Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi  Naskh ni kuondoka hukumu ya kisheria kwa sababu ya kuja hukumu nyengine ya kisheria katika tendo moja, basi inaondoka hukumu katika ya mwanzo (Mansuukh), na huzingatiwa hukumu iliyokuja kukaa pahala pake (Naasikh).
6.1 YANAYOINGIWA NA NASKH:
Yanayoingiwa na Naskh ni yale yanayokamatana na vitendo vya waja (FIQHI) katika maamrisho yake na makatazo ya kisheria peke yake.
Ama Tawhidi (Aqidah) na Tabia njema; kwa hakika kila Mtume anakuja akiwa ni mwenye kulingania katika hayo, basi tufahamu kuwa Dini ya Manabii wote ni Dini mmoja nayo ndiyo Dini ya Uislamu, basi hakuna naskh katika mambo ya khabari za kumjuwa muumba Allah mtukufu na sifa zake, wala katika kukufuliwa, malipo mema, adhabu, taarifa ya yale yatakayokuja, pia hakuna naskh katika khabari za yaliyopita.
Amesema Allah mtukufu kuhusiana na Mtume Issa mwana wa Mariam (a.s.w):
﴿وَلاِحِلَّ لَكُم بَعْضَ ٱلَّذِي حُرّمَ عَلَيْكُمْ وَجِئْتُكُمْ بِأَيَةٍ مّن رَّبّكُمْ فَٱتَّقُواْ ٱللَّهَ وَأَطِيعُونِ * إِنَّ ٱللَّهَ رَبّى وَرَبُّكُمْ فَٱعْبُدُوهُ هَـٰذَا صِرٰطٌ مُّسْتَقِيمٌ ﴾
﴾Na ili nihalalishe kwenu baadhi ya yale yaliyoharamishwa kwenu, na nimekujieni kwa dalili inayotoka kwa Mola wenu, basi mcheni Allah na munitii mimi * Hakika Allah ndie Mola wangu na Mola wenu; basi muabuduni yeye, hii ndio njia iliyonyooka﴿
[Al-imraan 50 -51]
6.2 SHERIA YA MTUME MUHAMMAD (S.A.W) IMEZIKALIA SHERIA ZA MITUME WOTE.
Kwa hakika sheria ya Mtume Muhammad (s.a.w) ndiyo sheria ya mwisho, basi imezikalia sheria zote za Mitume (a.s.w) waliotangua kabla yake; kwa hiyo sheria ya Mtume wetu Muhammad (s.a.w) ndiyo sheria ya kufuatwa na waja wote, nayo ndiyo sheria yenye kubakia; kwani hakuna sheria yoyote itakayokuja kuikalia mpaka kumalizika kwa Dunia, basi mja yoyote atakaye jishika na sheria ya Nabii wowote aliyekuwa kabla ya Mtume Muhammad (s.a.w) kwa hakika mja huyo siku ya malipo hali yake ni sawa na hali ya mwenye kwenda sokoni na pesa iliyoishiwa na wakati wa matumizi yake.
6.3 HEKIMA YA KUPATIKANA KWA NASKH.
Hekima iliyopo katika kupatikana hukumu ya naskh ni kuwa ndani yake kuna huruma ya Allah mtukufu kwa waja wake, nayo ni huruma ya kuchunga maslaha ya waja na yale ambayo yanakubalika zaidi katika zama tofauti, na ili waja wavutike kwa Mola wao kutokana na wepesi alioufanya juu yao, kwa hakika Allah ameneesha mengi na amelazimisha kidogo, na akafanya wepesi katika aliyoyalazimisha, basi ni zake yeye fadhila na neema, na unatoka kwake upole na wema, na lau ingalikuwa kinyume na hivi basi ingalikuwa ni uadilifu kutoka kwake, kwa sababu yeye ndie Mola na Mfalme mwenye kufanya anavyotaka.
﴿لاَ يُسْأَلُ عَمَّا يَفْعَلُ وَهُمْ يُسْـئَلُونَ﴾
﴾Haulizwi kwa kile ambacho anakifanya na wao (Waja) ndio wanaoulizwa﴿
[An-biyaa 23]
|