Funga (Saumu)

Funga (Saumu) (23)

Children categories

Maana ya Saumu

Maana ya Saumu (3)

View items...
Fadhila za Saumu

Fadhila za Saumu (3)

View items...
Written by

Saumu inahitajia uvumilivu na subira ya hali ya juu. Kwani yule anaefunga anajizuia na kula, kunywa, pamoja na matamanio mengine yote yale ambayo yalikuwa halali kwake, kabla ya saumu yake. Mtume S.A.W. akaifananisha ibada hii ya saumu kuwa ni sawa na nusu ya subira. Hadithi ya Abu Huraira R.A.A. kasema, “Kasema Mtume S.A.W.

لِكُلِّ شَيْءٍ زَكَاةٌ وَزَكَاةُ الْجَسَدِ الصَّوْمُ زَادَ مُحْرِزٌ فِي حَدِيثِهِ وَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ الصِّيَامُ نِصْفُ الصَّبْرِ.

Maana yake, "Kila kitu kina zaka, na zaka ya mwili ni saumu. Na akaongezea Muhriz, “Saumu ni nusu ya subira.” Kwa kule kusubiri kwake aliefunga, basi anapata thawabu zilizo sawa na  thawabu za wale wanao subiri kwa ajili ya kutii amri za  Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na ujira wa mwenye kusubiri ni marudufu usiokuwa na hesabu. Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu kuhusu fadhila za subira katika Surat Azzumar aya ya 10,”

﴿إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرون أجرهم بِغَيرِ حِسَابٍ.

Maana yake, “Na bila shaka wafanyao subira (wakajizuilia na maasia na wakaendelea kufanya mema) watapewa ujira wao pasipo na hisabu.” 

 

[1] Ibn Maajah 5/283 (1735).

Written by

Kila kitendo anachofanya mwanaadamu kwa ajili ya kutarajia fadhila, na malipo kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, kinalipwa na kuzidishiwa thawabu kuanzia mara kumi mpaka kufikia mara mia saba. Thawabu za saumu ni tofauti, na thawabu za vitendo vingine vile anavyofanya mwanaadamu, kwani saumu inalipwa mara nyingi bila hisabu. Hadithi ya Abu Huraira R.A.A kasema, “Kasema Mtume S.A.W

كُلُّ عَمَلِ ابْنِ آدَمَ يُضَاعَفُ الْحَسَنَةُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا إِلَى سَبْعمِائَة ضِعْفٍ قَالَ اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ إِلا الصَّوْمَ فَإِنَّهُ لِي وَأَنَا أَجْزِي بِهِ يَدَعُ شَهْوَتَهُ وَطَعَامَهُ مِنْ أَجْلِي.

Maana yake, "Kila kitendo cha binaadamu kina zidishiwa thawabu mfano wa mara kumi mpaka kufikia mara mia saba ziada. Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: Isipokuwa saumu kwani hiyo ni yangu na mimi nailipa na chakula chake kwa ajili yangu." kwa sababu (mtu) kaacha matamanio yake 

[1] Muslim 6/18 (1945).

Written by

Saumu ni miongoni mwa ibada iliyo na daraja ya juu mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na yenye  fadhila kubwa. Kwa ile daraja yake, na utukufu wake kaifanya ibada hii kuwa ni ya Kwake Peke Yake. Hadithi ya Abu Huraira R.A.A. kasema, “Kasema Mtume S.A.W, “Amesema Mwenyezi Mungu

كُلُّ عَمَلِ ابْنِ آدَمَ لَهُ إِلا الصِّيَامَ فَإِنَّهُ لِي وَأَنَا أَجْزِي بِهِ وَالصِّيَامُ جُنَّةٌ فَإِذَا كَانَ يَوْمُ صَوْمِ أَحَدِكُمْ فَلا يَرْفُثْ يَوْمَئِذٍ وَلا يَسْخَبْ فَإِنْ سَابَّهُ أَحَدٌ أَوْ قَاتَلَهُ فَلْيَقُلْ إِنِّي امْرُؤٌ صَائِمٌ وَالَّذِي نَفْسُ مُحَمَّدٍ بِيَدِهِ لَخُلُوفُ فَمِ الصَّائِمِ أَطْيَبُ عِنْدَ اللَّهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ مِنْ رِيحِ الْمِسْكِ وَللصَّائِمِ فَرْحَتَانِ يَفْرَحُهُمَا إِذَا أَفْطَرَ فَرِحَ بِفِطْرِهِ وَإِذَا لَقِيَ رَبَّهُ فَرِحَ بِصَوْمِهِ.

Maana yake, “Kila kitendo cha mwanaadamu ni chake isipokuwa saumu, hiyo ni Yangu, na Mimi nitamlipa ujira wake (anaefunga). Na saumu ni ngao (kinga). Ikiwa siku ambayo mtu amefunga, basi asiseme maneno machafu, wala asiwe mfidhuli, na wala asifanye vitendo vya kijinga. Na ikiwa mtu atamtukana au atamlaani basi aseme mara mbili, “Mimi Nimefunga”. Na kwa Yule aliemiliki nafsi ya Muhammad, harufu mbaya inayotoka mdomoni mwa aliefunga, ni bora mbele ya Mwenyezi Mungu siku ya kiyama kuliko harufu ya Miski. Na anaefunga ana furaha mbili: wakati wa kufuturu anafurahi kwa futari yake, na wakati akikutana na Mola wake (siku ya malipo) atakuwa na furaha kwamba alikuwa kafunga.”.

Zifuatazo ni miongoni ya baadhi ya fadhila nyingine za Saumu kama zilivyo thibiti kutokana na Hadithi za Mtume S.A.W:

[1]Muslim 6/17 (1944), Bukhaari 6/474 (1771).

Written by

Saumu ilikuwa pia ni wajibu kwa umma nyingine zote zile zilizopita kabla. Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Suratil Baqara aya ya 183, “

﴿يَأيُّها الَّذِينَ ءَامَنُوا كُتِبَ عَلَيكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الّذِينَ مِن قَبلِكُم.

Maana yake, "Enyi mlioamini! Mmelazimishwa kufunga (Saumu) kama walivyolazimishwa waliokuwa kabla yenu." Lakini kwa kadiri siku zilivyokuwa zinapita, na baada ya kuondoka Mitume ya umma zile, waliifanyia saumu mabadiliko kukidhi haja zao na matamanio yao. Mipaka yake ikarukwa na lengo na kusudio hasa la Saumu ikabadilika.

Leo hii katika kila dini duniani kuna athari ya funga, lakini athari hizo katika dini hizo hazilingani kabisa na funga  zile za asili ambazo Mwenyezi Mungu Mtukufu alizo wakusudia waja wake. Mfano Nabii Musa A.S. alikuwa akifunga siku 40, na pia Nabii Issa A.S. yeye na wafuasi wake walikuwa wakifunga siku 40. Na Manasara walikuwa wakifunga mwezi mzima wa Ramadhani, lakini mwezi huo ulipoangukia wakati wa joto, basi wanavyuoni wao wakaamuwa kutokufunga wakati huo kwa ajili ya shida ya joto na  badala yake wafunge siku nyingine za wakati wa baridi. Kwa ajili ya kubadilisha mwezi wa saumu wakaongeza ziada siku 10 za kufunga ili iwe kafara na toba yake na wakawa wakifunga siku 40, siku hizi zinajulikana maarufu kwao kama kwaresima

[1] Siku arubaini za mfungo wa Wakristo kabla ya sikukuu ya Pasaka.

Written by

Saumu ni moja ya nguzo ya dini ya Kiislamu  iliyothibiti kutokana na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, na Hadithi za Mtume Wake S.A.W., kama ifuatavyo. Kasema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat Al-Baqara aya ya 183,"

﴿يَأيُّها الَّذِينَ ءَامَنُوا كُتِبَ عَلَيكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الّذِينَ مِن قَبلِكُم لَعَلَّكُم تَتَّقُونَ.

Maana yake, "Enyi mlioamini! Mmelazimishwa kufunga (Saumu) kama walivyolazimishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mwenyezi Mungu." Pia Kasema katika Surat Al-Baqara aya ya 185, “

﴿فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ.

Maana yake, “Basi ataye kuwa mjini katika mwezi huu na afunge”. Ziko Hadithi nyingi za Mtume S.A.W., zinazoelezea kuwepo na kuwajibika kwa funga ya mwezi wa Ramadhani, ambazo tutazitaja baadhi yake kwa muhtasari, katika sehemu tofauti kufuatana na mahitajio yake. Kutoka kwa Ibn Umar R.A.A. kasema, "Kasema Mtume  S.A.W

[1] Bukhariy 1/11(7), Muslim 1/102 (20).

Zaidi ya saumu ya mwezi wa Ramadhani ambayo ni faridha kwa kila Mwislamu alietimiza shuruti zake, zipo saumu nyingine ambazo ni wajibu kwa yule ziliyomuwajibikia kufuatana na hali na sababu zenyewe, kama ifuatavyo.

 

1. Kafara ya kuapa.

Ikiwa mtu ataapa kwa jambo, na akataka kubadilisha kiapo chake alichoapa, mfano mtu kaapa: kutoingia katika nyumba ya ndugu yake, na akataka kukibadilisha kiapo chake, basi kafara yake ni kulisha, au kuvisha masikini kumi, au kumpa mtumwa uhuru, kwa asie kuwa na uwezo ni kufunga siku tatu. Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Al-Maida aya ya 89,"

﴿........فمَنْ لم يجدْ فصيامُ ثلاثة أيامٍ، ذلك كفارة أيْمانِكُم إذا حَلَفْتُمْ.

Maana yake, "[Mwenyezi Mungu hatakuteseni kwa viapo vyenu vya upuuzi, lakini atakukamateni kwa viapo mlivyoapa kwa nia mliofunga barabara. Basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa chakula cha katikati mnachowalisha watu wa majumbani mwenu, au kuwavisha, au kumpa uungwana mtumwa]. Lakini asiyeweza kupata hayo, basi afunge siku tatu." Maneno niliyo yatia katika kifungo (bracket) ni tafsiri ya mwanzo ya aya ambayo siku ileta kiarabu.

 

2.Kafara ya kumuua Mwislamu bila ya kukusudia.

Ikiwa mtu atamuua Mwislamu bila ya kukusudia, na hana mtumwa wa kuachia uhuru, basi itabidi afunge miezi miwili mfululizo. Kasema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat An-Nnisaai aya ya 92,"

﴿وَ مَنْ قتلَ مُؤْمناً خَطأ فتحرير رقبةٍ مؤمنة........فمن لم يجدْ فصيامُ شهْرينِ مُتتابِعَيْن.

Maana yake, "Na haiwi Muumini kumuuwa Muumini ila kwa kukosea. Na mwenye kumuuwa Muumini kwa kukosea basi amkomboe mtumwa aliye Muumini, na atoe diya kuwapa jamaa za maiti, isipo kuwa waache wenyewe kuwa ni sadaka. Na akiwa ni jamaa wa maadui zenu, hali yeye ni Muumini, basi ni kumkomboa mtumwa aliye Muumini. Na akiwa ni miongoni wa watu ambao pana ahadi baina yenu na wao basi wapewe diya watu wake na akombolewe mtumwa Muumini. Na asiye pata, basi afunge miezi miwili mfululizo, kuwa ni toba kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mwenye hikima”.

 

3.Kumtenga mke kwa kumfananisha na mama.

Ikiwa mtu atamtenga mkewe bila ya kumuacha kwa  kumfananisha kama vile mama yake, na baada ya muda akarudisha nafsi yake, na akataka kurudiana na mkewe, basi itambidi  atoe kafara ya kufunga miezi miwili mfululizo, kwa yule asieweza kuachia mtumwa uhuru. Na desturi hii ya mtu kumtenga mkewe bila kumuacha walikuwa nayo Waarabu wakati wa kabla ya Uislamu. Ilikuwa mtu akimchoka mkewe anamtenga bila ya kumuacha, akimuambia kuwa anamuona kama mama yake. Inakuwa mwanamke huyu hakuachika, na huyo mume, na haishi nae, lakini pia hawezi kuolewa na mtu mwingine, na wakati huo anakuwa hana haki na mumewe. Hali hii iliendelea mpaka mwanamke mmoja alipokwenda kumshtakia Mtume S.A.W. Mwenyezi Mungu Mtukufu akashusha hukumu Yake katika Surat Al-Mujaadalah aya ya 3 na ya 4,  ''

﴿والذين يُظاهرُون مِنْ نِسائهم ثمَّ يَعُودون لِمَا قالوا فتحرير رقبةٍ مِنْ قبل يتماسَّا.....فمنْ لم يجد فصيامُ شهْرينِ متتابِعَيْنِ.

Maana yake, "Na wale wawaitao wake zao mama zao, kisha wakawarudia katika yale waliyoyasema, (wakataka kuwarejea wake zao wakae nao kama kidasturi ya mke na mume), [basi wampe mtumwa uhuru kabla ya kugusana. Mnapewa maonyo kwa haya. Na Mwenyezi Mungu anajua (yote) mnayoyatenda]. Na asiyepata (mtumwa) basi afunge saumu ya miezi miwili mfululizo kabla ya kugusana. Maneno niliyo yatia katika kifungo (bracket) ni tafsiri ya mwanzo ya aya ambayo siku ileta.

 

4.Kafara kwa kuingiliana mchana Ramadhani.

Ikiwa mtu ataingiliana na mkewe mchana wa mwezi wa Ramadhani au atajitoa manii mchana kwa makusudi, saumu yake itaharibika na itaibidi ailipe siku ile na kafara yake ni kufunga miezi miwili mfululizo kwa yule asieweza kuachia mtumwa uhuru. Hadithi iliyotolewa na Abu Huraira kasema, "Mtu mmoja alimjia Mtume S.A.W. akasema, "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu mimi nimeangamia!" Mtume S.A.W akamuuliza kipi kilicho kuangamiza?" Akasema, "Nimemuingilia mke wangu mchana wakati wa Mwezi wa Ramadhani." Mtume S.A.W. akamuuliza, "Jee unaweza kuachia mtumwa huru?" Akajibu, "La sina." Mtume S.A.W. akasema, "Jee unaweza kufunga miezi miwili mfululizo?" Akasema, "La" Mtume S.A.W. akasema, "Jee unaweza kulisha masikini sitini?" Akasema, "La" Mtume S.A.W. akasema, "Kaa" Kikapu cha tende kikaletwa kwa Mtume S.A.W. na akasema, " Toa hizi kama sadaka."  Yule mtu akasema, "Kwa mtu alie masikini kuliko sisi? Hakuna mtu katika mji huu ambae ni alie masikini kuliko sisi!" Mtume S.A.W. akacheka mpaka mwanya wa meno yake ukaonekana akasema, "Nenda kailishe familia yako."        

 

5.Saumu ya Nadhiri.

Hii ni saumu ambayo mtu amejilazimishia mwenyewe nafsi yake. Mtu yoyote alieweka nadhiri ya kufunga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kufanikiwa na jambo fulani, na ikiwa litatokea jinsi alivyotarajia, basi itakuwa kwake ni lazima atimize nadhiri yake kwa kama jinsi alivyonuia.

 

6.Saumu ya asie na kichinjo katika Hijja ya Tamatu`u.

Ikiwa mtu atafanya Hijja ya Tamat`uu, inamuajibikia  kuchinja ikiwa ana uwezo, na ikiwa hana uwezo basi inamuajibikia kufunga siku kumi. Siku tatu akiwa bado yupo katika Hajj na siku Saba akirejea nyumbani kwake. Kasema Mola Mtukufu katika Suratil Baqara aya 196, “

﴿فَمَن تَمَتَّعَ بِالْعُمْرَةِ إِلَى الْحَجِّ فَمَا اسْتَيْسَرَ مِنَ الْهَدْيِ فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ ثَلاثَةِ أَيَّامٍ فِي الْحَجِّ وَسَبْعَةٍ إِذَا رَجَعْتُمْ تِلْكَ عَشَرَةٌ كَامِلَةٌ.

Maana yake, “Basi mwenye kujistarehesha kwa kufanya Umra kisha ndio akahiji, basi achinje mnyama aliye mwepesi kumpata. Na asiye pata, afunge siku tatu katika Hija na siku saba mtakapo rudi; hizi ni kumi kaamili”.

 

7. Kafara ya kuwinda wanyama pori kwa aliye Hirimia.

Ikiwa mtu amehirimia kwa ajili ya Haji, halafu akawinda na kumuua mnyama wa pori, basi itabidi atoe kafara ya kuchinja mnyama sawa na yule aliemuua. Mnyama huyo wa kafara achinjwe katika maeneo matukufu ya Al-Kaaba ya Makka. Nyama ya  mnyama yule walishwe masikini; au ikiwa hawezi kuchinja basi afunge. Kasema Mola Mtukufu katika Surat Al-Maida aya ya 95, “

﴿وَمَن قَتَلَهُ مِنكُم مُّتَعَمِّداً فَجَزَاء مِّثْلُ مَا قَتَلَ مِنَ النَّعَمِ يَحْكُمُ بِهِ ذَوَا عَدْلٍ مِّنكُمْ هَدْياً بَالِغَ الْكَعْبَةِ أَوْ كَفَّارَةٌ طَعَامُ مَسَاكِينَ أَو عَدْلُ ذَلِكَ صِيَاماً.

Maana yake, "Enyi mlio amini! Msiue wanyama wa kuwinda nanyi mmeharimia katika Hija. Na miongoni mwenu atakaye muuwa makusudi, basi malipo yake yatakuwa kwa kuchinja kilicho sawa na alicho kiuwa, katika mifugo, kama wanavyo hukumu waadilifu wawili miongoni mwenu. Mnyama huyo apelekwe kwenye Al Kaaba, au kutoa kafara kwa kuwalisha masikini; au badala ya hayo ni kufunga”. Na hii imekusudiwa wanyama wa pori tu na wala siyo wanyama wa baharini. Kasema Mola Mtukufu katika Surat Al-Maida aya ya 96, “

أُحِلَّ لَكُمْ صَيْدُ الْبَحْرِ وَطَعَامُهُ مَتَاعاً لَّكُمْ وَلِلسَّيَّارَةِ وَحُرِّمَ عَلَيْكُمْ صَيْدُ الْبَرِّ مَا دُمْتُمْ حُرُماً.

Maana yake, “Nyinyi mmehalalishiwa kuvua vinyama vya baharini na kuvila, kwa faida yenu na kwa wasafiri. Na mmeharamishiwa mawindo ya wanyama wa bara (nchi kavu) madamu mmeharimia Hija”.

Hali za watu zinatofautiana kufuatana na afya zao, na umri wao. Kwa hali hiyo uwezo wao wa kufanya ibada pia unatofautiana. Mwenyezi Mungu Mtukufu haikalifishi nafsi yoyote ile zaidi ya uwezo wake alioipa, Naye ni Mwenye kufahamu, na Mjuzi wa kila jambo, na kaifanya dini hii ni nyepesi kwa kwa waja Wake. Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Al-Hajj aya ya 78, “

﴿وَ مَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فىِ الدِّينِ مِنْ حَرَجِ مِّلَّةَ أَبِيكُمْ إِبْرَاهِيمَ.

Maana yake, “Wala hakuweka mambo mazito katika dini (Nayo dini hii) ni mila ya baba yenu Ibrahim.” Pia kasema katika Surat AN-Nisaai aya ya 28, “

﴿يُريِدُ الله أن يُخَفِّفَ عَنكُمْ وَ خُلِقَ الإِنسَانُ ضَعِيفًا.

Maana, “Mwenyezi Mungu anataka kukukhafifishieni maana mwanaadamu ameumbwa dhaifu.”

Watu wenye dharura walioruhusiwa kutofunga wamegawanyika sehemu tatu kama ifuatavyo:

(1) Watu ambao wameruhusiwa kutokufunga kufuatana na hali zao, na baadae wanalazimika kuzilipa saumu zao.

(2) Watu ambao wameruhusiwa kutokufunga kufuatana na hali zao, na badala yake  kutoa fidia.

(3) Watu ambao wameruhusiwa kutokufunga kufuatana na hali zao za wakati ule, na baadae kufunga, na kutoa fidia.

 

WANAO TAKIWA KULIPA SAUMU.

Wafuatao ni baadhi ya watu ambao wameruhusiwa kutokufunga kufuatana na hali zao, na baadae kuzilipa saumu zao kwa kufunga baada ya dhurufu zao kuondoka:

 

1.Wanawake wenye hedhi na ujusi:

Wanawake wenye hedhi, na wale wanaotoka damu ya ujusi[1], wao wanaruhusiwa kisheria kutokufunga, na baada ya kutoharika wafunge zile siku ambazo walikuwa hawa kuzifunga. Na ikiwa kama watafunga na hali wako katika hali hiyo basi saumu zao hazikubaliwi, na watakuwa wamefanya maasi. Hadithi ya Bibi Aisha R.A.A.H. kasema,[2]

كُنَّا نَحِيضُ عِنْدَ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَيَأْمُرُنَا بِقَضَاءِ الصَّوْم ولا نؤمر بقضاء الصلاة.

Maana yake, “Tulikuwa tukipata hedhi wakati wa Mtume S.A.W. na alikuwa anatuamrisha kulipa saumu (na wala hatukuamrishwa kulipa Sala)[3].”

 

2.Mtu alie na maradhi.

Mtu aliepatwa  na maradhi, na akahofia maradhi yake kuzidi, au kupata madhara iwapo atafunga, basi anaruhusiwa kutofunga, na baadae Mwenyezi Mungu Mtukufu akimuondolea maradhi yake kulipa siku zile ambazo alizokuwa hakuzifunga. Kasema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratil Baqara aya aya 184, “

﴿فمن كان منكم مَّريضًا أو على سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِنْ أَيَّامٍ أُخَرَ.

Maana yake, “Basi atakaekuwa mgonjwa miongoni mwenu au yuko safari (akafungua) basi (atimize) hisabu katika siku nyingine.”

 

4.Kuzidiwa na saumu:

Ikiwa mtu atazidiwa na saumu kwa sababu ya kiu,  au njaa, na akahofia kumsababishia madhara, basi anaruhusiwa kula, au kunywa, kiasi tu cha kumuondolea yale madhara. Ikimuondokea hali ile ya madhara basi, ajizue kula, au kunywa, tena mchana ule uliobakia. Baada ya Ramadhani siku hiyo itabidi ailipe. Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Suratil Baqara aya 195, “

﴿ولاَ تُلْقُواْ بِأَيْديكُمْ إلى التَّهْلُكَةِ.

Maana yake, “Wala msijitie kwa mikono yenu katika maangamizo.” Pia kasema katika Suratil Baqara aya ya 185, “

﴿يُريِدُ الله بِكُمُ الْيُسْرَ و لا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ.

Maana yake, “Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito.”

 

WANATOA FIDIA BADALA YA KUFUNGA.

Wafuatao ni baadhi ya watu ambao kufuatana na hali zao hawalazimiki kufunga, na badala yake kutoa fidia katika kila siku ambazo hawakufunga:

 

1.Wazee wasioweza kufunga.

Wale wote ambao kwa sababu ya umri wao kuwa mkubwa, na kuwafanya wawe dhaifu kiasi cha kutoweza kufunga au kutoweza kuvumilia njaa,  basi wao wanaruhusiwa kutokufunga na badala yake kutoa fidia kwa kulisha masikini. Kila siku moja ambayo hakuifunga atalisha masikini mmoja mlo mmoja. Kasema  Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratil Baqara aya ya 184, “ 

﴿وَ عَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ, فِديَةٌ طَعَامُ مِسكِينٍ.

Maana yake, “Na wale wasioweza (kufunga), watoe fidia kwa kumlisha masikini.” Na akasema Ibn Abbas aya hii imeshuka kwa ajili ya watu wazee sana, na ambao hawawezi kufunga. Pia Kasema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat At-Taghaabun aya ya 16, “

﴿فَاْتَّقُواْ الله مَااْستَطَعتُمْ.

Maana yake, “Mucheni Mwenyezi Mungu muwezavyo.” Yaani mtu afanye ibada kufuatana na uwezo wake. Na pia Kasema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratil Baqara aya ya 286, “

﴿لاَ يُكَلِّفُ الله نَفْسًا إلاَّ وُسْعَهَا.

Maana yake, “Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yeyote ila yaliyo sawa na uweza wake.” Pia kasema katika Surat AN-Nnisaai aya ya 29, “

﴿وَلاَ تَقْتُلُوا أَنفُسَكُمْ إِنَّ الله كَانَ بِكُمْ رَحِيمًا.

Maana yake, “Wala msijiue nafsi zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kukuhurumieni.”

 

2.Mtu alie na maradhi yasiyopona.

Mtu yoyote alie na maradhi yasiyopona ambayo yatamsababisha asiweze kufunga anaruhusiwa kutokufunga na baadae kulipa fidia kwa kila siku aliyoacha kufunga kulisha masikini mmoja siku moja mlo mmoja.

 

KULIPA SAUMU KWA KUFUNGA.

Wafuatao ni watu ambao wanaruhusiwa kutokufunga kufuatana na hali zao, na badala yake kufunga baada ya dharura zao kuondoka:

 

1.Mama mja mzito, au mama anaenyonyesha.

Inaruhusiwa kwa mama mja mzito, na mama anaenyonyesha, ikiwa atahofia yeye, au mtoto wake, kupata madhara ya aina yoyote yale ikiwa atafunga wakati wa mimba yake, au wakati wa kunyonyesha, kutokufunga, na badala yake kulipa siku alizokula. Hadithi ya Anas bin Malik R.A.A kasema, "Kasema Mtume S.A.W.,[4]

إِنَّ اللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ وَضَعَ لِلْمُسَافِرِ الصَّوْمَ وَشَطْرَ الصَّلَاةِ وَعَنْ الْحُبْلَى وَالْمُرْضِعِ.

Maana yake, “Mwenyezi Mungu Mtukufu amemuondolea saumu msafiri na nusu ya sala, na (mwanamke) mwenye mimba na (mama) anaenyonyesha (saumu).”

 

2.Mtu alie na maradhi yenye kupona.

Mtu alie na maradhi ambayo yanapona anaruhusiwa kutokufunga wakati wa maradhi yake, na baadae kuilipa siku aliyokula wakati wa maradhi yake. Kasema Mola Mtukufu katika Surat Al-Baqarah aya ya 184, “

﴿فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضاً أَوْ عَلَى سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ.

Maana yake, “Na atakaye kuwa miongoni mwenu mgonjwa au yumo safarini basi atimize hisabu katika siku nyengine”.

 

3.Msafiri.

Msafiri anaruhusiwa kutokufunga wakati wa safari yake, na akisha rejea kutoka  safarini kwake, alipe siku alizofungua. Na kiwango cha masafa ya safari  ni sawa sawa na kiwango kile kile cha masafa ya safari cha kupunguza sala, yaani masafa ya umbali wa kilometa kumi na mbili. Kasema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratil Baqara aya ya 184, “

﴿فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضاً أَوْ عَلَى سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ.

Maana yake, “Na atakaye kuwa miongoni mwenu mgonjwa, au yumo safarini basi atimize hisabu katika siku nyengine”.

Na pia kasema katika Surat Al-Baqara aya ya 185, ambayo tumekwisha itaja hapo mwanzo. Na kama vile inaruhusiwa kutokufunga, pia inaruhusiwa kufunga kwa mwenye uwezo. Hadithi ya Bibi Aisha R.A.A.H. kasema, “Kasema Mtume S.A.W. kumuambia Hamza Bin Umar R.A.A.,[5]

صُمْ إِنْ شِئْتَ وَأَفْطِرْ إِنْ شِئْتَ.

Maana yake, “Ukipenda unaweza kufunga na ukipenda unaweza kula.” Kasema Mola Mtukufu katika Surat al-Baqara aya ya 185, “

﴿وَمَن كَانَ مَرِيضاً أَوْ عَلَى سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ يُرِيدُ اللَّهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلاَ يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ وَلِتُكْمِلُواْ الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُواْ اللَّهَ عَلَى مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ.

Maana yake, “Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi, wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushukuru”. Kwa yule msafirir mwenye uwezo wa kufunga ni bora zaidi kwake kufunga kuliko kuacha kufunga.[1] Hali ya kutokuwa msafi mwenye tohara kwa kutokwa damu au yale yanayotoka baada ya damu anayopata mwanamke aliyejifungua. Hali hii inatofautiana baina ya mwanamke na mwanamke aghalabu kwa wengi wao huwa ni siku arubaini lakini inaweza kuwa chini ya hapo au zaidi hata kufikia siku sitini.

[2] Abu Daawud 1/334 (229), Ibn Maajah 5/177 (1660), Muslim 2/232 (508).

[3] Sehemu hii imeongezwa na Abu Daawud na Muslim.

[4] Abu Daawud 6/375 (2056), An-Nasaai`y 8/10 (2276).

[5] Abu Daawud 1/328 (2050), At-Tirmidhiy 3/148 (645), Bukhaari 7/34 (1807).

Mambo yaliyo ruhusiwa kwa aliefunga kuyafanya.

1.Kutia dawa masikioni. Haikatazwi kutia dawa masikioni kwani tundu la sikio halifiki kooni.”

2.Kutapika bila kukusudia. Kutapika bila kukusudia hakuharibu saumu ili mradi yale matapishi hayakurudi ndani.

3.Kuoga. Hadithi ya Abu Bakr bin AbduraRahman, kutokana kwa miongoni mwa masahaba, kasema, [1]"

رَأَيْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بِالْعَرْجِ يَصُبُّ عَلَى رَأْسِهِ الْمَاءَ مِنْ الْعَطَشِ أَوْ مِنْ الْحَرِّ

Maana yake, "Nimemuona Mtume S.A.W. akimwagia kichwa chake maji wakati akiwa amefunga kwa ajili ya kiu au joto kali". Lakini kwa anayeoga anahitajia achukue hadhari maji yasimuingie ndani ya koo.

 

4.Kuonja chakula ili kujua ladha yake, bila ya kukimeza hii ikiwa ni dharura kwa mpishi, inaruhusiwa hata kumtafunia chakula kwa ajili ya mtoto bila kukimeza.

 

5.Kujitia mafuta mazuri na au kuyanusa.

 

6.Kutoa jino. Inaruhusiwa mradi damu isiingie kooni.

 

7.Kunusa manukato makali kama ubani na udi inaruhusiwa ikiwa ni harufu, bila ya moshi wake kuingia katika koo, ama ikiwa moshi wake utaingia katika koo basi inafunguza saumu kwa kauli ya baadhi ya wanavyuoni. Na Mwenyezi Mungu ndie mjuzi zaidi kwa hili.

 

8.Kumeza mate inaruhusiwa lakini yasiwe yawe kwanza yamekusanyika mdomoni, au yakachanganyika na kitu kingine, au akayotoa halafu akayameza, ikiwa itakuwa hivyo basi yanafunguza saumu. Ama makohozi na makamasi mtu akiyameza na ana uwezo wa kuyatoa yanafunguza saumu.

 

9. Kutoa damu inaruhusiwa, ikiwa kwa kumsaidia mtu au kwa kuipima. Kipimo kimechukuliwa na kama vile kufanya hijama.

 

10.Kupaka mafuta nje ya mwili

 

11.Kukata kucha, kukata nywele, na kujisafisha kwapa na sehemu za siri inaruhusiwa.

 

12.Kumbusu mke, au kumkumbatia inaruhusiwa lakini yasiwepo matamanio. Hadithi ya Jabir R.A.A. kasema, "Kasema Umar R.A.A,[2]

هَشَشْتُ فَقَبَّلْتُ وَأَنَا صَائِمٌ، فَقُلْتُ: يَا رَسُولَ اللَّهِ صَنَعْتُ الْيَوْمَ أَمْرًا عَظِيمًا قَبَّلْتُ وَأَنَا صَائِمٌ، قَالَ:  أَرَأَيْتَ لَوْ مَضْمَضْتَ مِنَ الْمَاءِ وَأَنْتَ صَائِمٌ، قُلْتُ: لا بَأْسَ بِهِ، قَالَ: فَمَهْ"

Maana yake, “Nilikuwa nimefurahi, basi nikambusu mke wangu na mimi nimefunga,” (Akamuendea Mtume S.A.W akamuambia) “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu nimefanya jambo kubwa; nimembusu mke wangu nami nimefunga”. Akajibu, “Jee unafikiri vipi ukisukutua mdomo wako kwa maji na hali ya kuwa umefunga?”  Nikasema, “Haina tatizo” Akasema, “Ni mfano wake”.[1] Ahmad 32/70 (15338).

[2] Abu Daawud 6/346 (2037).

Yafuatayo hapa chini ni miongoni mwa mambo ambayo yamekatazwa kufanywa kwa aliefunga, wakati wa saumu yake, na ikiwa mtu atayafanya nae amefunga basi yanasababisha kufunguza saumu yake. Kama ifuatavyo:

 

1.Kuingiza kitu chochote kile mpaka ndani kooni.

Hairuhisiwi kuingiza chochote kile ndani kooni wakati mtu amefunga. Mfano wa: chakula, kinywaji, dawa, au kutia dawa kupitia puani, au machoni, kwani matundu hayo yanakwenda mpaka kooni. Kasema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratil Baqara aya ya 187, “

﴿وَ كُلُواْ وَاشْرَبُواْ حَتَّى يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الخَيْطُ الأَبْيَضُ مِنِ الخَيطِ الأسْوَدِ مِنَ الفَجْرِ ثُمَّ أَتِمُّوا الصِيَامَ إلى الَّيْلِ.

Maana yake, “Na kuleni na kunyweni mpaka ukubainikieni weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku, kisha timizeni saumu mpaka usiku.”

 

2. Kujitoa manii.

Ikiwa mtu atajitoa manii kwa kukusudia kama vile kwa kujichezea, au kwa kufikiria, au kwa njia nyingine yoyote ile, basi saumu yake itaharibika. Lakini saumu haiharibiki kwa mtu kutokwa na manii kwa ajili ya kuota kwani hilio hutokea bila ya yeye kukusudia. Mara akiamka aende haraka kukoga josho kubwa ili kujitoharisha na ile janaba iliyompata, akijichelewesha bila ya sababu basi saumu yake itaharibika.

 

3.Kujitapisha kwa makusudi.

Ikiwa mtu atajitapisha kwa kukusudia, na yakamtoka matapishi basi saumu yake itakuwa imeharibika.  Hadithi ya Abu Huraira R.A.A. kasema, “Kasema Mtume S.A.W.,[1]

مَنْ ذَرَعَهُ الْقَيْءُ فَلا قَضَاءَ عَلَيْهِ وَمَنْ اسْتَقَاءَ فَعَلَيْهِ الْقَضَاءُ.

Maana yake, “Ikiwa mtu atatapika bila kukusudia (nae amefunga) basi hailipi siku ile, na yule atakaejitapisha kwa makusudi inamuwajibikia ailipe siku ile.”

 

4. Kuingiliana mke na mume:

Kuingiliana mke na mume wakiwa wamefunga wakati wa mchana kuna haribu saumu, wakitokwa na manii, au wasitokwe na manii. Hadithi ya Abu Huraira, R.A.A. kasema[2], “Kasema Abu Huraira R.A.A., “Tulikuwa tumekaa pamoja na Mtume S.A.W. akaja mtu mmoja akasema, “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu nimeangamia.” Mtume S.A.W. akamuuliza ni jambo gani lilokutokea?. Akajibu akasema, “Nimeingiliana na mke wangu wakati nimefunga.” Mtume S.A.W. akamuuliza,, “Jee unaweza kuachia mtumwa huru?” Akajibu, “Hawezi”. Mtume S.A.W. akamuuliza, “Jee unaweza kufunga miezi miwili mfululizo?” Akajibu, “Hawezi”. Mtume S.A.W. akamuuliza, “Jee unaweza kulisha masikini sitini?” Akajibu akasema, “Hawezi”. Mtume S.A.W. Akakaa kimya kwa muda na wakati ule tuliokuwa tukisubiri likaletwa kapu kubwa la tende kwa Mtume S.A.W. Mtume S.A.W. akauliza, “Yuko wapi aliekuwa akiuliza?” Akajibu, “Niko hapa”. Mtume S.A.W. akasema, “Chukua kikapu hiki cha tende na utoe sadaka.” Yule mtu akasema, “Jee nimpe mtu masikini kuliko mimi? Haki ya Mungu (Naapa kwa Mungu) hakuna familia iliyo masikini kuliko mimi katikati ya milima hii miwili.” Mtume S.A.W. akatabasamu mpaka mwanya wa meno yake ukaonekana halafu akasema, “Ilishe familia yako kwayo.” Iko ruhusa mtu kuingiliana na mkewe baada ya kwisha wakati wa saumu, yaani baada ya  kuingia kwa magharibi mpaka kabla ya kuingia alfajiri. Kasema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratil Baqara aya ya 187, “

﴿أُحِلَّ لَكُمْ لَيْلَةَ الصِّيَامِ الرَّفَثُ إلى نِسآئِكُمْ، هُنَّ لباسّ لَكُمْ وَ أَنْتُمْ لِبَاس لَهُنَّ عَلِمَ الله أَنَّكُمْ كُنْتُمْ تَخْتانُون أَنْفُسَكُمْ فَتَابَ عَلَيْكُمْ وَعَفا عَنْكُمْ ، فَالئنَ بَاشِرُوهُنَّ وابْتَغُوا مَا كَتَبَ الله لَكُمْ.

Maana yake, “Mmehalalishiwa usiku wa saumu kuingiliana na wake zenu. Wao (hao wake zenu) ni (kama) nguo kwenu, na nyinyi ni (kama) nguo kwao. Mwenyezi Mungu anajua kwamba mlikuwa mkizihinisha nafsi zenu. Basi amekukubalieni toba yenu na amekusameheni. Basi sasa ingilianeni nao (wake zenu) na takeni aliyokuandikieni Mwenyezi Mungu.”

 

5.Kufanya madhambi:

Kufanya madhambi yote yamekatazwa wakati wote na kufanya madhambi makubwa wakati wa mchana kwa aliefunga ni katika madhambi makubwa na yana haribu saumu ya siku ile. Kasema Abu Huraira R.A.A., "Kasema Mtume S.A.W., [3]

رُبَّ صَائِمٍ حَظُّهُ مِنْ صِيَامِهِ الْجُوعُ وَالْعَطَشُ.

Maana yake, “Inawezekana mtu aliefunga hakupata katika saumu yake isipokuwa njaa na kiu.” Pia hadithi iliyohadithiwa na Ibn Abbas R.A.A. kasema, “Kasema Mtume S.A.W.[4],“

وَلاَ صَوْمَ إِلاَّ بِالْكَفِّ عَنْ مَحَارِمِ اللَّهِ.

 Maana yake, “Wala hakuna saumu isipokuwa kwa kujizuia na yaliyo haramishwa na Mwenyezi Mungu.” Pia hadithi ya Abu Huraira R.A.A. kasema, “Kasema Mtume S.A.W,[5]

مَنْ لَمْ يَدَعْ قَوْلَ الزُّورِ وَالْعَمَلَ بِهِ فَلَيْسَ لِلَّهِ حَاجَةٌ فِي أَنْ يَدَعَ طَعَامَهُ وَشَرَابَهُ.

Maana yake, “Mtu asieacha kusema uongo na kuutumilia (huo uongo), basi Mwenyezi Mungu hana haja kwake yeye ya kuacha chakula chake, na kinywaji chake (yaani funga yake).” Na makusudio hapa ya yaliyo haramishwa na Mwenyezi Mungu ni kujizuia na kufanya madhambi. Na madhambi mengi makubwa ni maarufu na yanafahamika ikiwa ni pamoja na kula riba, kuiba, kudharau wazazi, kusema uongo na mengineyo mengi kama hayo.

Yako baadhi ya madhambi ambayo yameenea sana katika jamii, hata imefikia jamii kuyaona kama vile ni mwenendo wa maisha wa kawaida, kwa jinsi vile yalivyoingiliana na vitendo vya mwanaadamu vya kila siku katika, mazungumzo, kusikiliza na kutizama. Mtu akiyafanya basi yanamuharibia saumu yake, kama ifuatavyo:

 

KUZUNGUMZA.

*Kusengenya[6] ni katika madhambi makubwa na kunaharibu saumu. Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu  katika Surat Al-H`ujuraat aya ya 12, “

﴿وَلاَ يَغْتَب  بعْضُكُمْ بَعْضًا أَيُحبُّ اَحَدُكُمْ أَ ن يَأكُلَ لَحْمَ أَخِيهِ مَيْتًا فَكَرِهْتُمُوُهُ.

Maana yake, “Wala baadhi yenu wasiwasengenye wengine. Jee mmoja wenu anapenda kula nyama ya nduguye aliekufa? La, hampendi.” Pia kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Al-Qalam aya ya 10 na aya ya 11, “

﴿وَلاَ تُطِعْ كُلَّ حَلاَّفٍ مَّهِينٍ ﴿هَمَّازٍ مَّشَآءِ بِنَمِيمٍ.

Maana yake, “Wala usimtii kila muapaji sana, aliye dhalili. Msengenyaji (msemaji watu), aendaye akitia fitina.”  Pia Hadithi iliotolewa na Ibn Abbas R.A.A., "Kasema Mtume S.A.W,[7]

الْغِيبَةُ تُفْطِرُ الصَّائِمَ وَتَنْقُضُ الْوُضُوءَ.

Maana yake, “Kusengenya (kusema watu kwa ubaya) kuna haribu saumu (yaani kuna futurisha) na kunaharibu udhu.” Pia kutoka kwa Hudhaifa R.A.A. kasema, "Kasema Mtume S.A.W.,[8]

لا يَدْخُلُ الْجَنَّةَ نَمَّامٌ.

Maana yake, “Haingii peponi msengenyaji.” Na hii ni ithibati yenye nguvu kuwa kusengenya ni katika jambo lililo katazwa na kukemewa kukubwa, na ni katika madhambi makubwa.

Na kama vile kusengenya kuna haribu saumu, basi pia maneno machafu, na maneno ya upuuzi, yanaharibu saumu, na mtu anayetaka kuihifadhi Saumu yake ajiepushe nayo. Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Al-Muuminun aya ya 3, “

﴿وَاْلَّذِينَ هُمْ عَنِ اْللَغْوِ مُعْرِضُونَ.

Maana yake, “Na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi.”

 

*Kusema uongo. Kusema maneno ya uongo kunaharibu saumu na ni katika maasia makubwa. Hadithi iliyohadithiwa na Abu Huraira R.A.A. kasema, "Kasema Mtume S.A.W[9]., “

مَنْ لَمْ يَدَعْ قَوْلَ الزُّورِ وَالْعَمَلَ بِهِ فَلَيْسَ لِلَّهِ حَاجَةٌ فِي أَنْ يَدَعَ طَعَامَهُ وَشَرَابَهُ.

Maana yake, “Mtu asieacha kusema uongo na kuutumilia (huo uongo), basi Mwenyezi Mungu hana haja kwake yeye ya kuacha chakula chake na kinywaji chake (yaani funga yake).” Pia hadithi iliyohadithiwa na Abu Huraira R.A.A. kasema, "Kasema Mtume S.A.W.,[10]

مَنْ غَشَّنَا فَلَيْسَ مِنَّا.

Maana yake, “Mwenye kutuhadaa sio katika sisi.” Na hii haijuzu kwa Mwisilamu wakati wowote ule.

 

KUANGALIA.

*Kuangalia mambo yaliyoharamishwa kwa kukusudia:

Kila jambo lililokatazwa na Mwenyezi Mungu kuliangalia, ikiwa mtu ataliangalia kwa kukusudia nae amefunga linaharibu saumu. Na kitu kilicho haramishwa kukiangalia dhati yake, basi hata picha ya kile kitu hukumu yake ni sawa na kama kitu chenyewe. Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat An-Nnur aya ya 30 na 31,"

﴿قُلْ لِلْمُؤْمِنِينَ يَغُضُّوا مِنْ أَبْصَارِهِمْ} {وَقُلْ لِلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ.

Maana yake, “Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao (wasitazame yaliyokatazwa). “Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao.” Wasitazame yaliyo katazwa. Na baadhi ya mambo ambayo tumeharamishiwa kuangalia kwa kukusudia ni mfano:

 

*Kuangalia uchi wa mwenzako kwa kukusudia.

Kuangalia uchi wa mwenzio kwa kukusudia ni katika madhambi makubwa na kunaharibu saumu.  Kasema Mtume S.A.W.,[11]

لعن الله الناظر والمنظور اليه.

Maana yake, “Amelaaniwa anaeungalia uchi wa mwenziwe na anayeangaliwa (yaani anae uonyesha kwa kusudi)” Pia kutoka kwa Ibn Abbas R.A.A. kasema, "Kasema Mtume S.A.W.,[12]

«مَلْعُونٌ مَنْ نَظَرَ إِلَى فَرْجِ أَخِيهِ»

Maana yake, “Amelaaniwa mwenye kuangalia uchi wa nduguye.” Na mtu haimstahikii laana ya Mwenyezi Mungu isipokuwa kwa kufanya madhambi makubwa. Jambo hili limeenea sana siku hizi kwani imekuwa ni jambo la kawaida watu kuangalia picha katika magazeti na television ambazo hazikukamilisha sitara, haya ni maasia na yanafunguza Saumu. Ikiwa mtu anataka kuihifadhi saumu yake basi ajiepushe na kuangalia kwa kukusudia picha hizo kwani hukumu yake ni kama kuangalia vitu vyenyewe. Sitara kwa ujumla na yale yanayokhusu mavazi na yanayokusudiwa katika uchi tumeyataja kata kitabu cha Fiqh juzuu ya kwanza na ya pili.

 

KUSIKILIZA.

Kusikiliza: Mambo yaliyo haramishwa kuyasikiliza kwa kukusudia kuyasikiliza ni maasia na yanaharibu saumu. Na jambo lililo haramishwa kulitamka ni haramu kulisikiliza kwa kukusudia. Mifano ya haya ni kama ifuatavyo:

*Kusikiliza muziki: Kusikiliza miziki na vinanda na zumari kwa kukusudia kumekatazwa na kunaharibu saumu. Kutoka kwa Ibn Abbas R.A.A. kasema, "Kasema Mtume S.A.W,[13]

صَوْتَانِ مَلْعُونَانِ فِي الدُّنْيَا وَالآخِرَةِ: صَوْتُ مِزْمَارٍ عِنْدَ نَغْمَةٍ، وَصَوْتُ مُرِنَّةٍ عِنْدَ مُصِيبَةٍ.

 Maana yake, “Sauti mbili zimelaaniwa duniani na akhera sauti za zumari[14] wakati wa neema, na sauti ya yule anaelia huku anaomboleza wakati wa musiba”. Pia kasema Mtume S.A.W., [15]

لَيَكُونَنَّ مِن أُمَّتِي أَقْوَامٌ يَسْتَحِلُّونَ الْحِرَ وَالْحَرِيرَ وَالْخَمْرَ وَالْمَعَازِفَ.

Maana yake, “Watakuwepo katika umma wangu watu wenye kuchukulia: Zinaa[16], na (kuvaa) hariri na (kunywa) pombe na (kutumia/kusikiliza) ala za muziki (kama vile zumari, vinanda, filimbi) kuwa ni yenye kukubalika (yaani watayahalalisha kwa kubadilisha majina yake)”.

*Kusikiliza maneno yoyote ya uongo yaliyo katazwa kisheria au maneno ya kusengenya (kwa ubaya) kwa kukusudia ni maasia na yanaharibu saumu.

 

6. Kutokwa na damu ya hedhi.

Ikiwa mwanamke itamjia ada yake ya mwezi wakati wa mchana nae amefunga basi saumu yake ya siku hiyo itakuwa imeharibika. Hadithi ya Abi Said R.A.A. kasema, "Kasema Mtume S.A.W. [17], “

أَلَيْسَ إِذَا حَاضَتْ لَمْ تُصَلِّ وَلَمْ تَصُمْ.

Maana yake, “Jee sio kweli kuwa mwanamke wakati akiwa na hedhi hasali na wala hafungi?.”

 

YAFUATAYO NI BAADHI YA MAMBO YA WAKATI HUU YALIOENEA AMBAYO YANAHARIBU  SAUMU.

7.Dawa ya pumu ya kuvuta (kibomba cha pumu), kikitumiwa wakati wa saumu.

8.Kusafisha mafigo.

9.Kuongezewa damu.

10.Kuongezwa maji kwa njia ya sindano kupitia mshipa wa damu (sakaya/drip).

11.Kutiwa dawa kupitia tundu la nyuma.

12.Sindano ya kuongeza chakula. Ama sindano ambayo inayotumika kwa ajili ya tiba isiyokuwa na virutubisho wanavyuoni wametofatiana katika jambo hilo, baadhi yao wanasema haiharibu saumu ili mradi dawa ile haikufika katika koo nah ii ndio kauli yenye nguvu zaidi. Na wengine wanasema zote zinaharibu saumu ya mtu zikitumika. Na Mwenyezi Mungu ndie mjuzi zaidi katika jambo hili.[1] Ibn Maajah 5/186 (1666), At-Tirmidhiy 3/162 (653).

[2] Muslim 1870.

[3] Ahmad 18/43 (8501)

[4] Al-Imamu Al Rabi`u 1/134 (329).

[5] Abu Daawud 6/316 (2015), Bukhaari 6/473 (1770).

[6] Kumsema mtu kwa jambo ambalo yeye hatopendezewa kulisikia wakati yeye akiwa hayupo, kumteta.

[7] Al-Imamu Al Rabi`u 1/130 (317).

[8] Muslim1/273 (151), Ahmad Hambal 5/391(23373).

[9] Bukhaari 6/472 (1770), Abu Daawud 6/316 (2015), Baihaqy 3/356 (1138).

[10] Muslim 1/366 (146), Al-Imamu Al Rabi`u 1/231 (582), Ibn Maajah 6/477 (2216).

[11] Baihaqy 7/99 (13344).

[12] Al-Imamu Al Rabi`u 1/250 (638).

[13] Al-Imamu Al Rabi`u 1/249 (636).

[14] Filimbi, kitu kinachotumiwa kutolewa sauti kikipulizwa na aghalabu huwa chembamba sehemu ya mdomoni na mwishoni huwa chenye kupanuka.

[15] Bukhaari 17/298 Mlango wa kuihalalisha pombe lakini namba ya Hadithi haikutajwa.

[16] Tendo la uasherati.

[17] Bukhaari 2/3 (293).

 

Vifuatavyo hapa chini ni vitendo visivyopendezwa kufanya na yule mwenye saumu wakati wa saumu yake.

 

1.Kubusiana na Kukumbatiana.

Haipendezi kwa mtu na mkewe kubusiana, na kukumbatiana wakati wa mchana wakiwa katika saumu zao, kwani inaweza kuwapelekea kufanya mambo yanayopelekea kufunguza saumu yao. Ingawa imethibiti kutoka kwa Mtume S.A.W. kuwa yeye alikuwa akimbusu Bibi Aisha R.A.A.H. wakati akiwa amefunga. Lakini Mtume S.A.W. alikuwa ni tofauti na watu wengine, yeye alikuwa ana uwezo wa kuimiliki nafsi yake zaidi kuliko mtu mwingine. Kasema Bibi Aisha R.A.A.H.[1]

كَانَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يُقَبِّلُ وَيُبَاشِرُ وَهُوَ صَائِمٌ وَكَانَ أَمْلَكَكُمْ لِإِرْبِهِ.

Maana yake, “Alikuwa Mtume S.A.W. akibusu, na akikumbatia nae amefunga, lakini yeye ni mwenye kuimiliki zaidi nafsi yake kuliko nyinyi.”  

 

2.Kufanya Hijama au kuumika.

Haipendezi kwa aliefunga kuumika, kwani kunaweza kumdhoofisha kwa ajili ya upungufu wa damu. Mtume S.A.W. Yeye aliumika hali ya kuwa  amefunga, lakini tusisahau kwamba uwezo wake ni tofauti na watu wengine. Kasema Ibn Abbas R.A.A, [2]

احْتَجَمَ وَهُوَ مُحْرِمٌ وَاحْتَجَمَ وَهُوَ صَائِمٌ.

Maana yake, “Mtume S.A.W. aliumika (alihajimu) wakati yeye alikuwa amehirimia, na aliuumika (alihajimu)  na yeye amefunga.”

 

3. Kutia maji puani na kuyavuta ndani.

Haipendezi kwa aliefunga kutia maji puani na kuyavuta ndani, kwa kukhofia maji yale yasije yakaingia ndani ya koo na yakamfunguza Saumu yake. Kasema Aasim kutoka kwa baba yake, "Kasema Mtume S.A.W.,[3]

إِذَا اسْتَنْشَقْتَ فَبَالِغْ إِلَّا أَنْ تَكُونَ صَائِمًا.

Maana yake, “Unapovuta maji puani (wakati wa kutawadha) basi hakikisha yamefika ndani isipokuwa ikiwa kama umefunga.”

 

4.Kugogomoa.

Kugogomoa ni kusukutua kwa kuyafikisha maji mpaka ndani kooni. Na kama vile haipendezi kutia maji puani na kuyavuta ndani kwa kukhofia yasiingie ndani  kooni, pia haipendezi kugogomoa kwa hofu ya yale maji kuingia ndani kooni yakamfunguza Saumu yake.[1] Bukhaari 7/9 (1792), Muslim 5/409 (1854).

[2] Bukhaari 7/28 (1802).

[3] Ibn Haziima 3/236 (1985), Ahmad 33/121 (15785). Al-Imamu Al Rabi`u 94.

Page 1 of 2
FaLang translation system by Faboba