالِكِ" kwa kuvuta kwa irabu mbili ili asitoke katika kisomo anachokifuata. Ama asome kwa kisomo cha msomaji mmoja kisha awe anachagua baadhi ya herufi katika visomo vingine, hilo halikubaliwi na Maulama wa wasomaji. Kwani wao wametaja namna tatu za usomaji kwa mwenye kutaka kusoma kwa zaidi ya kisomo kimoja:Ya Kwanza: Asome Qur'ani yote kwa kisomo kimojawapo pamoja na kuzingatia kila kinachopasa katika kisomo hicho, akimaliza aanze kusoma kwa kisomo kingine mpaka avimalize visomo vyote saba au kumi au visomo alivokusudia kuvisoma kati ya hivyo.Ya Pili: Asome sura kwa kisomo cha msomaji mmoja, akiimaliza airudie kwa kisomo anachotaka kuisomea kati ya visomo vyengine, na vivyo hivyo mpaka akhitimishe Qur'ani yote.Ya Tatu: Akariri aya moja moja, kila aya anaisoma kwa visomo vyote anavotaka kuisomea kati ya visomo saba au kumi, na vivyo hivyo afanye kwa Qur'ani yote.Ama kuchanganya baina ya visomo mbali mbali katika msomo mmoja akawa hapa anasoma kwa kisomo cha 'Aasim kwa mfano na akasoma kwengine kwa kisomo cha al Kisaai au Hamza au Naafi' au Abu 'Amr au Ibnu 'Aamir au Ibnu Kathir au Abu Ja'far au Khalaf au Ya'qub, hilo halikubaliwi na wataalamu wa ilmu za visomo, kwasababu linapelekea kuto kudhibitika kwa usomaji, bali linapelekea kupatikana visomo vingi mpaka viwe havina hisabu. Na kwa kuwa wewe kama waomani wengine unasoma Qur'ani kwa kisomo cha Hafs kwa njia ya 'Aasim ili kufuata ilivo katika misahafu iliyoenea baina yetu, ningalikushauri ufuate kisomo hicho katika kusoma ﭽ ﭞ ﭟ ﭠ ﭼ (Mmiliki wa Siku ya malipo), ili usitoke katika utaratibu unaofuatwa na wasomaji. Ama ningalikujua unasoma kwa kisomo cha Naafi' kwa mfano –kama hali ilivo katika nchi za Magharibi ya Kiarabu- ningalikunasihi usisome ila "Maliki" "ملِكِ" bila kuvuta ili usitoke katika kisomo cha Naafi'. Lakini utasomaje kisomo cha Naafi' nacho kimatamshi kinatafautiana na tulivozoea, maana ndani yake mna 'tafkhiimu' ya 'lam' katika mfano neno "الصلاة" "a'salaat", na kutamka kwa dhamma 'mim' ya wingi ikifuatiwa na 'hamza' kama katika kauli Yake Taala ﭽ ﯮ ﯯ ﯰ ﭼ , na kutamka kwa mkazo (shada) 'dhal' ya "يكذبون" katika kauli Yake Taala:ﭽ ﮊ ﮋ ﮌ ﮍ ﮎ ﮏ ﭼ badala ya kuikhafifisha tunakosoma sisi, na kutamka kwa dhamma 'sin' ya "سدّ" katika kauli Yake Taala:ﭽ ﯖ ﯗ ﯘ ﯙ ﯚ ﭼ pia kauli Yake Taala:ﭽ ﮙ ﮚ ﮛ ﮜ ﮝ ﮞ ﮟ ﮠ ﭼ badala ya kutamka kwa fat-ha katika kisomo chetu. Vile vile yeye kasoma "فِدْيَةٌ طَعامُ مَساكِين" kwa wingi badala ya "مِسْكِين" kwa umoja katika kisomo chetu, na kasoma kwa mkazo 'dal' katika kauli Yake Taala: ﭽ ﭮ ﭯ ﭰ ﭱ ﭼ wakati kisomo chetu ni kwa kukhafifisha, na kasoma pia "نَشْرًا" kwa 'nun' badala ya 'ba' katika kauli Yake Taala: ﭽ ﯤ ﯥ ﯦ ﯧ ﯨ ﯩ ﯪ ﯫ ﭼ na mfano wa hayo mengi.Nami kwa hakika nilisikitika kuwakuta wengi kati ya watu wa Omani wakati wa nyuma hawakushika kisomo cha msomaji mmoja maalumu katika Qur'ani yote. Walikuwa wakisoma "مَلِكِ يَوْمِ الدِّينِ" bila kuvuta 'mim' katika "ملِكِ" ingawa kisomo chao katika Qur'ani iliyobaki ni kisomo cha 'Aasim kinachofuatwa na watu wa Mashariki. Mfano mwengine karibu na huo ni kuto kufuata kwao kisomo cha upokezi wa Hafs kutoka kwa 'Aasim katika 'waw' ya "كُفُوًا" kwani wao waliitamka kwa hamza wakasoma "كُفُؤًا". Hapana shaka kuwa katika kusoma neno hilo kuna namna tatu : Ya kwanza ni kutamka kwa dhamma 'kaf’ na 'fa’ pamoja na kuwapo 'hamza’ mwisho wake, na hivi ndivo alivosoma Naafi’ na Abu 'Amr na Abu Bakr kutoka kwa 'Aasim na pia Abu Ja’far, isipokuwa Abu Ja’far aliisahilisha 'hamza’ na waliobaki waliisoma kwa 'tahqiqi’ pamoja na kuwapo khilafu katika mapokezi kutoka kwao au kwa baadhi yao. Ya pili ni kutamka kwa dhamma 'kaf’ na kuisakinisha 'fa’ na kuwapo 'hamza’ mwisho, ambacho ni kisomo cha Hamza na Ya’qub. Ya tatu ni kutamka kwa dhamma 'kaf’ na 'fa’ na kuibadili 'hamza’ kwa 'waw’, ambacho ni kisomo cha Hafs kutoka kwa 'Aasim. Na kwa kuwa sisi tunafuata katika Qur’ani yote upokezi wa Hafs kutoka kwa sheikh wake 'Aasim bin Abi A’Najuud haitupasi tuache kufanya hivyo. Haya ndiyo niliyotaka kuyabainisha, na Allah Ndiye Mwenye kutoa mafanikio. Allah amshushie rehma na amani Bwana wetu Muhammad na aali zake na sahaba zake. |