Kuoga josho (kubwa) ni kujimwagia maji tahir mwili mzima, kwa nia ya kujitoharisha kutokana na hadathi kubwa au kwa ajili ya kufuata sunna. Na tohara imegawika katika sehemu mbili, wajibu na Sunna.
1. JOSHO LA WAJIBU (FARIDHA).Josho la wajibu linakuwa kwa sababu zifuatazo: *Kuoga janaba. *Kuoga hedhi. *Kuoga nifasi. *Kuosha maiti ya Mwislamu. *Kuoga kwa mtu aliekuwa mushirik anaposilimu.
I. Kutokwa manii.Yoyote atakaetokwa na manii kwa sababu yoyote ile basi anakuwa katika hali ya janaba na itamuwajibikia kuoga. Kasema Mwenyezi Mungu katika Surat Al-Maida aya ya 6, " ﴿وَإِن كُنتُم جُنُباً فَا طَّهَّرُوا﴾. Maana yake, "Na mkiwa na janaba basi ogeni." Hadithi iliyo hadithiwa na Ibn Abbaas kuhusu mwanamke aliekuwa akiona katika ndoto na kutoka manii alipoulizwa Mtume S.A.W akasema,[1] “ عَلَيْهَا الْغُسْلُ إِذَا أَنْزَلَتْ. Maana yake, “Inamuajibikia kuoga ikiwa atashuka (yaani yakimtoka manii)”.
II.Zikigusana tupu mbili ya mwanamume na mwanamke.Zikigusana tupu mbili ya mwanamume na mwanamke hata kama hawakutokwa na manii basi kuoga josho kubwa ni lazima yaani wajibu. Hadithi iliyosimuliwa na Bibi Umm Salama R.A.A.H. kasema, “Kasema Mtume S.A.W[2],” إِذَا الْتَقَى الْخِتَانَانِ فَالْغُسْلُ وَاجِبٌ أَنْزَلَ الرَّجُلُ أَوْ لَمْ يُنْزِل. Maana yake, “Zikigusana tupu mbili kuoga ni wajibu akishusha manii au hakushusha”.
III. Baada ya kukatika Hedhi:Kuoga josho kubwa baada ya kukatika hedhi ni wajibu. Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Al-Baqara aya ya 222," ﴿فَاعتَزِلُوا النِّسآءَ فِى المَحِيضِ وَلاَ تَقرَبُوهُنَّ حَتَّى يَطهُرنَ﴾. Maana yake, "Basi jitengeni na wanawake wakati wa hedhi (zao). Wala msiwakaribie mpaka wataharike (waoge)."
IV.Baada ya kukatika Nifasi:Kuoga josho kubwa baada ya kukatika nifasi ni wajibu nayo ni kwa kuona alama ya utohara au ukavukavu.
V. Kuosha Maiti ya Muislamu:Kuosha maiti ya Muislamu kabla ya kuzikwa kwake ni faridha kwa kila Muislamu mwanamke au mwanamume ila tu kwa yule aliye kufa shahiid. Abu `Ubeyda kasema, “Nimearifiwa kutoka kwa Mohammed bin Siyriyn amesema, “Ummu `Atiyyah L-Ansariyyah amesema, “Mtume S.A.W. alituijia wakati binti yake alipofariki dunia akasema, [3]" اِغْسِلْنَهَا ثَلاَثًا أَوْ خَمْسًا أَوْ أَكْثَرَ مِنْ ذَلِكَ، إِنْ رَأَيْتُنَّ ذَلِكَ بِمَاءٍ وَسِدْرٍ وَاجْعَلْنَ فِي الآخِرَةِ شَيْئًا مِنْ كَافُورٍ، فَإِذَا فَرَغْتُنَّ فَآذِنَّنِي. Maana yake, “Muosheni mara tatu au mara tano au zaidi ya hivyo, mkiona inahitajia kwa maji na majani ya mkunazi. Na mwisho mumpake kafuur au kitu kutokana na kafuur na mkimaliza nijulisheni.”
VI. Kuoga kwa aliyekuwa mshirikina akisilimu:Kuoga kwa aliyekuwa mushrik akisilimu ni faridha.. Hadith iliyotolewa na Abu Huraira kasema, “Mtume S.A.W alimwamrisha Thamama Al Hanafii kuoga baada tu ya kusilimu kwake[4]." 2. JOSHO LA SUNNA.Kuoga josho la sunna linakuwa katika hali zifuatazo:
1.Kuoga kwa ajili ya kuhirimia Umra au Hijja.Hadithi iliyosimuliwa na Ibn Abi Ziyad kasema baba yake Zaid bin Thabit,[5] “ أَنَّهُ رَأَى النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ تَجَرَّدَ لِإِهْلَالِهِ وَاغْتَسَلَ. Maana yake, “Yeye alimuona Mtume S.A.W. alivaa ihram zake na akaoga kwa ajili ya kuhirimia,” Hata wale wenye hedhi na wenye nifasi wanatakiwa kuoga josho wakati wa kuhirimia. Abu `Ubayda kutoka kwa Jaabir bin Zaid kutoka kwa (Seyyida) `Aisha mama wa Waislamu (R.A.A.H.) amesema, “Asmaa bint `Umaysi alimzaa Muhammad bin Abi Bakar jangwani. Abu Bakar akamtajia hayo Mtume (S.A.W.) akamjibu akasema, [6]“ مُرْهَا فَلْتَغْتَسِلْ ثُمَّ لِتُهِلَّ. Maana yake, “Mwamrishe akoge halafu ahirimie.”
2. Kuoga kwa ajili ya kuingia Makka.Kuoga wakati wa kuingia Makka ni Sunna, kwani Mtume S.A.W. alikuwa akioga kila mara anapoingia Makka. Hadithi iliyo hadithiwa na Nafii, kasema, [7]“ أَنَّ ابْنَ عُمَرَ كَانَ إِذَا قَدِمَ مَكَّةَ بَاتَ بِذِي طَوًى حَتَّى يُصْبِحَ وَيَغْتَسِلَ ثُمَّ يَدْخُلَ مَكَّةَ نَهَارًا وَيَذْكُرُ عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنَّهُ فَعَلَهُ. Maana yake, “Alikuwa Ibn Umar R.A.A. wakati wa kuingia Makka alikuwa akilala Dhu Khulaifa mpaka kuchwe na anaoga halafu anaingia Makka na imetajwa pia Mtume S.A.W. alikuwa akifanya hivyo
3. Kuoga kwa ajili ya kusimama Arafa.Kuoga kwa ajili ya kusimama Arafa siku ya Hajj ni sunna ya Mtume S.A.W. Kutoka kwa Ibn Umar R.A.A kasema[8], " كَانَ يَغْتَسِلُ لِإِحْرَامِهِ قَبْلَ أَنْ يُحْرِمَ وَلِدُخُولِهِ مَكَّةَ وَلِوُقُوفِهِ عَشِيَّةَ عَرَفَةَ. Maana yake, “Alikuwa Mtume S.A.W. akioga kabla ya kuhirimia na wakati wa kuingia Makka na kwa kusimama Arafa mchana”.
4.Kuoga kwa ajili ya Salaa ya Ijumaa.Kuoga siku ya Ijumaa ni Sunna ya Mtume S.A.W. na ni kitu alichoamrisha tukifanye. Hadithi iliyohadithiwa na Abu Said al Kudhry R.A.A. kasema, “Kasema Mtume S.A.W,[9] “ الْغُسْلُ يَوْمَ الْجُمُعَةِ وَاجِبٌ عَلَى كُلِّ مُحْتَلِمٍ. Maana yake, “Kuoga (ghusul) siku ya ijumaa ni wajibu kwa kila aliye baleghe”. Wanavyuoni wamekhitilifiana makusudi ya josho la siku ya ijumaa baadhi yao wamesema ni kwa ajili ya siku ya ijumaa, na baadhi yao wamesema ni kwa ajili ya Salaa ya ijumaa. Wanavyuoni wengi wanasema kuoga huko ni sunna na sio wajibu ama kutumika neno wajibu katika hadithi ni kwa ajili ya kutilia nguvu na kusisitiza umuhimu wake. Na baadhi ya wanavyuoni wengine wanaona kuoga siku ya ijumaa inafikia daraja ya wajibu.
5.Kuoga katika Idi mbili.Kuoga katika Iddi mbili ni Sunna. Ingawa ziko Hadithi zinaozoelezea kuoga kwa siku za Iddi hadithi hizo hazikuthibiti. Kipimo walichochukulia wanavyuoni ni kuoga kwa siku ya ijumaa na kwa vile Masahaba walikua wakioga wakati wa Idd mbili. [1] Al Rabi`u 1/65 (136). [2] Al Rabi`u 1/65 (135). [3] Al Rabi`u 1/156 (475), Abu Daawud 8/414 (2734), ATtirrmidhy 4/103 (911), Nnasaai 6/436 (1858), Bukhaari 4/478 (1175), Muslim 5/17 (1557), Al Rabi`u (480). [4] Baihaqy 1/112 (145). [5] Ttirmidhy 3/344 (760), Ibn Haziim 4/161 (2595). [6] Al Rabi`u 1/144 (442) [7] Abu Daawud 5/207 (1589). [8] Muwataa 3/465 (1152). [9] Al Rabi`u 1/91 (281/282), Abu Daawud 1/417 (288), Baihaqy 1/293 (1304), Bukhaari 2/293 (830), Muslim 4/309 (1397). |