Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi
Kuhiji kuna namna tatu, nazo:
1- Tamat-tu': Nayo ni kuhirimia umra peke yake katika miezi ya hija, akimaliza atatokana na ihramu ya ibada hiyo, kisha atahirimia hija siku ya Tarwiya (8 Dhul-hija) au kabla yake. Tamat-tu' ndio namna bora ya kuhiji, na inashurutiziwa iwe umra na hija katika mwaka mmoja, safari moja na asirejee nchini kwake au mfano wake kwa umbali baina ya ibada mbili hizo.
Mfanya-tamat-tu' humwajibikia kichinjo cha Tamat-tu'.
2- Qiraanu: Nayo ni kuhirimia hija pamoja na umra katika miezi ya hija kisha kubaki na ihramu mpaka atakapotokana na ihramu ya ibada mbili hizo kwa pamoja siku ya kuchinja (10 Dhul-hija).
Mfanya-Qiraanu huwajibika pia kuchinja. Yeye inamtosheleza Tawafu moja na Sa'yi moja kwa hija na umra yake, kutokana na kauli yake - rehma za Allah na amani zimshukie: “Mwenye kuhirimia hija pamoja na umra itamtosha Tawafu moja na Sa'yi moja kwa zote mbili mpaka ajihalalishe nazo pamoja.” Ameipokea a'Tirmidhi na Ibnu Maajah. Na kuna kauli kuwa lazima kuwe na Tawafu mbili na Sa'yi mbili.
Mwenye kufanya hija ya Qiraanu akiingia Maka atatufu Tawaful-Quduumi[1], na anaweza kufanya Sa'yi kabisa akitaka, halafu atakaporejea siku ya kufanya Tawafu ya Ifadha akatoshelezeka kwa Tawafu tu; kwasababu ameshafanya Sa'yi hapo kabla kwa uoni wa baadhi ya wanazuoni.[2] Na kuna kauli aakhirishe Sa'yi apate kuifanya pamoja na Tawafu ya Ifadha.
3- Ifraadu: Nayo ni kuhirimia hija peke yake na kubaki na ihramu mpaka utakapolirushia vijiwe Jamratul-Aqaba siku ya kuchinja (10 Dhul-hija), kisha baada ya hapo unatahalal (yaani unatokana na ihramu).
MAZINGATIO
Mfanya-Ifraadu haimlazimu umra anapofanya hija pekee. Akitaka kufanya umra ni baada ya siku za Tashriiq (ambazo ni 11 – 13 Dhul-hija).
Inajuzu kuhirimia hija pekee hata kwa ambaye hakufanya umra hapo kabla.
Mfanya-Ifraadu inamjuzia kutufu Tawaful-Quduumi bila kufanya Sa'yi, na kwa kauli nyengine anaweza kufanya na Sa'yi ya hija kabisa.[3]
Mfanya-Ifraadu na Mfanya-Qiraanu wakiwa hawajasai baina ya Safa na Marwa walipotufu Tawaful-Quduumi itawalazimu wafanye Sa'yi watakapotufu Tawaful-Ifadha kwa mawafikiano ya wote.
[1]- Tawaful-Quduumi ni tawafu iliyosuniwa kwa mwenye kuingia Makka akiwa amehirimia hija ya Qiraanu au ya Ifraadu; ama anayekwenda Mina au Arafa moja kwa moja bila kuingia Makka hakusuniwa kufanya Tawaful-Quduumi. Kuna kauli kuwa tawafu anayotufu kabla ya kwenda Mina mwenye kuchanganya hija na umra (Qiraanu) ni tawafu ya umra na humtosheleza badala ya Tawaful-Quduumi. Pia mwenye kufanya umra kabla ya hija (yaani Tamattu'), inamtosheleza tawafu ya umra badala ya Tawaful-Quduumi - yaani hakusuniwa kufanya Tawaful-Quduumi mbali na tawafu ya umra.(Mfasiri)
[2]- Kuruhusiwa mwenye hija ya Qiraanu au ya Ifraadu aliyetufu Tawaful-Quduumi kufanya Sa'yi kabisa ndiyo sahihi kwa Sheikh wetu Al-Allaama Said Al-Qannuubi; bali kasema ndiyo bora kwa kuwa ndivo alivofanya Mtume wa Allah –rehma za Allah na amani zimshukie. Kwani yeye –rehma za Allah na amani zimshukie- alifanya hija ya Qiraanu (hakuweza kufanya Tamattu' kwasababu alikuwa amekwenda na wanyama wa kuchinja), na hakufanya Sa'yi baada ya Tawafu ya Ifadha kwa kuwa aliitanguliza Sa'yi baada ya Tawaful-Quduumi, na ndivo pia walivofanya masahaba kwa idhini yake kati ya waliohirimia hija ya Qiraanu na waliohirimia hija ya Ifraadu.(Rejea Sualu Ahli 'Dhikri, kipindi cha tarekhe 6 Dhul-qa'da 1425AH / 19-12-2004CE, jawabu ya suali la tano). Hivyo, Sa'yi anayoifanya mwenye hija ya Qiraanu baada ya Tawaful-Quduumi inamtosheleza kwa umra na hija yake, pia Tawafu ya Ifadha inamtosheleza kwa hija na umra yake na kwa hiyo hatafanya Sa'yi baada ya Tawafu ya Ifadha. Halikadhalika mwenye hija ya Ifraadu iwapo atatanguliza Sa'yi ya hija yake baada ya Tawaful-Quduumi hatafanya Sa'yi baada ya Tawafu ya Ifadha. Hili bila shaka linawapa watu wepesi mkubwa hususan katika zama hizi kutokana na zahma iliyozidi ya mahujaji wakati wa Tawafu ya Ifadha.(Mfasiri) [3]- Angalia maelezo ya chini nam. 2 yaliyotangulia.(Mfasiri)
|
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi § Inapendelewa ajinadhifishe kwa kuondoa msokotano wa nywele, kunyoa nywele za siri, kukata kucha, kunyonyoa kwapa, kupunguza sharubu na kuondoa manukato, kwa ambaye bado hajafanya hayo. § Inapendelewa kuoga na kutawadha kabla kuhirimia kwa kila anayekusudia kuhirimia hata mwenye hedhi au nifasi.[1] § Mwanamme avue nguo zilizoshonwa na za kujivika[2] na avae kikoi, shuka ya kujifunika mabegani na viatu vya ndara; kutokana na kauli yake - rehma za Allah na amani zimshukie: “Na ahirimie kila mmoja wenu katika kikoi, shuka na viatu vya ndara.” Ameipokea Ahmed. § Ama mwanamke, kuhirimia kwake ni usoni; haimjuzii kufunika uso wake ila akiogopa kushawishi wanaume atauteremshia uso wake nguo kutoka kichwani. Yeye anaruhusiwa kuvaa nguo iliyoshonwa, lakini aepuke kila ambayo ina mapambo, na anakatazwa kuvaa glavu, kama ilivyokuja kwenye hadithi: “Mwanamke mwenye kuhirimia asijifunge nikabu wala asivae glavu.” Imepokewa na al-Bukhari na wengineo. § Asali rakaa mbili za ihramu kwa kauli ya baadhi ya wanazuoni baada ya kuoga. Iwapo umefika wakati wa sala ya fardhi basi bora ahirimie baada ya sala hii na atamke talbia baada yake moja kwa moja. Na kuna kauli atamke talbia akishapanda kipando cha safari yake. § Anuie ibada anayokusudia (hija au umra) kama ilivyotangulia katika mlango wa namna za kuhiji na afanye talbia kwa kuainisha namna ya kuhiji anayokusudia. Aseme katika talbia: [لَبَّيْكَ اللَّهُمَّ لَبَّيْكَ، لَبَّيْكَ لاَ شَرِيكَ لَكَ لَبَّيْكَ، إِنَّ الْحَمْدَ وَالنِّعْمَةَ لَكَ وَالْمُلْكَ، لاَ شَرِيكَ لَكَ] (Labbayka-LLahumma labbayk. Labbayka laa shariika laka labbayk. Innal-hamda, wan-ni'mata laka wal mulk. Laa shariika lak) (Yaani: Nakuitika tena na tena ewe Allah. Nakuitika tena na tena, huna mshirika, nakuitika tena na tena. Hakika shukrani na neema ni Zako pamoja na ufalme; huna mshirika) Akishakuwa juu ya kipando chake atanyanyua sauti kwa talbia. § Atakithirisha kutamka talbia hususan zinapobadilika hali na nyakati, k.m. akipanda kilima au akiteremka bonde na wakati wa kupanda kipando na wa kushuka, na kila baada ya sala; kwani talbia inaushughulisha wakati kwa kumdhukuru Mwenyezi Mungu. Imepokewa kwa Sahlu bin Saad kuwa Mtume - rehma za Allah na amani zimshukie - amesema: “Hatamki talbia Muislamu ye yote ila vitatamka naye talbia viliopo kuliani na kushotoni kwake vikiwa mawe au miti au udongo mpaka mwisho wa ardhi kwa upande huu na upande huu.” Imepokewa na Ibnu Majah, al-Baihaqi, a'Tirmidhi na al-Haakim akaisahihisha. § Akifika Masjidul-Haram ataacha talbia na kuanza ibada ya umra. MAZINGATIO § Bora ahirimie katika nguo nyeupe ingawa hazikatazwi nyenginezo, kutokana na kauli ya Mtume –rehma za Allah na amani zimshukie: "Zishikeni hizi nguo nyeupe; wavikeni walio hai kati yenu na wakafinieni maiti zenu, kwani hizi ndiyo bora kati ya nguo zenu…". Kaipokea Imam a'Rabii' bin Habib. § Mwenye kusafiri kwa ndege atahirimia kabla hajafika kwenye miiqati ili asiivuke miiqati ila amehirimia, na hapana ubaya kwake akitamka talbia baada ya kuondoka na ndege. § Inamjuzia muhrimu (yaani aliye katika ihramu) kuoga na kubadili nguo za ihramu alizovaa kwa nguo nyingine za ihramu akiepuka yaliyozuiwa katika ihram. § Kuhirimia na kuvaa ihramu hakumlazimu mwenye kuingia Makka kama hajakusudia kufanya umra au hija. § Hakuna nia ya matamshi inayomlazimu mwenye kuhiji au mwenye kufanya umra anapohirimia, lakini inamlazimu kufanya talbia kwa kutamka na sio kwa kuileta moyoni. § Muhrimu inamharamikia kujitia manukato akiwa katika ihramu. § Akishahirimia, muhrimu haruhu-siwi kuondoa vinavyo kamata taka mwilini: kama kunyoa nywele, kukata kucha, kunyonyoa kwapa, kunyoa nywele za siri na nyinginezo, isipokuwa kwa dharura ya ugonjwa n.k.[3] § Ni haramu kwa muhrimu maingiliano ya kijinsia baina mume na mke na kushikana kwa matamanio k.m. kulala pamoja katika nguo moja, kubusiana n.k. § Muhrimu hafungi ndoa wala hafungishi ndoa kutokana na kauli yake - rehma za Allah na amani zimshukie: “Muhrimu hafungi ndoa wala hafungishi ndoa wala haposi.” Imepokewa na a'Rabi'u na Muslim. § Ni haramu kwa muhrimu kuwinda kiwindo cha nchi-kavu kutokana na kauli Yake Aliyetukuka: )وَحُرِّمَ عَلَيْكُمْ صَيْدُ الْبَرِّ مَا دُمْتُمْ حُرُماً( {Na mumeharamishiwa viwindo vya nchi-kavu maadamu mumo kwenye ihramu} [Al-maida 96]. Ama viwindo vya bahari havikatazwi. § Muhrimu mwanamme hafuniki kichwa chake kwa cho chote ila kwa dharura kama matibabu, joto au baridi, ambapo itamwajibikia fidya[4]. § Muhrimu anakatazwa kubishana kunako sababisha ghadhabu, kutokana na kauli Yake Aliyetukuka: )الْحَجُّ أَشْهُرٌ مَّعْلُومَاتٌ فَمَن فَرَضَ فِيهِنَّ الْحَجَّ فَلاَ رَفَثَ وَلاَ فُسُوقَ وَلاَ جِدَالَ فِي الْحَجِّ( {Hija ni miezi maalumu; anayekusudia katika miezi hiyo kufanya hija basi hakuna kusema maneno machafu wala kufanya maasi wala kubishana katika hija} [Albaqarah 197]. § Hakatazwi muhrimu kupiga msuwaki hata kama utakifanya kinywa chake kitoke damu. § Maneno machafu yanapingana na tabia za muislamu, na katika ihramu huwa yanachusha zaidi. § Mwenye kuhirimia hija katika miezi isiyo ya hija ihramu yake hugeuka ya umra, na kuna kauli kwamba hubatilika. § Inamjuzia Muhrimu kuvaa ukanda akiuhitaji kufungia shuka aliyovaa na kuhifadhia pesa zake. § Haikatazwi kuvaa viatu vya ndara vilivoshonwa. § Hakatazwi mwanamke aliyehirimia kuvaa mapambo yake ya madini (dhahabu n.k.) katika ihramu ikimwia shida kuyavua, kwa sharti ayafunike kwani kudhihirisha mapambo kwa wasiokuwa mahramu hakujuzu katika hija wala kwengineko. [1]- Kumekuja katika hilo baadhi ya mapokezi yaliyo nasibishwa na Mtume, na kumekuwa na khilafu katika kuyasahihisha au kuyadhoofisha, isipokuwa yaliyopokewa na Muslim kwa njia ya Bibi Aisha - Mwenyezi Mungu amridhie - amesema: “Alijifungua Asma bint Umais Muhammad bin Abi Bakr penye mti (katika eneo la Dhul-hulaifa), Mtume S.A.W. akamuamuru Abu Bakr amuamuru aoge kisha ahirimie.” Kuna riwaya nyingine imemalizikia kwa Ibnu Umar amesema: "Ni katika sunna mtu aoge akitaka kuhirimia na akitaka kuingia Makka.” Ameisimulia al-Bazzaar na a'Daaraqutniy na a'Tabaraaniy kwenye ‘al-Kabiir’ na al-Haakim akaisahihisha. [2]- Nguo zinazouzunguka mwili au baadhi yake kwa kushonwa au vinginevyo. [3] - Muhrimu atakayefanya kati ya hayo kwa dharura ya ugonjwa n.k. hana budi kufidia ima kwa kufunga siku tatu po pote atakapo, au kulisha maskini sita walioko Makka (au katika al-Haram, kila mmoja milo miwili [na kuna kauli mlo mmoja] au vibaba viwili [sawa na 1.025 kg] vya chakula, kama mchele, ngano, n.k.) au kuchinja mbuzi mmoja au kondoo kuwasadakia maskini walioko Makka (au katika al-Haram). Haya ni ufafanuzi wa Mtume –rehma za Allah na amani zimshukie- wa kauli ya Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala: {وَلَا تَحْلِقُوا رُءُوسَكُمْ حَتَّى يَبْلُغَ الْهَدْيُ مَحِلَّهُ فَمَنْ كَانَ مِنْكُمْ مَرِيضًا أَوْ بِهِ أَذًى مِنْ رَأْسِهِ فَفِدْيَةٌ مِنْ صِيَامٍ أَوْ صَدَقَةٍ أَوْ نُسُكٍ} {Wala msinyoe vichwa vyenu mpaka wanyama wa hadyu wafike machinjoni mwao. Na atakaye kuwa mgonjwa au ana vya kumuudhi kichwani mwake basi afidiye kwa kufunga au kwa kutoa sadaka au kuchinja mnyama} Albaqara: 196 [4] - Nayo ni kama ilivotajwa katika maelezo ya chini yaliyotangulia. |
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi
Ni kuizunguka al-Kaaba kuanzia kwenye Jiwe Jeusi na kumalizia hapo hapo ili utimie mzunguko wa mwanzo, na hurudiwa mara saba pamoja na kutamka “SubhaanaLLah walhamduliLLah, walaa ilaaha illa-LLah waLLahu akbar” na kuomba dua.
VIPI KUTUFU: è Tawafu huanza kwa kulibusu Jiwe Jeusi ikiwezekana; isipowezekana atatosheka na kuligusa au kuliashiria kwa mkono wake pamoja na kutamka “Allahu Akbar” wakati wa kulishika.[1] è Ataanza kutufu na hali ameifanya Nyumba ya Allah iwe kushotoni kwake. è Ataomba dua atakazo wakati wa kutufu na atasoma “Albaaqiyaatu-ssaalihaatu” yaani: سُبْحَانَ اللَّهِ وَالْحَمْدُ لِلَّهِ وَلاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ وَاللَّهُ أَكْبَرُ (Subhaana'Llah walhamduli'Llah, walaa ilaaha illa'Llah wa'Llahu akbar) è Anapokuwa sawa na Pembe ya Yamani ataigusa ikiwezekana na hataiashiria kama hakuweza kuigusa. è Akifika kwenye Jiwe Jeusi mzunguko wa kwanza unakuwa umemaliza, na ataanza mzunguko wa pili kama alivyofanya mwanzo mpaka atimize mizunguko saba.
SUNNA ZA TAWAFU: 1. “Ramal”: Nayo ni kutembea kwa haraka na hatua zinazokaribiana bila kwenda mbio na kuchupa; hili linasuniwa katika mizunguko mitatu ya mwanzo. 2. “Idh-tiba'u”: Nayo ni kupitisha sehemu ya kati ya shuka anayojifunika chini ya bega la kulia kwenye kwapa na kuzitupia ncha zake juu ya bega lake la kushoto, yaani aweke wazi bega lake la kulia. “Idh-tiba'u” huwa katika mizungu-ko yote saba[2]. Tanbihi: “Ramal” na “Idh-tiba'u” haziwi ila katika tawafu ya “al-quduumi” au tawafu ya umra[3]. 3. Rakaa mbili za tawafu: Nazo ni rakaa mbili zinazosaliwa baada ya tawafu nyuma ya Maqamu ya Nabii Ibrahim - amani imshukie - au po pote itapowezekana. Dalili ya hilo ni hadithi ya Ibnu Umar Allah amridhie iliyoko kwa al-Bukhari anasema: Alikuja Mtume - rehma za Allah na amani zimshukie - akaizunguka Nyumba ya Allah mara saba kisha akasali nyuma ya Maqamu rakaa mbili kisha akatoka kwenda kwenye Safa, na Allah Aliyetukuka amesema: ) لَقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ( {Bila shaka katika Mtume wa Allah mmekuwa na kigezo kizuri} [Al-ahzaab 21].
MAZINGATIO ¨ Inajuzu kusali rakaa mbili za tawafu baada ya sala ya alfajiri kabla ya kuchomoza jua na baada ya sala ya alasiri kabla ya kuchwa jua kwa kauli iliyopewa uzito na wenye ilmu, kwasababu hiyo ni sala yenye sababu iwapo atatufu katika nyakati mbili hizi. ¨ Inajuzu kutufu Nyumba Takatifu wakati imamu anahutubu Ijumaa lakini bora kusubiri. ¨ Haijuzu kutufu ndani ya ule ukuta mfupi wa “alhatiim” kwasababu ni sehemu ya Kaaba. ¨ Inajuzu kwa mwenye kuhiji au kufanya umra anapotufu au anaposai kupumzika katika ibada hizo akihitaji hilo. ¨ Haikatazwi kutufu katika nyakati tatu zilizoharamishwa kwani kinachokatazwa ni kusali nyakati hizo. ¨ Mwenye kutufu akawa na shaka katika idadi ya mizunguko aliyozunguka atachukulia idadi iliyo ndogo kati ya idadi mbili anazozifikiria, kisha ataendelea na mizinguko iliyobaki. [1] - Inasuniwa kukabir katika kila mzunguko hata katika mzunguko wa mwisho, na akitamka “BISMILLAHI” kabla yake itakuwa vizuri kwa vile hilo limepokewa kutoka kwa Ibnu Umar – Allah amridhie – kwamba alikuwa anapolishika Jiwe hilo husema: “BISMILLAHI WALLAHU AKBAR”. Ameipokea al-Baihaqi na wameisahihisha jumla ya wenye ilmu. [2] - Hii ndiyo sahihi kwa Al Allaama Al-Qannuubi, ingawa iliyo mashuhuri kwamba idh-tiba'u ni kama ramal huwa katika mizunguko mitatu ya mwanzo tu. Angalia Sualu Ahli 'Dhikri kipindi cha tarekhe 9 Dhul-qa'da 1423AH / 12-1-2003CE, jawabu ya suali la kwanza.(Mfasiri) [3] - Tawafu ya umra ina hukumu ya tawaful-quduumi kwa kuwa ni ya mwazo anapofika Makka.(Mfasiri) |
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi
î Inapendelewa kwa mwenye kuhiji aoge mwili mzima huko Mina kwa nia ya kusimama Arafa. î Mwenye kuhiji ataondoka Mina siku ya tarehe 9 Dhul-hija baada ya kuchomoza jua kuelekea Arafaat huku anatamka takbira na ‘laa ilaaha ila-LLah’ na talbia. î Akifika Arafaat na jua likapindukia (wakati wa adhuhuri) atahudhuria khutba ya imamu kisha atasali adhuhuri na alasiri kwa kujumuisha na kufupisha mwanzoni mwa wakati wa adhuhuri. î Kusimama Arafa ndiyo nguzo kuu ya hija kutokana na kauli yake - rehma za Allah na amani zimshukie: “Hija ni Arafa.” Imepokewa na a'Nasai, a'Tirmidhi na Abu Daud. î Kinachokusudiwa kwa kusimama Arafa ni kuhudhuria sehemu yo yote ya Arafa isipokuwa ndani ya Urana (bonde liliopo upande wa magharibi ya Arafaat) tangu baada ya kupindukia jua (adhuhuri) hadi lizame kwa siku hiyo.
MAZINGATIO · Tohara si sharti katika kusimama Arafa. · Katika sunna ni kujitahidi kwa dua na kumdhukuru Allah baada ya sala ya adhuhuri na alasiri mpaka kutua kwa jua. · Mwenye kuhiji hataondoka Arafaat kuelekea Muzdalafa ila baada ya kuzama kwa jua. Maulama wetu wamekemea sana kuondoka mwenye kuhiji pahala pake kwenda kwingine kwa nia ya ifadha (kuondoka Arafa) kabla ya kuchwa kwa jua na wamekufanya sawa na ifadha japokuwa hajatoka nje ya mipaka ya Arafa ila baada ya jua kuzama. · Wengi wa Maulama wa madhehebu yetu na madhehebu ya Malik wanaona kuwa kuondoka Arafa kabla ya kuchwa jua hubatilisha hija; wengineo wanaona hakubatilishi lakini kunawajibisha kuchinja. · Inapendelewa kwa mwenye kuhiji kuomba dua zilizopokewa na kutamka talbia katika Arafa, kwani kutamka talbia kuna kheri na kwa hiyo haipasi kusitishwa kabla kulipiga jamra siku ya kuchinja (10 Dhul-hija). · Mwenye kudiriki kabla ya kuchwa jua kusimama Arafaat kadiri ya kusoma “Albaaqiyaat Assaalihaat” (SubhaanaLLah walhamduliLLah, walaa ilaaha illa-LLah waLLahu akbar) amewahi hija kwa maafikiano ya wote. Hitilafu ipo kuhusu atakayewahi hayo wakati wa usiku kabla alfajiri ya siku ya kuchinja (10 Dhul-hija); na fatwa inayotolewa kwetu ni kwamba mwenye kuwahi kusimama Arafaat usiku au mchana kisha akasimama Muzdalafa usiku wa kuamkia siku ya kuchinja na akaiwahi sala ya alfajiri hapo Muzdalafa basi huyo ameiwahi hija. · Katika sunna ni kuondoka Arafa kwa utulivu kutokana na kauli yake - rehma za Allah na amani zimshukie - wakati alipoondoka huko: “Enyi watu! Kuwenu watulivu; hakika wema si katika kwenda mbio.” Imepokewa kwa maafikiano. Vilevile imekuja kwenye Musnad ya Imam A'Rabi'u - Allah amridhie - kutoka kwa Abu Ubaida kutoka kwa Jabir bin Zaid amesema: Ameulizwa Usama bin Zaid vipi Mtume wa Mwenyezi Mungu - rehma za Allah na amani zimshukie - alikuwa akienda katika ‘hija ya maagano’ alipoondoka Arafa, akasema: Alikuwa akikazana na akipata nafasi huzidisha kasi ya mwendo.[1] [1] - Sk. Saalimiy amesema katika sherehe ya Musnad hii uk. 233: “Amesema Ibnu AbdilBarri: hamna katika hadithi hii zaidi ya ujuzi wa hali ya mwendo wa kuondokea Arafa kuelekea Muzdalafa. Akasema: nalo ni katika yanayowalazimu viongozi wa hija na walio chini yao kuyafanya kwa ajili ya kuharakia sala, kwasababu magharibi haisaliwi ila pamoja na isha huko Muzdalafa, yaani zijumuishwe maslahi mbili – utulivu wakati wa msongamano na kuharakiza pasipo msongamano kwa ajili ya sala.” |
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi
¨ Kulala Muzdalafa baada kuondoka Arafaat. ¨ Katika sunna ni kuchanganya sala mbili: ya magharibi na isha huko Muzdalafa kutokana na hadithi ya Mtume - rehma za Allah na amani zimshukie: “Kuwa yeye - rehma za Allah na amani zimshukie - alifika Muzdalafa akachanganya magharibi na isha kwa adhana moja na iqama mbili na hakusali cho chote baina yao.”[1] ¨ Muzdalafa yote ni pa kusimama isipokuwa ‘Waadi Muhas-sir’, kutokana na kauli yake - rehma za Allah na amani zimshukie: “Muzdalafa yote ni pa kusimama na msikae kwenye Muhas-sir.” Imepokewa na Ahmad. Muhas-sir ni njia ya maji bina ya Muzdalafa na Mina na ni karibu zaidi na Muzdalafa (ni eneo alipofikwa na adhabu Abraha). ¨ Imeruhusiwa kwa wanawake, watoto na wachungaji kuondoka Muzdalafa usiku baada ya kutua kwa mwezi[2]. ¨ Inapasa kulivuka bonde la Muhas-sir kabla kuchomoza kwa jua ila kwa dharura. ¨ Kuomba dua kwenye ‘Al-mash-ar Al-haraam’ (Muzdalafa) ni wajibu, na inatosheleza dua yo yote au kutamka ‘Laa ilaha illa LLah’ au kuhimidi au kutamka talbia. Akifanya lo lote kati ya hayo wajibu umeshamuondokea.
MAZINGATIO · Walio dhaifu na wenye udhuru wameruhusiwa kuondoka Muzdalafa baada ya nusu ya usiku. · Mwenye kuhiji ajitahidi kufika Muzdalafa hasa pakiwa na zahama; asipowahi kukaa usiku huko kwa sababu hiyo hapana kitu juu yake. · Akikhofia wakati wa sala kumfutu akiwa njiani kuelekea Muzdalafa atasali pahala alipo. |
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi
Atasali alfajiri Muzdalafa wakati wa kiza kisha moja kwa moja baada ya sala ataomba dua na kumdhukuru Mwenyezi Mungu, kisha ataondoka kuelekea Mina. Ataondoka Muzdalafa kabla kuchomoza jua kuelekea Mina.
Akifika mwenye kuhiji Mina ataanza kwa kulipiga Jamra la Aqaba, ambalo linaitwa Al-Jamratu L-kubra (jamra kuu). Kupiga jamra kunakuwa kwa vijiwe vidogo kama punje ya dengu, na huwa kwa vijiwe saba.
VIPI KUPIGA JAMRA:
Jamra la Aqaba hupigwa kutokea ndani ya bonde liliopo hapo kwa kuifanya Maka iwe kushotoni na Mina kuliani, kijiwe kimoja kimoja mpaka vitimie vijiwe saba pamoja na kukabir kwa kila kijiwe. Imepokewa kutoka kwa Jabir: “Kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu - rehma za Allah na amani zimshukie - alikuwa akikabir kwa kila kijiwe.” Imepokewa na Muslim. Wakati wa kulipiga jamra hili huwa baada ya kuchomoza jua siku ya idi hadi kupindukia jua (adhuhuri). Inaruhusiwa kupiga jamra hili hadi kuchwa kwa jua la siku ya idi kwa dharura na kwa wenye udhuru. Mwenye kuhiji atasita kutamka talbia akitupa kijiwe cha kwanza kulipigia jamra la Aqaba, kutokana na hadithi ya Al-fadhlu ibnu Abbaas: “Niliendelea kumsikia - rehma za Allah na amani zimshukie - akitamka talbia mpaka akalipiga Jamra la Aqaba.” Imepokewa na A'Rabi'u.
MAZINGATIO Kupiga Jamra la Aqaba ni siku ya mwanzo ya kuchinja (10 Dhul-hija) kuanzia baada kuchomoza jua na kuendelea, na kupiga jamra zote tatu ni katika siku za Tashriq kuanzia kupindukia kwa jua (adhuhuri) na kuendelea. Haitoshelezi kuvifunga vijiwe kwenye mfuko na kuvirembea bali lazima kila kijiwe kitupwe peke yake. Hakuna ubaya kwa mwenye kuhiji kumwakilisha mtu mwengine ampigie jamra anaposhindwa kufanya hilo mwenyewe. Ni lazima kuhakikisha kuwa vijiwe vinavyorembewa vimelifikia jamra.[1] [1] Si sharti vijiwe vilipige jamra lenyewe; vikiingia kwenye hodhi la jamra inatosheleza; kwani Maulama wanasema nguzo ya jamra haikuwapo mwanzo, bali palikuwapo hodhi baadae ikawekwa na nguzo iwe alama. Rejea 'Sualu Ahli'Dhikri' hasa kipindi cha tarekhe 8 Ramadhan 1424 / 3-11-2003, jawabu ya suali la kwanza.(Mfasiri)
|