Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi  Maji ya asili ni maji yale yaliyo katika hali yake ya kawaida ya asili, hayakuingiliwa na kitu, na wala hayakubadilika rangi na au wala ladha yake. Maji haya ni tahiri na yanafaa kwa kujitilia udhu na kujitoharishia. Kama ifuatavyo:
1.1 Maji ya mvua. Maji ya mvua, na barafu inayoanguka kutoka mawinguni na baridi yenye umaji umaji ni tahiri masafi. Kasema Mola Mtukufu katika Surat Al-Furqan aya ya 48, ,"
وَأَنزَلنَا مِنَ السَّمَآءِ مَآءً طَهُوراً Maana yake, "Na tunayateremsha kutoka mawinguni maji safi kabisa." Pia katika Surat Al-Anfaal aya ya 11 kasema,"
وَيُنَزِّلُ عَلَيكُم مِّنَ السَّمَآءِ مَآءً لِّيُطَهِّرَكُم بِهِ Maana yake, "Na akakuteremshieni maji mawinguni ili kukutahirisheni."
1.2. Maji ya bahari.
Maji ya bahari ni tahir na masafi. Kasema Ibn Abbaas R.A.A., “Kasema Mtume S.A.W. [1] ,
“هُوَ الطَّهُورُ مَاؤُهُ الْحِلُّ مَيْتَتُهُ.
Maana yake, "Nayo Maji yake ni tahir na maiti zake ni halali."
1.3 Maji yanayo tembea.
Maji yale yanayo tembea kama vile maji ya mito au ya mifereji ya asili (falaj), na pia siku hizi mabomba ya maji ikiwa yamebakia katika hali yake ya kawaida hayo yote pia ni tahiri na masafi.
1.4 Maji ya kisima.
Maji ya kisima au maji yaliyotulia yaliyo chini ya magudulia mawili ikiwa kama yamebakia katika hali yake ya asili, bila yakuingiliwa na kitu kinachoweza kuyanajisisha au kuyabadilisha rangi na au ladha yake, au yakiwa zaidi ya magudulia mawili yenye ujazo wa karibu lita 200 mpaka 216 na ni tahiri na masafi hata kama yamebadilika rangi na au ladha yake.
1.5 Maji mengi.
Maji yoyote ya kadiri ya ujazo wa qullatain[2] (magudulia mawili) hayanajisiki isipokuwa yakibadilika rangi au ladha au harufu yake. Kasema Jabir bin Zaid, “Kasema Mtume S.A.W.[3],"
إِذَا كَانَ الْمَاءُ قدرقُلَّتَيْنِ لَمْ يَحْتمِلِ خَبثا.
Maana yake, "Ikiwa maji kadiri ya qullatain[4] (magudulia mawili) hayachukui uchafu”.
1.6. Maji ya Zam Zam.
Hakuna dalili yoyote ya kuyakirihisha, au kuyaharamisha kuyatumia kwa ajili ya kujisafishia, au kwa kutawadhia, au kuogea, au kustanjia. Lakini ziko dalili ambazo zina onyesha kutumika kwa kutawadhia na kama hivyo, hivyo basi yanafaa kutawadhia na hata kuogea josho kubwa hapana neno.
Yaliyokatazwa kwa maji yaliyosimama.
Yafuatayo ni baadhi ya yale yaliyo katazwa kufanyiwa maji yaliyo simama kama vile madimbwi, mabwawa na kadhalika:
Mwenye janaba kuoga ndani ya madimbwi.
Mtume S.A.W. kakataza mwenye janaba kuingia na kuoga ndani ya maji yaliyosimama kama vile maji ya mabwawa, madimbwi, na kadhalika. Kasema Ibn Abbaas R.A.A.,[5] "
نَهَى رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ الْجُنُبَ أَنْ يَغْتَسِلَ فِي الْمَاءِ الدَّائِمِ، وَنَهَى عَنِ الْوُضُوءِ بِفَضْلِ الْمَرْأَةِ، وَكَذَلِكَ فِي الرَّجُلِ.
Maana yake, “Amekataza Mjumbe wa Mola S.A.W. mwenye janaba kuoga katika maji yaliosimama na kakataza kutawadha maji yaliyobakizwa na mwanamke na hali kadhalika kwa mwanamume (maji yaliyo bakizwa na mwanamume)”. Kukojolea ndani ya maji yaliyosimama. Mtume S.A.W. kakataza kukojolea ndani ya maji yaliyosimama halafu akaoga au akatawadhia. Kasema Jabir bin Zaid R.A.A., “Kasema Mtume S.A.W.,[6],
"لا يَبُولَنَّ أَحَدُكُمْ فِي الْمَاءِ الدَّائِمِ ثُمَّ يَغْتَسِلُ مِنْهُأو يتوضا.
Maana yake, "Asikojolee mtu katika maji yaliyo simama halafu akaoga au akatawadha."[7]
Kuingiza mkono ndani ya chombo chenye maji ya kutawadhia kabla ya kuuosha.
Mtume S.A.W. kakataza kwa aliyetoka usingizini kuingiza mkono wake kabla hajausafisha ndani ya maji ya kutawadhia. Kutoka kwa Abu Huraira R.A.A. kasema, "Kasema Mtume S.A.W, [8]"
إِذَا اسْتَيْقَظَ أَحَدُكُمْ مِنْ نَوْمِهِ فَلا يَغْمِسْ يَدَهُ فِي الإنَاءِ حَتَّى يَغْسِلَهَا ثَلاثًا فَإِنَّهُ لا يَدْرِي أَيْنَ بَاتَتْ يَدُهُ.
Maana yake, "Akiamka mmoja wenu kutoka usingizini kwake asiingize mkono wake katika chombo (cha maji) mpaka aukoshe mara tatu, kwani hajui wapi mkono wake ulilala ."
-----------------------------------------------------------------------------------------
[1]Al Rabi`u 1/72 (161). Mfano wa Hadithi hii imetolewa pia na Abu Daawud 1/118 (76), Ibn Maajah 1/467 (380), Ddaraqtuny 1/34 (4), Ahmad 17/422 (8380), ATtirmidhy 1/118 (64)
[2] Qulattain ni kipimo kilicho kuwa kikitumiwa awali. Kwa sasa ujazo wake wa maji ni karibu na lita 200 mpaka lita 216.
[3] Al Rabi`u 1/71 (157). Mfano wa hadith hii pia imetolewa na Ahmad Hambal 2/28 (4961), Abu Daawud 1/92 (58,59), Naasai 1/97 (52), 2/36 (326), Ibn Maajah 2/134 (510, 511) Ddaaramy 13/1 (1), Baihaqy 1/55 (200).
[4] Katika maelezo yaliyotolewa katika Sunan A`Ttirimidhiy. Abdah kasema kutoka kwa Muhamad bin Ishaq kuwa Qullah ni mfano wa Jirar nacho ni kitu cha kuhifadhia maji ya kunywa. As-Shaffi`i na Ahmad na Ishaq wamesema ujazo wake ni karibu na viriba 50 vya maji.
[5] Al Rabi`u 1/45 (144). Mfano wa Hadithi hii pia imetolewa na Abu Daawud 1/115 (74), An-Nassai`y 2/60 (341) na Masheikh wengineo kwa maneno tofauti na wao wametaja tu maji yaliyobakizwa, hawakutaja mwenye janaba.
[6] Al Rabi`u 1/72 (162). Mfano wa hadithi hii pia imetolewa bila kutaja kutawadha na Bukhaari 1/398 (232), Muslim 2/126 (424), Abu Daawud 1/100 (62), Ahmad Hanbal 2/259 (7517) wao hawakutaja kutawadha, Nnasaai 1/104 (57.
[7] Kukojolea katika maji yaliyosimama kunasababisha uchafu ule kubakia katika yale maji, na ikiwa yamebadilika harufu au rangi au ladha yake basi yatakuwa yamenajisika, na hayafai kwa kujitoharishia.
[8] Al Rabi`u 1/53 (87). Mfano wa Hadith hii pia umetolewa na A`Ttirmidhy 1/44 (24), Muslim 2/117(417) |