Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi 
Ni lazima kuzijua neema za Allah mtukufu, na kuwa neema zote ni mapeo na fadhila za Allah mtukufu kwa mazuri ya neema alizotupa, kuanzia kupatikana kwetu kwani hatukuwepo, afya na uzima baada ya magonjwa, na kuwa na fahamu na akili, na aina zote za neema zake Allah mtukufu, na kubwa ya neema hizo na iliyo mzuri zaidi ni neema ya Uislamu na uongofu wa Imani na Taufiki yake Allah mtukufu, na Elimu ambayo ndio rafiki mkuu na kiongozi katika njia ya kufika katika maridhio ya Allah mtukufu, na kuokoka na kila lenye kudhuru, basi Uislamu ni neema kubwa kabisa na katika hilo amesema Allah mtukufu katika Kitabu chake kitukufu:
((Leo nimekamilisha kwenu dini yenu, na nimetimiza kwenu neema yangu, na nimeridhia kwenu kuwa Uislamu ndiyo dini kwenu))
Basi tujue kuwa kila amri ni neema na kila katazo ni neema, basi ni lazima kumshuru Allah kwa neema zake, na shukurani ni kuhakikisha maridhio ya Allah katika maamrisho yake kwa kuyafanya na makatazo yake kwa kuyaepuka, na iwe hilo kwa ajili ya Allah mtukufu peke yake.
Ulazima wa kujua Dalili
Basi inalazimika kujua dalili ambazo Allah mtukufu ameziweka kuwa ni ushahidi wa kuwepo kwake na upweke wake.
﴿وَفِى ٱلاْرْضِ ءايَـٰتٌ لّلْمُوقِنِينَ * وَفِى أَنفُسِكُمْ أَفَلاَ تُبْصِرُونَ﴾
﴾Na katika Ardhi kuwa dalili nyingi kwa wenye yakini * na katika nafsi zenu jee!! Basi hamuoni?﴿
[Dhaariyaat 20-21]
وَفِيْ كُلِّ شَيْءٍ لَهُ آيَةٌ * تَدُلُّ عَلَى أَنَّهُ وَاحِدٌ
﴾Na katika kila kitu anayo yeye dalili * inayoonyesha kuwa yeye ni mmoja﴿
Ulazima wa Kukhofu na Kutaraji
Ni lazima kwa Mja kuwemo katika Kutaraji Thawabu za Allah bila ya kujiweka katika amani.
Ni lazima Mja kuwemo katika Khofu ya kuogopa Adhabu ya Allah bila la kukata tamaa.
Hayo ni kwa sababu Mja yumo katika neema za Allah mtukufu, neema ambazo ni mtihani kwake katika maisha haya ya duniani, na kuwa mja hafikii kujua uhakika uliofichika, basi waja wema ambao ndio ruwaza njema kwa waumini mpaka siku kitaposimama Kiama ndivo alivyozieleza hali zao na sifa zao Allah mtukufu katika Kitabu chake Qur-ani tukufu kuwa wao ni wale wanaomuomba yeye wakiwa na Matarajio na Kuogopa basi amesema:
﴿إِنَّهُمْ كَانُواْ يُسَارِعُونَ فِى ٱلْخَيْرٰتِ وَيَدْعُونَنَا رَغَباً وَرَهَباً وَكَانُواْ لَنَا خـٰشِعِينَ﴾
﴾Hakika wao walikua wakikimbilia katika mambo ya Kheri, na wanatuomba kwa matarajio na kuogopa, na walikua kwa ajili yetu wakinyenyekea﴿
[Anbiyaa 90]
Na kwa hakika kusifiwa na Allah kwa kufanya kitendo kunajuilisha kuwa ni lazima, na wala hakuna tatizo katika moja ya haya mawili ya kuogopa na kutaraji kumzidi mwenzake ikiwa tu haijafikia Khofu katika daraja ya kukata tamaa kulikoharamishwa.
﴿إِنَّهُ لاَ يَايْـئَسُ مِن رَّوْحِ ٱللَّهِ إِلاَّ ٱلْقَوْمُ ٱلْكَـٰفِرُونَ﴾
﴾Hakika yalivyo ni kuwa hawakati tamaa katika Rehema za Allah isipokua ni Watu Makafiri﴿
[Yuusuf 87]
Au kukamfikisha Kutaraji katika kujiweka katika Amani iliyokatazwa.
﴿أَفَأَمِنُواْ مَكْرَ ٱللَّهِ فَلاَ يَأْمَنُ مَكْرَ ٱللَّهِ إِلاَّ ٱلْقَوْمُ ٱلْخَـٰسِرُونَ﴾
﴾Jee!! Wamejiaminisha na Njama (Adhabu) za Allah? Basi hawajiaminishi na Njama (Adhabu) za Allah isipokua Watu waliokhasirika﴿
[Aaraf 99]
Basi Mja hajipi amani kwa sababu inaweza kuwa:-
1. Allah hatozikubali amali zake kwa kuwa yeye hakuzifanya kwa njia iliyoamrishwa kama kuvunja sharti zake au nguzo zake na hali yeye hajui.
2.Kuwa yeye hatomaliziwa umri wake katika Toba kutokana na Maasi yake.
3.Au akaja akafa na yeye hayumo katika Imani ya kweli.
4.Au akaja akafanya mambo yenye kuvunja Aamali zake na huku haongoki katika kujiondosha ndani yake kwa njia ya kutubia.
5.Au hakupata Toba ya kweli ikiwa atatubia, kwa sababu Allah ameahidi kukubali Toba ya kweli,na haifai kuwa na shaka katika mema aliyoahidi Allah lakini inakhofiwa kuwa hatopata Toba iliyoahidiwa ili akubaliwe.
6.Au kuwa yeye humo alimo katika Neema za Allah uhakika wake yumo katika kuchukuliwa kwa ajili ya Adhabu.
Basi Muumini ni mwenye khofu, ni mwenye kutaraji, ni mwenye kufanya mema kwa kutaraji, tena ni mwenye kuepuka maasi kwa kuhadhari .
|