Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi
Ieleweke wazi kwamba mambo yote ambayo yalikuwa yanajuzu kwa mwenye hedhi kabla ya hedhi yake, yote yanajuzu pia wakati wa hedhi yake ila mambo yafuatayo:
1.Kuingiliana na mumewe.
Mwanamke yetote yule aliye na hedhi haijuzu kabisa kuingiliana na mumewe wakati wa hedhi yake. Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Al-Baqara aya ya 222, kasema,"
﴿وَ يَسئَلُونَكَ عَنِ المَحِيضِ قُل هُوَ أَذًى فَاعتَزِلُوا النِّسَآءَ فِى المَحِيضِ وَلاَ تَقرَبُو هُنَّ حَتَّى يَطهُرنَ﴾.
Maana yake "Na wanakuuliza juu ya hedhi, waambie huo ni uchafu. Basi jitengeni na wanawake zenu wakati wa hedhi zao, Wala msiwakaribie (yaani msiwaingilie) mpaka watoharike." Hadithi iliyohadithiwa na Abu Huraira R.A.A. kasema, "Kasema Mtume S.A.W.,"
مَنْ أَتَى حَائِضًا أَوْ امْرَأَةً فِي دُبُرِهَا أَوْ كَاهِنًا فَصَدَّقَهُ بِمَا يَقُولُ فَقَدْ كَفَرَ بِمَا أُنْزِلَ عَلَى مُحَمَّدٍ.
Maana yake, "Atakayemuingilia mwanamke wakati wa hedhi yake au kwa tundu ya nyuma, au atakayekwenda kwa mpiga ramli na akamsadiki atakayo sema, atakuwa amekufuru yaliyoshuka kwa Muhammad." (S.A.W.)
Wakati mwanamke yuko katika hedhi mwanamume ana ruhusiwa kustarehe na mkewe kuanzia juu ya kitovu kwenda juu mpaka amalize haja yake, lakini asimwingizie mdomoni wala katika tundu lake la kikalio. Kasema Mtume S.A.W.,"
وَاصْنَعُوا كُلَّ شَيْءٍ غَيْرَ النِّكَاحِ.
Maana yake, "Fanyeni kila kitu ila kuwaingilia." Pia Hadithi ya Muadh bin Jabal R.A.A. aliyoitoa Razin, kasema, "Nilimuuliza Mtume S.A.W. jambo gani ni halali kwangu kwa mke wangu akiwa ana hedhi." Akajibu kwa kusema, "
مَا فَوْقَ الْإِزَارِ وَالتَّعَفُّفُ عَنْ ذَلِكَ أَفْضَلُ.
Maana yake, "Yaliyo juu ya kikoi na kujizuia na hilo ni bora." Ilivyokusudiwa ni juu ya kitovu ni sehemu mtu anapofungia kikoi au kuvalia suruwali, yaani ni kuanzia juu ya kitovu mpaka sehemu ya juu. Ajihadhari na kumuwekea mdomoni huu ni uchafu na ni jambo lililo kinyume na maumbile, na kazi ya sheitani, na njia ya kudhalilisha kwani mdomo una karama yake, na ni sehemu ambayo linatajwa jina la Mola Mtukufu.
2.Kusali Salaa ya aina yoyote ile.
Mwanamke mwenye hedhi amesamehewa asisali wakati wa hedhi yake, na wala Salaa zake alizoacha wakati wa hedhi yake hazilipi. Lakini kwa ukumbusho tu, ikiwa kama mwanamke atapata hedhi baada ya kuingia wakati wa Salaa basi ni lazima Salaa ya wakati ule ailipe, kwani Salaa ya wakati ule ilikwisha kuwa wajibu kwake. Hadithi ya Bi Fatma bint Habish yeye alikuwa anapata damu ya istihadha, Mtume S.A.W akamwambia.,"
إِذَا كَانَ دَمُ الْحَيْضَةِ فَإِنَّهُ أَسْوَدُ يُعْرَفُ فَإِذَا كَانَ ذَلِكَ فَأَمْسِكِي عَنْ الصَّلَاةِ فَإِذَا كَانَ الْآخَرُ فَتَوَضَّئِي وَصَلِّي فَإِنَّمَا هُوَ عِرْقٌ.
Maana yake, "Kama damu ya hedhi nyeusi inajulikana, na ikiwa ni hivyo basi uache kusali na kama ikiwa vingine atawadhe na asali, maana hiyo ni damu ya mishipa."
3.Kufunga Saumu.
Mwanamke mwenye hedhi haruhusiwi kufunga saumu wakati wa hedhi yake, na ikiwa hedhi imemjia katika mwezi wa Ramadhani basi siku zote zile ambazo hakufunga kwa ajili ya hedhi ni lazima azilipe baada ya kumaliza hedhi yake, na hatoi kafara yoyote ile. Kasema Bibi Aisha R.A.A.H,"
كُنَّا نَحِيضُ عِنْدَ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَيَأْمُرُنَا بِقَضَاءِ الصَّوْمِ
Maana yake, "Tulikuwa tunakwenda hedhi wakati wa Mtume S.A.W. alituamrisha kulipa Saumu."
4.Kufanya Tawafu.
Mwanamke aliye na hedhi haruhusiwi kutufu Al Kaaba. Kutoka kwa Ibn bin Abbaas R.A.A kasema, "Kasema Mtume S.A.W.,"
الْحَائِضُ وَالنُّفَسَاءُ إِذَا أَتَتَا عَلَى الْوَقْتِ تَغْتَسِلَانِ وَتُحْرِمَانِ وَتَقْضِيَانِ الْمَنَاسِكَ كُلَّهَا غَيْرَ الطَّوَافِ بِالْبَيْتِ.
Maana yake, "Wenye hedhi na damu ya ujusi (nifasi) wakifika kwenye Miqat (sehemu wanayo hirimia watu wakati wa Hijja na Umra), wataoga na watahirimia na watafanya mambo yote ya haji (wakati wa Haji) isipokuwa kutufu Al Kaaba."
5.Kukaa Itikafu.
Moja ya shuruti ya kukamilika itikaf ni lazima iwe ndani ya msikiti, na wanawake wenye hedhi hawaruhusiwi kuingia misikitini wakati wa hedhi zao. Hadithi aliyoitoa Ummu Attiyah na kutolewa na Abu Daud na Ibn Maajah kasema, "Mtume S.A.W. amewaamrisha wanawake wenye hedhi kujitenga na misikiti." (Yaani kutokuingia ndani.")
6.Kusoma Qur`ani.
Wanawake wenye hedhi hawaruhusiwi kusoma Qur`ani na wala kuushika msahafu, kwani wakati wa hedhi zao wanakuwa hawana tohara. Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Al-Waaqia`h aya ya 79,"
﴿لاَ يَمَسُّهُ إِلاَّ المُطَهَّرُونَ﴾.
Maana yake, "Hapana akigusae ila aliyetakaswa na mabaya."
Hadithi ya Jabir R.A.A. kasema, Mtume S.A.W. kawakataza wenye janaba na wanawake wenye hedhi kushika na kusoma Qur`aani.,"
لاَ يَقْرَؤُونَ الْقُرْآنَ، وَلاَ يَطَؤُونَ مُصْحَفًا بِأَيْدِيهِمْ حَتَّى يَكُونُوا مُتَوَضِّئِينَ.
Maana yake, "Hawasomi Qur`aani na wala hawaushiki msahafu kwa mikono yao mpaka wawe wenye kutawadha (waliotoharika)." Lakini kasema Jabir bin Zaid mwanamke mwenye hedhi anaweza kusoma Qur`aani kichwani yaani kile alichohifadhi bila kuangalia msahafu (yaani kimoyomoyo). Na siku hizi wanavyuoni wengi wamewaruhusu wanafunzi na waalimu kuisoma ikiwa ni wakati wa darasa zao.
7.Kupewa Talaka.
Haijuzii kwa mtu kumpa talaka mke wake wakati wa hedhi yake, na ikiwa mtu atafanya hivyo atakuwa amehalifu amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake S.A.W, lakini talaka itakuwa ni sahihi. Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat ATTalaaq aya ya 1,"
﴿فَطَلِّقُوهُنَّ لِعِدَّتِهِنَّ﴾.
Maana yake, "Mtakapotoa talaka kwa wanawake (mtakapo wawacha) toeni talaka wakati wa eda zao." (Yaani waacheni katika tohara zao ambazo katika hizo tohara hamjawahi kuwaingilia.) Na pia hadithi waliyokubaliana wanavyuoni wote, wanasema, "Wakati wa Mtume S.A.W. Ibn Umar R.A.A. alimpa talaka mke wake naye yuko katika hedhi, akaja Umar bin Khatab R.A.A. kumuuliza Mtume S.A.W. aliyofanya mtoto wake, akasema Mtume S.A.W.,"
مُرْهُ فَلْيُرَاجِعْهَا ثُمَّ لِيُمْسِكْهَا حَتَّى تَطْهُرَ ثُمَّ تَحِيضَ ثُمَّ تَطْهُرَ ثُمَّ إِنْ شَاءَ أَمْسَكَ بَعْدَ ذَلِكَ وَإِنْ شَاءَ طَلَّقَ.
Maana yake, "Mwamrishe amrejee (mke wake), na akaye naye mpaka atoharike, halafu aende hedhi halafu atoharike akipenda akaye naye na akipenda amwache."
8.Kuumika damu.
Wanakatazwa wanawake wenye hedhi kuumika damu kwa sababu ya hofu ya kuwa wadhaifu.
|