Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi
Allah mtukufu amewapa Wanaume nafasi ya kuchaguwa wale waliopendeza kwao katika wanawake waumini, basi amesema: ﴿فَٱنكِحُواْ مَا طَابَ لَكُمْ مّنَ ٱلنّسَاء مَثْنَىٰ وَثُلَـٰثَ وَرُبَاعَ فَإِنْ خِفْتُمْ أَلاَّ تَعْدِلُواْ فَوٰحِدَةً أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَـٰنُكُمْ ذٰلِكَ أَدْنَىٰ أَلاَّ تَعُولُواْ﴾ ﴾Basi oweni wale waliopendeza kwenu katika wanawake, wawili, na watatu, na wanne([1]), na mukiogopa ya kuwa hamutofanya uadilifu basi mmoja anatosha, au yule aliyemilikiwa na mikono yenu ya kiume (mjakazi), hayo ndio uchache ili musije mukapata uzito﴿ [Nisaa 04/03] Muislamu wa kike au wa kiume haruhusiwi kufunga ndoa na asiyekuwa muislamu mpaka aamini dini ya kiislamu, amesema Allah mtukufu: ﴿وَلاَ تَنْكِحُواْ ٱلْمُشْرِكَـٰتِ حَتَّىٰ يُؤْمِنَّ وَلامَةٌ مُّؤْمِنَةٌ خَيْرٌ مّن مُّشْرِكَةٍ وَلَوْ أَعْجَبَتْكُمْ وَلاَ تُنكِحُواْ ٱلْمُشِرِكِينَ حَتَّىٰ يُؤْمِنُواْ وَلَعَبْدٌ مُّؤْمِنٌ خَيْرٌ مّن مُّشْرِكٍ وَلَوْ أَعْجَبَكُمْ أُوْلَـئِكَ يَدْعُونَ إِلَى ٱلنَّارِ وَٱللَّهُ يَدْعُواْ إِلَى ٱلْجَنَّةِ وَٱلْمَغْفِرَةِ بِإِذْنِهِ وَيُبَيِنُ آيَـٰتِهِ لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَتَذَكَّرُونَ﴾ ﴾Na musiwaowe washirikina mpaka waamini, na mjakazi muumini ni bora kuliko mshirikina hata kama atakupendezeni. Na musiwaozeshe washirikina mpaka waamini, na mtumwa muumini ni bora kuliko mshirikina hata kama atakupendezeni; hao wanaita katika moto, na Allah anaita katika Pepo na Usamehevu kwa idhini yake. Na anabainisha aya zake kwa watu ili wao wakumbuke﴿ [Baqarah 02/221]. Lakini inaruhusiwa kwa wanaume wa Kiislamu kuwaowa wanawake wa Ahli l-kitabu (Mayahudi na Wakiristo) wale waliojihifadhi vizuri, na kwa kuheshimu usimamizi wa mume katika nyumba, na ruhusa hiyo inazingatiwa pale watakapokuwa Waislamu ndio watawala katika nchi, na serikali inazingatia kuwa Uislamu ndio dini yake, kwa sababu lengo la ndoa sio kupitisha matamanio tu, bali na kuhifadhi kizazi vile vile, amesema Allah mtukufu: ﴿ٱلْيَوْمَ أُحِلَّ لَكُمُ ٱلطَّيّبَـٰتُ وَطَعَامُ ٱلَّذِينَ أُوتُواْ ٱلْكِتَـٰبَ حِلٌّ لَّكُمْ وَطَعَامُكُمْ حِلٌّ لَّهُمْ وَٱلْمُحْصَنَـٰتُ مِنَ ٱلْمُؤْمِنَـٰتِ وَٱلْمُحْصَنَـٰتُ مِنَ ٱلَّذِينَ أُوتُواْ ٱلْكِتَـٰبَ مِن قَبْلِكُمْ إِذَا ءاتَيْتُمُوهُنَّ أُجُورَهُنَّ مُحْصِنِينَ غَيْرَ مُسَافِحِينَ وَلاَ مُتَّخِذِى أَخْدَانٍ وَمَن يَكْفُرْ بِٱلإيمَـٰنِ فَقَدْ حَبِطَ عَمَلُهُ وَهُوَ فِى ٱلاْخِرَةِ مِنَ ٱلْخَـٰسِرِينَ﴾ ﴾Leo yamehalalishwa kwenu yaliyo mazuri. Na chakula cha waliopewa kitabu (mayahudi na wakiristo) ni halali kwenu, na chakula chenu ni halali kwao, na wanawake waliojihifadhi vizuri katika waumini, na wanawake waliojihifadhi vizuri katika waliopewa kitabu kabla yenu (mayahudi na wakiristo) ikiwa mutawapa mahari zao na hali mumejihifadhi vizuri, sio kwa njia ya uzinifu wala kwa urafiki wa kinyumba, na atakayeikufuru Imani basi hakika zimeporomoka amali zake, na yeye katika Akhera ni katika waliokhasirika﴿ [Maidah 05/05]. Mwanamke pia halazimishwi kufunga ndoa na mwanamme asiyemtaka, imepokewa kuwa alikuja Binti kwa Mjumbe wa Allah (s.a.w) na akasema: "Hakika baba yangu amenifungisha ndoa na mtoto wa ndugu yake ili anyanyue kwa hilo udhaifu wake". Basi Mtume wa Allah (s.a.w) akampa huyo bint khiyari yake katika hilo. Hapo huyo Binti akasema: "Nimelipitisha alilolifanya baba yangu, lakini nimetaka wanawake wajue ya kuwa Mababa hawana chochote katika hili (yaani katika kulazimisha ndoa bila ya ridhaa ya mwanamke)" [Ibnu maajah 1874]. Basi hakuna ndoa mpaka yapatikane haya yafuatayo: 1. Maridhio matatu: 1) Maridhio ya mwanamme anayetaka kuowa. 2) Maridhio ya mwanamke anayetaka kuolewa. 3) Maridhio ya Walii([2]) wa mwanamke anayetaka kuolewa. Amesema Mtume wa Allah (s.a.w) ((Mjane ana haki zaidi ya nafsi yake kuliko walii wake, na bikra anatakiwa idhini katika nafsi yake, na idhini yake ni kunyamaza kwake)) na amesema (s.a.w) vilevile: ((na hakuna ndoa isipokuwa kwa Walii na Mahari na Ushahidi)) [Rabii 511]. 2. Mahari: nacho ni kiwango maalumu cha mali kinachobainishwa kwa makubaliano kuwa ni sadaka ya mwanamke, na mahari haina kiwango maalumu, nayo ni haki ya mwanamke anayeolewa, amesema Allah mtukufu: ﴿وَءاتُواْ ٱلنّسَاء صَدُقَـٰتِهِنَّ نِحْلَةً فَإِن طِبْنَ لَكُمْ عَن شَىْء مّنْهُ نَفْساً فَكُلُوهُ هَنِيئاً مَّرِيئاً﴾ ﴾Na wapeni wanawake mahari zao, ni tunzo, basi wakiwa safi kwa kuwapa nyinyi chochote humo -kwa nafsi zao- kuleni kwa uzuri na usafi﴿ [Nisaa 04/04] 3. Fungo la ndoa: Fungo hilo ni lazima lishuhudiwe na wanaume waislamu wasiopungua wawili, amesema Mtume Muhammad (s.a.w): ((Hakuna doa isipokuwa kwa Walii, na Mahari, na Ushahidi)) [Rabii 510]. [1]. Hii <na> hapa sio <na> ya kuchanganya, basi usije ukafahamu kuwa inaruhusiwa kuowa wake tisa, lakini <na> hii ni <na> ya kuwa nao hao wake, yaani unaweza ukawa na wawili au watatu au wanne, na hayo yanafahamika kwa vielelezo vilivyomo katika matamshi ya Qur-ani, basi ulijuwe hili vizuri. [2]. Walii ni msimamiaji wa mwanamke katika familia kwa upande wa Baba, na huyo ni Baba, ikiwa hayupo ni Babu, ikiwa hayupo ni Ndugu, ikiwa hayupo ni mwana, ikiwa hayupo ni mtoto wa ndugu, ikiwa hayupo ni Ami, ikiwa hayupo ni mtoto wa Ami, ikiwa hayupo ni mashauriano ya waislamu. |
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi
Mume hana ruhusa kumuingilia mke wake akiwa katika Hedhi na Nifasi([1]) mpaka atoharike kwa kumaliza kwake damu hizo na kukoga, wala hakuna tatizo katika kupitisha matamanio yake katika sehemu yoyote ya mwili wa mke wake, kwani uharamu ni kumwingilia tu, ni sawa kumwingilia huko ni katika sehemu hiyo ya damu chafu, au katika sehemu ya nyuma, yote ni haramu, amesema Allah mtukufu: ﴿ وَيَسْـئَلُونَكَ عَنِ ٱلْمَحِيضِ قُلْ هُوَ أَذًى فَٱعْتَزِلُواْ ٱلنّسَاء فِي ٱلْمَحِيضِ وَلاَ تَقْرَبُوهُنَّ حَتَّىٰ يَطْهُرْنَ فَإِذَا تَطَهَّرْنَ فَأْتُوهُنَّ مِنْ حَيْثُ أَمَرَكُمُ ٱللَّهُ إِنَّ ٱللَّهَ يُحِبُّ ٱلتَّوبِينَ وَيُحِبُّ ٱلْمُتَطَهّرِينَ﴾ ﴾Na wanakuuliza kuhusu hedhi, sema hiyo ni maudhi, basi waepukeni wanawake wakati wa hedhi, na musiwakaribie mpaka watoharike, basi wakisha toharika waendeeni kama vile alivyokuamrisheni Allah, hakika Allah anawapenda wenye kutubia, na anawapenda wanaojisafisha﴿ [Baqarah 02/222]. Basi ameruhusu Allah mtukufu kumwingilia mke akiwemo katika tohara yake kwa namna yoyote ile anayoipenda mume, lililokuwa muhimu kilimo kiwe katika shamba tu, na mke amridhie mume wake katika hilo kadiri anavyoweza, ikiwa jihadi ya mwanamme ni katika vita vya maadui na katika kutimiza mahitaji ya nyumbani, basi jihadi ya mwanamke ipo katika kumridhisha mume wake, na kila wanavyoridhiana basi thawabu za Allah pia huwa nyingi, na mapenzi huongezeka, amesema Allah mtukufu: ﴿نِسَاؤُكُمْ حَرْثٌ لَّكُمْ فَأْتُواْ حَرْثَكُمْ أَنَّىٰ شِئْتُمْ وَقَدّمُواْ لاِنفُسِكُمْ وَٱتَّقُواْ ٱللَّهَ وَٱعْلَمُواْ أَنَّكُم مُّلَـٰقُوهُ وَبَشّرِ ٱلْمُؤْمِنِينَ﴾ ﴾Wake zenu ni konde (sehemu ya kuweka mbegu za mazao) zenu, basi ziendeeni konde zenu namna([2]) munavyopenda, na mutangulize kwa ajili ya nafsi zenu, na mcheni Allah, na mujuwe kuwa nyinyi ni wenye kukutana naye, na wabashirie Waumini﴿ [Baqarah 02/223]. Na kama mke hakutimiza haki ya kitandani kwa aliyokuwa anao uwezo nayo basi anapata makasiriko ya Allah mtukufu, amesema Mtume wa Allah (s.a.w): ((إِذَا دَعَا الرَّجُلُ امْرَأَتَهُ إِلَى فِرَاشِهِ فَأَبَتْ أَنْ تَجِيْءَ لَعَنَتْهَا الْمَلاَئِكَةُ حَتَّى تُصْبِحَ)) ((Atakapoitwa mwanamke na mume wake katika kitanda chake, basi akakataa kuja, atalaaniwa na Malaika mpaka kutapambazuka)) [Bukhari 5193] Na mwanamke asije akamtii mume wake katika kumuasi Allah mtukufu, kwani hakuna kumtii kiumbe katika kumuasi Muumba, alikuja mwanamke kwa Mtume wa Allah (s.a.w) na akasema: "Hakika mume wangu ameniamrisha kuunganisha nywele zangu"([3]). Akasema Mtume (s.a.w): ((Hapana, hakika wamelaaniwa wanawake wenye kuunganisha nywele zao)) [Rejea, Bukhari 5205] [1]. Hedhi ni damu inayokuja kwa mwanamke katika kipindi cha mwezi uchache wake ni siku tatu na wingi wake ni siku kumi, na nifasi ni damu inayokuja baada ya kuzaa uchache wake ni siku tano na wingi wake ni siku arubaini 40. [2]. Tahadhari sana, kuna wajanja wanaifasiri sehemu hii kwa neno <<popote munapopenda>> kwa lengo la kumuingilia mwanamke katika sehemu ya haja kubwa (nyuma), basi tafsiri yake ni <<namna munayopenda>> kwa maana ya hali yoyote ile, na Allah mtukufu amewalaani kwa Ulimi wa Mtume wake (s.a.w) wale wanaowaingilia wanawake katika sehemu ya chuma. [3]. Amesema Mtume (s.a.w): ((Amewalaani Allah: Mwenye kuchonga nyusi na mwenye kuwachonga wenzake, mwenye kuunganisha nywele na mwenye kuunganisha wenzake nywele, mwenye kupiga chapa katika mwili na mwenye kuwapiga wenzake chapa katika mwili, na wenye kuchonga meno kwa ajili ya uzuri)) [Rabii 637]. |
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi
Wataishi mume na mke kwa wema na mapenzi, na kuchunga heshima baina yao, na kizazi chao, kila mmoja atimize haki za lazima kwa mwengine, na Allah mtukufu amejaalia kuwa mwanamme ndie mwenye kushika amri ya nyumba, na iwapo mke atakuwa ni mzito wa kutimiza haki kwa mume wake katika anayoyaweza, na akawa ni mzito wa kuchunga heshima ya nyumba, basi mume atapita kwa mujibu wa hatua za utaratibu wa Sheria ya Allah mtukufu kama alivyoongozwa na Allah mtukufu katika neno lake: ﴿ ٱلرّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى ٱلنّسَاء بِمَا فَضَّلَ ٱللَّهُ بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ وَبِمَا أَنفَقُواْ مِنْ أَمْوٰلِهِمْ فَٱلصَّـٰلِحَـٰتُ قَـٰنِتَـٰتٌ حَـفِظَـٰتٌ لّلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ ٱللَّهُ وَٱللَّـٰتِى تَخَافُونَ نُشُوزَهُنَّ فَعِظُوهُنَّ وَٱهْجُرُوهُنَّ فِى ٱلْمَضَاجِعِ وَٱضْرِبُوهُنَّ فَإِنْ أَطَعْنَكُمْ فَلاَ تَبْغُواْ عَلَيْهِنَّ سَبِيلاً إِنَّ ٱللَّهَ كَانَ عَلِيّاً كَبِيراً﴾ ﴾Wanaume ndio wasimamizi juu ya wanawake, kwa vile alivyofadhilisha Allah baadhi yenu juu ya wengine, na kwa yale waliyoyatowa katika mali zao, basi wanawake wema ni wale walio wanyenyekevu, wanye kuhifadhi kwa siri kwa yale aliyoyahifadhi Allah. Na wanawake ambao munaogopa kuacha utiifu wao basi wapeni mawaidha hao, na muwahame hao katika malazi, na wapigeni([1]) hao, basi wakiwa watiifu kwenu musije mukawapa njia. Hakika Allah amekuwa ni mwenye kuheshimika aliye mkuu﴿ [Nisaa 04/34]. Ikiwa kwa njia hizo tatu za mwanzo haikuwezekana mwanamke kunyooka, basi hapo itakuwa ni kutaka usuluhisho baina yao kwa wema, na usuluhisho huo utatimizwa kwa njia ya waamuzi wawili, muamuzi kutoka upande wa mume na mwengine kutoka kwa upande wa mke, amesema Allah mtukufu: ﴿ وَإِنْ خِفْتُمْ شِقَاقَ بَيْنِهِمَا فَٱبْعَثُواْ حَكَماً مّنْ أَهْلِهِ وَحَكَماً مّنْ أَهْلِهَا إِن يُرِيدَا إِصْلَـٰحاً يُوَفّقِ ٱللَّهُ بَيْنَهُمَا إِنَّ ٱللَّهَ كَانَ عَلِيماً خَبِيراً﴾ ﴾Na ikiwa mutaogopa mafarakano baina yao wawili, basi pelekeni muamuzi kutoka katika jamaa wa mume na muamuzi kutoka katika jamaa wa mke, wakitaka hao (waamuzi) wawili mapatano atawezesha Allah baina yao. Hakika Allah ndie mjuzi mwenye khabari ya yote﴿ [Nisaa 04/35]. Na mwanamke akifikiwa na matatizo kutoka kwa mume wake, basi sheria imampa na yeye njia yake, nayo ni njia ya kufanya suluhu, na hakuna tatizo kuyafikisha kwa wazee wake ili wayasimamie kwa watakayoelewana, amesema Allah mtukufu: ﴿وَإِنِ ٱمْرَأَةٌ خَـٰفَتْ مِن بَعْلِهَا نُشُوزاً أَوْ إِعْرَاضاً فَلاَ جُنَاْحَ عَلَيْهِمَا أَن يُصْلِحَا بَيْنَهُمَا صُلْحاً وَٱلصُّلْحُ خَيْرٌ وَأُحْضِرَتِ ٱلأنفُسُ ٱلشُّحَّ وَإِن تُحْسِنُواْ وَتَتَّقُواْ فَإِنَّ ٱللَّهَ كَانَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيراً﴾ ﴾Na mwanamke akichelea kutupwa au au kutojaliwa (na mumewe), basi hakuna tatizo juu yao wakisikilizana kwa suluhu. Na suluhu ni bora. Na nafsi zimewekewa (kuwa na) choyo. Na mukifanya wema na mukamcha mungu basi hakika Allah kwa munayoyafanya ni mwenye kuyajua vizuri sana﴿ [Nisaa 04/128] [1]. Pigo hili sio pigo la kuumiza, lakini ni pigo la kuonyesha kutoridhika na yeye, na kumrejesha mke katika njia sahihi ya kumtii mume wake katika wema na kumtimizia haki zake, na Mtume wa Allah (s.a.w) amekataza kuwapiga wanawake pigo la kuwaumiza na kuwajeruhi, na amekataza kuwapiga katika Uso na sehemu zao za hatari kupigwa, kama vile matiti. |
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi
Amesema Allah mtukufu: ﴿وَإِن يَتَفَرَّقَا يُغْنِ ٱللَّهُ كُلاًّ مّن سَعَتِهِ وَكَانَ ٱللَّهُ وٰسِعاً حَكِيماً﴾ ﴾Na kama wakitengana atamtosheleza Allah kila mmoja wao kwa ukunjufu wake, amekuwa Allah ni mkunjufu mwingi wa hekima﴿ [Nisaa 04/130] Sababu za kumalizika ndoa: 1. IILAAI: Iilaai ni maneno yanayomaanisha mume kujizuia kukutana na mke wake, ikiwa kwa njia ya kuapa au nadhiri, au talaka, anayatumia mume kumaanisha ya kuwa hatamgusa mke wake, na sana sana iilaai inakuwa kwa njia ya kiapo, au kuitundika talaka. Basi mume ikiwa atajizuwia kumuingilia mke wake kwa njia hiyo ya iilaai, hapo amekuwa amefanya makosa ya kuzuwia haki ya mke, na Sheria inampa huyo mume muda wa miezi minne([1]). Basi huyo Bwana aliyefanya iilaai akitimiza muda huo wa miezi minne bila ya kumuingilia mke wake hapo atakuwa huyo mke ameachika, na itahesabiwa kuwa ni talaka, wala hakuna eda kwake, isipokuwa kama atakuwa ni mja mzito, basi yeye atamaliza ujauzito wake tu. Na kama iilaai ilikuwa kwa kiapo basi italazimika kwa huyo mume kafara ya kiapo, na Kafara hiyo ni kuwalisha masikini kumi chakula cha wastani, au kuwavisha, au kugomboa mtumwa, na ikiwa atashindwa na hayo basi atafunga siku tatu([2]), amesema Allah mtukufu: ﴿ لّلَّذِينَ يُؤْلُونَ مِن نّسَائِهِمْ تَرَبُّصُ أَرْبَعَةِ أَشْهُرٍ فَإِن فَآءوا فَإِنَّ ٱللَّهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴾ ﴾Kwa wanaoapa kuwa watajitenga na wake zao, ni kusubiria miezi minne, basi wakireja hakika Allah ni mwingi wa kusamehe mwingi wa kurehemu﴿ [Baqarah 02/226]
2. TALAKA NA KHULUGH: Ikiwa haiwezekani tena maisha baina ya mume na mke kwa sababu yoyote ile ya kilazima([3]), basi Allah mtukufu amempa mume haki ya talaka, yaani kumuacha mke wake, na amempa mke haki ya khulugh, yaani kujivua na ndoa ile, amesema Allah mtukufu: ﴿ٱلطَّلَـٰقُ مَرَّتَانِ فَإِمْسَاكٌ بِمَعْرُوفٍ أَوْ تَسْرِيحٌ بِإِحْسَـٰنٍ وَلاَ يَحِلُّ لَكُمْ أَن تَأْخُذُواْ مِمَّا ءاتَيْتُمُوهُنَّ شَيْئًا إِلاَّ أَن يَخَافَا أَلاَّ يُقِيمَا حُدُودَ ٱللَّهِ فَإِنْ خِفْتُمْ أَلاَّ يُقِيمَا حُدُودَ ٱللَّهِ فَلاَ جُنَاحَ عَلَيْهِمَا فِيمَا ٱفْتَدَتْ بِهِ تِلْكَ حُدُودُ ٱللَّهِ فَلاَ تَعْتَدُوهَا وَمَن يَتَعَدَّ حُدُودَ ٱللَّهِ فَأُوْلَـئِكَ هُمُ ٱلظَّـٰلِمُونَ﴾ ﴾Talaka (ya kuweza kumrejea mke) ni mara mbili, basi ni kushika kwa vizuri au kuacha kwa wema, na sio halali kwenu kuchukua katika muliyowapa (wake zenu) chochote kile, isipokuwa ikiwa watakhofia (mume na mke) kuwa hawatasimamisha mipaka ya Allah, na ikiwa mutakhofia ya kuwa hawatasimamisha mipaka ya Allah basi hakuna tatizo juu yao (mume na mke) katika atakayojifidia (mke) kwayo, hiyo ni mipaka ya Allah, na mwenye kuichupa mipaka ya Allah basi hao ndio Madhalimu﴿ [Baqarah 02/229]. Basi mume atatoa talaka kwa mke wake ikiwa ameshindwa kubakia naye, na mke atajifidia kwa kiwango kisichozidi mahari yake aliyoolewa kwayo ili ajivue na ndoa iliyomshinda kwa mume wake huyo, na hapa inadhihiri hekima na barka ya mahari ndogo. [1]. Miezi minne ndio muda wa mke kuweza kumsubiria mume wake bila ya kumuingilia, na kwa hivyo mume afanye kila njia aweze kukutana na mke wake katika kipindi kisichozidi hapo, isipokuwa kama wataridhiana wenyewe, hapo tena hakuna tatizo. [2]. Amesema Allah mtukufu: ﴿لاَ يُؤَاخِذُكُمُ ٱللَّهُ بِٱللَّغْوِ فِى أَيْمَـٰنِكُمْ وَلَـٰكِن يُؤَاخِذُكُم بِمَا عَقَّدتُّمُ ٱلاْيْمَـٰنَ فَكَفَّارَتُهُ إِطْعَامُ عَشَرَةِ مَسَـٰكِينَ مِنْ أَوْسَطِ مَا تُطْعِمُونَ أَهْلِيكُمْ أَوْ كِسْوَتُهُمْ أَوْ تَحْرِيرُ رَقَبَةٍ فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ ثَلَـٰثَةِ أَيَّامٍ ذٰلِكَ كَفَّارَةُ أَيْمَـٰنِكُمْ إِذَا حَلَفْتُمْ وَٱحْفَظُواْ أَيْمَـٰنَكُمْ كَذٰلِكَ يُبَيّنُ ٱللَّهُ لَكُمْ ءايَـٰتِهِ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ﴾ ﴾Hatakushekeni Allah kwa viapo vyenu vya upuuzi, lakini anakushekeni kwa munayoyafungia kweli viapo, basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa chakula cha wastani munachowalisha watu wenu, au kuwavisha, au kumkomboa mtumwa. Basi asiyepata ni kufunga siku tatu, hiyo ndio kafara ya viapo vyenu mutakapoapa, na hifadhini viapo vyenu, namna hiyo anabainisha Allah kwenu aya zake ili muwe wenye kushukuru﴿ [Maaidah 07/89] [3]. Amesema Mtume wa Allah (s.a.w): ((Hayuko pamoja na sisi mwenye kumchukiza mwanamke kwa mume wake, au mtumwa kwa Bwana wake)) [Al-hakim 2849]. Na amesema (s.a.w): ((Mwanamke yoyote atakayeomba talaka kwa mume wake bila ya sababu (inayokubalika kisheria) basi Allah atamuharamishia kunusa harufu ya Pepo)) [Al-hakim 2863]. |
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi
Mwanamke aliyeolewa ikiwa ataachwa kabla ya kukutana na mume wake kwa tendo la ndoa basi mwanamke huyo hana eda kwa mume huyo([1]), na Bwana huyo hawezi kumrejea huyo mwanamke isipokuwa kwa ndoa nyengine iliyo mpya, na mwanamke huyo atakuwa na haki ya kupata nusu ya mahari tu, amesema Allah mtukufu: ﴿ يٰأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءامَنُواْ إِذَا نَكَحْتُمُ ٱلْمُؤْمِنَـٰتِ ثُمَّ طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ فَمَا لَكُمْ عَلَيْهِنَّ مِنْ عِدَّةٍ تَعْتَدُّونَهَا فَمَتّعُوهُنَّ وَسَرّحُوهُنَّ سَرَاحاً جَمِيلاً﴾ ﴾Enyi mulioamini mutakapowaowa waumini wa kike kisha mukawapa talaka kabla ya kuwagusa (kuwaingilia) basi hamuna nyinyi haki juu yao ya eda ya kuwahesabia, basi waliwazeni (kwa kuwapa kifunga nyumba chao) na muwaache maacho mazuri﴿ [Ah-zaab 33/49]. Na amesema vile vile: ﴿وَإِن طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ وَقَدْ فَرَضْتُمْ لَهُنَّ فَرِيضَةً فَنِصْفُ مَا فَرَضْتُمْ إَّلا أَن يَعْفُونَ أَوْ يَعْفُوَاْ ٱلَّذِى بِيَدِهِ عُقْدَةُ ٱلنّكَاحِ وَأَن تَعْفُواْ أَقْرَبُ لِلتَّقْوَىٰ وَلاَ تَنسَوُاْ ٱلْفَضْلَ بَيْنَكُمْ إِنَّ ٱللَّهَ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ﴾ ﴾Na mutakapowapa talaka kabla ya kuwagusa (kwa kuwaingilia) na hali mumeshawakatia mahari, basi ni nusu ya mulichowakatia, isipokuwa kama watasamehe (wanawake) au akasamehe yule ambae amemiliki fungo la ndoa (mume), na kama mutasamehe (nyinyi waume), basi ni ukaribu zaidi wa Uchamungu, na musisahau wema baina yenu. Hakika Allah kwa munayoyafanya ni mwenye kuwona﴿ [Baqarah 02/237] [1]. Mwanamke aliyeolewa na kabla ya kukutana na mume wake ikiwa atafiliwa na mume wake itamlazimikia eda ya kufiliwa, nayo ni miezi minne na siku kumi. |
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi
Mume akiacha mke wake talaka tatu hatoweza tena kumrejea mpaka aolewe na mume mwengine, kisha waonjane asali zao, tena baada ya hapo ikiwa atatengana naye huyo mwengine kwa njia miongoni mwa njia za haki bila ya kuwepo ujanja kati yake([1]), hapo ndio ataweza kurejeana tena na yule mume wake wa mwanzo, amesema Allah mtukufu: ﴿فَإِن طَلَّقَهَا فَلاَ تَحِلُّ لَهُ مِن بَعْدُ حَتَّىٰ تَنْكِحَ زَوْجًا غَيْرَهُ فَإِن طَلَّقَهَا فَلاَ جُنَاحَ عَلَيْهِمَا أَن يَتَرَاجَعَا إِن ظَنَّا أَن يُقِيمَا حُدُودَ ٱللَّهِ وَتِلْكَ حُدُودُ ٱللَّهِ يُبَيّنُهَا لِقَوْمٍ يَعْلَمُونَ﴾ ﴾Ikiwa atamuacha (baada ya talaka mbili) basi hatokuwa halali kwake baada ya hapo mpaka aowane na mume mwengine, ikiwa atamuacha (huyo mume mwengine) basi hakuna tatizo juu yao kurejeana ikiwa watadhani ya kuwa watasimamisha mipaka ya Allah, na hiyo ni mipaka ya Allah anaibainisha kwa watu wanaojuwa﴿ [Baqarah 02/230]. Na yamepokewa kuwa Aisha bint Abdirahman Nadhariyah alikuwa ameolewa na mtoto wa Ami yake Rifaah bin Wahab, basi alimuacha talaka tatu, kisha yule mwanamke akaolewa na Abdurahman bin Zubair kisha akamuacha, basi akaenda huyo mwanamke kwa Mtume wa Allah (s.a.w) na akasema: "Hakika yeye ameshaniacha kabla ya kunigusa (yaani hakumuingilia), hivi naweza kurejea kwa Mtoto wa ami yangu mume wangu wa mwanzo?" Akasema (s.a.w): ((Hapana)), yaani mpaka aolewe na mume na waonjane asali zao. [Rejea Fat-hu l-bari, Sherhe ya hadithi no. 5317]. [1]. Imepokewa kuwa Mtume (s.a.w) alisema: ((Hivi nikuambieni kuhusu beberu la kuazima?)). Wakasema: "Ndio. Ewe Mjumbe wa Allah!". Akasema: ((Huyo ni yule mwenye kuhalalisha. Amelaaniwa na Allah mwenye hukahalalisha na mwenye kuhalalishiwa)) [Ibn maajah 1936] |
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi
Ikiwa mume atamtuhumu mke wake kwa kosa la uzinifu, au kwa kukataa mtoto([1]), na hali hana mashahidi wanaokubalika katika hilo, basi italazimika kulaaniana na mke wake iwapo mwanamke atakataa kuhusika na kosa hilo. ﴿وَٱلَّذِينَ يَرْمُونَ أَزْوٰجَهُمْ وَلَمْ يَكُنْ لَّهُمْ شُهَدَاء إِلاَّ أَنفُسُهُمْ فَشَهَـٰدَةُ أَحَدِهِمْ أَرْبَعُ شَهَـٰدَاتٍ بِٱللَّهِ إِنَّهُ لَمِنَ ٱلصَّـٰدِقِينَ * وَٱلْخَامِسَةُ أَنَّ لَعْنَةَ ٱللَّهِ عَلَيْهِ إِن كَانَ مِنَ ٱلْكَـٰذِبِينَ * وَيَدْرَؤُاْ عَنْهَا ٱلْعَذَابَ أَن تَشْهَدَ أَرْبَعَ شَهَادَاتٍ بِٱللَّهِ إِنَّهُ لَمِنَ ٱلْكَـٰذِبِينَ * وَٱلْخَامِسَةَ أَنَّ غَضَبَ ٱللَّهِ عَلَيْهَا إِن كَانَ مِنَ ٱلصَّـٰدِقِينَ﴾ ﴾Na wale wanaowalengea (kosa la uzinifu) wake zao, na ikawa hawana mashahidi isipokuwa nafsi zao wenyewe, basi ni kushuhudia mmoja wao kwa mashuhudio manne ya kuapa kwa Allah kuwa yeye ni katika wakweli * na shuhudio la tano ya kuwa laana za Allah ziwe juu yake ikiwa yeye ni katika waongo * Na itamwondokea (mwanamke) adhabu kwa kushuhudia mashuhudio manne ya kuapa kwa Allah kuwa huyo (mume wake) ni katika waongo * na shuhudio la tano ya kuwa Makasiriko ya Allah yawe juu yake (huyo mke) ikiwa yeye (mume) ni katika wakweli﴿ [Nuur 24/06-09] Wakilaaniana mume na mke basi ndoa inavunjika baina yao, na haihesabiwi kuwa ni talaka, na ndoa haitowakusanya tena baina yao milele, hayo ni kwa sababu ya yale yaliyothibiti kuwa Mtume (s.a.w) alimtenganisha mume aliyemtupia mke wake kosa la uzinifu, basi baada ya kulaaniana baina yao, kama alivyoamrisha Allah mtukufu; Mtume (s.a.w) akasema: "إِنَّهُمَا لاَ يَجْتَمِعَانِ أَبَداً" "Hakika hao wawili hawatokutana tena milele (yaani kindoa)” [Rejea: Rabii 606, Muslim 1492: 2, 3, Bukhari 5306, 5311] [1]. Imekuja kuwa Mtume wa Allah (s.a.w) amesema: ((Mwanamke yoyote atakayeingiza katika watu asiyekuwemo katika wao, basi hana kitu kwa Allah, na hatoingizwa na Allah katika pepo, na mwanamme yoyote akimkataa mtoto wake na yeye anamuona, basi Allah atamfungia rehma zake, na atamfedhehesha juu ya vichwa vya viumbe kuwanzia wa mwanzo mpaka wa mwisho)) [Al-hakim 2868], Na mwanamke kuingiza katika watu asiyekuwemo yaani amechukuwa mimba kwa uzinifu na hali anaye mume, basi akaingizia katika familia ya bwana wake asiyekuwa wake, na mwanamme anayekataa mtoto wake, yaani ameowa mke wake kisha akamzalia mtoto, na huyo Bwana akakataa huyo mtoto, na hali hana yakini kuwa mtoto sio wake. |
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi
Iwapo Allah amechukua maisha ya mume na hali mke yumo katika fungo la ndoa, au yumo katika talaka ya kurejewa([1]), basi italazimika kwa huyo mke kukaa eda ya kufiliwa, nayo ni Miezi minne na siku kumi, na atapata haki yake ya mirathi katika mali ya mumewe, amesema Allah mtukufu: ﴿ وَٱلَّذِينَ يُتَوَفَّوْنَ مِنكُمْ وَيَذَرُونَ أَزْوٰجًا يَتَرَبَّصْنَ بِأَنفُسِهِنَّ أَرْبَعَةَ أَشْهُرٍ وَعَشْرًا فَإِذَا بَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَلاَ جُنَاحَ عَلَيْكُمْ فِيمَا فَعَلْنَ فِى أَنفُسِهِنَّ بِٱلْمَعْرُوفِ وَٱللَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ﴾ ﴾Na wale waliofishwa katika nyinyi na wakaacha wake, basi watasubiria (hao wake zao) kwa nafsi zao miezi minne na siku kumi, basi wakishatimiza muda wao hakuna tatizo juu yenu katika watakayoyafanya katika nafsi zao kwa wema, na Allah kwa munayoyafanya ni mwenye kuyajuwa vizuri sana﴿ [Baqara 02/234]. Ama mwanamke mwenye mimba ikiwa atafiliwa na mume wake ajue kuwa kuna kauli mbili katika eda yake: 1. Itamalizika eda kwa kuzaa mimba yake tu hata kama atazaa baada ya saa, na hii ndio inayotegemewa sana na Jamuhuri ya umma, na ndio aliyoipa nguvu Msitahiwa Mufti Sheikh Wetu Ahmed bin Hamed Al-khalili, Allah amuhifadhi. 2. Itamlazimikia mwanamke kukaa eda yenye muda mrefu zaidi katika hizo mbili, na hii ndio iliyochukuliwa na Wengi wa wanavyuoni wetu wa Ahli l-haqi wa l-isqaamah Allah awaridhie na kuwarehemu. Zingatia: Kuna mambo mengi ya uzushi yanaingizwa katika eda ya kufiliwa, na kwa uhakika mwanamke aliyefiliwa na mume wake hayalazimiki juu yake sipokuwa mambo matatu tu, nayo ni: 1. Kujizuwia na manukato (vitu vyenye harufu nzuri kama udi, marashi, na maloshani, na baadhi ya aina za sabuni kama vile lux,,) 2. Kujizuwia na kujipamba na kujipodowa. 3. Kujizuwia na kulala katika nyumba isiyokuwa nyumba ya kukalia eda yake tu. Basi ni hayo matatu tu, na yaliyobakia yeye na wanawake wengine ni sawa katika sheria ya Allah mtukufu, isipokuwa ndoa na kuchumbiwa, hayo mpaka imalizike eda kama ilivyo kwa wanawake wote walioachwa na waume zao na hali wao katika eda. [1]. Ikiwa mume yumo katika maradhi ya kudhaniwa kifo, kisha atamuacha mke wake talaka tatu -kwa sababu mke alieachwa talaka tatu hana mirathi-, lakini hapa ikiwa huyu Bwana atakufa katika maradhi yake hayo basi mke atapata fungu lake kamili, kwa sababu huyo Bwana alikusudia kumdhuru huyo mwanamke kwa kumkosesha fungu lake, na kama hakufa basi talaka zimeshapita hawezi tena kumrejea. |
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi
Huu ni uwanja wa Msitahiwa Sheikh Wetu Ahmed bin Hamed Al-khalili -Allah amuhifadhi na atupe faida katika elimu yake- katika kujibu baadhi ya masuali: Suali: Pana tofauti gani baina ya eda ya kufiliwa na eda ya talaka katika mapambo na manukato na matumizi na malazi([1])? Jawabu: 1. Ama eda ya kufiliwa, mwanamke anakuwa hana matumizi ndani yake, isipokuwa ikiwa ni mja mzito katika mtazamo wa baadhi ya wanaelimu, lakini yeye atapata makazi kwa mujibu wa pale alipofikiwa na habari za kifo cha mumewe, na italazimika juu yake kulala hapo hapo, na italazimika juu yake kuacha mapambo na manukato (vitu vyenye harufu nzuri kama marashi udi ,,,). 2. Ama hukusu eda ya talaka ikiwa ni talaka ya kurejewa basi atapata matumizi na makazi, na anaamrishwa kujitia manukato na kujipamba ili kumvutia mume wake katika kumrejea, na hatakiwi kutoka katika nyumba isipokuwa kwa haja zake, wala haifai kwa mume kumtoa mkewe. 3. Na ikiwa sio talaka ya kurejewa -na hiyo ni kwa talaka ya tatu- basi katika hali hii hapati matumizi wala makazi, na yeye ana khiyari katika mambo ya manukato na mapambo ikiwa hakuwa pamoja na aliyemuacha, na anayo ruhusa ya kutoka wakati wowote akitaka. Na Allah anajuwa zaidi. [Al-khalili - Fatwa Nikaahi 373]
Suali: Nini hukumu ya Uislamu kuhusu Mzinifu ambae limethibiti kwake kosa la uzinifu -Allah atuepushie- kwa kuwa yeye alizini na mwanamke bikra na akazaa naye mtoto kwa njia ya haramu, jee inafaa kwake kuowana na mwanamke aliyejihifadhi? Na jee inafaa kwa Binti huyo mzinifu kuowana na mwanamme wenye kujihifadhi? Na ipi hukumu ya Uislamu yakitokezea hayo bila ya kuuliza wanaelimu? Jee! kuna kosa? Na ipi hukumu ya watoto? Jee! Watakuwa ni ndugu na mtoto aliyezaliwa kwa njia ya uzinifu? Jawabu: Inafaa kwa kila mmoja katika hao kuowana na mwenye sifa ya kujihifadhi ikiwa hajui yaliyotokea, na vilevile ikiwa watatubia kwa Allah mtukufu na wakawa ni wenye kujihifadhi, na wajisitiri kwa sitara ya Allah, basi wasijifedheheshe mbele ya watu kwa machafu yao, na mtoto wa uzinifu hawi mtoto wa Mzinifu wa kiume wa kisheria, basi hakuna usimamizi kwake, wala kwa huyo mtoto, wala hakuna kurithiana baina yao, na hayo ni kwa neno la Nabii (s.a.w): ((Mtoto ni wa mwenye kitanda, na mzinifu lake ni jiwe)), na kutokana na hapo hakuna undugu baina yake na watoto wa huyo aliyezini aliowapata kisheria, wala hakuna chochote kati yao katika hukumu za undugu isipokuwa uharamu wa kuowana tu. Na Allah anajuwa zaidi. [Al-khalili - Fatwa Nikaahi 156-157]
Suali: Msitahiwa Sheikh: Hakika alinighururi mchumba wangu, na akaingia Shetani baina yetu, na yakawa hayo yaliyokuwa, kwani alinisikuma msukumo mkubwa katika Uzinifu, juu ya kuwa mimi nililichukia sana hilo, na nilijaribu kushindana naye kwa kila nilivyoweza lakini sikufanikiwa, basi vipi uhalali wa uchumba huu?, jee! sheria inalazimisha kwa huyu kijana kuowana na mimi? Jawabu: Amesema Mtume wa Allah (s.a.w): ((Hatokaa mwanamme na mwanamke peke yao isipokuwa shetani atakuwa wa tatu wao)) na kwenda kinyume na amri ya Mtume wa Allah (s.a.w) hakupeleki isipokuwa katika mahuzuniko, na nani mwenye dhamana ya kutoripuka vikikutana moto na mafuta, na Ndoa ni fungo tukufu halifikiwi na chochote kichafu, kwani hilo ni makutano ya kiroho kabla ya kuwa makutano ya kimwili, kutokana na hapo ikawa katika masharti yake iwe imejengwa katika usafi na kujihifadhi, sio katika uchafu na maovu, kwa hakika Allah mtukufu amesema: ﴾Na katika ishara zake ni kuumba kwa ajili yenu kutokana na nafsi zenu wake, ili mupate utulivu kwao, na amejaalia baina yenu mapenzi na rehema; hakika katika hilo kuna ishara za wazi kwa watu wanaofikiri﴿ [Ruum 30/21], na utulivu hapa ni utulivu wa moyo na kufarijika kwake, jee! Utatulizana moyo wa mume kwa mke baada ya kuwa kila mmoja kati yao ameshamjaribu mwenzake kwa nafsi yake, kutokana na hayo wamesema jamaa katika Masahaba (r.a): "Mwanamume yoyote akizini na mwanamke kisha akamuowa, basi hao ni wenye kuzini milele" na hili ndio wanalolifanyia kazi As-habu wetu([2]) -Allah awarehemu- bila ya kutofautiana, basi ukate tamaa na kuowana na huyo, na tubia kwa Allah na umtake msamaha kwa dhambi yako, na Allah atakupatia mwengine aliye mwema, na uhadhari kuingia katika makosa hayo, basi itakuwa vipi mwisho wa kondoo aliyejiweka mbele ya mbwa mwitu isipokuwa kuvamiwa tu, na Allah ndie wa kutegemewa. [1]. Matumizi na malazi au makazi katika kipindi cha eda hukumu yake inazingatiwa kwa upande wa mume, ikisemwa kuwa hana haki ya hayo yaani kutoka kwa mume, na katika hali hiyo hayo asiyokua na haki nayo yanarejea kwa mawalii wake. [2]. Inafaa kutaja kuwa Mheshimiwa Mufti hapa anakusudia kuwa huu ndio msimamo wa Ahli l-haqi wa l-istiqamah, ambao wanajulikana kwa jina la Ibadhi, na wao wanahusika na misimamo madhubiti sana ya kiislamu inayotofautiana na misimamo mengine, na hapana budi kuiweka wazi kwa ufupi nayo ni: 1). Kumuabudu Allah mtukufu bila ya kufananisha, na kujua kuwa Allah mtukufu hana Sifa ya kutegemea, basi hana sifa ya kuonekana Duniani na Akhera [42/11], [06/102-103]. 2). Kuitakidi kuwa hakuna Sifa ya Imani kwa mwenye kumuasi Allah na Mtume wake (s.a.w) kwa kosa kubwa lolote mpaka atubie kwa Mola wake [10/33] [24/47] [33/36]. 3). Kuitakidi kuwa mwenye kufa hali ya kuwa yanamlazimu makosa Makubwa bila ya Kutubia kwa Allah mtukufu, huyo ameangamia katika Makasiriko ya kudumu [04/18]. 4). Kuitakidi kuwa hakuna kutoka wala kumalizika katika Adhabu ya Moto [82/15-16] [72/23]. 5). Kuitakidi kuwa hakuna Uombezi wa Mtume (s.a.w) wala wa Mja yoyote kwa waliokufa bila ya Kutubia kwa Madhambi yao makubwa [40/18] [09/96]. 6). Kuitakidi kuwa mwenye kukubaliwa matendo yake mema zimekuwa mzito mizani zake, na mwenye kumlazimu maovu yake zimekuwa nyepesi mizani zake wala hayakubaliwi matendo yake, kwani Allah anakubali ya Wachamungu, na yeye haridhii Mafasiki [05/27] [09/96] [07/08-09]. 7). Hakuna ndoa milele baina ya Muislamu wa kike au wa kiume na aliyeonjana naye kwa njia ya Uzinifu [24/03] [04/24] [05/05]. 8). Kumpenda Muumini kwa ajili ya Allah mtukufu kwa sababu ya Kutii kwake, na kujitenga na kila Fasiki -kwa ajili ya Allah mtukufu- kwa sababu ya Kuasi kwake [05/55] [09/114]. |