Maana ya neno udhu kilugha ni usafi, na kisheria ni kusafisha viungo makhsusi, kwa kutumia maji yaliyo safi tahiri, kwa makusudi ya kufanya ibada, au kwa kuwa msafi mwenye tohara kama alivyoamrisha Mwenyezi Mungu Mtukufu, na Mtume Wake S.A.W. Na kuwa na udhu ni wajibu kwa kutimia baadhi ya ibada, kama vile Salaa na kadhalika. Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Al-Maida aya ya 6," ﴿يَأَيُّهَا الَّذِينَ ءآمَنُوا إِذَا قُمتُم إِلَى الصَّلاَةِ فَاغسِلُوا وُجُوهَكُم وَأَيدِيَكُم إِلَى المَرَافِقِ وَامسَحُوا بِرُءُوسِكُم وَأَرجُلَكُم إِلَى الكَعبَينَ﴾. Maana yake, "Enyi Mliyoamini mnaposimama ili mkasali osheni nyuso zenu na mikono yenu mpaka vifundoni na mpake (maji) vichwa vyenu, na osheni miguu yenu mpaka vifundoni." Hadithi ya Ibn Abbaas R.A.A. kasema, "Kasema Mtume S.A.W.[1]" لا إيمان لِمَنْ لا صَلاةَ لَهُ وَلا صَلاةَ لِمَنْ لا وُضُوءَ لَهُ. Maana yake, "Hana imani asiyekuwa na Salaa na wala (hana) Salaa asiyekuwa na udhu." Pia hadithi waliyokubaliana wanavyuoni wote, kasema Mtume S.A.W.[2]," لَا صَلاةً بِغَيْرِ طُهُورٍ. Maana yake, "Hana Salaa asiyekuwa na tohara.".
1. ALIYE FARADHISHIWA UDHU.Kuwa na udhu ni wajibu kwa kila muisilamu mwenye akili timamu aliewajibikiwa kutimiza ibada ambayo inahitajia kuwa na udhu, kama vile kusali. Wale ambao hawana akili wamesamehewa kufanya ibada zote. Kasema Alii R.A.A., "Kasema Mtume S.A.W.,[3]" رُفِعَ الْقَلَمُ عَنْ ثَلَاثَةٍ عَنْ النَّائِمِ حَتَّى يَسْتَيْقِظَ وَعَنْ الصَّبِيِّ حَتَّى يَحْتَلِمَ وَعَنْ الْمَجْنُونِ حَتَّى يَعْقِلَ. Maana yake, "Wamesamehewa (watu aina) tatu aliyelala mpaka aamke, mtoto mdogo mpaka abaleghe, na aliepungukiwa na akili mpaka zirudi."
2. HUKUMU YA UDHU.Hukumu ya udhu inahitilafiana kufuatana na hali na sababu inayokusudiwa, inaweza ikawa ni udhu wa Faridha au udhu wa Mubah (jambo linalopendeza) kama ifuatavyo:
3. UDHU WA FARIDHA.*Udhu unakuwa wa faridha wakati ambao: kuwa na udhu ni sharti ya lazima kutimia kwanza kwa ibada inayotaka kufanywa ili iweze kutimia na kukubalika. Mfano:
1.Kusali Salaa yoyote ile ya faridha, au Sunna, au nafla:Mtu asiyekuwa na udhu anakatazwa kusali Salaa zote za faridha, za Sunna, na za nafla. Kwani kuwa na udhu ni sharti ya lazima kutimia kwa kukubaliwa Salaa. Kasema Mola Mtukufu katika Surat Al-Maida aya ya 6, “ ﴿يَأَيُّهَا الَّذِينَ ءآمَنُوا إِذَا قُمتُم إِلَى الصَّلاَةِ فَاغسِلُوا وُجُوهَكُم وَأَيدِيَكُم إِلَى المَرَافِقِ وَامسَحُوا بِرُءُوسِكُم وَأَرجُلَكُم إِلَى الكَعبَينَ﴾. Maana yake, "Enyi Mliyoamini mnaposimama ili mkasali osheni nyuso zenu na mikono yenu mpaka vifundoni na mpake vichwa vyenu, na osheni miguu yenu mpaka vifundoni." Pia Kasema Mtume S.A.W.[4]," لَا يَقْبَلُ اللَّهُ صَلَاةَ أَحَدِكُمْ إِذَا أَحْدَثَ حَتَّى يَتَوَضَّأَ. Maana yake, "Hakubali Mwenyezi Mungu Salaa ya yeyote yule aliyepata tokeo la kuharibu udhu (kama vile kutokwa na choo kidogo au kikubwa, au upepo na kadhalika) mpaka atawadhe."
2. Kutufu Al Kaaba:Ibada ya tawafu inahitajia kuwa na udhu kamili. Tawafu imefananishwa na Salaa, na kama vile udhu ni sharti ya lazima kutimia kwa Salaa basi ni vivyo hivyo udhu ni sharti ya lazima kutimia kwanza kwa kukamilika kwa tawafu. Kasema Ibn Abbaas R.A.A., “Kasema Mtume S.A.W.[5]," الطَّوَافُ حَوْلَ الْبَيْتِ مِثْلُ الصَّلَاةِ إِلَّا أَنَّكُمْ تَتَكَلَّمُونَ فِيهِ فَمَنْ تَكَلَّمَ فِيهِ فَلَا يَتَكَلَّمَنَّ إِلَّا بِخَيْرٍ. Maana yake, "Tawafu kuizunguka nyumba (Al Kaaba) ni kama Salaa isipokuwa nyinyi mnazungumza humo, (yaani mnaruhusiwa kuzungumza), na yeyote atakayezungumza humo basi asizungumze ila maneno ya kheri."
3. Kusoma Quraani kwa kuukamata msahafu.Yeyote asiyekuwa na udhu anakatazwa kusoma Quraani kwa kuukamata msahafu kufuatana na rai ya baadhi ya wanavyuoni, na kauli hiyo ina uzito zaidi. Rai hiyo wameiegemeza na dalili kutokana na kitabu cha Mwenyezi Mungu na Hadithi za Mtume S.A.W. Kasema Mola Mtukufu katika Surat Al-Waaqia`h aya ya 79,” ﴿لَّا يَمَسُّهُ إِلَّا الْمُطَهَّرُونَ﴾. Maana yake, Hapana akigusaye ila walio takaswa.”. Kutoka kwa Jabir R.A.A. kasema, "Kasema Mtume S.A.W.[6], “ ﴿الْجُنب والْحَائِض والذينَ لَمْ يكونوا عَلَى طهارة لا يَقرؤون الْقُرْآن ولاَ يَطؤونَ مصحفا بِأيديهم حَتَّى يكونوا مُتوضئين﴾. Maana yake, “Wenye janaba na hedhi, na wale ambao hawana tohara hawasomi Quraani na wala hawaukamati msahafu kwa mikono yao mpaka wawe wametawadha”. Asiekuwa na udhu anaweza kusoma kile alichohifadhi katika nafsi yake ali mradi hana hadath[7] kubwa.
UDHU ULIO WA MUBAHI (Wakupendeza). Udhu wa kupendeza na wa murua, ni ule ambao kuwa na udhu sio sharti ya lazima kuwepo, au kutimia kwa kufanya kitendo au ibada inayotaka kufanywa, na mtu anajitia udhu ili apate thawabu, na kujikaribisha karibu zaidi na Mola Mtukufu. Mfano: *Anapotaka kulala: Kasema Al`Baraa bi Aazb, “Kasema Mtume S.A.W.[8], “ إِذَا أَتَيْتَ مَضْجَعَكَ فَتَوَضَّأْ. Maana yake, “Unapokwenda kwenye kilalo chako basi tawadha”. *Anapoamka kutoka usingizini: Kasema Anas bin Malik R.A.A., "Kasema Mtume S.A.W.[9], “ فإِذَا اسْتيقَظَ وَذَكَرَ اللهَ انحلَّتْ عُقْدةٌ، فإِذَا توضَّأَ انحلَّتْ عُقْدَةٌ. Maana yake, “Na akiamka na akamdhukuru Mwenyezi Mungu inafunguka kifungo, na akitawadha kinafunguka kifungo”. *Wakati wa kuoga janaba: Kasema Bibi Aisha R.A.A.H., [10] “ كانَ رسُولُ الله صلى الله عليه وسلّم إذا أرادَ الغُسلَ من الجَنابةِ بدأَ فغَسلَ يَديْهِ ثمَّ يتوضأُ كَما يتوضأُ للصَّلاةِ. Maana yake, “Alikuwa Mtume S.A.W. akitaka kuoga janaba anaanza kwa kuosha mikono yake halafu anatawadha kama anavyotawadha wakati wa Salaa” *Akiwa na janaba akitaka kula au kulala. Kasema Bibi Aisha R.A.AH.,[11] “ كانَ النَّبِيّ صلى الله عليه وسلّمإذا كَانَ جنبًا، فأرادَ أنْ يأكلَ أو ينامَ توضأَ. Maana yake, “Alikuwa Mtume S.A.W. ikiwa ana janaba, na alikuwa akitaka kula au kulala akitawadha”. *Kwa kuondoa ghadhabu: Kutoka kwa Babu wa Attia kasema, "Kasema Mtume S.A.W[12], “ إِنَّ الْغَضَبَ مِنْ الشَّيْطَانِ وَإِنَّ الشَّيْطَانَ خُلِقَ مِنْ النَّارِ وَإِنَّمَا تُطْفَأُ النَّارُ بِالْمَاءِ فَإِذَا غَضِبَ أَحَدُكُمْ فَلْيَتَوَضَّأْ. Maana yake, “Hakika ghadhabu inatokana na sheitani, na sheitani kaumbwa na moto, na moto unazimwa kwa maji, akighadhibika mmoja wenu basi na atawadhe”. *Kuomba dua, kusoma Quraani na kadhalika: Ikiwa mtu anataka kusoma Qur`ani aliyoihifadhi, kuadhini, kuomba dua, kuingia msikitini, kupanda kipando, au anapotaka kuwa msafi na kadhalika basi anatawadha. [1] Al Rabi`u 1/54 (91). Mfano wa hadith hii imetolewa pia na Abu Daawud 1/141 (92), Ibn Maajah 1/482 (392), Ddaraquturun 1/72 (5). [2] Abu Daawud 1/86 (54), Ahmad 10/6 (4470), Ibn Maajah 1/320 (269), Ddaaramy 1/185 (686), ANnaasai 1/245 (139), Ibn Haaban 4/605 (1705) [3] Abu Daawud 11/481 (3825). [4]Abu Daawud 1/87 (55). Mfano wa Hadithi hii pia imetolewa na Bukhaari 1/232 (132), Muslim 2/6 (330), Ahmad 16/273 (7732). [5] ATtirimidhy 4/60 (883) [6] Al Rabi`u 1/26 (11) . Mfano wa Hadithi hii pia imetolewa na ATtirmidhy 1/221 (121), na Ibn Maajah 2/242 (5880) wao wametaja mwenye janaba na mwenye hedhi. [7] Hali ya kuwa na janaba, huwa na hedhi, au damu ya nifasi. [8] Abu Daawud 13/243 (4389), Bukhaari 1/412 (239), Muslim 13/235 (4884). [9] Al Rabi`u 1/63 (130). Mfano wa hadithi hii imetolewa pia na Abu Daawud 4/70 (1111), Bukhaari 4/310 (1074). [10] Bukhaari 1/415 (240), Muslim 2/193 (475), Ddaraqutun 1/113 (11), Ibn Haaban 3/469. [11] Muslim 2/176 (461). [12] Abu Daawud 12/403 (4152), Ahmad 36/421 (17302). |