Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi
3.Amesema Ar-Rabi`i bin Habiyb, "Amenihadithia Abu Ubaydah, kutoka kwa Jaabir bin Zayd kasema, “Imenifikia kutoka kwa Mtume wa ALLAH (S.A.W.) amesema, "
«عَلِّمُوا أَوْلاَدَكُمُ الْقُرْآنَ فَإِنَّهُ أَوَّلُ مَا يَنْبَغِي أَنْ يُتَعَلَّمَ مِنْ عِلْمِ اللَّهِ هُوَ».
Maana yake, “Wasomesheni watoto wenu Qur-ani, kwani kitu cha mwanzo kinachopasa kusomwa katika elimu ya ALLAH ni hiyo (Qur-ani)” .
4. Abu Ubaydah, kutoka kwa Jaabir Bin Zayd, kutoka kwa Abu Hurairah (R.A.A.) kutoka kwa Mtume wa ALLAH (S.A.W.) kasema, "
«إِذَا قَرَأْتَ الْقُرْآنَ فَرَتِّلْهُ تَرْتِيلاً وَلاَ تَغَنَّوْا بِهِ فَإِنَّ اللَّهَ يُحِبُّ أَنْ تَسْمَعَ الْمَلاَئِكَةُ لِذِكْرِهِ».
Maana yake, “Ukiisoma Qur-ani isome kwa sauti nzuri ya kupendeza, na wala (msiisome) kwa njia ya sauti ya kuimba, kwani ALLAH anapenda Malaika wasikie utajo wake (Qur-ani)”
5. Abu Ubaydah, kutoka kwa Jaabir bin Zayd, kutoka kwa Abu Sa`id L-Khudriyy, kasema, “Kasema Mjumbe wa ALLAH (S.A.W.), "
«مَثَلُ صَاحِبِ الْقُرْآنِ كَمَثَلِ صَاحِبِ الإِبِلِ الْمُعَقَّلَةِ، إِنْ عَاهَدَ عَلَيْهَا أَمْسَكَهَا، وَإِنْ أَطْلَقَهَا ذَهَبَتْ».
Maana yake, “Mfano wa (mtu) mwenye kuhifadhi Qur-ani, ni kama (mfano wa mtu) mwenye ngamia aliyemfunga na kamba, akimhifadhi atamkamata, na akimwachia huru atakwenda zake.”
6. Abu Ubaydah, kutoka kwa Jaabir Bin Zayd, kutoka kwa Ibn Abbas (R.A.A.) kasema, "Kasema Mtume wa ALLAH (S.A.W.), "
«مَنْ تَعَلَّمَ الْقُرْآنَ ثُمَّ نَسِيَهُ حُشِرَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ أَجْذَمُ».
Maana yake, “Atakaejifunza Qur-ani kisha akaisahau, atafufuliwa siku ya Kiyama mkono mmoja umekatwa.”
7. Abu Ubaydah, kutoka kwa Jaabir Bin Zayd kutoka Anas bin Maalik (R.A.A) kasema, "
مَا جَمَعَ الْقُرْآنَ عَلَى عَهْدِ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إِلاَّ سِتَّةُ نَفَرٍ كُلُّهُمْ مِنَ الأَنْصَارِ: أُبَيُّ, وَمُعَاذُ, وَ زَيْدٍ, وَأَبُو زَيْدٍ, وَأَبُو أَيُّوبٍ, وَعُثْمَانُ وَالْبَاقِي مِنَ الصَّحَابَةِ قَدْ يَحْفَظُ السُّوَرَ الْمَعْدُودَاتِ مِنَ الْقُرْآنِ، وَمِنْهُمْ مَنْ يَحْفَظُ السُّورَةَ وَالسُّورَتَيْنِ.
Maana yake, “Haikukusanywa Qur-ani zama za Mtume (S.A.W.) isipokuwa na watu sita na wote ni miongoni mwa L-Ansaary: Ubayyu, na Mu`adh, na Zayd na Abu Zayd, na Abu Ayyuub na Uthmaan Na wengine waliokuwa katika Masahaba, wakiwemo waliyohifadhi idadi za Sura za Qur-ani na wengineo wamehifadhi Sura au Sura mbili”.
8. Abu Ubaydah, kutoka kwa Jaabir Bin Zayd, kutoka kwa Abu Sa`id L-Khudriyy (R.A.A.) kasema, “Mtu mmoja alimsikia mtu akisoma (Qul-Huwa-Llaahu)
{قُلْ هُوَ اللَّهُ أَحَدٌ اللَّهُ الصَّمَدُ لَمْ يَلِدْ ولَمْ يُولَدْ ولَمْ يَكُن لَّهُ كُفُؤًا اَحَدٌ}
Na alikuwa akiirudia rudia Sura hiyo kila mara. Ilipofika asubuhi alimwendea Mtume (S.A.W.) akamhadithia khabari hiyo, na alikuwa yule mtu anajifundisha. Akasema Mtume (S.A.W.), "
«وَالذِي نَفْسِي بِيَدِهِ لإِنَّهَا لَتَعْدِلُ ثُلُثَ الْقُرْآنِ».
Maana yake, “Naapa kwa Yule ambaye nafsi yangu iko mkononi Mwake, hakika (Sura hiyo) ni sawa sawa na theluthi ya Qur-ani.”
9. Abu Ubaydah, kutoka kwa Jaabir Bin Zayd, kutoka kwa Abu Huraira (R.A.A.) kasema, “Nilifuatana pamoja na Mtume wa ALLAH (S.A.W.), akamsikia mtu mmoja anaisoma Qul-Huwa-Llaahu (Suratul Ikhlaas) mpaka mwisho wa Sura. Akasema, "
«وَجَبَتْ».
Maana yake, "Amestahiki". Nikauliza, “Kitu gani (kimemuwajibikia) ewe Mtume wa ALLAH?” Akajibu, "
«الجَنَّةُ»
Maana yake, " Pepo". Abu Huraira akasema, “Nilitaka nimwendee (yule) mtu nikambashirie (Pepo), (lakini) nilichelea kisinipite chakula cha mchana pamoja na Mtume (S.A.W.). Nikaona bora kula chakula cha mchana pamoja na Mjumbe wa ALLAH (S.A.W.), baadaye nikamwendea yule mtu (lakini kwa bahati mbaya) nikamkuta amekwisha ondoka”.
10. Abu Ubaydah, kutoka kwa Jaabir Bin Zayd kasema, “Nilisikia kuwa Umar Bin L-Khattaab (R.A.A.) alitoka pamoja na Mjumbe wa ALLAH (S.A.W.) katika baadhi ya safari zake. Umar Bin L-Khattaab (R.A.A.) alimuuliza (Mtume (S.A.W.) kitu fulani, (lakini) Mjumbe wa ALLAH (S.A.W.) hakumjibu. Halafu akamuuliza (tena) mara tatu (lakini pia) hakumjibu. Umar akasema katika nafsi yake, “Amekukosa mama yako ewe Umar! Umeng`ang`ania kumuuliza Mjumbe wa ALLAH (S.A.W.), na kwa mara zote hizo hakukujibu.” (Akaendelea) Umar akasema, "Nikamuendesha ngamia wangu, tukaenda mpaka nikawatangulia watu, nilikhofia isije ikashushwa Qur-ani dhidi yangu. Sikwenda (mbali) mara nikasikia ukelele wa mtu anaita, nikaongeza mwendo mpaka nikamfikia mjumbe wa ALLAH (S.A.W.) nikamtolea salamu, akasema, "
«لَقَدْ أُنْزِلَتْ عَلَيَّ سُورَةٌ هِيَ أَحَبُّ إِلَيَّ مِمَّا طَلَعَتْ عَلَيْهِ الشَّمْسُ»، ثُمَّ قَرَأَ: {إنَّا فَتَحْنَا لَكَ فَتْحًا مُّبِينًا}.
Maana yake, “Nimeteremshiwa Sura ambayo ninaipenda sana kuliko kila kinachochomozewa na jua. Kisha akasoma: {Inna Fatahna laka fat-han mubiinaa}”.
11.Abu Ubaydah, kutoka kwa Jaabir Bin Zayd, kasema, “Kasema Mjumbe wa ALLAH (S.A.W.), “Kwa wale waliopatwa na janaba, na wenye hedhi, na wale ambao hawako katika hali ya tohara, "
«لاَ يَقْرَؤُونَ الْقُرْآنَ، وَلاَ يَطَؤُونَ مُصْحَفًا بِأَيْدِيهِمْ حَتَّى يَكُونُوا مُتَوَضِّئِينَ».
Maana yake, “Wasiisome Qur-ani, na wala kuugusa msahafu kwa mikono yao, mpaka wawe wametawadha.”
12. Abu Ubaydah, kutoka kwa Jaabir Bin Zayd, kutoka kwa Sa`id L-Khudriyy (R.A.A.), kasema, “Mtume (S.A.W.) amekataza (mtu) kusafiri na huku amebeba Qur-ani kwenda kwenye nchi ya adui isije ikaangukia katika mikono ya maadui”.
Khofu inaweza kuwa sababu ya wao kuifanyia mambo machafu, au ya wao kukamatwa. Kasema Ar-Rabi`i Qur-ani kutajwa hapa inakusudiwa msahafu”.
13. Abu Ubaydah, kutoka kwa Jaabir Bin Zayd, kutoka kwa Ibn Abbas (R.A.A.) kutoka kwa Mtume wa ALLAH (S.A.W.), “Siku moja alikuwa ameketi na Sahaba zake, nikataja hadithi akasema Mtume (S.A.W.), "
«ذَلِكَ أَوَانُ يُنْسَخُ الْقُرْآنُ»
Maana yake, “Huo ndio wakati ambao Qur-ani itafutwa (itaondoshwa)” Akasema mtu mmoja Bedui, “Ewe Mtume wa ALLAH (S.A.W.) “Nini maana ya kuondoshwa, na vipi itaondoshwa?” Akajibu, "
«يُذْهَبُ بِأَهْلِهِ وَيَبْقَى رِجَالٌ كَأَنَّهُمُ الْبُغَاثُ».
Maana yake, “Kuondoshwa kwa watu wake (Wanavyuoni), na kubakia watu mfano wa ndege waliopotea.” (Yaani watu watakuwa hawafahamu hukumu za dini).
14. Abu Ubaydah kasema, “Imenifikia khabari kuwa Umar bin L-Khattaab (R.A.A.) alimsikia Hishaam bin Hakiim, akiisoma Suratil Furqaan kwa kisomo kingine tofauti na vile anavyosoma yeye, akasema Umar “Alikuwa Mjumbe wa ALLAH (S.A.W.) akinisomesha namna ya kusoma. Nikamkamkamata nguo yake shingoni, nikampeleka hadi kwa Mtume (S.A.W.) nikamwambia, “Ewe Mtume wa ALLAH, mimi nimemsikia (mtu) huyu anaisoma Suratil Furqaan namna nyingine si kama (vile) ulivyonifundisha kusoma. Mjumbe wa ALLAH (S.A.W.) akamwambia (yule mtu), "
«إقْرأ»
Maana yake, “Soma!” Akaisoma, Mjumbe wa ALLAH (S.A.W.) akasema, "
«هَكَذَا أُنْزِلَتْ»
Maana yake, “Hivi ndivyo ilivyoteremshwa.” Akasema Umar, “Akaniambia, “Soma!” Nikaisoma akaniambia, "
«هَكَذَا أُنْزِلَتْ، إِنَّ هَذَا الْقُرْآنَ نَزَلَ عَلَى سَبْعَةِ أَحْرُفٍ كُلُّهَا شَافٍ كَافٍ، فَاقْرَأُوا مَا تَيَسَّرَ مِنْهُ».
Maana yake, “Hivi ndivyo ilivyoteremshwa, hakika hii Qur-ani imeteremka kwa herufi saba, (na) zote zinaponesha, zenye rehema, na zenye kujitosheleza. Someni kiasi mnachoweza kuisoma”. Kasema Abu Ubaydah, “Watu wametofautiana katika maana ya usemi wa Mtume (S.A.W.). "
«نَزَلَ الْقُرْآنُ عَلَى سَبْعَةِ أَحْرُفٍ»
Maana yake, “Imeteremka Qur-ani kwa herufi saba.” Baadhi yao wamesema, “Kwa lugha saba.” Wengine wamesema, “Kwa namna saba: Ahadi ya kuingia Peponi, waadi wa kuingia Motoni, halali, haramu, mawaidha (maonyo), methali (mifano) na kutolea hoja” Na wengineo wamesema: “Halali, haramu, amri, makatazo, khabari zilizokwisha tokea kabla, khabari zitakazotokea wakati ujao, na mifano.” Na pia imesemwa: “Hakuna hata herufi moja ya Qur-ani inasomwa namna saba, na ALLAH ni mjuzi zaidi wa ukweli kwa tafsiri ya kuteremshwa.”
15. Abu Ubaydah kasema, "Nimepata khabari ya kuwa Mtume wa ALLAH (S.A.W.) alikuwa ikimteremkia Aya husema, "
«اِجْعَلُوهَا فِي سُورَةِ كَذَا وَكَذَا وَفِي مَوْضِعِ كَذَا وَمَا تُوُفِّيَ رَسُوْلُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إِلاَّ وَالقُرْآنُ مَجْمُوْعٌ مَتْلُوٌّ»
Maana yake, “Iwekeni kunako Sura kadha wa kadha, na katika sehemu kadha, na hakufariki Mtume wa ALLAH rehma na amani ziwe juu yake, isipokuwa Qur-ani yote imekusanywa na imesomwa.”
16. Kasema Ar-Rabi`i Bin Habiyb, kutoka kwa Abdul-`Alaa bin Daud, kutoka kwa Ikrima kutoka kwa Ibn Abbas (R.A.A.) kutoka kwa Mjumbe wa ALLAH (S.A.W.) kasema, "
«أُنْزِلَ الْقُرْآنُ كُلُّهُ جُمْلَةً وَاحِدَةً فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ إِلَى السَّمَاء الدُّنْيَا، وكَانَ اللَّهُ إِذَا أَرَادَ أَنْ يُحْدِثَ فِي الأَرْضِ شَيْئًا أَنْزَلَ مِنْهُ، حَتَّى جَمَعَهُ».
Maana yake, “Imeteremshwa Qur-ani yote kamili kwa pamoja, wakati wa usiku wa Lailatul Qadri mpaka kwenye mbingu ya dunia, na ilikuwa ALLAH Mtukufu akitaka kupitisha jambo ardhini, (basi) huiteremsha miongoni mwake (hiyo Qur-ani) mpaka (hatimaye) akaikusanya yote.” Akasema, "Alikuwa Mtume wa ALLAH (S.A.W.) akitoa hukumu katika jambo, basi ikishuka Qur-ani kinyume na hukumu yake, basi hairudishwi hukumu yake, na kufuatwa hukumu ya Qur-ani kwa jambo litakalokuja mbele.”
17.Kasema Ar-Rabi`i, kutoka kwa Yahya bin Kathiir, kutoka kwa Shu`ayb, kutoka kwa Qataada, kutoka kwa Ikrima, kutoka kwa Ibn Abbas (R.A.A.), kutoka kwa Mtume wa ALLAH (S.A.W.) kasema, "
«الْبَقَرَةُ وَآلُ عِمْرَانَ وَالنِّسَاءُ وَالْمَائِدَةُ وَالتَّوْبَةُ مَدَنِيَّاتٌ، وَالرَّعْدُ مَدَنِيَّةٌ إِلاَّ آيَةً وَاحِدَةً وَهِيَ: {وَلَوْ أَنَّ قُرْءَانًا سُيِّرَتْ بِهِ الْجِبَالُ أَوْ قُطِّعَتْ بِهِ الاَرْضُ...}
Maana yake, “Suratil Baqarah, na (Surat) Aal-`Imraan, na (Suratin) Nnisaa, na (Suratil) Maaidah, na (Surat) Tawba, ni Madaniyyaatu (yaani Sura zilizoteremshwa Madina), na (Suratir) Ra`ad ni Madaniyya isipokuwa Aya moja nayo:
{ وَلَوْ أَنَّ قُرْءَانًا سُيِّرَتْ بِهِ الْجِبَالُ أَوْ قُطِّعَتْ بِهِ الاَرْضُ...}
{Na kama ingelikuwa Qur-ani ndiyo inayoendeshewa milima, na kupasuliwa ardhi….}.
Na (Suratin) Nahl kuanzia aya ya arobaini, mpaka mwisho ni Madaniyy. Na (Suratil) Hajj ni Madaniyya isipokuwa Aya nne nazo ni,
{وَمَآ أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ...}
{ Na hatukumtuma kabla yako Mtume …………}
mpaka kauli ya Mola, “
{...عَذَابُ يَوْمٍ عَقِيمٍ}
{ …..adhabu ya Siku Tasa}
Makkiyya (yaani zimeteremshwa Makka). (Suratin) Nuur yote Madaniyya, na (Suratil) Ahzaab yote Madaniyya, na (Suratil) Qitaal, na (Suratil) Fat-h, na (Suratil) Hujuraat, ni Madaniyya. Na kuanzia (Suratil) Hadiyd Sura kumi mfululizo mpaka kauli isemayo:
{يَآ أَيُّهَا النَّبِيُّ لِمَ تُحَرِّمُ مَآ أَحَلَّ اللَّهُ لَكَ...}
{Ewe Nabii! Kwa nini unaharimisha alicho kuhalilishia ALLAH?}
Hizi zote ni (Sura) Madaniyya. Na (Surat) Lam Yakunil Ladhiina Kafaruu ni Madaniyya, na (Surat) Idhaa Ja-a Nasru Llaahi Walfat-h ni Madaniyya, na L-Mu`awwidhataani (yaani Surat Qul `Audhu Birabbi Nnaas na Qul `Audhu Birabbil Falaq, zote mbili) ni Madaniyya. Hizi ni Sura ishirini na Saba ziliokuwa Maddaniyya. Na Qur-ani kwa Sura zilizobakia zinatabiriwa kwamba ni Makkiyya.”
Kasema Ar-Rabi`i maana ya tamko la (الأَجْذَمُ) aliyekatwa mkono mmoja.
Watoharike, ama wenye janaba, na hedhi, na wenye damu ya ujusi hadi waoge josho kubwa.
|