Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi 
بسم الله الرحمن الرحيم
Shukurani zote ni kwa Allah mtukumu, na rehma na amani ziwe kwa Mtume wake Muhammad pamoja na kila aliyeongoka kwa uongofu wake kuanzia kwa masahaba wake na aali zake na waliofuatia kwa wema mpaka siku ya malipo.
Tujue kuwa Allah mtukufu kwa fadhila zake ameikamilisha neema yake ya Uislamu katika uhai wa Mtume wetu Muhammad (s.a.w), basi ilisimama hukumu yake ya kuhukumu jamii kwa sheria ya Allah katika uhai wa Mtume (s.a.w), na baada ya kufariki Mtume (s.a.w) Waumini walichagua viongozi walioongoza kiuadilifu mpaka mwaka wa 38 Hijiria, kisha baada ya hapo zikatanda fitna ambazo ziliathiri uongozaji moja kwa moja, na katika hali hiyo walipatikana watetezi wa haki waliohifadhi mafundisho na kuisoma hali ya jamii iliyokua ikijiri, kwa kuweka misingi madhubuti ya kuihifadhi dini ili isije ikaathirika na mapenyezo ya kimafundisho kutoka kwa maadui zake; kwani bila ya shaka mafundisho ndio muhimu zaidi katika risala ya uislamu.
Basi ilipatikana madrasa ya Imam Jabir bin Zaidi Al-Uzdi (r.a) naye ni mwanachuoni muomani aliyezaliwa katika kipindi cha utawala wa Omar bin Al-Khattabi (r.a) na kufariki mwisho wa karne ya mwanzo hijiria mwaka 96 Hijiria, mwanachuoni huyu alichukua elimu yake moja kwa moja kutoka kwa Masahaba wa Mtume wetu (s.a.w) Allah awe radhi nao, basi chuo chake kwa taufiqi ya Allah kiliweza kutoa maulamaa wenye ujuzi mzuri sana katika Dini, wafuasi wa chuo hichi ndio waliojulikana baadae kwa jina la Ibadhi.
Chuo hichi kiliweza kutoa viongozi bora walisimamisha utawala wa kiislamu kwa misingi ya Qur-ani na Sunna ya Mtume wetu Muhammad (s.a.w), na sisi hatujui kuwa katika tarehe ya Waislamu tokea kuangushwa utawala wa Imam Aliy (k.a.w) kuwa iliweza kusimama Dola kwa misingi ya Shuura na Uadili isipokua kaatika safu za Maibadhi peke yao, hatukatai kuwa alikuja Mtawala mmoja muadilifu katika Dola ya Bani Umayyah naye ni Omar bin Abdilaziz (r.a) ambaye alihukumu kipindi cha miaka miwili mwishoni mwa karne ya mwanzo.
Basi Maibadhi waliweza kufanyia kazi msingi wa Shuura kikamilifu na kuteua viongozi waadilifu katika sehemu walizokuwepo na kupata nguvu ndani yake, nazo ni sehemu tatu maarufu.
1. Yemen.
2. Oman.
3. Afrika Kaskazini.
Basi katika sehemu yetu hii tutakua na utambulisho wa Maimamu wa Kiibadhi waliohukumu.
Tunamuomba Allah atukubali na atupe taufiqi yake katika njia hii njema.
Asanteni sana. |