Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi  2.1 UKAFIRI KILUGHA:
Ukafiri -kiasili- ni neno la lugha ya kiarabu, na maana yake ni kuficha na kusitiri, na ukafiri pia ni kinyume na Imani, basi usiku katika lugha ya kiarabu -ambayo ndiyo asili ya neno hili- unaitwa kafiri kwa sababu ya kuficha kwake, na ukafiri pia ni kuzipinga neema, nako ndiko kuzikufuru neema, kutokana na hapa, neno ukafiri lina maana pana sana kilugha, ingawa baadhi ya maana zake hazitumiki kwa sababu ya kuzoeleka maana za kisheria katrika Jamii.
2.2 UKAFIRI KISHERIA:
Ukafiri kisheria ni kuasi kwa kosa kubwa lolote; kwa maana hiyo makosa makubwa yote ni ukafiri kwa mujibu wa sheria ya Allah mtukufu, basi ukafiri huu kiaina umegawika kwa mujibu wa vigawanyo vya madhambi makubwa kisheria, na madhambi makubwa kisheria yamegawika katika vigao viwili vikuu, navyo ni:
a. Madhambi makubwa ya kishirikina.
b. Madhambi makubwa yasiyokuwa ya kishirikina.
Basi vile vile ukafiri umegawika katika vigao hivi viwili vikuu navyo ni:-
2.2.1 UKAFIRI WA KISHIRKINA.
Ukafiri wa kishirkina ni ukafiri unaohusika na madhambi ya kishirkina tu, na madhambi hayo yamegawika sehemu mbili kubwa, nazo ni:
2.2.1.1 Madhambi ya kumfanyia Allah msawa.
Ushirikina huu anasifika nao mwenye kukubali kuwepo uungu, kwa hiyo mshirikina aliyemo katika ushirkina huu anakua ni mwenye dini, lakini amekosea katika ibada ya kumuabudu mungu wa haki -Allah mtukufu- kwa kumfanyia Allah msawa katika ibada au hukumu, na kwa hiyo basi ushirikina huu pia umegawika sehemu mbili:
2.2.1.1.1 Ushirikina kwa kujifanyia chengine kuwa katika daraja ya uungu kiibada, kwa kukiabudu pasina Allah mtukufu au pamoja na Allah mtukufu kwa kukishirikisha katika ibada ya Allah mtukufu, kama kuabudia masanamu au watu au wafu au mawalii au makaburi au mito au mizimu au miti au mapango au jini au jua au mwezi n.k.
2.2.1.1.2 Ushirkina kwa kukifanya chengine kuwa katika daraja ya uungu katika hukumu za Allah mtukufu, basi kikapelekea hicho kuhalalisha alichoharamisha Allah mtukufu, au kuharamisha alichohalalisha Allah mtukufu, au kupinga kuhumu zake Allah mtukufu.
2.2.1.2 Kumkataa Allah mtukufu.
Huu ni ushirikina wa kupinga kuwepo kwa Muumba, na kwa maana hiyo aliyemo katika ushirkina huu huwa hakubali kuwemo katika ibada maalumu, wala hazikubali sheria ya dini yoyote katika maisha yake.
Pia huingia katika ushirikina huu mwenye kupinga kuhumu za Allah mtukufu.
2.2.2 UKAFIRI USIO WA KISHIRKINA.
Ukafiri huu anahusika nao muislamu, kwa hiyo mwenye kuwemo ndani yake si Mshirikina, bali atabakia kuwa ni Muwahhidi mwenye kukiri dini ya Uislamu katika nafsi yake, lakini yeye amekua kafiri kwa kuwepo katika asi kubwa lolote miongoni mwa maasi ya Allah mtukufu bila ya kuhalalisha asi hilo; kwani akifikia hali ya kuhalalisha asi lake atakuwa ameingia katika ukafiri wa kishirkina wa kumfanyia Allah msawa katika hukumu zake.
Ukafiri huu umeitwa katika Ibadhi kwa jina ukafiri wa neema kwa kuzingatia kuwa Dini ya Uislamu ni neema ya Allah mtukufu naye ameisifu hivyo pale aliposema:
((Leo nimekukamilishieni dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimeridhia kwenu uislamu kuwa ndio dini))
[Maaidah 3].
Pia wanavyuoni wetu wa Magharibi wameuita ukafiri huu kwa jina la ukafiri wa kinafiki kwa kuzingatia hali ya aliyejitosa ndani yake; kwani hakika yeye yumo katika hali ya Unafiki ikiwa tu hajatubia kwa Allah mtukufu kutokana na asi lake kubwa alilolivaa. |