Published By Said Al Habsy  Je wanaruhusiwa walimu wa kike na wanafunzi wa kike kusoma Qur'ani na kuihifadhi wakiwa katika hedhi ?
Rai niionayo na kuitegemea ni kuwepo ulazima kwa mwenye hadathi kubwa - hedhi au nifasi au janaba wa kuepuka kusoma Qur'ani Tukufu kwa ajili ya utakatifu wa maneno ya Allah Taala. Na hii ndiyo inayooneshwa na hadithi aliyoipokea Imam A'Rabii' kwa Abu 'Ubaida kwa Jabir bin Zaid kasema: Kasema Mtume wa Allah –rehma za Allah na amani zimshukie- kuhusu mwenye janaba na mwenye hedhi na wale ambao hawako katika tohara "Hawasomi Qur'ani wala hawaushiki Msahafu kwa mikono yao mpaka wawe wametawadha", yaani wamejitoharisha tohara iliyowekwa na Sharia kwa ibada. Hadithi hii ingawa ni mursal (hakutajwa sahaba ambaye Jabir kaipokea kwake) lakini hadithi mursal za Jabir zina hukumu ya hadithi iliyotimia sanad yake. Juu ya hivyo inapewa nguvu kwa riwaya nyenginezo, ikiwamo waliyopokea Mashekhe Watano na akaisahihisha A'Tirmidhi, na akaitoa pia Ibnu Khuzaima, Ibnu Hibban, Alhaakim, Albazzaar, A'Daaraqutni na Albaihaqi, na kaisahihisha pia Ibnu Hibban, Ibnu A'Sakan, Abdul-Haq, na Albaghawi katika Sharhi A'sunna kutoka kwa Ali bin Abi Talib –Allah auenzi uso wake- kasema: "Alikuwa Mtume wa Allah –rehma za Allah na amani zimshukie- hufanya haja yake kisha hutoka akasoma Qur'ani, na alikuwa akila na sisi nyama na hakimzuilii kitu kusoma Qu'ani isipokuwa janaba". Tamko alopokea A'Tirmidhi: "Alikuwa akitusomesha Qur'ani katika kila hali ispokuwa akiwa na janaba". Na wenye ilmu wameitukuza hadithi hii kupita kiasi hata Ibnu Khuzaima akasema: Hadithi hii ni thuluthi ya rasilimali yangu. Na Shu'ba akasema: Sina hadithi nzuri kushinda hii. Na inajulikana kuwa hedhi na nifasi hazitafautiani na janaba, kwani kila moja yao ni hadathi kubwa kama janaba. Wala haisemwi huko ni kuacha tu kwa Mtume –rehma za Allah na amani zimshukie- hakufanywi dalili ya hukumu; itasemwaje hivo wakati mpokezi hadithi – naye ni Imam Ali – anataja wazi wazi kuwa janaba ndilo kizuizi baina yake na kusoma Qur'ani. Wala si katika yanayokubalika akilini kuwa Imam Ali aseme hayo kwa kubahatisha kwani yeye si katika wanaojisemea ovyo hususan kuhusu hukumu za kisharia. Abu Ya'la kapokea kutoka kwake kuwa kasema: "Nimemuona Mtume wa Allah –rehma za Allah na amani zimshukie- katawadha kisha akasoma kitu katika Qur'ani kisha aksema: Namna hivi kwa asiyekuwa na janaba; ama mwenye janaba hapana wala aya", nalo ni tamko wazi kuhusiana na suala hili. Vile vile Abu Daud, A'Tirmidhi na Ibnu Majah wametoa kutoka kwa Ibnu Umar –Allah awaridhie- kutoka kwa Mtume –rehma za Allah na amani zimshukie- kasema: "Hasomi mwenye janaba wala mwenye hedhi cho chote katika Qur'ani". Na haidhuru isemwe ilivosemwa kuhusu sanadi ya hadithi hii, kwani Ibnu Sayidin-naasi - ambaye ni miongoni mwa maimamu wa hadithi – kasema baadhi ya njia zake za upokezi ni sahihi. Na A'Daaraqutni kapokea kwa Jabir –Allah amridhie- kasema: Mtume –rehma za Allah na amani zimshukie- kasema "Hasomi mwenye hedhi wala mwenye nifasi katika Qur'ani cho chote". Riwaya hizi haijathibiti dalili inayozipinga na hilo linapasa isijuzu kuzipuuza. Mkijua hayo basi inabidi mujue kuwa kusoma wanafunzi wa kike na walimu wa kike Qur'ani siku zao za hedhi kwa ajili ya mitihani hakuna njia ya kukuruhusu. Kwani saumu ni fardhi isiyo budi kufafanuliwa, kaifafanua Allah katika Qur'ani, na kasamehewa mwenye hedhi na mwenye nifasi wakaamrishwa kuichelewesha mpaka watahirike, basi itakuwaje kwa kitu walichokipanga wanaadamu. Ni juu ya wakuu wanaohusika kuto kuubana wakati wa mtihani, bali inapasa uwe na vipindi viwili. Na Allah anajua zaidi, na Kwake mafanikio hupatikana. |