Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi ![29. KUTOONEKANA ALLAH, QURANI KIUMBE, UKAFRI NEEMA, SHUFAA NA ALIY]() Asalamu alaykum wa Rahmatullahi wa Barakatuh.
Nimesikia kuhusu Ibadhi, na kuwa ni moja ya Madhehebu ya Kiislamu, nimetaka kujua nini Ibadhi wanaitakidi kuhusu masuala yafuatayo:
- Kumuona Allah mtukufu siku ya Kiama.
- Quraani jee ni Maneno ya Allah au ni kiumbe?
- Hukumu ya mteda maasi makubwa lakini ni mtu wa Tauhidi nimesikia anakua kafiri kwa mujibu wa Itikadi wanayoamini Ibadhi.
- Mtenda maasi lakini ni mtu wa Tawhidi jee atapata Shufaa ya Mtume S.A.W?
- Muono wenu kuhusu Khalifa wa nne Ali bin Abi Twalib Allah amridhie.
Asanteni.
JAWABU
Waalaykum Salam wa Rahamtullahi wa Barakatuh.
Naam Ibadhi ni moja ya Madhehebu za Kiislamu, nayo katika mafundisho yake inategemea Quraani tukufu na Sunna ya Mtume Muhammad S.A.W na Makubaliano ya Umma, na njia ya Ibadhi ni uadilifu usiokua na upendeleo, na usawa usiokua na ubaguzi, na dira yetu ni HAKI KWA DALILI.
Jina la Ibadhi ni anuani ya kudhibiti mafundisho katika yaliyoingiwa na tafauti baina ya Waislamu; ili kila Madhehebu ihusike na majukumu yake, kutokana na hapo Wanavyuoni wetu wa mwanzo hawakujiita jina la Ibadhi, pia huwezi kukutia katika mafundisho ya Madhehebu hii kauli za Ibu Ibadhi R.A si katika mlango wa Itikadi wala Kifiqhi.
Ama kuhusu masuala husika tunasema:
1. KUTOONEKANA ALLAH MTUKUFU:
Itikadi yetu ni kuwa Allah mtukufu ametakasika na uwezekano wa kuonekana Duniani na Akhera na Peponi, basi kama ilivokua Allah mtukufu hasifiki kwa sifa ya kufanana na kitu chochote, wala kwa sifa ya kuwa na mtoto, vile vile Allah mtukufu hasifiki kwa sifa ya kuonekana wala kwa uwezekano wa kuonekana.
Allah mtukufu alikuwepo wala hapana sehemu, wala wakati, wala nuru, wala kiza, wala mbingu, wala ardhi, wala arshi, wala chochote kisichokua yeye, hayo ni kwa sababu Allah ndiye Muumba wa kila kitu, basi yeye peke yake ndiye asiyekua kiumbe wa sababu ndiye Muumba, na vilivobakia vyote ni viumbe vyake, na hakuna shaka yoyote kuwa kuonekana ni sifa za vyenye umbo na mwili, na Allah mtukufu ametakasika na kuwa na umbo na mwili, yeye amejisifu kuwa:
((Vyenye kuona havimdiriki))
[Al-An`aam 103]
Bila shaka macho yakiona yatakua yamediriki yalichokiona, basi Allah hadirikiwi na vyenye kuona ikiwa ni jicho au kamera au moyo au chochote kile.
Vile vile Allah mtukufu alimuambia Mtume Mussa A.S :
((Hutaniona))
[Al-A`araf 143]
Basi sisi tukasema na kuitakidi kama alivosema Allah mtukufu kuwa Mtume Mussa A.S hatamuona, wala hatuwezi kusema: "Hapana ewe Allah bali Mtume Mussa A.S atakuona". Huko kutakua ni kumkosea heshima Allah mtukufu.
Ama kuhusu Aya inayosema:
((Nyuso siku hiyo zitan`gara kwa Mola wake ni zinaan`galia))
[Al-Qiyaamah 22-23]
Tunasema huo ni muangalio wa kusubiria thawabu za Allah na fadhila zake kwao, na sio muangalio wa kumuona yeye.
AMA KUHUSU THAWABU KUBWA YAO KATIKA PEPO:
Tunasema Thawabu hiyo ni Maridhio yake Allah mtukufu kama alivobainisha mwenyewe katika neno lake:
((Sema: Jee! Nikuambieni yaliyo bora kuliko hayo? Watapata wale wamchao kwa Mola wao Pepo zinazopita chini yake mito watabakia humo, na wake waliotoharishwa, na MARIDHIO KUTOKA KWA ALLAH....))
[Aala Imraan 15]
Wala hajasema na kumuona Allah kama wanavodai wenye kudai madaihewa ya kuwa kumuona Allah katika Pepo ndio thawabu kubwa, wamejidanganya hao na kudanganya wengine, hivi ni nani mkweli zaidi kuliko Allah mtukufu?!! Yeye anatumbia kuwa Maridhio yake ndio thawabu kubwa yao katika Pepo:
((Allah amewaahidi Waumini Wanaume na Waumini Wanawake Pepo zinazopita chini yake mito, wabakie humo, na makazi bora katika Pepo za Aden, NA MARIDHIO KUTOKA KWA ALLAH NDIO KUBWA ZAIDI. Hayo ndiyo mafanikio makuu))
[Ataubah 72]
Imekuja katika Hadithi sahihi kuwa Mtume S.A.W amesema:
((Pepo mbili ni vya fedha vyombo vyake na vilivyomo ndani yake, na Pepo mbili ni vya dhahabu vyombo vyake na vilivyomo ndani yake, na hakuna kilichozuia baina ya watu wa peponi na kumuona Mola wao isipokua sifa ya kiburi katika dhati yake ndani ya Pepo ya Adeni))
[Bukhari 7444 Muslim 180]
Amesema Al-Haafidh Ibnu Hajar Al-Asqalani katika ufafanuzi wake wa hadithi hii: ((Na maana ya hadithi ya mlango huu ni kuwa: KWA MUJIBU WA UTUKUFU WA ALLAH NA KUJITOSHELEZA KWAKE ASIONEKANE NA YOYOTE)), basi hadithi hii inabainisha wazi wazi kuwa kilichozuia kuonekana Allah mtukufu ni utukufu wake na kujitosheleza kwake, pia Hadithi hii ni hoja ya wazi kuwa Allah hataonekana na watu wa Peponi, na kuhusu thawabu kuu anasema Mtume S.A.W:
((Hakika Allah mtukufu atawambia watu wa Peponi: Enyi watu wa Peponi. Nao watasema: Tunakuitika Mola wetu na ukuu ni wako na kheri imo mikononi mwako. Atasema: Jee!! Mumeridhia? Nao watasema: Na vipi sisi tusiridhie? Ewe Mola wetu hakika umetupa ambayo hujampa yoyote katika viumbe wako. Atasema: Hivi nikupeni bora zaidi kuliko hayo? Watasema: Ewe Mola na kitu gani kilicho bora zaidi kuliko haya? Atasema: NAWEKA KWENU MARIDHIO YANGU, BASI SITAKASIRIKA KWENU BAADA YA HAPO MILELE))
[Bukhari 6549, 7518 Muslim 2829].
2. QURAANI NI KIUMBE NA MANENO YA ALLAH
Ama kuhusu Quraani jee ni maneno ya Allah au ni kiumbe?
Tunasema hili suali limejengwa juu ya makadirio ya kukabiliana hukumu mbili ima Quraani iwe ni maneno ya Allah au iwe ni kiumbe, na kwa sababu hakuna mkabala baina ya hukumu hizo mbili, yaani kuwa Quraani ni kiumbe hakukabiliani na kuwa kwake meneno ya Allah, basi suali hilo linakua ni batili, ni sawa na kuuiza Jee! Quraani ni maneno ya Allah au ni Kitabu cha Allah? Au kuuliza: Jee! Muhammad ni Mtume wa Allah au ni kiumbe cha Allah? Kuwa Muhamaad ni Mtume wa Allah hakukabiliani na kuwa kwake kiumbe cha Allah, kama ilivokua kuwa Quraani ni maneno ya Allah hakukabiliani na kuwa kwake Kitabu cha Allah, vile vile kuwa Quraani ni maneno ya Allah hakukabiliani na kuwa kwake kiumbe cha Allah, kutokana na hapo jawabu yetu inasema: Quraani ni kiumbe nayo ni maneno ya Allah.
Na hapa inapasa tuzinduke vizuri katika suala hili, kwa sababu -sisi Ibadhi- tunaitakidi kuwa Allah mtukufu ni Msemaji (Mutakallimu) kwa hiyo sifa yake ni Usemaji (Attakallumu) kwa hiyo maneno yake ni athari ya sifa yake ya usemaji na sio sifa yake, kwani maneno si sifa bali usemaji ndio sifa, basi kama ilivokua viumbe vyote ni athari za sifa vitendo za Allah mtukufu vile vile Maneno yake Allah mtukufu ni athari ya sifa kitendo ya Allah mtukufu na sifa hiyo ni Usemaji.
Mauti ni kuiumbe, uhai ni kiumbe, riziki ni kiumbe, kwani vyote hivo ni athari za sifa vitendo za Allah mtukufu, kuhuisha katika uhai, kufisha katika mauti, kuruzuku katika riziki, vile vile kusema katika maneno. Kuhuisha, kufisha, kuruzuku, kusema, zote hizo ni sifavitendo mahususi, ama kuumba hiyo ni sifakitendo ya kijumla nayo inakusanya kila kilichopatikana kwa sifakitendo mahususi.
Vile vile kuwa Quraani ni kiumbe kumejulishwa kwa dalili nyingi kama vile kuteremshwa, kuhifadhiwa, kutokezeshwa, kujaaliwa na Allah, kubarikiwa, na kupambanuliwa.
Bila shaka kila chenye kusifika kwa sifa hizo hicho ni kiumbe tu.
Sisi tunawashangaa sana wenye kusema kuwa Quraani ni sifa ya Allah kwa sababu ni maneno ya Allah na maneno ya Allah ni sifa ya Allah.
Hivi wao wanaitakidi kuwa Allah ameteremsha sifa yake na kuibariki na kuitokezesha na kuihifadhi na kuijaalia na kuipaambanua?!!!
Quraani itakuja siku ya Kiama siku ambayo Allaha atakisemesha kila kitu, na Quraani nayo itasema: "Ewe Mola wangu mpambe"..... "Ewe Mola wangu muongezee"..... "Ewe Mola wangu mridhie"...... [Tirmidhi 2915].
Bila shaka dalili za kua Quraani ni kiumbe ziko nyingi sana, wala hazirejeshi dalili hizo na kupinga Itikadi hii isipokua mja aliyejifunga na kasumba kinafsi au aliyeingiwa na kiburi mbele ya haki.
Allah awaongoe wenye kuitakidi kuwepo kitu kisichokua Allah mtukufu na kitu hicho si kiumbe.
3. HUKUMU YA MTENDA DHAMBI KUBWA
Kuhusu hukumu ya Muislamu fasiki mtenda maasi jee! ni kafiri au si kafiri?
Kwa mujibu wa Itikadi yetu tuliyoichukua moja kwa moja katika Quraani tukufu na Sunna ya Mtume S.A.W ni kuwa kila mtenda dhambi kubwa ni kafiri na dhalimu na fasiki na fajiri, hukumu hii ni sawa ikiwa asi ni la kishirikina au si la kishirikina, kinachozingatiwa katika hukumu ni asi kuwa katika madhambi makubwa tu, yaani kila dhambi kubwa ni ukafiri na ufasiki na udhalimu na ufajiri, hii ndio itikadi yetu Ibadhi.
Kwetu sisi ukisema fasiki au dhalimu au fajiri ni sawa sawa na kusema kafiri, kutokana na hapa hailazimiki ukafiri kubatilisha tawhidi kama ilivokua hailazimishi ufasiki na udhalimu na ufajiri kubatilisha tawhidi; hayo ni kwa sababu Ibadhi hatuitakidi ulazima wa kuwa ukafiri ni ushirikina kama wanavoitakidi Masunni na walivoitakidi Makhawariji wa mwanzo. Na kwa sababu ya kuondosha utata huo Wanavyuoni wetu wakasema Ukafiri uko aina mbili kama ilivokua Madhambi makubwa yako aina mbili, basi uko Ukafiri wa Kishirikina nao unakamatana na madhambi ya kishirikina tu mwenye nao ni Mshirikina, na uko Ukafiri wa Neema unaokamatana na madhambi yasiyokua ya kishirikina mwenye nao ni Mnafiki.
Kwa hiyo kusema kwetu na kuitakidi kwetu kuwa Muislamu fasiki ni kafiri hakumtoi muislamu huyo nje ya duara la Tauhidi wala nje ya safu za Waislamu, wala hakumuhukumu kuwa yeye ni Mshirkina lifahamu hili vizuri.
Ukituuliza dalili yetu, tunasema kuwa Allah mtukufu amehukumu kwenye kitabu chake kuwa kila wenye kukengeuka utiifu wa Allah na Mtume ni kafiri amesema:
((Sema mtiini Allah na Mtume, na kama watakengeuka hakika Allaha hawapendi Makafiri))
[Aala Imaraan 32]
Pia Allah mtukufu ameondosha sifa ya Imani kwa aliyekengeuka utiifu amsema:
((Na wanasema: Tumemuamini Allah na Mtume na tumetii. Kisha wanakengeuka kundi kati yao baada ya hayo, na hao si Waumini))
[Anuur 47].
Anatuambia Allah mtukufu neno la haki la kutafautisha baina ya Waumini wa kweli na Wanafiki:
((Alif. Laam. Miiim. Hivi watu wanafikiria wataachwa waseme tumeamini na wao hawatajaribiwa?!!! * Kwa hakika tuliwajaribu waliopita kabla yao. Kwa hakika Allah atawajua walio wakweli na atawajua waongo))
Atawajua bila shaka Allah mtukufu aliwajua kabla lakini ni kuthibiti yale aliyoyajua kwao kwa kujibu wa matendo yao wenyewe bila kutezwa nguvu, bila Wakweli hao ndio Waumini halisi na Waongo hao ni Wanafiki.
4. SHUFAA YA MTUME S.A.W.
Ama kuhusu Shufaa ya Mtume S.A.W hiyo ni haki ya Waumini peke yao nao ni Wachamungu; kwa hiyo kafiri, dhalimu, fasiki, faajiri, hana sehemu yoyote katika Shufaa ya Mtume S.A.W, Allah mtukufu anatumbia kwenye kitabu chake:
((Hawana Madhalimu rafikikipenzi yoyote wala muombezi yoyote atakae tiiwa))
[Ghaafir 18]
Na ametuambia
((Ubaya ulioje jina la Ufasiki baada ya Imani. Na asiyetubia hao ndio Madhalimu))
[Hujuraati 11]
Na ametuambia katika ulimi wa waja wake wema:
((Ewe Mola wetu hakika wewe yule utakayemtia motoni hakika huyo umemdhalilisha na hawana madhalimu wa kuwanusuru))
[Aala Imraan 192].
Ibadhi ni kama alivotuongoza Mola wetu, hatuna sisi mlango wa kukubalisha maasi, wala hatuwapi watu matarajiohewa ya kujidanganya, ukiwa unaitaka pepo utalazimika na thamani yake ambayo ni uchamungu wa kweli, ama kuwambia watu wewe madamu ni Muislamu basi pepo ni yako tu hata ufanye maasi namna gani, au kuwambia wewe madamu ni Muibadhi pepo ni yako tu hata ufanye maasi namna gani, sisi kwetu hilo hakuna.
Itikadi yetu Pepo ni kwa Waumini Wachamungu tu peke yao, ukiitaka kama una dhambi itakulazimu utubie, la sivo huinusi wala huipati; kwani Allah anawakubalia Wachamungu tu wala haridhii ufasiki na Mafasiki.
Na ajabu watu wanaambiwa kuwa Mtume S.A.W kasema:
((Uombezi wangu ni kwa watenda akosa makubwa katika uma wangu))
Hii si sahihi wala Mtume S.A.W hakuisema, vipi Mtume S.A.W aseme maneno hayo hali ya kuwa anawahadharisha Masahaba wake R.A asije akafika mmoja wao siku ya kiama na kitu amekidhulumu, ikiwa ni mbuzi, au ghamia, au nguo, au dhahabu, kisha atake msaada kwa Mtume S.A.W. "Ewe Mtume wa Allah niokoe" Nae atamjibu:
((Kwa hakika nilikufikishia, similiki kwao chochote leo))
[Bukhari 1402, 3073 Muslim 1831]
Kama ni kweli ataombea waasi mafasiki madhalimu, angaliwambia musiwe na wasi wasi nitawaombea tu hasa hasa nyie ni Masahaba wangu, lakini alijua kuwa Allah amemwambia:
((Hivi yule mwenye kustahiki hukumu ya adhabu, hivi wewe unaweza kumuokoa aliyemo Motoni?!!!))
[Zumar 19].
Enyi Waislamu nyi, acheni kujidanganya na musikubali kudanganywa, jueni kuwa Pepo ni kwa Wachamungu tu, na Mtu wa Peponi hafikwi na huzuni wala khofu siku ya kiama, wala hafiki motoni, bali hata mvukuto wake hausikii achilia mbali kusema kuwa ataingia motoni kisha atolewe, musijidanganye wala musikubali kudanganywa kwa kuambiwa kuwa Waislamu mafasiki watasamehewa, na kama hawatasamehewa basi motoni siku chache tu kisha watatolewa na kuingizwa Peponi pamoja na Mtume S.A.W.
Mumepata wapi nyinyi kuwa Motoni ataingia asiyekua kafiri?!!!!
Hivi hamusomi Quraani kuwa Moto Allah amewaandalia Makafiri, naam Moto ni kwa makafiri peke yao, ni sawa wakiwa Makafiri wa Kishirkina au Makafiri wa neema, Allah atuepushe nao.
5. KUHUSU SAHABA KHALIFA WA NNE ALI BIN ABI TWALIB.
Ama kuhusu Ali bin Abi Twalib, bila shaka yeye ni mmoja wa Masahaba wa Mtume wetu S.A.W, na katika walioupigania Uislamu na kuuenzi vizuri, na katika watu wa karibu na Mtume wetu S.A.W kifamilia, kwa hakika yeye ni mtoto wa Ami wa Mtume S.A.W, pia ni Mkwe wake Mume wa Binti wa Mtume S.A.W Fatima R.A, na Waislamu walimchagua Aliy kuwa Kiongozi baada ya Othman bin Affaan, basi yeye ni miongoni mwa Makhalifa wanne waliochaguliwa kwa Shuura baada ya Mtume S.A.W hili hatuna shaka nalo, lakini juu ya yote hayo anabakia Ali bin Abi Twalibu kuwa ni mja aliyemo katika mtihani wa kulazimishwa kisheria kama wengine waliobakia, alitakiwa kuwemo katika njia ya Uchamungu hadi mwisho wa maisha yake ili kupata maridhio ya Allah mtukufu, wala hakuwa mwenye kuhifadhika na uwezekano wa kukosea, yaani yeye ni sawa na Masahaba wengine katika hilo, wala hatujaona sisi katika Quraani tukufu andiko mahususi lililomtaja Ali kwa jina lake wala kwa Kuniya yake wala kwa Laqabu yake, kutokana na hapo hukumu yake ya Ghaibu iko kwa Allah mtukufu, ama sisi kwetu ni kwa mujibu wa vile itavodhihirika kwa Muumini, ikiwa imedhihirika kwao kuwa yeye kafa akiwa ni Mchamungu mridhie hiyo ni haki yake kwako, na ikiwa imedhihirika kwao kuwa yeye kafa akiwa ni Fasiki usimridhie na hiyo itakua ni haki yake kwako, na ikiwa hali yake imeingiwa na uatata kwako tulizana bila kumridhia wala kutomridhia, na hukumu hii ni kwa kila asiyekua na andiko mahususi alilotajwa ndani yake kiuanisho kuwa ni mja wa Peponi ni mja wa Motoni.
Wabillahi Taufiiqi. |