Hakika mwezi wa Ramadhani ni msimu wa kufanya kheri, kwa hali hiyo isikupite fursa hii muhimu. Kufanya kheri ni jambo ambalo linahitajia kila muisilamu alikimbilie kwani mbali ya kumsogeza karibu na Mola Mtukufu, mtu hajui safari yake lini itafika, na mafao ya vitendo vyake alivyofanya kama vinamtosheleza, na nini kitamfalia anapokwenda. Hadithi ya Abu Huraira R.A.A. kasema, "Kasema Mtume S.A.W, [1] “Kasema Mola Mtukufu, “
وَمَا يَزَالُ عَبْدِي يَتَقَرَّبُ إِلَيَّ بِالنَّوَافِلِ حَتَّى أُحِبَّه،ُ فَإِذَا أَحْبَبْتُهُ كُنْتُ سَمْعَهُ الَّذِي يَسْمَعُ بِهِ، وَبَصَرَهُ الَّذِي يُبْصِرُ بِهِ، وَيَدَهُ الَّتِي يَبْطِشُ بِهَا، وَرِجْلَهُ الَّتِي يَمْشِي بِهَا، وَإِنْ سَأَلَنِي لأُعْطِيَنَّه،ُ وَلَئِنِ اسْتَعَاذَنِي لأُعِيذَنَّهُ.
Maana yake, “Ataendelea mja kunisogelea kwa vitendo vya nafla mpaka nampenda, na nikimpenda nakua masikio yake ambayo anasikia, na macho yake anayo onea, na mikono yake anayokamatia, na miguu yake ambayo anatembelea, na akiniomba nitampa, na akiniomba kinga namkinga (kinga kwa ajili ya moto, sheitani, mabalaa na kadhalika)”. Hivyo basi yeyote anae amini kuwepo kwa siku ya malipo, na kiyama, ajitahidi kuikimbilia kufanya kila kheri, kwani hayo ndio mafao yake pekee yatakayo mfaa, siku ambayo kutakuwa hakuna muombezi na wala msaidizi.
Yafuatayo ni mambo ambayo inapendeza kwa mtu aliyefunga kuyafanya wakati wa mwezi wa Ramadhani.
1.Kula daku.
Inapendeza mtu anaetaka kufunga, ale daku usiku wa kuamkia Saumu yake, ili kufuata Sunna ya Mtume S.A.W., na ili aweze kupata nguvu ya kufunga saumu, bila kudhoofika. Hadithi iliyohadithiwa na Anas R.A.A. kasema, "Kasema Mtume S.A.W.,[2] “
تَسَحَّرُوا فَإِنَّ فِي السُّحُورِ بَرَكَةً.
Maana yake, “Kuleni daku kwani katika (kula) daku kuna baraka.” Pia hadithi ya Abi Said R.A.A. kasema, "Kasema Mtume S.A.W.,[3] “
السَّحُورُ أَكْلُهُ بَرَكَةٌ فَلَا تَدَعُوهُ وَلَوْ أَنْ يَجْرَعَ أَحَدُكُمْ جُرْعَةً مِنْ مَاءٍ فَإِنَّ اللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى الْمُتَسَحِّرِينَ.
Maana yake, “Kula daku kuna baraka, basi msiiache daku hata kwa funda la maji. Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika wake wanawasalia (wana wabariki) wale wanaokula daku.” Pia hadithi iliyo hadithiwa na Ibn Abbas R.A.A. kasema, “Kasema Mtume S.A.W.,[4] “
لاَ تَزَالُ أُمَّتِي بِخَيْرٍ مَا عَجَّلُوا الإِفْطَارَ وَأَخَّرُوا السَّحُورَ.
Maana yake, “Bado umma wangu utakuwa katika kheri ikiwa wataharakisha kufuturu na watachelewesha kula daku.” Hadithi iliyohadithiwa na Abu Huraira R.A.A. kasema, "Kasema Mtume S.A.W.,[5] “
تَسَحَّرُوا فَإِنَّ فِي السَّحُورِ بَرَكَةً.
Maana yake, “Kuleni daku kwani katika kula daku kuna baraka.”
Kula daku pia ni miongoni wa kitendo kinachotofautisha funga yetu na funga za watu wa dini nyingine. Hadithi ya Umar bin A`as R.A.A. kasema, "Kasema Mtume S.A.W.,[6] “
فَصْلُ مَا بَيْنَ صِيَامِنَا وَصِيَامِ أَهْلِ الْكِتَابِ أَكْلَةُ السَّحَرِ.
Maana yake, “Tofauti baina ya saumu yetu na saumu ya watu wa kitabu (mayahudi na manasara) ni kula daku.” Na inapendeza mtu ale daku wakati wa mwisho wa usiku. Hadithi ya Anas bin Zaid bin Thabit R.A.A.. Kasema Anas, [7]“
تَسَحَّرْنَا مَعَ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ثُمَّ قَامَ إِلَى الصَّلاةِ قُلْتُ كَمْ كَانَ بَيْنَ الْأَذَانِ وَالسَّحُورِ قَالَ قَدْرُ خَمْسِينَ آيَةً.
Maana yake, “Tulikula daku pamoja na Mtume S.A.W. halafu akasimama kwa ajili ya kusali.” Nikasema, “Jee ilikuwa muda gani baina ya adhana na kula daku?” Akasema, “Kiasi cha (mtu kusoma) aya hamsini.” (Yaani takriban kiasi ya dakika kumi hivi).
2.Kuwa mkarimu na kusoma Quraani kwa wingi:
Inapendeza mtu aliefunga azidishe ukarimu wake, na azidishe kusoma Quraani. Hadithi ya Ibn Abbas R.A.A. kasema,[8] “
كَانَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَجْوَدَ النَّاسِ وَكَانَ أَجْوَدَ مَا يَكُونُ فِي رَمَضَانَ حِينَ يَلْقَاهُ جِبْرِيلُ وَكَانَ جِبْرِيلُ يَلْقَاهُ فِي كُلِّ لَيْلَةٍ مِنْ شَهْرِ رَمَضَانَ فَيُدَارِسُهُ الْقُرْآنَ قَالَ كَانَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ حِينَ يَلْقَاهُ جِبْرِيلُ عَلَيْهِ السَّلام أَجْوَدَ بِالْخَيْرِ مِنْ الرِّيحِ الْمُرْسَلَةِ.
Maana yake, “Mtume S.A.W. alikuwa mtu mkarimu sana kuliko watu wengine, na alikuwa mkarimu zaidi wakati wa mwezi wa Ramadhani wakati akikutana na (Malaika) Jibril. Na alikuwa Jibril akikutana nae kila usiku wa mwezi wa Ramadhani na kumfundisha Qur`ani”. Na akasema, “Mtume S.A.W. alikuwa mkarimu kwa kheri kuliko upepo mkali.”
3.Kuomba dua na kumdhukuru sana Mwenyezi Mungu.
Inapendeza kwa yule aliefunga kuzidisha kuomba dua za kheri kwa ajili ya dunia yake, na akhera yake, na pia kuwaombea waisilamu dua kwa wingi wakati wa saumu yake, kwani dua za mtu aliefunga zinapokelewa na kujibiwa haraka. Hadithi iliyohadithiwa na Abu Huraira R.A.A. kasema, "Kasema Mtume S.A.W.,[9] “
ثَلاثَةٌ لا تُرَدُّ دَعْوَتُهُمْ الْإِمَامُ الْعَادِلُ وَالصَّائِمُ حَتَّى يُفْطِرَ وَدَعْوَةُ الْمَظْلُومِ.
Maana yake, “Watu watatu dua zao hazirudishwi: Imam muadilifu na Mtu aliefunga mpaka afuturu, na dua ya mtu aliedhulumiwa.”
4.Kufuturu haraka.
Inapendeza yule aliefunga afuturu mara tu linapozama jua, yaani mara tu ikishaingia wakati wa magharibi. Kasema Sahl bin Saad, "Kasema Mtume S.A.W, [10]“
لَا يَزَالُ النَّاسُ بِخَيْرٍ مَا عَجَّلُوا الْإِفْطَارَ.
Maana yake, “Bado watu watakuwa wamo katika kheri ikiwa watakuwa wakiharakisha kufuturu.”
5.Kufuturu kwa vitu ambavyo havikugusa moto.
Wanavyuoni wanaonelea inapendezewa kufungua kinywa kwa kufuturu iwe kwa kile ambacho hakijagusa moto, kama ilivyokuwa mwenendo wa Mtume S.A.W. Hadithi iliyohadithiwa na Ibn Abbaas R.A.A. kasema, Ibn Abbas R.A.A, [11]“
كَانَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يُفْطِرُ عَلَى رُطَبَاتٍ قَبْلَ أَنْ يُصَلِّيَ فَإِنْ لَمْ تَكُنْ رُطَبَاتٌ فَعَلَى تَمَرَاتٍ فَإِنْ لَمْ تَكُنْ حَسَا حَسَوَاتٍ مِنْ مَاءٍ.
Maana yake, “Alikuwa Mtume S.A.W. anafuturu kwa tende mbivu kabla ya kusali, na ikiwa hakuna alikuwa akifuturu kwa tende kavu, na kama hizo hakuna (alikuwa akinywa) kwa funda za maji.”
6.Kuomba dua wakati wa kufuturu.
Inapendeza aliefunga wakati wa kufuturu kuomba dua, kwani wakati wa kufuturu ni wakati ambao dua hazirudishwi hujibiwa, na zinakubaliwa haraka. Hadithi ya Abdallah bin Umar bin Aas R.A.A. kasema, “Kasema Mtume S.A.W., [12] “
إِنَّ لِلصَّائِمِ عِنْدَ فِطْرِهِ لَدَعْوَةً مَا تُرَدُّ.
Maana yake, “Kwa yule aliefunga wakati wa kufuturu dua yake hairudishwi”. Na imethibiti kutoka kwa Mtume S.A.W. kwamba alikuwa akiomba dua wakati wa kufuturu. Hadithi ya Marwan bin Salim kasema, “Kasema Ibn Umar R.A.A., “Mtume S.A.W. wakati wa kufuturu alikuwa akisema,[13]“
ذَهَبَ الظَّمَأُ وَابْتَلَّتْ الْعُرُوقُ وَثَبَتَ الْأَجْرُ إِنْ شَاءَ اللَّهُ.
DHAHABA DHAMA`U WABTALLATIL-URUUQU, WA THABATAL-AJRU INSHAA` ALLAH.
Maana yake, “Kiu kimeondoka, na mishipa imerowana, na ujira utapatikana Mungu akipenda.” Pia hadithi nyingine iliyo hadithiwa na Mua`dh bin Zuhrah kasema, “Mtume S.A.W. alikuwa akisema wakati wa kufuturu,[14] “
اللَّهُمَّ لَكَ صُمْتُ وَعَلَى رِزْقِكَ أَفْطَرْتُ.
ALLAAHUMMA LAKA SUMTU WA ALAA RIZIQIKA AFTARUTU.
Maana yake, “Ewe Mwenyezi Mungu kwa ajili Yako nimefunga, na kwa riziki Yako nimefuturu.” Na ikiwa mtu amekaribishwa kufuturu kwa watu, inapendeza aseme (kuomba) dua hii, hadithi ya Anas R.A.A., kasema, “Mtume S.A.W alipokula kwa Sain bin Ubada alisema (aliomba dua hii),[15] “
أَكَلَ طَعَامَكُمُ الأَبْرَارُ، وَصَلَّتْ عَلَيْكُمُ الْمَلائِكَةُ، وَأَفْطَرَ عِنْدَكُمُ الصَّائِمُونَ.
AKALA TAAMAKUMU L`ABRARU WA SALLAT ALEIKUMU L`MALAAIKATU WA AFTARA INDAKUMU SSAAIMUUNA.
Maana yake, “Wamekula chakula chenu watu wema, na wakuombeeni dua Malaika, na wamefuturu kwenu walio funga”.
7. Kusali sala za usiku.
Kwa hakika sala za usiku zinafadhila kubwa sana, na ni sala zilizo bora baada ya sala za faridha. Hadithi iliyotolewa na Abu Huraira R.A.A. kasema, "Kasema Mtume S.A.W, “Kasema Mola Mtukufu,[16] “
يَقُولُ رَبُّنَا تَبَارَكَ وَتَعَالَى حِينَ يَبْقَى ثُلُثُ اللَّيْلِ الآخِرُ: مَنْ يَدْعُنِي فَأَسْتَجِيبُ لَهُ، مَنْ يَسْأَلُنِي فَأُعْطِيهِ، مَنْ يَسْتَغْفِرُنِي فَأَغْفِرُ لَهُ.
Maana yake, “Anasema Mola wetu Mtukufu inapobakia thuluthi ya (mwisho ya) usiku, “Nani ananiomba Nimjibu, nani Anaenitaka (haja) Nimpe, nani anaiomba msamaha Nimsamehe”.
Pia hadithi ya Jabir R.A.A. kasema, “Kasema Mtume S.A.W,“[17]
مَنْ خَافَ أَنْ لا يَقُومَ مِنْ آخِرِ اللَّيْلِ فَلْيُوتِرْ أَوَّلَهُ وَمَنْ طَمِعَ أَنْ يَقُومَ آخِرَهُ فَلْيُوتِرْ آخِرَ اللَّيْلِ فَإِنَّ صَلاةَ آخِرِ اللَّيْلِ مَشْهُودَةٌ وَذَلِكَ أَفْضَلُ.
Maana yake, “Ikiwa mtu atakhofia hawezi kusimama (kwa ibada) usiku wa mwisho, basi asali (sala ya) witri mwanzo (wa usiku), na yule mwenye shauku ya kusimama usiku wa mwisho, basi aisali (sala ya) witri usiku wa mwisho, kwani sala ya usiku wa mwisho inashuhudiwa na ni bora”.
8. Kusali Sala ya Tarawehe.
Sala ya Tarewehe ni sunna iliyothibiti kutoka kwa Mtume S.A.W. Naye Mtume S.A.W. aliiacha kuisali jamaa kwa kuhofia isije ikafaradhishwa kwa umma wake. Na aliye wakusanya watu kuisali pamoja jamaa ni Seyyidna Umar bin Khatab R.A.A. Baadhi ya wanavyuoni wanaonelea hii ni Sunna iliyotiliwa nguvu. Na sala hii ina fadhila kubwa. Kasema Abu Huraira R.A.A., "Kasema Mtume S.A.W., [18]“
مَنْ قَامَ رَمَضَانَ إِيمَانًا وَاحْتِسَابًا غُفِرَ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ.
Maana yake, “Atakaesimama (kufanya ibada usiku wa) Ramadhani akiwa na imani, na makini, basi atasamehewa madhambi yake yaliyopita.”
Sala hii iliitwa tarewehe kwa sababu watu walikua wakikirefusha kisomo chake katika sala. Nayo inasaliwa baada ya Sala ya Ishai, na wakati wake wa kusaliwa unamalizika pale unapoingia wakati wa kuingia wakati wa sala ya alfajiri. Nayo inasaliwa rakaa mbili mbili (yaani kila baada ya rakaa mbili mtu anatoa salam). Hadithi ya Ibn Umar R.A.A kasema, “Kasema Mtume S.A.W.,[19] “
صَلاةُ اللَّيْلِ مَثْنَى مَثْنَى.
Maana yake, “Sala ya usiku ni rakaa mbili mbili”.
Inasaliwa rakaa kumi na moja, rakaa nane Sunna ya Sala ya Tarawehe, na rakaa tatu Sala ya witri kama jinsi vile alivyosali Mtume S.A.W. Kutoka kwa Bibi Aisha R.A.A.H. kasema,[20] “
مَا كَانَ رَسُولُ اللَّهِ يَزِيدُ فِي رَمَضَانَ وَلا غَيْرِهِ عَلَى إِحْدَى عَشْرَةَ رَكْعَةً، يُصَلِّي أَرْبَعًا فَلا تَسْأَلْ عَنْ حُسْنِهِنَّ وَطُولِهِنَّ، ثُمَّ يُصَلِّي أَرْبَعًا فَلا تَسْأَلْ عَنْ حُسْنِهِنَّ وَطُولِهِنَّ ثُمَّ يُصَلِّي ثَلاثًا.
Maana yake, “Alikuwa Mtume S.A.W. hazidishi katika mwezi wa Ramadhan wala wakati mwingine zaidi ya rakaa kumi na moja. Alikwa akisali rakaa nne na usiniulize unyenyekevu wake na urefu wake, halafu anasali rakaa nne nyingine usiniulize unyenyekevu wake, na urefu wake, halafu anasali rakaa tatu”. Na ni wakati wa Seyyidna Umar R.A.A. ambapo iliongezwa kufikia rakaa ishirini, hivyo basi si vibaya mtu akitaka kuzidisha.
9. Kuzidisha ibada siku za mwisho za Ramadhani.
Katika usiku mmoja wa siku kumi za mwisho wa mwezi wa Ramadhani, kuna usiku wenye heshima kubwa ambao unajulikana kama usiku wa “Lailatul Qadri”. Usiku huu una fadhila sana, ibada ya usiku huu ni bora zaidi kuliko ibada ya miezi elfu moja. Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Al-Qadr aya ya 3, “
﴿لَيْلَةُ الْقَدْرِ خَيْرٌ مِّنْ أَلْفِ شَهْرٍ﴾.
Maana yake, “Huo usiku wa heshima ni bora kuliko miezi elfu”. Ikiwa mtu atasimama usiku huo kufanya ibada kwa dhati na yakini, basi Mwenyezi Mungu Mtukufu, atamsamehe madhambi yake yote. Hadithi ya Abu Huraira R.A.A. kasema, “Kasema Mtume S.A.W.,[21] “
وَمَنْ قَامَ لَيْلَةَ الْقَدْرِ إِيمَانًا وَاحْتِسَابًا غُفِرَ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ.
Maana yake, “Atakaesimama usiku wa Lailatul Qadr (kwa ajili ya kufanya ibada) akiwa na imani, na kwa makini, basi atasamehewa madhambi yake yaliyopita.” Na inapendeza katika usiku wa siku hizi za kumi la mwisho za mwezi wa Ramadhani mtu kuomba dua ambayo Mtume S.A.W., aliyomueleza Bibi Aisha R.A.A.H. kuiomba. Kasema Bibi Aisha R.A.A.H. kumuuliza Mtume S.A.W.[22], “
يا رَسُولَ اللَّهِ أَرَأَيْتَ إِنْ وَافَقْتُ لَيْلَةَ الْقَدْرِ مَا أَدْعُو قَالَ تَقُولِينَ اللَّهُمَّ إِنَّكَ عَفُوٌّ تُحِبُّ الْعَفْوَ فَاعْفُ عَنِّي.
Maana yake, “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.) jee ikiwa nitaupatia usiku wa Leilatul Qadr, jee niombe nini? Akajibu, “Sema, "ALLAHUMMA INAKA AFUUN TUH`B`BU AL`AFUAA FAA AFUANII"
Maana yake, “Ewe Mwenyezi Mungu Wewe ni Msamehevu, unapenda kusamehe basi nisamehe.”
Inshaallah tutaeleza kwa kirefu habari zinazohusiana na usiku wa Lailatul Qadr hapo mbele. Yeye Mtume S.A.W. wakati wa kumi la mwisho la Ramadhani alikuwa akizidisha sana kufanya ibada kuliko siku nyingine zozote zile. Kasema Bibi Aisha R.A.A.H, [23]“
وَكَانَ إِذَا دَخَلَ الْعَشْرُ أَحْيَا اللَّيْلَ وَشَدَّ الْمِئْزَرَ وَأَيْقَظَ أَهْلَهُ.
Maana yake, “(Mtume S.A.W.) Na likiingia kumi la mwisho la Ramadhani alikuwa akiuuhiisha[24] usiku wake na kupania kikoi chake[25] na akiiamsha ahali[26] yake (kufanya ibada za usiku),” Pia hadithi nyingine ya Bibi Aisha R.A.A.H, kasema, [27]“
كَانَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَجْتَهِدُ فِي الْعَشْرِ الْأَوَاخِرِ مَا لَا يَجْتَهِدُ فِي غَيْرِهِ.
Maana yake, “Alikuwa (Mtume S.A.W.) akijitahidi zaidi (kwa ibada) katika kumi la mwisho zaidi kuliko alivyokuwa akijatihidi wakati mwingine wowote ule.”
10. Kufuturisha watu.
Inapendeza kwa mtu aliye na uwezo awafutarishe waliyofunga, kwani sio watu wote wanamiliki cha kufutilia, na kitendo hiki kina fadhila sana. Hadithi iliyohadithiwa na Zaid bin Khalid R.A.A. kasema, “Kasema Mtume S.A.W.,[28] “
مَنْ فَطَّرَ صَائِمًا كَانَ لَهُ مِثْلُ أَجْرِهِ غَيْرَ أَنَّهُ لَا يَنْقُصُ مِنْ أَجْرِ الصَّائِمِ شَيْئًا.
Maana yake, “Atakaemfurisha aliyefunga, basi ujira wake utakuwa kama ujira wa yule aliefunga bila ya kupungua ujira wa aliyefunga chochote kile”.
11.Kufanya umra katika mwezi wa Ramadhani.
Kufanya umra katika wa mwezi wa Ramadhani ni moja ya ibada yenye fadhila kubwa sana. Hadithi ya Atta kasema, “Nimemsikia Ibn Abbas R.A.A akisema, “Nimemsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. akimueleza mwanamke mmoja wa ki Ansar akisema, “Kipi kilichokuzuia kufanya Hajj pamoja na sisi.” Akajibu kwa kusema, “Tulikuwa na ngamia, na baba wa Fulani, na mtoto wake walimchukua na wakatuachia ngamia mwingine kwa ajili ya kumwagilia maji.” Mtume S.A.W. akajibu akasema,[29] “
فَإِذَا كَانَ رَمَضَانُ اعْتَمِرِي فِيهِ فَإِنَّ عُمْرَةً فِي رَمَضَانَ حَجَّةٌ.
Maana yake, “Ikifika Ramadhani fanya umra, kwani umra wakati wa Ramadhani, ni (kama) Haji (kwa zile thawabu zake).” (Au alisema kitu kinachofanana na hicho).” Pia hadithi iliyo hadithiwa na Ibn Abbas R.A.A. kasema, "Kasema Mtume S.A.W., [30]“
فَعُمْرَةٌ فِي رَمَضَانَ تَقْضِي حَجَّةً أَوْ حَجَّةً مَعِي.
Maana yake, “Umra wakati wa Ramadhani kama Haji, au Haji pamoja na mimi.”
12. Kufanya itikafu.
Kufanya itikafu ni kujitenga kwa kukaa msikitini kwa ajili ya ibada. Na huu ulikuwa ni mwenendo wa Mtume S.A.W. kukaa itikafu siku kumi za mwisho za mwezi wa Ramadhani kwa ajili ya ibada. Hadithi ya Ibn Umar R.A.A. kasema, [31]“
كَانَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَعْتَكِفُ الْعَشْرَ الْأَوَاخِرَ مِنْ رَمَضَانَ.
Maana yake, “Alikuwa Mtume S.A.W. anakaa itikafu siku kumi za mwisho za Ramadhani.” Pia kasema Bibi Aisha R.A.A.H.,[32] “
كَانَ يَعْتَكِفُ الْعَشْرَ الْأَوَاخِرَ مِنْ رَمَضَانَ حَتَّى تَوَفَّاهُ اللَّهُ ثُمَّ اعْتَكَفَ أَزْوَاجُهُ مِنْ بَعْدِهِ.
Maana yake, “Alikuwa Mtume S.A.W. akikaa itikafu siku kumi za mwisho za Ramadhani, mpaka Mwenyezi Mungu S.W.T. alipomfisha, halafu wake zake walikuwa wakikaa itikafu baada yake.”
13.Kupiga Msuwaki.
Katika kupiga msuwaki kuna fadhila kubwa. Hadithi ya Abu Huraira R.A.A. kasema, “Kasema Mtume S.A.W., [33]“
لَوْلا أَنْ أَشُقَّ عَلَى أُمَّتيْ لأمَرْتُهمْ بِالسِّواكِ عِنْدَ كُلِّ صَلاةٍ وَكُلِّ وُضُوءٍ.
Maana yake, “Lau kama sioni taabu kuutia umma wangu katika mashaka basi ningeliwaamrisha kupiga msuwaki wakati kila Sala na kila udhu”.
[1] Bukhaari 20/158 (6021).
[2] Bukhaari 7/3 (1789), Muslim 5/387 (1835), Ibn Maajah 5/208 (1682) na wengineo.
[3] Musnad Ahmad 22/209 (10664), Ahmad Hambal 3/12 (11101).
[4] Al-Imamu Al Rabi`u 1/130 (320).
[5] AAn-Nasaai`y 7/310 (2119).
[6] Abu Daawud 6/287 (1996), At-Tirmidhiy 3/144 (643), Muslim 5/388 (1836).
[7] Ibn Maajah 5/211 (1648), At-Tirmidhiy 3/136 (638), Bukhaari 6/500 (1787), Muslim 5/389 (1839).
[8] AAn-Nasaai`y 7/242 (2068), pia imetolewa na Bukhaari na Muslim kwa lafdhi tofauti kidogo.
[9] Ibn Maajah 5/294 (1742), At-Tirmidhiy 12/25 (3522), Ahmad 16/241 (7700).
[10] Ibn Maajah 5/215 (1687), At-Tirmidhiy 3/132 (635), Bukhaari 7/59 1821), Muslim 5/390 (1838).
[11] Abu Dawud 6/306 (2009), At-Tirmidhiy 3/126 (632), Ahmad 25/251 (12215).
[12] Ibn Maajah 5/295 (1743).
[13] Abu Daawud 6/308 (2010), Ddaraqtuny 2/185 (25)
[14] Ttabaarany 2/133 (912), Abu Daawud 6/309 (2011).
[15] Ahmad 25/3 (11957).
[16] Al-Imamu Al Rabi`u 1/202 (501).
[17] Muslim 4/129 (1255).
[18] Abu Daawud 4/135 (1164), Ibn Maajah 4/321 (1316), At-Tirmidhiy 3/303 (736), An-Nasaai`y 6/69 (1584), Bukhaari 1/65 (36).
[19] Bukhaari 4/71 (936)
[20] Abu Daawud 4/111 (1143), Bukhaari 4/319 (1079), Muslim 4/89 (1219).
[21] Abu Daawud 4/136 (1165), Bukhaari 1/61 (34).
[22] Ibn Maajah 11/305 (3840), Ahmad Bin Hambal 6/183 (25536).
[23] Abu Daawud 139/4 (1168), Ibn Maajah 5/319 (1758), Muslim 6/95 (2008).
[24] Akikesha huku akifanya ibada.
[25] Yaani akijitahidi kwa juhudi zote kamilifu kuzidisha ibada.
[26] Watu wa familia moja inaweza kuwa mke au watu wengine wa nyumbani lakini aghlabu inatumika sana kwa kumtambulisha mke.
[27] Ibn Maajah 5/318 (1757), Muslim 6/96 (2009).
[28] Ibn Maajah 5/385 (1736), At-Tirmidhiy 3/301 (735).
[29] Bukhaari 6/284 (1658), Ddaaramy 2/73 1859).
[30] Muslim 6/327 (2202).
[31] Abu Daawud 6/463 (2109), Bukhaari 7/156 (1885).
[32] Bukhaari 7/157 (1886), Muslim 6/91 (2006).
[33] Al-Imamu Al Rabi`u 1/52 (86).
- Published in Yanayopendeza mwezi wa Ramadhani
- Written by SH. Abdullah Al Shueli