Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi
Haja ndogo ya binaadamu au mnyama ni najisi. Haja ndogo ya mtoto mchanga wa kiume mwenye umri ulio chini ya miaka miwili ambaye hajaanza kula kitu isipokuwa maziwa yenyewe siyo najisi, na ikimdondokea mtu, basi anarashia maji sehemu ile iliyomwagikiwa na anaikamua. Hivi ndivyo ilivyothibiti kutoka kwa Mtume S.A.W. Kasema Ibn Abbaas R.A.A, [1], “ إن أم قيس بنت محصنأَتَتْ بِابْنٍ لَهَا صَغِيرٍ لَمْ يَأْكُلْ الطَّعَامَ إِلَى رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَأَجْلَسَهُ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فِي حَجْرِهِ فَبَالَ عَلَى ثَوْبِهِ فَدَعَا بِمَاءٍ فنضحه نضحا وَلَمْ يَغْسِلْه. Maana yake, "Kwamba Umm al Qaisy bint Muhsin alikuja na mtoto wake mwanamme mdogo hajaanza kula chakula kwa Mtume S.A.W, Mtume S.A.W. alimkalisha (yule mtoto mchanga) kwenye mapaja yake na akamkojolea juu ya nguo zake, Mtume S.A.W. akaagiza maji na akayarashia rashia kwenye nguo halafu akakamua na wala hakuiosha." Ama ikiwa ni mkojo wa mtoto wa kike basi ni lazima uioshe sehemu ile vizuri. Kasema Lubabah bint Harith, "Kasema Mtume S.A.W.,[2] " إِنَّمَا يُغْسَلُ مِنْ بَوْلِ الْأُنْثَى وَيُنْضَحُ مِنْ بَوْلِ الذَّكَرِ Maana yake, “Ni mkojo wa mtoto wa kike tu ambao unatakiwa kuoshwa, na unarashia maji kwa mkojo wa mtoto wa kiume.” Lakini ikiwa wote wataanza kula chakula chochote kile basi ni lazima ioshwe vizuri.
2 .KINYESI (HAJA KUBWA).Kinyesi cha binaadamu, na cha wanyama wanaokula nyama, au cha wanyama wale walioharamishwa, ni najisi. Kasema Mwenyezi Mungu S.W.T katika Surat AN-Nnisaai aya ya 43 kasema,"
﴿أَو جَآءَ أَحَدٌ مِّنكُم مِنَ الغَآئِطِ﴾.
Maana yake, "Au mmoja wenu akitoka msalani." Inavyokusudiwa ikiwa mtu akitoka msalani kwa ajili ya haja.". Ama kinyesi cha wanyama wale wasiokula nyama siyo najisi. Vinyesi vya wanyama wenye kwato kama vile: Ng`ombe, mbuzi, farasi, punda, numbu na kadhalika sio najisi.
3. MADHII.Madhii[3] ni maji meupe mepesi yanayotoka kwa matamanio au kwa kupandwa na ashiki[4] na hii ni inakuwa kwa wote wanawake na wanaume. Kutoka kwa Ali bin Abi Talib R.A.A. kasema, "Kulikuwa na mwanamume mmoja ambaye alikuwa akitokwa na madhii kila mara, na aliona haya kumuuliza Mtume S.A.W., akamtuma Mikidadi bin Al-Aswad R.A.A. amuulizie kwa Mtume S.A.W., akamuulizia, Mtume S.A.W akamjibu[5],''
فِيهِ الْوُضُوءُ.
Maana yake, "Na atawadhe."
4. WADII.Wadii ni maji meupe mazito yanoyotoka bila matamanio baada ya haja ndogo. Hadithi iliyo hadithiwa na Ibn Abbaas R.A.A., "Kasema Mtume S.A.W,[6] “
الْمَنِيُّ وَالْوَذِيُّ وَالْوَدِيُّ وَدَمُ الْحَيْضَةِ وَدَمُ النِّفَاسِ نَجِسٌ لاَ يُصَلَّى بِثَوْبٍ وَقَعَ فِيهِ شَيْءٌ مِنْ ذَلِكَ حَتَّى يُغْسَلَ وَيَزُولَ أَثَرُهُ.
Maana yake, "Manii, na Alwadhii, na Alwadii na damu ya hedhi, na damu ya nifasi ni najisi. Haifai kusalia na nguo iliyopata chochote katika hivyo mpaka ioshwe na iondoke ile najasa."
5. MANII.Manii ni maji meupe mazito yenye mbegu za uzazi yanayotoka kwenye utupu wa mwanamke, au mwanamume, kwa kujichezea, au kwa kuingiliana kati ya mwanamume na mwanamke, au kwa kuota, au kwa kupatwa na khofu, au furaha. Kasema Ibn Abbaas R.A.A, "Kasema Mtume S.A.W.[7],"
الْوُضُوءَ مِنَ الْمَذْيِ والغُسْلُ مِنَ المنيّ.
Maana yake, "Udhu kwa aliyetokwa na madhii na kuoga kwa aliyetokwa na manii." Kasema Bibi Aisha R.A.A.H.[8],
كُنْتُ أَغْسِلُ ثَوْبَ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ مِنَ الْمَنِيِّ، ثُمَّ يَخْرُجُ إِلَى الصَّلاَةِ وَالْمَاءُ يَقْطُرُ مِنْهُ.
Maana yake, "Nilikuwa nakosha nguo za Mtume S.A.W. zenye manii, halafu anatoka kwenda kusali na maji bado yanadondoka kwenye nguo."
6 DAMU YA HEDHI.Damu ya hedhi ni damu ambayo anayotoka mwanamke aliye baleghe ambayo humtoka kila mwezi. Damu hii ni najisi. Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Al-Baqara aya ya 222,"
{ وَيَسئَلُونَكَ عَنِ المَحِيضِ قُل هُوَ أَذَىً}
Maana yake, "Na wanakuuliza juu ya hedhi waambiye huo ni uchafu." Pia kasema Ibn Abbaas R.A.A., “Kasema Mtume S.A.W., [9]"
وَدَمُ الْحَيْضَةِ وَدَمُ النِّفَاسِ نَجِسٌ.
Maana yake, "Na damu ya hedhi na damu ya nifasi najisi." . Damu ya hedhi ni maarufu kwa wanawake, na inajulikana na inatofautiana na damu nyingine, yenyewe ni nzito na nyeusi. Kasema Fatima bint Abu Hubeish, “Kasema Mtume S.A.W.[10],"
إِذَا كَانَ دَمُ الْحَيْضِ فَإِنَّهُ دَمٌ أَسْوَدُ يُعْرَفُ.
Maana yake, "Ikiwa ni damu ya hedhi basi ni nyeusi inajulikana." Damu hii ni najisi.
7. DAMU YA ISTIHADHA.Damu ya Istihadha ni damu nyekundu nyepesi inayotoka kwenye uke wa mwanamke kwa ajili ya maradhi, damu hii ama inatoka mfululizo au baada ya kwisha siku zake za hedhi za kawaida. Kasema Ibn Abbaas R.A.A., “Kasema Mtume S.A.W.[11],"
«دَمُ الاِسْتِحَاضَةِ نَجِسٌ، لأَنَّهُ دَمُ عِرْقٍ، يَنْقُضُ الْوُضُوءَ».
Maana yake, ''Damu ya istihadha najisi, kwani ni damu ya mishipa inaharibu udhu."
MUHIMU YALIYO TOFAUTI KATI YA DAMU YA HEDHI NA DAMU YA ISTIHADHA. *Damu ya hedhi ni tokeo la kuharibu tohara kubwa na mtu anaacha kusali, kufunga, tawafu na kuingiliana na mkewe. Na anahitajia kuoga josho kubwa wakati wa kujitoharisha. Wakati istihadha ni hadath ndogo na anajitoharisha kwa kutawadha tu na hakatazwi yaliyotajwa hapo juu. * Hedhi ni damu anayotoka mwanamke aliebaleghe kila mwezi. Istihadha ni damu inayotokana na maradhi na sio ya kawaida. *Hedhi ni nzito nyeusi yenye harufu. Istihadha ni nyepesi nyekendu isiyo kuwa na harufu. *Hedhi inatoka katika tumbo la uzazi. Istihadha inatoka katika mishipa ya damu nje ya tumbo la uzazi.
8. DAMU YA NIFASI.Damu ya nifasi, au damu ya ujusi, au damu ya uzazi, ni damu inayomtoka mwanamke baada ya kujifungua au kwa ajili ya kuharibu mimba. Nayo hii ni najisi. Kasema Ibn Abbaas R.A.A., “Kasema Mtume S.A.W.[12],"
ودَمُ الحَيْضَةِ ودَمُ النِّفاسِ نجَسٌ.
Maana yake, "Na damu ya hedhi na damu ya nifasi najisi."
9. TOHARA YA WANAWAKE.Tohara ya wanawake ni maji maji yanayotoka ukeni kwa mwanamke baada ya kukatika hedhi na kutoharika. Rangi yake ni nyeupe na hutoka baada ya mwanamke kumaliza siku zake za hedhi, au nifasi. Haya maji maji ni najisi, kwa sababu yanatokana na damu ya hedhi, au nifasi, na pia yanapitia katika sehemu ile ile inayopitia haja ndogo, hedhi, nifasi na kadhalika.
10. MATAPISHI NA MACHEUZI.Matapishi na macheuzi ni najisi. Kutoka kwa Jabir bin Zaid kasema, “Kasema Mtume S.A.W[13],"
مَن قَاءَ أو قَلَسَ فليتوضأْ.
Maana yake, "Mwenye kucheua au kutapika na atawadhe.". Baadhi ya wanavyuoni wanaona macheuzi na matapishi na damu inayotoka puani inaharibu udhu, lakini haiharibu Salaa ya wakati ule. Na ikimtokea mtu basi anatawadha tu na anaunganisha Salaa yake pahala alipofikia ali mradi hakuzungumza au kufanya kitendo kingine.
11. DAMU INAYOTIRIRIKA KUTOKA PUANI.Damu inayotiririka kutoka puani kwa sababu au bila sababu ni najisi. Kasema Bibi Aisha R.A.A.H., "Kasema Mtume S.A.W.[14],"
مَنْ أَصَابَهُ قَيْءٌ أَوْ رُعَافٌ أَوْ قَلَسٌ أَوْ مَذْيٌ فَلْيَنْصَرِفْ فَلْيَتَوَضَّأْ
Maana yake, "Atakaye tapika au kutoka damu puani au kucheua au kutokwa na madhi atoke aende akatawadhe."
12. DAMU INAYOTIRIRIKA.Damu inayotoka kwa kutiririka kwa sababu au bila sababu, inayotoka mwilini mwa binaadamu, au mnyama wa ardhini, au wadudu. Ambayo inayotoka kwenye jeraha, au masikioni, au machoni, au puani, au sehemu nyingine katika mwili ni najisi, ikiwa ni kidogo au ni nyingi. Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu, katika Surat Al-An-a`am aya ya 145,"
﴿أَوْدَماً مَّسفُوحاً﴾.
Maana yake, "Au damu inayomwagika." Kutoka kwa Ibn Abbaas R.A.A. kasema, "Kasema Mtume S.A..W [15],"
دَمُ الاِسْتِحَاضَةِ نَجِسٌ، لأَنَّهُ دَمُ عِرْقٍ، يَنْقُضُ الْوُضُوءَ.
Maana yake, "Damu ya istihadha najisi kwa sababu ni damu ya mishipa na inaharibu udhu." Lakini damu ya wanyama wa baharini na damu ya bandama/wengu na maini ya wanyama waliyochinjwa kihalali zenyewe sio najisi
13. MAITI (MIZOGA).Mizoga iliyokusudiwa ni ile ya maiti ya kila mnyama anaeishi nchi kavu mwenye damu, aliekufa kwa kunyongwa, kupigwa umeme, kufa kwa ajili ya maradhi na sababu kama hizo. Yaani hawakuchinjwa kisheria. Kasema Mwenyezi Mungu katika Surat Al-Maida aya ya 3,"
﴿حُرِّمَت عَلَيكُمُ المَيتَةُ وَالدَّمُ وَلَحمُ الخِنزِيرِ وَمَآ أُهِلَّ لِغَيرِ اللهِ﴾.
Maana yake, "Mmeharamishiwa nyamafu (mizoga) na damu na nyama ya nguruwe, na kinyama kilichochinjwa si kwa ajili ya Mwenyezi Mungu." Pia kasema Mola Mtukufu katika Surat Al`An-a`am aya ya 145, “
﴿أَوْ فِسْقاً أُهِلَّ لِغَيْرِ اللَّهِ بِه﴾.
Maana yake, “Au kwa upotofu kimechinjwa kwa jina la asiye kuwa Mwenyezi Mungu”. Pia kipande au sehemu ya nyama ilio katwa cha mnyama wa nchi kavu nae bado yuko hai, hukumu yake ni sawa sawa na hukumu ya mzoga nacho ni najisi. Kasema Atta bin Yasir, “Kasema Mtume S.A.W.[16]"
مَا قُطِعَ مِنْ الْبَهِيمَةِ وَهِيَ حَيَّةٌ فَهِيَ مَيْتَةٌ.
Maana yake, "Kikikatwa kipande (au kiungo) cha mnyama na yeye yu hai hicho ni mzoga ." Samaki, wanyama wa baharini, na wadudu wa mfano wa nzige hawahisabiwi kama ni mizoga na najisi,na maiti zao kwa wale wenye kuliwa ni halali kuliwa. Kasema Ibn Abbaas R.A.A., “Kasema Mtume S.A.W.[17] ,"
أُحِلَّتْ لَكُمْ مَيْتَتَانِ وَدَمَانِ : فَالْمَيْتَتَانِ الْجَرَادُ والسَّمَكُ ، وَ الدَّمَانِ الْكَبِدُ وَالطِّحَالُ.
Maana yake, "Mmehalalishiwa mizoga miwili na damu aina mbili ama mizoga ni panzi nasamaki. Na damu mbili ni maini na bandama." Hapa kahusishwa panzi kwa sababu hana damu, na kiasi kwa hukumu hiyo imechukuliwa pia kwa wanyama wote wasiokuwa na damu. Kasema Abu Huraira R.A.A., kuhusu bahari na vile vinavyo ishi ndani yake, “Kasema Mtume S.A.W."[18]
هُوَ الطَّهُورُ مَاؤُهُ الْحِلُّ مَيْتَتُهُ.
Maana yake, "Maji yake ni tahiri na maiti zake ni halali (kuliwa)."
Ama kuhusu vijidudu ambavyo havina damu kama vile vipepeo, nzi, mchwa, nge, na vidudu vinavyofanana na hivyo, hivi navyo sio najisi, na hata vikiangukia ndani ya chakula, au ndani ya maji, na vikifia humo, basi chakula au maji hayo hayanajisiki, na kipimo ni hadithi iliyohadithiwa na Jabir bin Zaid R.A.A. kasema, "Kasema Mtume S.A.W.[19],"
إِذَا وَقَعَ الذُّبَابُ فِي إِنَاءِ أَحَدِكُمْ فَامْقُلُوهُ، فَإِنَّ فِي أَحَدِ جَنَاحَيْهِ دَاءً، وَفِي الآخَرِ شِفَاءً، وَإِنَّهُ يُقَدِّمُ الدَّاءَ وَيُؤَخِّرُ الدَّوَاءَ.
Maana yake, Atakapoangukia nzi katika moja ya vyombo vyenu, mzamisheni, kwani katika moja la mabawa yake mawili kuna maradhi, na katika lingine kuna dawa, naye hutanguliza kwanza bawa lenye maradhi na akaliakhirisha lenye ponyo.” Ar-Rabi`i kasema, “(أمقُلُوهُ.) mzamisheni.Kwa maana hii maiti hio sio najisi na kinywaji au chakula kile hakikunajisika na kinaweza kunywewa au kuliwa hata akifia humo. Na kipimo hiki kimetumiwa kuhukumia wadudu wengine wasiokuwa na damu kama panzi na kadhalika kuwa sio najisi.
14. NGURUWE.Nguruwe na kila kitu chake ni najisi na haramu, na imeharamishwa kutumia vitu vyake kama vile nyama, ngozi, manyoya, mafuta na mafupa vyote hivyo pia ni haramu. Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Al-Baqara aya ya 173 kasema,"
﴿إنَّما حَرَّمَ عَلَيكُمُ المَيتَةَ وَالدَّمَ وَلَحمَ الخِنزِيرِ وَمَآ أُهِلَّ بِهِ لِغَيرِ اللهِ﴾.
Maana yake, "Yeye amekuharamishieni mzoga na damu na nyama ya nguruwe na kilichochinjwa, katika kuchinjwa kwake, sio kwa ajili ya jina la Mwenyezi Mungu."
Na pia kasema Mola Mtukufu katika Surat Al Ana`am aya 145 kasema,"
﴿أَو لَحمَ خِنزِيرٍ فَإِنَّهُ, رِجس﴾.
Maana yake, "Au nyama ya nguruwe, kwani hiyo ni uchafu." Na pia katika Surat Al-Maida aya ya 3 kasema,"
﴿حُرِّمَت عَلَيكُمُ المَيتَةُ وَالدَّمُ وَلَحمُ الخِنزِيرِ وَمَا أُهِلَّ لِغَيرِ اللهِ﴾.
Maana yake, "Mmeharamishiwa nyamafu na damu na nyama ya nguruwe, na kinyama kilichochinjwa si kwa ajili ya Mwenyezi Mungu."
15. MBWA.Mbwa ni najisi. Kasema Abu Huraira R.A.A., “Kasema Mtume S.A.W[20]., “
إذا وَلَغَ الكلبُ في إناءِ أحدِكم فليغسلْهُ سبعَ مراتٍ.
Maana yake, "Akiramba mbwa ndani ya chombo cha mmoja wenu basi akioshe mara saba”. (Inaweza kuwa kwa sababu ya jinsi vile sehemu ya pua ya mbwa ina unyevu nyevu wakati wote, na ananusa kila sehemu pamoja na sehemu zile zenye uchafu, kwa hivyo ile sehemu inachukua uchafu na vijidudu. Muandishi kuhusu makala inayohusiana na mbwa katika Encylopaedia Brittanica Vol VII ukarasa wa 497 amesema, "Hakika kichaa cha mbwa ni kitu cha kawaida kwa mbwa kuliko wanyama wengine" Hivyo basi uisilamu umemnajisisha mbwa kwa ajili ya mate yake, na unyevunyevu wa pua yake, kwa ajili ya kuchukua hadhari ya maradhi na mabaki ya najasa. Wanavyuoni wame tofautina katika unajisi wa mbwa yule aliefunzwa kwa ajili ya kuwindia kwa vile pua yake imehifadhiwa.
16. WANYAMA MBUA NA NDEGE WENYE KUCHA.Wanyama mbua wawindaji, na ndege wenye makucha wawindaji wenye kula nyama ni haramu kuliwa, na ni najisi. Kasema Mtume S.A.W,[21] “
أَكْلِ كُلِّ ذِي نَابٍ مِنْ السَّبُاعِ وَ ذِي مِخاْلَبٍ مِنْ الطَّيْرِحرام .
Maana yake, “Kula kila mnyama mbua wenye meno ya chonge katika wanyama walao nyama na ndege wenye makucha (za kuwindia) (wanao kula nyama) ni haramu” (Hawa ni wanyama na ndege wawindaji wanaokula nyama).
17. POMBE.Wanavyuoni wametofautiana unajisi wa pombe katika makundi matatu. Kundi la kwanza linasema pombe ni najisi, na wamechukuwa dalili zao kutokana na vile walivyoifasiri aya iliyo haramisha ulevi katika Surat Al-Maida aya ya 90. Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu,"
﴿إِنَّمَا الَخَمرُ وَالمَيسِرُ وَاْلأَنصَابُ وَاْلأَزلاَمُ رِجسٌ مِّن عَمَلِ الشَّيطاَنِ فَاجتَنِبُوهُ لَعَلَّكُم تُفلِحُونَ﴾.
Maana yake, "Bila shaka ulevi na kamari na kuwabudiwa (na kuombwa) asiyekuwa Mwenyezi Mungu, na kutazamia kwa mishale ya kupigia ramli (na vinginevyo yote haya) ni uchafu na ni katika kazi ya sheitani. Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufaulu."
Kundi la pili linasema pombe iliyo najisi ni ile tu iliyotengenezwa kwa ajili ya kunywewa, ama pombe ambayo iliyo tengenezwa kwa ajili ya kufanyia tiba kama vile ya kuuia vidudu kama vile spirit, au iliyowekwa ndani ya mafuta mazuri ili kusaidia kurashia, hiyo si najisi, na wameruhusu mtu kujitia mafuta haya, ikiwa tu katika kutengenezwa kwake hakuna kitu kilichokuwa haramu kimetumika. Na ikiwa kama kwa kutengenezea kwake vimetumika vitu vilivyo haramishwa basi ni haramu.
Na kundi la tatu limesema pombe ya aina yoyote ile sio najisi, lakini ni haramu kunywea kwa sababu asili yake, au vitu vilivyo tumiwa kutengenezea sio najisi.
UKUMBUSHO MUHIMU UHARAMU WA POMBE: Wanavyuoni wote wamekubaliana bila kuhitilafiana kuwa pombe ni haramu kunywewa. Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Al-Maida aya ya 90,"
﴿إِنَّمَا الَخَمرُ وَالمَيسِرُ وَالأَنصَابُ وَاْلأَزلاَمُ رِجسٌ مِّن عَمَلِ الشَّيطَانِ فَاجتَنِبُوهُ لَعَلَّكُم تُفلِحُونَ﴾.
Maana yake, "Bila shaka ulevi na kamari na kuwabudiwa (na kuombwa) asiyekuwa Mwenyezi Mungu, na kutazamia kwa mishale ya kupigia ramli (na vinginevyo yote haya) ni uchafu na ni katika kazi ya sheitani. Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufaulu" Pia Mtume S.A.W. ameitolea pombe onyo ya adhabu kali kwa yule atakaeinywa. Kasema Jabir R.A.A., “Kasema Mtume S.A.W[22],"
إِنَّ عَلَى اللَّهِ عَزَّ وَجَلَّ عَهْدًا لِمَنْ يَشْرَبُ الْمُسْكِرَ أَنْ يَسْقِيَهُ مِنْ طِينَةِ الْخَبَالِ.
Maana yake, "Mwenyezi Mungu amemuahidi atakaye kunywa ulevi, kuwa atamnyweshwa jasho la wakaazi wa motoni[23]." Pia Kasema Ibn Umar R.A.A, "Kasema Mtume S.A.W[24],"
لَا يَدْخُلُ الْجَنَّةَ مَنَّانٌ وَلَا عَاقٌّ وَلَا مُدْمِنُ خَمْرٍ.
Maana yake, "Hatoingia Peponi anaewasumbulia watu na wala atakayewatupa wazazi wake (yaani kuwadharau), na mnywaji wa pombe." Kasema Abdullahi bin Umar R.A.A, "Kasema Mtume S.A.W.[25],"
ثَلَاثَةٌ قَدْ حَرَّمَ اللَّهُ عَلَيْهِمْ الْجَنَّةَ مُدْمِنُ الْخَمْرِ وَالْعَاقُّ وَالدَّيُّوثُ الَّذِي يُقِرُّ فِي أَهْلِهِ الْخَبَثَ.
Maana yake, ''Watatu amewaharamishia Mwenyezi Mungu Pepo nao ni mnywaji ulevi, na anayewadharau wazazi wake, na mwanamume asiye kuwa na wivu ambaye anaye shuhudia mkewe anazini (naye akakaa kimya bila kusema chochote." Na dhambi na laana za pombe zinawapata wote wale waliojihusisha nayo akiwemo mnywaji, mtengenezaji, muuzaji, mbebaji, na anakae na mlevi wakati analewa. Kasema Ibn Umar R.A.A., “Kasema Mtume S.A.W[26]., “
لَعَنَ اللَّهُ الْخَمْرَ وَشَارِبَهَا وَسَاقِيَهَا وَبَائِعَهَا وَمُبْتَاعَهَا وَعَاصِرَهَا وَمُعْتَصِرَهَا وَحَامِلَهَا وَالْمَحْمُولَةَ إِلَيْهِ.
Maana yake, “Ameilaani Mwenyezi Mungu pombe, na mnywaji, na mhudumiaji wake, na muuzaji, na mnunuzi, na mtengenezaji, na yule anayetengenezewa, na anayebeba, na yule anayebebewa.”
Hadithi zinazo zungumzia uharamu wa kunywa pombe ni nyingi, hapa sio pahala pake. Ama kuhusu jasho la mlevi, wanavyuoni wametofautiana kwa kauli mbili, wale wanaosema pombe ni najisi basi wao wamesema hata jasho lake ni najisi pia, na wale waliosema pombe siyo najisi wao wanasema jasho lake sio najisi.
18. WANYAMA AU NDEGE WANAOKULA UCHAFU.Wanyama wote wanaokula najasa ni najisi na hawaruhusiwi kuliwa, au maziwa yao kunywewa mpaka wafungwe na kulishwa chakula safi na uchafu waliokula uwatoke. Kasema Ibn Umar R.A.A.,[27] “
نَهَى رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَنْ أَكْلِ الْجَلَّالَةِ وَأَلْبَانِهَا.
Maana yake, “Kakataza Mtume S.A.W. kula mnyama anayekula uchafu na kunywa maziwa yake." Sababu ni kwamba nyama au maziwa yale yanakuwa yameathiriwa na uchafu ule anaokula. Wanavyuoni wanasema ili aweze kutoharika na uchafu huo ndege anafungwa mchana na usiku mmoja, mbuzi anafungwa siku tatu, na ngamia na ng`ombe wanafungwa siku saba.
[1] Al Rabi`u 1/70 (152). Mfano wa hadithi hii pia imetolewa na Abu Daawud 1/456 (319), An-Nassai`y 1/491 (300), na wengineo. [2] Abu Daawud 1/457 (320). [3] Ulendelende wa kama vile wa manii unaotoka kwenye tupu za mbele za mwanamume au mwanamke kwa kupanda hamu ya kuingiliana. [4] Hamu ya kuingiliana inayompata mwanamume, au mwanamke, nyege. [5] Ibn Maajah 2/116 (497), Bukhaari 1/224 (129, 172). [6] Al Rabi`u 1/69 (148). [7]Al Rabi`u 1/57 (102/132). [8] Al Rabi`u 1/46 (151) [9] Al Rabi`u 1/69 (148). [10] Abu Daawud 1/378 (261), ANaasai 1/355 (215). [11] Al Rabi`u 1/69 (149). [12] Al Rabi`u 1/69 (148) [13]Al Rabi`u 1/58 (109), Ibn Maajah 4/80 (1211). [14] Ibn Maajah 4/80 (1211) [15] Al Rabi`u 1/69 (149). [16] Abu Daawud 8/41(2475), Ibn Maajah 9/409 (3207), ATtirmidhy 5/421 (1400), Ddarqatuni 4/292 (83) [17] Al Rabi`u 1/243 (618). Mfano wa Hadithi hii pia imetolewa na Ibn Maajah 10/51 (3305) [18] Abu Daawud 11/118 (876), Ibn Maajah 1/487 (380,381,382, 9/449 (3237), Baihaqy 15/51 (197), A`ttirmidhy 1/117 (64), Darqtuni 1/34 (4), Nnasaai 2/42 (380), Ibn Habaan 4/449 (1243). [19] Al Rabi`u 1/148 (371). Mfano wa hadithi hii imetolewa pia na Abu Daawud 10/323 (3346), Ibn Maajah 10/332 (2039), Ddaaramy 2/135 (2039), Bukhaari 11/99 (3073) 18/73 (5336). [20] Al Rabi`u 1/71 (155) , Bukhaari 1/298 (168), Muslim 2/120 (419). [21] Al Rabi`u 1/153 (387). Mfano wa Hadithi hii pia imetolewa na Muslim 10/73 (3574), Ibn Maajah 12/85 (5280), Abu Daawud 10/270 (3309), ATtirmidhy 5/412 (1394). [22] Muslim 10/257 (3732). Mfano wa Hadith hii pia imetolewa na Nnaasai 17/190 (5613), Ibn Haaban 12/183 (5360), Ahmad 29/400 (1435), 23/162 (14880), [23] Pia imesemwa ni usaha wa watu wa motoni. [24] ANnaasai 17/151 (5577) [25] Ahmad 11/153 (5117) [26] Abu Daawud 10/96 (3189). [27] Abu Daawud 10/244 (3291), ATtirmidhy 6/498 (1747), Ibn Maajah 9/369 (3180).
|
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi Zifuatazo ni aina tofauti za kusafisha najasa na kutoharisha kutegemea na aina ya najasa yenyewe, mahali ilipo na mahitajio yake.
1. KUSAFISHA KWA MAJI.Ikiwa najasa iko katika mwili, nguo au vyombo, basi unasafisha kwa maji sehemu ile mpaka athari yake iondoke.
2. KUFUTA.Ikiwa najasa iko juu ya kioo au kisu au sehemu ambayo inaonekana na inaweza kufutika na athari yake kuondoka basi unaifuta. Kwa mwanamke anaye vaa nguo ndefu yenye kuburuza chini na anapita akitembea huku na kule, basi ile nguo inajitoharisha kila anapotembea ikiwa athari ya najasa haitobakia. Kasema Jabir Bin Zaid R.A.A kuhusu mwanamke aliemuulizia Bibi Umm Salama R.A.A.H. hukumu ya nguo yake ambayo ilikuwa ikiburuta chini, alimuulizia kwa Mtume S.A.W. akasema, "Mimi nguo yangu ni ndefu na ninaiburuta chini wakati nikitembea na napita kwenye uchafu". Akajibu Mtume S.A.W[1].," يُطَهِّرُهُ مَا بَعْدَهُ. Maana yake, "Ina toharisha baada yake." (Kila unavyozidi kutembea uchafu ule unafutwa na ardhi, na ardhi ni tahiri).
3. KUFUNGA JELA. (KUZUIA ZIZINI).Hali hii hasa ni kwa wanyama ikiwa wamekula vitu ambayo ni haramu basi asichinjwe na wala maziwa yake yasinywewe mpaka ule uchafu utoke katika mwili wake, hakuna muda maalum wa kufunga jela au kumzuia yule mnyama zizini kwake, isipokuwa mpaka aende haja baada ya kupewa chakula kingine. Wanavyuoni wanasema ili aweze kutoharika na uchafu huo ndege anafungwa mchana na usiku mmoja, mbuzi anafungwa siku tatu, na ngamia na ng`ombe wanafungwa siku saba.
4. KUTEMBEA.Ikiwa mtu kakanyaga uchafu basi kila anapotembea ule uchafu unakuwa unatoka na kitendo hicho cha kutembea kinakuwa kinasafisha sehemu ile iliyopata uchafu. Kasema Abu Huraira R.A.A., “Kasema Mtume S.A.W[2].," إِذَا وَطِئَ أَحَدُكُمْ بِنَعْلِهِ الْأَذَى فَإِنَّ التُّرَابَ لَهُ طَهُورٌ. Maana yake, "Akikanyaga mmoja wenu kwa viatu vyake uchafu basi udongo ni tohara (utavitoharisha)."
5. VITU VYA ASILI.Vitu vya asili kama udongo, jua, moto, mvua, upepo vina toharisha uchafu uliyokaa juu ya ardhi, uchafu ulio juu ya mimea au udongo na vinginevyo kama hivyo. Wakati pia unaweza kutoharisha ikiwa athari ya najasa itatoweka katika vitu vile.
6. KUITENGENEZA NGOZI.Ngozi ya mnyama ikitengenezwa inakuwa tahir isipokuwa ngozi ya nguruwe na mbwa. Kasema Ibn Abbaas R.A.A, "Kasema Mtume S.A.W[3].," أَيُّمَا إِهَابٍ دُبِغَ فَقَدْ طَهُرَ. Maana yake, "Na kila ngozi itakayotengenezwa imetoharika." Pia kasema Bibi Aisha R.A.A.H.,[4] “ أَمَرَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنْ يُنْتَفَعَ بِجِلْدِ الْمَيْتَةِ إِذَا دُبِغَ. Maana yake, “Ameamrisha Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. kunufaika kwa ngozi ya kibudu (myama aliyejifia) ikitengezwa.”
UKUMBUSHO MUHIMU. Uisilamu kama vile ulivyotilia nguvu na hima kuutoharisha, mwili, chakula, na pahala, pia imetilia nguvu sana kuitoharisha nafsi kutokana na maradhi au uchafu usioonekana ambao unaweza kusababisha madhara makubwa na kuleta chokochoko, ugomvi, chuki, mtafarakano na kadhalika, na kusasabisha kuondoa utulivu na amani kwa mtu na kwa jamii. Mfano wa maradhi haya hatari ambayo anatakiwa kila mtu ajitoharishe nayo ni kama vile: kiburi, jeuri, nifak[5], hasad[6], wivu na mambo yote yanayofanana na haya. Yote haya yamekemewa na kukatazwa kwa nguvu katika Uisilamu. Mfano wa maradhi haya hatari ni kama haya yafiutayo chini: Nifaki. Hadithi iliyotolewa na Abu Huraira R.A.A. kasema, "Kasema Mtume S.A.W.[7]," مِنْ شَرِّ النَّاسِ ذُو الْوَجْهَيْنِ الَّذِي يَأْتِي هَؤُلَاءِ بِوَجْهٍ وَهَؤُلَاءِ بِوَجْهٍ Maana yake, "Katika shari ya watu (watu wabaya) wenye nyuso mbili ambao akienda kwa huyu anakuwa na uso tofauti na akienda kwa huyu anakuwa na uso tofauti." Hasad. Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Al-Nisaai aya ya 54," ﴿أم يَحسُدُونَ النَّاس عَلى مآ آتاهُمُ الله مِن فَضلِهِ﴾. Maana yake, "Au wanawafanyia watu husuda kwa yale aliyowapa Mwenyezi Mungu kwa ukarimu wake.?". Pia hadithi ya Abu Huraira kasema, "Kasema Mtume S.A.W, [8]," إِيَّاكُمْ وَالْحَسَدَ فَإِنَّ الْحَسَدَ يَأْكُلُ الْحَسَنَاتِ كَمَا تَأْكُلُ النَّارُ الْحَطَبَ. Maana, "Jiepusheni na husuda kwani husuda inakula thawabu kama vile moto unavyokula kuni."
7. USAFI WA CHAKULA.Chakula kinajenga mwili na pia kinasaidia kujenga tabia ya mwanaadamu. Kula chakula bora na kisafi ni kitu ambacho kimetiliwa nguvu sana katika Uislamu. Ubora na usafi uliokusudiwa katika chakula ni uhalali wake yaani chakula kile machumo yake ni ya halali, na wala hakikuchanganyika na yale yaliyo haramishwa. Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Al-Baqara aya ya 168," ﴿يـَأَيُّهَا النَّاسُ كُلُوا مِمَّا فِى الأَرضِ حَلَـلاً طَيِّباً﴾. Maana yake, "Enyi watu kuleni vilivyomo katika ardhi halali na vizuri." Pia kasema katika Surat Al-Baqara aya ya 172," ﴿يَـأَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُلُوا مِن طَيِّبَاتِ مَا رَزَقناَكُم﴾. Maana yake, "Enyi Mlioamini. Kuleni vizuri tulivyo kuruzukuni”
8. USAFI WA MAVAZI.Usafi wa mavazi ni jambo ambalo pia limetiliwa nguvu sana katika Uislamu, makusudio sio nguo za fahari, lakini nguo zilizopatikana kihalali, nadhifu, zinazositiri stara ya kisheria, na hazikunajisika na chochote kile. Kasema Mola Mtukufu katika Surat Al Muddathir aya ya 4," ﴿وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ﴾. Maana yake, "Na nguo zako uzisafishe."
9. USAFI WA VYOMBO.Iwapo vyombo vichafu vitatumiwa athari ya ule uchafu utaingia katika chakula, na kuathiri afya ya atakaye kula chakula kile. Mtume S.A.W. alisisitiza kuviosha vizuri vyombo vilivyo nuswa na mbwa. Kasema Abu Huraira R.A.A., "Kasema Mtume S.A.W[9].," إِذَا وَلَغَ الْكَلْبُ فِي إِنَاءِ أَحَدِكُمْ فَلْيَغْسِلْهُ سَبْعَ مَرَّاتٍ. Maana yake, "Akiramba mbwa ndani ya chombo cha mmoja wenu basi akioshe mara saba”.
[1] Al Rabi`u1/69 (150). Mfano wa Hadithi hii pia imetolewa na Abu Daawud 1/486 (326), Ibn Maajah 2/152 (524), ATtirimidhy 1/244 (133), Baihaqy 2/406 (3905), Ahmad 53/445 (25283), Ddaaramy 1/206 (742). [2] Abu Daawud 1/489 (328). [3] Al Rabi`u 1/154 (389), ANnaasai 13/164 (4168), Ibn Maajah 10/487 (3599), Muslim 2/283 (547) Ahmad 4/329 (1797). [4] Al Rabi`u 1/154 (390), wahadithiaji wengine wafuatao wametaja ikiwa ngozi itatengenezwa basi imetoharika Abu Daawud 11/166 (3594), Ibn Maajah 10/476 (3599), A`Ttirmidhiy 6/338 (1650), An-Nassai`y 13/164 (4168), Muslim 2/283 (547), Ahamd 3/382 (1895). [5] Udanganyifu wa vitendo na maneno kwa kudihirisha jambo tofauti na jinsi ilivyokusudiwa. [6] Tabia ya kumuonea mtu kijicho, yaani mtazamo mbaya juu ya mtu na anavyomiliki ili aharibikiwe, au ile neema imuondokee. [7] Abu Daawud 13/15 (4229), Bukhaari 18/497 (5598), Muslim13/6 (4714), Ahmad 21/67 (10023). [8] Abu Daawud 13/56 (4257), Ibn Maajah 4200. [9] Al Rabi`u 1/71 (155) , Bukhaari 1/298 (168), Muslim 2/120 (419). |