Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi  Inalazimika kwa mja kuamini Qadhaa na Qadar.
Qadhaa: ni kuekwa kwa pamoja vile vitakavyokua katika Lauhi l-mah-fuudhi.
Qadar: ni kupatikana kwa vile vitakavyokua katika muweko wake wa nje wa kiwakati, kwa kuwepo kwake kimoja baada ya chengine, kwa mujibu wa vilivyothibitishwa katika Qadhaa.
Na kwa msemo mwengine Qadhaa inakamatana na Elimu kidhati ya Allah mtukufu kwa vyote vitakavyokua, ni vipi hivyo vitakavyokua? Na vipi vitakua? na wapi vitakua? na ukubwa wake, ikiwa ni kidogo au kikubwa, cheusi au cheupe, na mfano wake, na uhakika wa kufanyika kwake, na idadi ya sehemu zake, na wakati wa kupatikana kwake, na sehemu yake, na kuyaandika hayo katika Lauhi l-mah-fuudhi.
Na Qadar ni kudhihiri kila kitu kwa wakati wake kama kilivyo katika Qadhaa.
Na maana ya kuwa ni Lazima kuamini Qadhaa na Qadar, ni kuitakidi -kwa yakini bila ya shaka yoyote- kuwa hakitikisiki chenye kutikisika, wala hakitulizani chenye kutulizana, isipokua ni kwa kukijua Allah mtukufu na kutaka kwake, hata kushindwa na uvivu ambazo ni tabia mbili za kimaumbile.
Na kuwa lolote lililokupata haikua kabisa likukose, na lililokukosa haikua kabisa likupate, na kuwa -uhakika ulivyo- watu lau watakusanyika kuanzia wa mwanzo hadi wa mwisho ili wakufae kwa kitu ambacho Allah hajakikadiria kwako basi hawatoweza, na lau watakusanyika kuanzia wa mwanzo hadi wa mwisho ili wakudhuru kwa kitu ambacho Allah hajakikadiria kwako basi hawatoweza, basi kalamu zimeshanyanyuliwa, na wino umeshakauka, na sahifa zimeshakunjwa, kwa yote yatakayokua mpaka siku ya Kiama.
Na haya yote ni kwa kuangalia upande wa Elimu yake Allah mtukufu na Uwezo wake, kwani yeye amevienea viumbe vyote kielimu na kiuwezo, basi kuyapitisha hayo makadirio katika wakati wake ni kwa mujibu wa Hekima zake Allah mtukufu. |