Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi  ASHIRAA maana yake ni UNUNUZI, hilo ni neno la kiistilahi ililochukuliwa katika Aya tukufu:
((إِنَّ اللَّهَ اشْتَرَى مِنَ الْمُؤْمِنِينَ أَنْفُسَهُمْ وَأَمْوَالَهُمْ بِأَنَّ لَهُمُ الْجَنَّةَ يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللَّهِ فَيَقْتُلُونَ وَيُقْتَلُونَ....))
((Hakika Allah amenunua kwa Waumini nafsi zao na mali zao kwa kupata wao Pepo wanapigana katika njia ya Allah basi wanaua na wanauliwa...))
[Tauba 111]
Na wahusika wa Ashiraa wanaitwa Ashuraatu yaani Wanunuzi na akiwa mmoja naitwa Ashaari yaani Mnunuaji.
Ashuraatu huwa wameziuza nafsi zao kwa ajili ya Allah mtukufu peke yake. wamo katika njia ya kumalizika nafsi zao na mali zao kwa kutafuta maridhio yake Allah mtukufu.
Na Ashiraa inapatikana katika hali ya kukosekana uwezekano wa kudhihiri neno la wana wa Haki katika jamii na kufungika uwezekano wa kuelimisha jamii, na hilo hupatikana kwa kuwepo adui aliye mbabe aliyesalitishwa juu yao, adui huyo huwakandamiza wana wa haki na kuwadhalilisha na kufanya kila juhudi za kuwazuia kunako uongofu, wala yeye hajali kuvunjwa kwa heshima, wala kupotea haki za waja, wala kupora mali zao kidhulma, basi hapo kutokeza kundi miongoni mwa Waumini nao huziuza nafsi zao kwa ajili ya Allah kwa kuingia katika kuelekeana na mbabe aliyealitishwa dhidi ya Umma ili kuzuia uharibifu wake, na kumtia katika mahangaiko, na kufanya kila jaribio la kuondokana nae, hayo yote huwa ni adabu ya vitendo vyake viovu katika jamii.
Na hayo ni kama yalivopatikana katika zama za utawala wa Bani Umayyah wakati walipomtawalisha Ziyadi bin Abiihi katika Wilaya ya Iraqi, kwani yeye alianza kufuatilia wana wa haki, na kuwaua, na kuwakandamiza, na kuwakatakata. Hawakusalimika na shari zake hata wanawake; kwa hakika alimchukua Bibi Mchamungu aitwae Al-Baljaa na kumuingiza katika dimbwi la dhulma zake akipoza chuki za nafsi zake kwa kumuua Bibi huyo na kumkatakata na kumuanika uchi sokoni, kwa hakika Bibi huyo -Allah amrehemu- alikua ni mfano nzuri wa kujifunga na haki na kuthibiti katika msimamo mbele ya udhalimu na chuki zake na mawimbi yake, naye aliendelea katika njia hiyo mpaka akaondoka duniani akiwa ni shahidi wa haki katika maridhio ya Allah mtukufu.
Basi hapo wakajitokeza watu wenye wivu wa haki na heshima, walivaa nguo ya ushujaa, nao wakampa Baia Imamu Abu Bilali Al-Mirdaas bin Hudair Atamimi -Allah amrehemu-, naye akatoka nao kwa kuelekeana na udhalimu wa Liwali Ziyaad bin Abiihi, walifanya hivo bila ya kuudhi watu kwa silaha zao isipokua yule atakayeingia katika vita dhidi yao tu, basi walikua ni mwiba katika koo ya adui, waliweza kulishinda jeshi lake la askari 2000 katika mji wa Aasak hali ya kuwa idadi yao ni 40 tu, kwa hakika walikua ni mfano mwema kwa ukakamavu na ushujaa na nguvu ya haki na azimio la kweli, waliweza kumtikisa Ziyaadi na jeshi lake, na waliendelea katika njia hiyo mpaka wakamalizika wote katika njia ya Allah mtukufu wakiwa ni Mashahidi, kwa hakika Mashahidi hao waliandika kwa damu zao tarehe ya ushujaa na kujitolea kwa ajili ya haki na maridhio ya Allah mtukufu.
Aliwapa Baia wenzake kwa Shiraa * ulirefuka wakati wake mpaka akakirimiwa.
walipata shahada walokua wakiitaka * na maridhio ya Allah waliyafikia..
Na uchache wa Ashiraa ni wanaume mashujaa 40, na hayo ni kwa mujibu wa yaliyothibiti katika zama za Mtume -salla lwaahu alayhi wa sallama- wakati aliposilimu Omar bin Al-Khattaab -Allah amridhie-; kwani ilitimia -kwa kusilimu kwake- idadi ya Waislamu wanaume 40, nao walikua kabla ya hapo wanamuabudu Allah mtukufu kifichoficho katika nyumba ya Al-Arqam -Allah amridhie-, lakini waliweza kutoka baada ya kusilimu Omar R.A. wakiwa wameshikana pamoja na kutoa ushindani mbele ya kiburi ya ujinga wa Washirkina wa Makka.
Na mwenye kuingia katika Ashiraa anakua hana nafasi ya kurudi nyuma, basi inamlazimu kuendelea katika njia yake mpaka akutane na Allah mtukufu akiwa ni shahidi; kwa sababu yeye hutoa ahadi ya utiifu kwa kupigana hadi kufa, hayo yatamlazimu hata kama atabakia peke yake, na imesemwa iwapo idadi yao itapungua hadi kufikia Ashuraatu watatu hapo ndio wanapata nafasi ya kujiamulia katika jambo lao.
Na lililo mashuhuri katika Madhehebu ni kuwa Ashaari haipasi kwake taqiyah, na Mhakikishaji Al-Khalili -Allah amrehemu- amekubalisha kutumia Taqiyah ikilazimika, naye ametoa sababu kuwa hilo ambalo Ashaari amejilazimisha nalo juu ya nafsi yake haliwezi kuzidi daraja ya alilolazimisha Allah mtukufu kwake yeye huyo Ashaari.
Pia Mashuraati baada ya Baia huwa hawana watani tena ya makazi, na kwa hilo watani yao inakua ni pale walipo katika harakati yao, basi hapo ndipo wao watatimiza rakaa 4 za katika sala zao, na nje ya hapo huwa katika hukumu ya safari wanasali sala za rakaa 4 rakaa 2. |