Published By Said Al Habsy  Inapendeza wakati wa kuosha maiti awekwe juu ya ubao au kitanda cha kamba. Na inapendeza watakaomwosha maiti wawe ni jamaa zake wa karibu na ikiwa hakuna jamaa zake wa karibu basi wamwoshe wacha Mungu wenye kuhifadhi amana, na ikiwa hakuna basi sio neno yeyote yule atakaekuwepo katika waisilamu anaweza kumwosha. Kutoka kwa Bibi Aisha R.A.A.H, kasema, “
قَالَ لِيَلِهِ أَقْرَبُكُمْ مِنْهُ إِنْ كَانَ يَعْلَمُ فَإِنْ كَانَ لَا يَعْلَمُ فَمَنْ تَرَوْنَ أَنَّ عِنْدَهُ حَظًّا مِنْ وَرَعٍ وَأَمَانَةٍ.
Maana yake, “Kasema amsogelee (amkoshe) alie karibu nae kwa nasaba ikiwa anajua (kuosha), ikiwa hajui (kuosha), basi awe yule mnaye muona ana sehemu ya ucha mungu na mwaminifu”.
Na wakati wa kuosha wataanza kumsafisha sehemu ya utupu wake, kuanzia kitovuni mpaka magotini, bila ya kuufunua na kuuona utupu wake. Mwoshaji ataangiza mkono wake kwenye nguo iliyomstiri maiti na kumwosha ndani yake. Na ikiwa maiti alikuwa na maradhi ya kuambukiza, au waoshaji wana khofu ya kupata maradhi ya aina yeyote ile si vibaya ikiwa watakuwa wamevaa mipira ya mikono (glovusi). Halafu atakua kama anamkalisha, na kumkama tumboni kuondoa uchafu ulio tumboni. Na wakati wa kumwosha ataanzia kumwosha viungo vinavyotiwa udhu wa Salaa kwanza kwa kuanzia kuliani kwake. Hadithi ya Umm Attiya kasema, "Tulipokuwa tunamuosha Bint yake Mtume S.A.W., alisema, "
ابْدَأْنَ بِمَيَامِنِهَا وَمَوَاضِعِ الْوُضُوءِ مِنْهَا.
Maana yake, "Anzeni kumwosha kuliani kwake, na (waanze kwanza kumuosha) viungo vinavyooshwa wakati wa udhu." Yaani atamtia udhu kama udhu wa Salaa, na atamuosha kwa maji safi kama vile mtu anayekoga janaba, na mwisho atamuogesha kwa maji yaliyotiwa manukato. Na inatakiwa wanaoosha maiti wasitoe siri ya maiti. Kasema Mtume S.A.W, “
وَمَنْ سَتَرَ مُسْلِمًا سَتَرَهُ اللَّهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ.
Maana yake, "Na atakaye mstiri Mwislamu; Mwenyezi Mungu atamstiri siku ya kiyama." Pia kasema Mtume S.A.W,”
مَنْ غَسَّلَ مَيِّتًا فَأَدَّى فِيهِ الْأَمَانَةَ وَلَمْ يُفْشِ عَلَيْهِ مَا يَكُونُ مِنْهُ عِنْدَ ذَلِكَ خَرَجَ مِنْ ذُنُوبِهِ كَيَوْمِ وَلَدَتْهُ أُمُّهُ.
Maana yake, "Atakaemwosha maiti na akatimiza amana aliyopewa na wala asitoe siri ya aibu yake yoyote ile aliyonayo, atatokana na madhambi yake kama siku alivyozaliwa na mama yake."
|