Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi
574. Abu Ubayda, kutoka kwa Jaabir bin Zayd, kutoka kwa Ibn Abbas (R.A.A.) kasema, "Kasema Mtume (S.A.W.), "
«الذَّهَبُ بِالذَّهَبِ وَالْفِضَّةُ بِالْفِضَّةِ وَالْبُرُّ بِالْبُرِّ وَالشَّعِيرُ بِالشَّعِيرِ وَالْمِلْحُ بِالْمِلْحِ يَدٌ بِيَدٍ».
Maana yake, “Dhahabu kwa dhahabu, na fedha kwa fedha, na ngano kwa ngano, na shayiri kwa shayiri, na chumvi kwa chumvi, mkono kwa mkono”.
575. Abu Ubayda, kutoka kwa Jaabir bin Zayd, kutoka kwa Abu Said L-Khudriyyi (R.A.A) kasema, “Kasema Mtume (S.A.W.):
«لاَ تَبِيعُوا الذَّهَبَ بِالذَّهَبِ وَلاَ الْفِضَّةَ بِالْفِضَّةِ وَلاَ الْبُرَّ بِالْبُرِّ إِلاَّ مِثْلاً بِمِثْلٍ، وَلاَ تَبِيعُوا بَعْضَهَا بِبَعْضٍ عَلَى التَّأْخِيرِ ».
Maana yake, “Msiuze dhahabu kwa dhahabu, wala fedha kwa fedha, wala ngano kwa ngano, isipokuwa kama zenye uzito na mfano mmoja, wala msiuze yenyewe kwa yenyewe ikiwa malipo yatakuwa baadae”.
576. Abu Ubayda, kutoka kwa Jaabir bin Zayd kasema, "Nilipata khabari kutoka kwa Talha bin Ubaydi Llaahi kwamba yeye alitaka fedha kwa mtu, Talha akachukua dhahabu mkononi mwake huku akiigeuza geuza akasema mpaka aje bwana fedha wangu kutoka msituni, na Umar bin Khattaab (R.A.A.) alikuwepo pale anasikia mazungumzo yao, akasema, "Ninaapa kwa Mola sitawaacha mpaka litimie jambo baina yenu, kwani nimemsikia Mtume (S.A.W.) akisema, "
«الذَّهَبُ بِالْوَرِقِ رِبًا إِلاَّ هَاءَ وَهَاءَ، وَالْبُرُّ بِالْبُرِّ رِبًا إِلاَّ هَاءَ وَهَاءَ، وَالتَّمْرُ بِالتَّمْرِ رِبًا إِلاَّ هَاءَ وَهَاءَ، وَالشَّعِيرُ بالشَّعِيرِ رِبًا إِلاَّ هَاءَ وَهَاءَ».
Maana yake, “Dhahabu kwa fedha ni riba ila nipe nikupe, na ngano kwa ngano ni riba ila nipe nikupe, na tende kwa tende riba ila nipe nikupe, na shayiri kwa shayiri riba ila nipe nikupe”.
577. A-Rrabi`I, kutoka kwa `Ubaada bin Ssaamit kasema, "Tulitoka kwenda vitani, na Mu`aawiyah alikuwa pamoja na sisi, tukapata dhahabu na fedha. Mu`aawiyah akamuamuru mtu mmoja awauzie watu kitakachopatikana kiwekwe katika hazina ya mali ya Waislamu, watu wakaziharakishia, akasimama `Ubaadat akawakataza wakazirudisha, yule mtu akaja kushtakia kwa Mu`aawiyah. Akasimama Mu`aawiyah akahutubia akasema, "Vipi wale watu wanaohadithia hadithi za Mtume (S.A.W.) ndani yake wakamsingizia Mtume (S.A.W.) Hadithi za uwongo ambazo hatujapata kuzisikia?” Akasimama `Ubaadat akasema, "Naapa kwa Allah kwamba nitawahadithia niliyosikia kutoka kwa Mtume (S.A.W.) hata kama atachukia Mu`aawiyah”. Akasema, "Mtume (S.A.W.) kasema, "
«لاَ تَبِيعُوا الذَّهَبَ بِالذَّهَبِ وَلاَ الْفِضَّةَ بِالْفِضَّةِ وَلاَ الْبُرَّ بِالْبُرِّ وَلاَ الشَّعِيرَ بِالشَّعِيرِ وَلاَ الْمِلْحَ بِالْمِلْحِ إِلاَّ مِثْلاً بِمِثْلٍ، يَدًا بِيَدٍ، سَوَاءً بِسَوَاءٍ، عَيْنًا بِعَيْنٍ».
Maana yake, “Msiuze dhahabu kwa dhahabu, wala fedha kwa fedha, wala ngano kwa ngano, wala shayiri kwa shayiri, wala chumvi kwa chumvi, isipokuwa kwa mfano mmoja, mkono kwa mkono, sawa kwa sawa za jinsi moja”.
578. Abu Ubayda, kutoka kwa Jaabir bin Zayd, kutoka kwa Ibn Abbas (R.A.A.), kutoka kwa Mtume (S.A.W.) kwamba, "Alinunua ngamia mmoja kwa wawili, na akaruhusu kumuuza mtumwa mmoja kwa wawili ila malipo yawe nipe nikupe".
(579) Abu Ubayda, kutoka kwa Jaabir bin Zayd, kutoka kwa Abu Said L-Khudriyyi (R.A.A.), “Kwamba Mtume (S.A.W.) alimtuma mtu kwenda Khaybar akamletea tende za aina nzuri kabisa. Mtume (S.A.W.) akasema, "
«أَكُلُّ تَمْرِ خَيْبَرٍ هَكَذَا»؟
Maana yake, “Jee, tende zote za Kheybar ni za aina hii?”.
Akasema, "Naapa kwa Mola si hivyo. Sisi tunachukua kipimo kimoja kwa tende za Khaybar kwa vipimo viwili za tende za huku, na kipimo kimoja kwa vipimo vitatu”. Mtume (S.A.W.) akasema, "
«لاَ تَفْعَلْ، بِعِ الْجَمْعَ بِالدَّرَاهِمِ، وَابْتَعْ بِالدَّرَاهِمِ جَنِيبًا».
Maana yake, “Usifanye hivyo. Uza tende mbaya kwa fedha, na ununue tende za aina nzuri kwa fedha”.
580. Abu Ubayda, kutoka kwa Jaabir bin Zayd, kutoka kwa Abu Said L-Khudriyyi (R.A.A.) kwamba, "Mtume (S.A.W.) alimruhusu mwenye mtende wa Ariya auze tende zilizo mtini kwa kadiri ya makadirio ya kipimo cha tende kavu zitakazotoa".
A-Rrabi`i kasema, "(العرايا) maana yake ni mtende ambao mazao yake yanachukuliwa, na kupewa watu wengine baadaye huambiwa, “Hapana chochote kingine kutoka kwangu”. Mtume (S.A.W.) alimruhusu auze tende zake kwa kipimo chake.
581. Abu Ubayda, kutoka kwa Jaabir bin Zayd, kutoka kwa Ibn Abbas (R.A.A.), kutoka kwa Abi Raafi`i mtumwa wa Mtume (S.A.W.) kasema, "Mtume (S.A.W.) alikopa (kwa mtu mmoja) ngamia dume mdogo, akaletewa ngamia wa zaka, akaniamuru nimlipe yule mtu ngamia wake mdogo, nikasema, "Sikumpata katika ngamia isipokuwa ngamia bora wa kiasi cha umri wa miaka saba kwenda juu, (Mtume (S.A.W.)) akasema, "
«اِقْضِهِ إِيَّاهُ فَإِنَّ خَيْرَ النَّاسِ أَحْسَنُهُمْ قَضَاءً».
Maana yake, “Mlipe, kwani bora ya watu ni yule mbora wao anayelipa”.
582. Abu Ubayda, kutoka kwa Jaabir bin Zayd, kutoka kwa Ibn Abbas (R.A.A.) kutoka kwa Mtume (S.A.W.) kasema, "
«أَلاَ وَمَنْ غَشَّنَا فَلَيْسَ مِنَّا، وَمَنْ لَمْ يَرْحَمْ صَغِيرَنَا وَلَمْ يُوَقِّرْ كَبِيرَنَا فَلَيْسَ مِنَّا».
Maana yake, “Hakika atakae tughushi hayuko na sisi. Na asiye waonea huruma wadogo wetu, na kuwaheshimu wakubwa wetu hayuko na sisi”.
583. Na kwa njia yake (Mtume (S.A.W.)) kasema, "
«إِذَا اخْتَلَفَ الْجِنْسَانِ...»
Maana yake, “Zikitofautiana jinsi mbili”. Hadithi hii imetajwa kikamilifu katika mlango wa, “Uuzaji wa khiyari na kwa shuruti”.
584. Abu Ubayda, kutoka kwa Jaabir bin Zayd, kutoka kwa Ibn Abbas (R.A.A.) kutoka, kwa Mtume (S.A.W.) kasema, "
«إِذَا اخْتَلَفَ الْجِنْسَانِ فَبِيعُوا كَيْفَ شِئْتُمْ».
Maana yake, “Zikitofautiana jinsi mbili uzeni mpendavyo”.
585. Abu Ubayda, kutoka kwa Jaabir bin Zayd, kutoka kwa Ibn `Abbas (R.A.A.), kutoka kwa Mtume (S.A.W.) kwamba, aliulizwa kuhusu mwaka wa shida, umeitwa hivyo kwa sababu ya kupanda bei, awawekee bei ya bidhaa masokoni, lakini Mtume (S.A.W.) akajizuia, akasema, "
«الْقَابِضُ الْبَاسِطُ هُوَ الْمُسَعِّرُ، وَلَكِنْ سَلُوا اللَّهَ».
Maana yake, “(Mola Ndiye) Mwenye kuzuia, Mwenye kutoa, Naye ndie Muwekaji wa bei, lakini mwombeni Allah”.
586. Abu Ubayda, kutoka kwa Jaabir bin Zayd, kutoka kwa Abu Hurayrah (R.A.A.), kutoka kwa Mtume (S.A.W.) kasema, "
«أَيُّمَا رَجُلٍ أَفْلَسَ فَأَدْرَكَ الرَّجُلُ مَالَهُ بِعَيْنِهِ فَهُوَ أَحَقُّ بِهِ مِنْ غَيْرِهِ».
Maana yake, “Akifilisika mtu (mnunuzi), na mtu aliyemuuzia akakuta mali yake bado iko kwake, na hakijapungua kitu, basi yeye ana haki zaidi katika ile mali kuliko mwingine (Yaani anaweza kuchukua ile mali yake kama alikuwa hakupewa thamani yake)”.
587. Abu Ubayda, kutoka kwa Jaabir bin Zayd, kutoka kwa Ibn Abbas (R.A.A.) kasema, "Mtume (S.A.W.) kasema, "
«لاَ شُفْعَةَ إِلاَّ لِشَرِيكٍ، وَلاَ رَهْنَ إِلاَّ بِقَبْضٍ، وَلاَ قِرَاضَ إِلاَّ بِعَيْنٍ».
Maana yake, “Hapana shufaa (ruhusa ya kuuza milki ya kitu) ila kwa mshirika wake, wala rehani ila kwa kukabidhi (kitu), wala kukopesha ila kwa kukiona kitu chenyewe (kwa macho yako)”.
|