Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi Suali:Kweli kiumbe kinaweza kumwambia kiumbe mwengine: ((Hakika mimi ndiye Mwenyezimungu hakuna mungu mwengine isipokuwa mimi, basi niabudu mimi?)). JAWABU:Ama kuhusu uwezekano wa kiumbe kuweza kumwambia kiumbe mwengine neno hilo, kwa hakika Maluuni Firauni aliwambia watu neno la kudai uungu, aliwambia: ((Sijui mimi kama munae nyinyi mungu mwengine asiyekuwa mimi)) [Qasas 38], na neno lake hilo lilimuingiza katika ukafiri wa kishirikina, na likamtopeza katika dhulma nyingi za kuwadhulumu waja, na sote tunalifahamu hilo, kwa hiyo ikiwa inakusudiwa uwezekano wa kutokezea hilo, basi hilo limetokezea nalo amelieleza Allah mtukufu katika Kitabu chake wazi wazi. Ama ikiwa inakusudiwa kuweza kiumbe kulisema hilo nalo likawa ni haki kwa kiumbe huyo, kwa hakika hilo haliwezekani, na kiumbe yoyote atakayelisema hilo kwa kulidai kwa nafsi yake basi kiumbe huyo atakuwa ni mbatilifu muovu mpofu mpotovu, na nafasi yake itakuwa katika ukafiri ni sawa na nafasi ya Mlaaniwa Firauna katika hilo, isipokuwa kama atatubia kabla ya kufikiwa na mauti. Ama ikiwa inakusudiwa kuweza kiumbe kulifikisha neno hilo kwa kiumbe mwengine kwa kulisikia kiumbe mkusudiwa kupitia kwa kiumbe mwenzake hali ya kuwa ni ujumbe unaotoka kwa Allah mtukufu uliomfikia kiumbe mkusudiwa kwa kupitia kwa kiumbe mwengine, kwa hakika hilo linafaa, nalo lina dalili ya wazi ndani ya Qur-ani tukufu, na sisi hatumjui anayelipinga hilo asalan. Imekuja katika Kitabu cha Allah kilichobarikiwa: ((Isipokuwa wale waliotubia na wakaboresha na wakabainisha basi hao nitawasamehe, na mimi ni msamahevu mrehemevu)) [Baqarah 160]. Kwa hakika neno hili amelisema Kiumbe (Jibrilu (a.s)) kumwambia Kiumbe (Mtume wetu Muhammad (s.a.w)) na Kiumbe (Mtume wetu) amelisema hivo hivo kuwambia Viumbe (Umati wake), na kila mwenye kusalisha anapolifika neno hilo hulisoma, na hapo bila shaka huwa analisema kama lilivyo. Kwa hakika sisi huwa tunawashangaa sana wale wenye kuleta suala hili mbele ya Ibadhi, kwa lengo la kudai kwao kuwa Qur-ani haiwezekani kuwa ni Kiumbe kwa sababu ndani ndani yake limo neno ((Hakika mimi ndiye Allah hakuna mungu isipokuwa mimi basi niabudu)) wakidai kuwa vipi kiumbe atayasema haya?! Na kwa vile Qur-ani imeyasema haya basi haitakuwa kiumbe. Tunawambia hawa: Kwa hakika neno lenu hilo ni la ajabu sana, tena sana, hivi hamufikiri nyinyi?!! Basi inakulazimuni nyinyi -kwa mujibu wa neno lenu hilo- kuanzia leo kuiabudu Qur-ani na kuitakidi kuwa Qur-ani ndiye Allah hasa wa kuabudiwa; kwa sababu Qur-ani ndiyo iliyoyasema hayo kwa mujibu wa madai yenu hayo, basi watangizieni walimwengu kuanzia leo kuwa Qur-ani ndiye Mungu, na Allah ndiye Qur-ani, na Qur-ani ni Kitabu kilichobarikiwa kwa hiyo Allah atakuwa ni kitabu kilichobarikiwa, hayo ni kwa mujibu wa maneno yenu hayo. Ama sisi -tunamshukuru Allah mtukufu kwa uongofu wake- tunawambia hawa kuwa Qur-ani ni kiumbe mfikishaji wa mkusudiwa wa maneno hayo, na maneno ni kwa muhusika wake na sio kwa mfikishaji wake. Na kwa hakika Mtume Mussa (a.s.w) aliyasikia hayo kupitia Kiumbe kinachoitwa maneno yaliyobebwa na kiumbe kinachoitwa sauti, na yeye alifahamu ni nani mkusudiwa, basi hakuabudu sauti iliyobeba ujumbe, wala hakuabudu ujumbe ambao ni maneno; kwani vyote hivo ni viumbe havipasi kuabudiwa, bali alimuabudu mkusudiwa aliyeumba hayo maneno na sauti iliyomfikia. Na sisi tunafahamu bila ya shaka yoyote kuwa maneno yote ni viwakilishi vya maana kusudiwa; kwa hiyo maneno yote ni viumbe, ama mkusudiwa katika maana yake ikiwa sio kiumbe basi siyo kiumbe, na ikiwa ni kiumbe basi ni kiumbe. Katika Qur-ani kuna maneno kama vile Moto, Pepo, Mbingu, Iblisi, Firauni, jee ndio tuseme kuwa hao sio viumbe?!!! au tusema hayo maneno sio viumbe?!!! Na hoja za kuwa Qur-ani ni miongoni mwa viumbe ziko wazi kwa anayetaka haki na kuikusudia, unaweza kufuata kiunganishi katika somo hilo. https://ibadhi.com/vipindi/161-vitabu/5775 Wabillahi Taufiqi. Wallahu aalamu wa ahakamu.
|
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi SUALI:Jee! Huu ulimwengu Allah aliuumba kutoka ndani na nafsi yake au nje ya nafsi yake, au aliuumba ulimwengu huu si kutoka ndani ya nafsi yake au nje ya nafsi yake? JAWABU:Hili suali ni batili; kwa sababu muulizaji anaulizia kuhusu Allah mtukufu kwa makadirio batili, nayo ni makadirio ya kuwa Allah mtukufu ni mwili miongoni mwa miili; kwa sababu mwili ndio wenye ndani na nje, kwa hiyo ni suali batili kwa kubeba kwake madhumuni batili yasiyostahiki kwa Allah mtukufu. Hatuwezi kumuulizia Allah mtukufu kwa lazimisho la maumbile, na suali lolote linalomuulizia Allah mtukufu kwa malazimisho ya kimaumbile suali hilo ni batili katika haki yake Allah mtukufu, kwa hiyo ni batili kumuulizia Allah mtukufu kuwa eti kauumba ulimwengu ndani ya nafsi yake au nje ya nafsi yake? au yumo ndani ya ulimwengu au amechana na ulimwengu kimasafa? au yuko wapi.... n.k. Masuala haya huyauliza wenye kumuitakidi Allah kuwa ni mwili (Mujassimah), au asiyemjua Muumba wa huu ulimwengu. Kwa hiyo jawabu yetu: Allah mtukufu ametakasika na kuwa na sifa za kudhibitika kimipaka; kwani yeye ndiye wa Mwanzo aliyeumba sehemu na mambo yake yote, na akili zetu na fahamu zetu sisi waja hazina uwezo wa kufikiria nje ya mipaka ya sehemu na wakati, kwa hiyo hatuwezi sisi kukifikiria chochote kilichoko katika mipaka ya sehemu na wakati isipokuwa kitakuwa ni kiumbe tu, basi kila kinachodhibitiwa kifikra kwa mipaka ya sehemu hicho ni kiumbe bila ya shaka yoyote, na Allah mtukufu hajafanana nacho hicho kwani yeye ndiye Muumba. Allah mtukufu kuwepo wake ni kabla ya sehemu na wakati; kwa hiyo kuwepo kwa sehemu na wakati na kukosekana kwa sehemu na wakati ni sawa kwake yeye Allah mtukufu wala hakuathiri chochote kwake yeye Allah mtukufu, basi sehemu zote ni sawa kwake yeye Allah mtukufu. Sisi tunamjua Allah mtukufu kwa dalili za vitendo vyake, na sio kwa kumjengea sura fulani yenye mipaka ya sehemu. Tunamsifu Allah mtukufu kwa yanayokubaliana na utukufu wake wa kidhati, pia tunamtakasa Allah mtukufu na yote yasiyokubaliana na utukufu wake wa kidhati, na msingi wetu katika hilo ni kuwa yeye ni Mkwasi (ALGHANIYYU); kwa hiyo hasifiki na sifa yoyote kwa namana ya kuihitajia sifa hiyo, wala kwa namna ya kuwa na sifa hiyo lazimisho la kuhitajia. Kwa dalili za kumjua Allah mtukufu fuata kiunganisho hapo chini. https://ibadhi.com/vipindi/jamii/384-allah-mtukufu Wabillahi Taufiiq. Wallahu aalamu wa ahkam |
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi SUALI:Tumesoma kuwa Qur-ani ni kiumbe, kwa kweli dalili ni zenye kukinaisha lakini tumeambiwa Qur-ani ni maneno ya Allah na Allah ametuambia akitaka kuumba kitu hukiambia (KUN) nacho huwa, sasa ikiwa maneno ya Allah ni kiumbe italazimika kuwa (KUN) ni kiumbe, na ikiwa (KUN) ni kiumbe itahitajia kuambiwa na Allah (KUN) ya kuiumba na italazimika katika hii (KUN) yaliyolazimika katika (KUN) iliyotangulia na hapo itakuwa kila (KUN) inahitajia (KUN) na kupelekea hilo mtiririko usiowezekana, sasa hivi kweli hii (KUN) imeumbwa? Kwani ikiwa haikuumbwa itakuwa maneno ya Allah sio kiumbe, naomba ufafanuzi katika hili. JAWABU:Ni hakika isiyokuwa na shaka kuwa Qur-ani tukufu imeumbwa hayo ni kwa mujibu wa dalili nyingi zisizopingika katika kuthibitisha usahihi wa Itikadi ya kuumbwa kwake, na tunaweza kurejea kusoma maudhui ya kuumbwa Qur-ani kwa kubofya hapa. Basi hakuna shaka katika kuumbwa neno (KUN) kwani neno hilo ni miongoni mwa meneno ya Qur-ani tukufu ambayo ni maneno ya Allah mtukufu, na malazimisho yaliyokuja katika suali hayana dalili ndani yake kwa sababu zifuatazo:-
Katika kuthibitisha haya tuangalie katika uumbwaji wa Baba yetu Adam, anatuambia Allah mtukufu. إِنَّ مَثَلَ عِيسَى عِنْدَ اللَّهِ كَمَثَلِ آدَمَ خَلَقَهُ مِنْ تُرَابٍ ثُمَّ قَالَ لَهُ كُنْ فَيَكُونُ ((Hakika mfano wa Issa kwa Allah ni kama mfano wa Adamu, alimuumba kutokana na dongo kisha akamuambia kuwa basi akawa)) [Aala Imaran 59] Udhahiri wa neno hili kuwa Allah mtukufu alimuumba Adamu (a.s) umbile la mwanzo bila ya (KUN) kisha akamtoa katika umbile la mwanzo na kumuingiza katika umbile la pili kwa (KUN) kama walivosema Wafasiri kuwa umbile la mwanzo bila ya roho na umbile la pili ni la kupewa roho. Na Allah mtukufu ndiye muwafikishaji na yeye ndiye anayejua zaidi. Wabillahi Taufiqi. |
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi SUALI:Limetufikia suali kuhusu matendo ya mja ikiwa Allah ameyapanga kabla na kwa hiyo mja yumo katika aliyotaka Allah yafanyike kwa nini kuwe na lawama katika anayoyafanya mja hali ya kuwa amefanya aliyotaka Allah yaafanyike? JAWABU:Kwanza: Suali hili linakamatana na kuamini Qadhaa na Qadar nayo ni nguzo ya sita katika nguzo za Imani katika Uislamu. Pili: Kwa hakika Allah mtukufu ameumba watu kwa kuwafanyia mitihani ni nani kati yao atafanya matendo mema?; kutokana na hapo amejaalia kwao kuwa na hiyari katika yote wanayoyafanya katika vitendo vyao, basi akasimamisha hoja kwa kutuma Mitume na kuteremsha Vitabu, na kuwapa Akili ya kufikiri na kupambanua, basi akawaongoza katika njia ya kujua na akawapa khiyari katika uwanja wa vitendo vyao ikiwa ni kauli ya kusema au itikadi ya kuitakidi au vitendo vya kufanywa, na hakuna shaka yoyote katika kutofanyika wala kupatikana chochote isipokuwa kwa kutaka Allah mtukufu; kwani kupatikana ambacho Allah mtukufu hataki kipatikane kunalazimisha kushindwa Allah mtukufu kwa kupatikana katika mamlaka yake asiyotaka yapatikane, na lazimisho hilo ni batili bila shaka yoyote, kwa hiyo ikalazimika kuamini kuwa hakuna chochote kinachopatiakana ikiwa cha kheri au shari isipokuwa ni kwa kutaka Allah mtukufu, na kutaka kwake hakulazimishi kuridhia kwake, bali kunalazimisha uwezo wake katika kuwakalifisha waja wake na kuwalipa kwa machumo yao wenyewe na kupatikana uadilifu wake Allah mtukufu, basi huwapoteza Allah mtukufu walio madhalimu nayo ni malipo ya kujichagulia wenyewe njia ya kuasi na kudhulumu katika maisha yao, na kuwaongoa Allah wachamungu ni malipo ya kujichagulia kwao njia ya utiifu na kunyenyekea kwake Allah mtukufu; kwa hiyo mja ni mwenye kulaumiwa au kusifiwa kwa yale aliyojichagulia katika maisha yake mwenyewe. Tatu: Tunafahamu sote kuwa Allah mtukufu na mjuzi wa kila kitu; kwa hiyo ameshajua yote yatakayofanywa na waja wake moja moja kwa khiyari zao wenyewe, na hayo ni kabla ya kuwaumba, kwa hiyo Allah mtukufu ameshathibitisha matendo ya waja na yote yanayotokea na yatakayotokea mpaka siku ya Kiama, ameyathibitisha si kwa kwa njia ya kulazimisha bali ni kwa njia ya kuyajua. Nne: Ni wajibu wetu sisi waja kushughulikia majukumu yetu katika yale yenye maridhio ya Mola wetu; kwani huo ndio uwanja wetu, na sio tujiingize katika maasi ya Allah mtukufu kisha tumlaumu Allah tukufu kwa yale aliyoyajua kwetu na kutulipa kwa machumo ya mikono yetu wenyewe. Mara moja Kiongozi wa Waumini Omar bin Al-Khattabi (r.a) alilirejesha jeshi kwa sababu ya kufikiwa na habari kuwa mji watakaouingia kumeingia maradhi ya Twaauni nao ni maradhi ya kuambukiza na kusababisha kifo cha haraka kama kolera au ebola, basi mmoja wa Masahaba wenzake akasema: Hivi ni kukimbia Qadhaa ya Allah ewe Kiongozi wa Waumini?!! Hapo akamjibu: "Ndio ni kukimbia Qadhaa ya Allah kwa kukimbilia Qadari yake Allah mtukufu" Akimaanisha kuwa huku kurudi kwetu pia kumeshakadiriwa na Allah mtukufu kama alivyokadiria kule kufikwa na balaa lilifika. Kwa hiyo tukusudie mazuri anayoyardhia Mola wetu na tuchukue sababu zake na tuachane na mabaya na sababu zake ili tuweze kufanikiwa kwa Mola wetu kwa kutujaalia Taufiqi yake na kutuepusha na Khudhulani yake. Wallahu aalamu wa Ahkamu. Wabillahi Taufiqi. |
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi SUALI:Jana nimeangalia kipindi cha maswali na majibu Shekhe aliulizwa Jee! Qurani ni kiumbe au ni maneno ya Allah? Naye akajibu kuwa Qurani ni maneno ya Allah ni kalaamu lwaah na wanaosema ni kiumbe wanakufuru. Naomba ufafanuzi juu ya hili In shaa Allah JAWABU:Neno la kuwa Quraani ni kiumbe ndilo neno la haki kidalili, na hakuna shaka yoyote katika usahihi wake, na kwa hakika wenye kusema kuwa Quraani si kiumbe wamekosea na dalili hawana, na ajabu zaidi ni kukufurisha kwao wenye kusema neno la haki kidalili katika suala hili kama ulivyomsikia huyo Sheikh aliyejibu Allah amuongoe. Unaweza kupata dalili za kuwa Quraani ni kiumbe kwa kufuata kiunganishi hichi hapa. Ama kuhusu hilo suali na jawabu yake kama ulivotunakilia; kwa hakika yote mawili ni ya kushangaza kwani hayamo katika mantiki, si ulizo wala jawabu; kwa sababu unapouliza: Jee!! Quraani ni maneno ya Allah au ni kiumbe? Ni sawa sawa na kuuliza: Jee!! Muhammad ni Mtume wa Allah au ni kiumbe? Au kuuliza: Jee!! Alqaaba ni nyumba ya Allah au ni kiumbe? Kwa hakika hakuna mkabala baina ya sifa mbili hizo, kama ilivyokua Muhammad ni Mtume wa Allah nako hakupingani na kuwa kwake kiumbe, na Alqaaba kuwa ni nyumba ya Allah hakupingani kuwa Alqaaba ni kiumbe basi vilevile kuwa Qurrani ni maneno ya Allah hakupingani na kuwa Quraani ni kiumbe, kutokana na hapo utawakuta wenye kusema kuwa Quraani ni kiumbe vilevile wanasema kuwa Quraani ni maneno ya Allah, kwa hiyo Quraani ni maneno ya Allah, nayo ni kiumbe cha Allah. Huenda mtu akasema kuwa maneno ya Allah ni sifa ya Allah vipi sifa ya Allah iwe ni kiumbe?!! Jawabu yake ni kuwa Allaha ni msemaji wala si maneno; kwa hiyo sifa yake ni usemaji na sio maneno; kwani maneno ni athari ya sifa hiyo ya usemaji ambayo ni sifa ya kitendo, na kila kilichopatikana kwa sifa ya kitendo bila shaka hicho ni kiumbe. Kwa hiyo utafahamu kuwa sisi Ibadhi tunaposema kuwa Quraani ni kiumbe tunasema pia kuwa Quraani ni maneno ya Allah (KALAAMU LWAAHI) na maneno ya Allah sio sifa ya Allah bali ni athari ya sifa ya Allah ya Usemaji (TAKALLUMU). Wabillahi taufiqi. |