Ibadhi.com

WANAFUNZI WAKE

WANAFUNZI WAKE

 1. Al-Imamu Al-Rabiu bin Habib
 2. Abu Mawduud Al-Taaiy
 3. Salmat bin Saad
 4. Abu Ayyub Wail Al-Hadhramiy
 5. Abu Hamzatu Al-Shariy
 6. Abdu Rahman bin Rustum Al-Faarisiy
 7. Abraha bin Al-Sabaah Al-Humairiy
 8. Balah bin Uqbah
 9. Abu Sufyan Mahbuub bin Al- Ruhayl Al-Qurashi Al-Makhzumiy
 10. Al-Mu'utamir bin Ammara Al-Hilaliy
 11. Abu Al-Muurij Al-Sadusiy
Hayo ndiyo yaliyothibiti kwa Maibadhi kiufupi kuhusu Imamu huyu Adhiim Abu Ubayda Muslim bin Abi Karima, na kama utatupia macho kwa vizuri basi utaona kwamba maneno ya Sheikh huyo wa Kiwahabi Saad Aal Humayd hayana mwega wa kuegemea wala muundi wa kusimamia, pale alipodai kuwa hali ya huyu Abu Ubaida ni sawa na Al-Rabiu kwamba wote hawajazaliwa kamwe, na akatoa challenge  kwa kutaka apelekewe Maraajiu (references) kutoka kwa Maibadhi au Ahlu Sunna au Shia au Mayahudi au wengine wowote waliowataja watu hawa, lakini suali la kujiuliza je kweli akipelekewa ataamini au atatafuta chochoro nyengine? Kwa vyovyote vile hakuna ulazima kwetu kuthibitisha kuwepo kwa Maimamu wa Kiibadhi kutoka kwa yoyote katika aliowataja, si Ahlu Sunna wala Shia wala Mayahudi wala wengine wowote wale, bali lililolazima ni kuthibitisha kutoka katika vitabu vyetu, na madamu hilo yeye kaliridhia pia, basi ushahidi wa kuwepo kwa Imamu huyu Abu Ubaida ni huo tulioutanguliza kutoka katika vitabu vyetu kwa ufupi yenye kuelezea athari zake za kielimu baina ya wanafunzi wake na walimu wake.
Lakini kwa vile madai yake aliposema kwamba Maimamu hao yaani Abu Ubaida Muslim bin Abi Karima na Imamu Al-Rabiu, ni watu waliovumbuliwa tu na Maibadhi wa mwishoni na wakaaminiwa na waliokuja baade, basi hapana shaka kwamba kauli yake ya kutaka apelekewa Maraajiu (references) kutoka kwa Maibadhi yaliowataja Maimamu hao ni maneno tu anajisemea (إنها كلمة هو قائلها). Naam, vipi ataamini marejeo (references) kutoka kwa Maibadhi baada ya kudai kwake kwamba huyo ni mtu waliembuni tu?
Kwahivyo ni wazi kwamba alikuwa anataka kufurahisha jamuhuri yake ya wanafunzi wa Kiwahabi ili waseme kwamba katoa challenge, kwa hali yoyote hile, basi wacha sasa tutupie macho kwa yaliyosemwa na wale ambao anaona Sheikh huyo wa Kiwahabi Saad Aal- Humayd kwamba hoja inajengeka kwa maneno yao, ambao ni Ahlu Sunna, je wao wamesema nini kuhusu huyu Imamu Abu Ubayda? Je wamesema na wao kwamba hajazaliwa kabisa wala kubebewa mimba au vipi ?
 
Soma pamoja nami yafuatayo:
 
 
a) Imamu Ahmad bin Hanbal katika kitabu chake "AL-'ILAL WA MA'ARIFATU AL-RIJAAL" chapa ya kwanza ya mwaka (1308H – 1988AD) kilichochapishwa na AL-MAKTABU AL-ISLAMI" katika ( J.3 uk.11) kuna haya yafuatayo:
 
Riwaya (no. 3922) Nilimwambia Yahya (Ibn Ma'iin): Kuna Sheikh anaitwa Abu Ubayda anahadithia Mu'utamir kutoka kwake, na anahadithia (huyu) Abu Ubayda kutoka kwa Dhumam kutoka kwa Jabir bin Zayd, alikuwa (Huyu Abu Ubayda) anachukia kula hali ya kuwa kaegemea, ni nani huyu Abu Ubaida? Akasema: ni mtu ambae kapokea Mu'utamir kutoka kwake naye (huyo Abu Ubayda) ni mtu asie na matatizo (لا بأس به) anaitwa Abdullahi bin Al-Qassim. Nikamuuliza Yahya (Ibn Ma'iin), Je huyu Dhumam ambae Abu Ubayda kapokea kutoka kwake yeye ni nani? Akasema: ni Sheikh ambaye kapokea kutoka kwa Jabir bin Zayd, na huyu Abu Ubayda akapokea kutoka kwake (Dhumam) na akapokea Muammar kutoka kwake (yaani kutoka kwa Dhumam)
 
Riwaya (no. 3923) Anasema Abdallah bin Ahmad mtoto wa Imamu Ahmad kwamba: Nilimuuliza baba yangu kuhusu Abu Ubayda huyu, akasema: Jina lake ni Abdallah bin Al-Qassim ambaye ni maarufu kwa jina la Kuuriin.
 
Riwaya (no. 3924) Nilimuuliza Yahya nikasema: Mu'utamir kutoka kwa Abu Ubayda kutoka kwa Ammara bin Hayyan kutoka kwa Jabir bin Zayd. Je huyu Ammara bin Hayyan ni nani? Akasema ni mtu ambae huyu Abu Ubayda kapokea kutoka kwake naye ni katika watu wa Jabir bin Zayd, na kahadithia Abu Ubayda kutoka kwa Salih Al-Dahhan. Nimemsikia Yahya anasema kwamba: "Abu Ubayda hakusikia kutoka kwa Jabir bin Zayd kutoka kwa mtu yoyote kutoka kwake[1]
Ndugu msomaji zingatia kwamba hapa tupo katika kuporomoa madai ya Kiwahabi kuhusu Imamu Abu Ubayda Muslim bin Abi Karima, pale walipodai kwamba hakuna aliyemtaja na wala hajazaliwa kamwe mtu huyu, nawe kama unavyoona kwamba madai yao ni kama vumbi katika upepo wa kimbunga, kwasababu riwaya hizo zote zinamtaja huyo ambae wanamkanusha, na uchambuzi wa riwaya hizo utakuja baadae kidogo – Inshaallah – tuendelee na dondoo hizi fupi ili tuzidi kuona je mambo yaliishia hapo katika kutajwa Imamu huyu wa pili wa Kiibadhi katika vitabu vya Kisunni au vipi ?
 
TAARIKH IBN MA'IIN (J. 2 UK. 157 NO.3940)
Katika "Al-Taarikh" ya Ibnu Ma'iin katika riwaya ya Al-Duuriy, iliyochapishwa na DAARU AL-QALAM - BEIRUT – (J. 2 UK. 157
 

 
[1] - Yatakuja maelezo huko mbele kuhusu kauli hii ya Ibnu Ma'iin kuhusu  alivyosema hapa – Inshallah
 

 
NO.3940) anasema Al-Duuriy kwamba: Nimemsikia Yahya (Ibnu Ma'iin) anasema: Kasikia Mu'utamir kutoka kwa Abu Ubayda, na Abu Ubayda huyu ni mtu wa Basra naye ni Abdullahi bin Al-Qassim, na akapokea Abu Ubayda kutoka kwa Dhumam, na Dhumam huyu ni mtu wa Basra, nikamuuliza: Nani kapokea kutoka kwa huyu Dhumam zaidi ya Abu Ubayda? Akasema (yaani Ibnu Ma'iin): kapokea Mu'utamir na wengine wasiokuwa yeye miongoni mwa watu wa Basra.
 
 
TAARIKH IBN MA'IIN (J. 2 UK. 268 NO. 4723) Anasema Al-Duuriy: Katuhadithia Yahya kasema: katuhadithi Mu'utamir bin Suleiman kutoka kwa Abu Ubayda Al-Bisriy umaarufu wake ni Kuuriin kutoka kwa Dhumam kutoka kwa Jabir bin Zayd kuhusu – mwenye kuhirimia – anaeuwa kiwindwa kimakosa, akasema Je hasomi Qur-ani? Bali hukumu ni kwa mwenye kuuwa kwa kukusudia.
 
AL-JARHU WA AL-TA'ADIIL (J. 5 UK. 141 NO.657) Anasema Abdul Rahman bin Hatim Al-Razi kwamba: Abdallah bin Al-Qassim Abu Ubayda  kapokea  kutoka kwa Salih Al-Dahhan kutoka kwa Jabir bin Zayd na akapokea kutoka kwa mtoto (msichana) wa Abu Bakra, na kapokea Mu'utamir kutoka kwa Abu Ubayda, nimemsikia baba yangu anasema hivyo. Katuhadithia Abdul Rahman katuhadithia Abdallah bin Hanbal kwa aliyoniandikia akasema: "Nilimwambia Yahya bin Ma'iin, Kuna Sheikh anahadithia Mu'utamir kutoka kwake anaitwa Abu Ubayda naye kapokea kutoka kwa Salih Al-Dahhan kutoka kwa Jabir bin Zayd, ni nani huyu Abu Ubayda, akasema ni mtu anaeitwa Abdallah bin Al-Qassim, na hana matataizo yoyote (لا بأس به)
 
AL-DULABIY KATIKA KITABU "AL-KUNAA WAL-ASMAA"
 (J. 2 UK. 73) Anasema Al-Dulabi kwamba: Abu Ubayda ni Abdallah bin Al-Qassim kahadithia Mu'utamir bin Sulaiman kutoka kwake.
 
 
(J. 2 UK. 74) Anasema Al-Dulabiy kwamba: Kanihadithia Abdallah bin Ahmad bin Hanbal kasema: Nilimwambia Yahya bin Ma'iin. Kuna Sheikh anaitwa Abu Ubayda ambae Mu'utamir kahadithia kutoka kwake kutoka kwa Jabir bin Zayd kwamba alikuwa anachukia au anapinga kula na hali kaegemea, akasema (Yahya bin Ma'iin) Huyo ni mtu ambae hana matatizo kapokea kutoka kwake Mu'utamir naye anaitwa Abdallah bin Al-Qassim..Kasema Abbas kwamba nimemsikia Yahya (Ibn Ma'iin) anasema: Mu'utamir kasikia kutoka kwa Abu Ubayda na Abu Ubayda huyu ni mtu wa Basra naye ni Abdallah bin Al-Qassim, na akapokea Abu Ubayda huyu kutoka kwa Dhumam, na Dhumam huyu ni mtu wa Basra….Nikasema: Je ni nani kapokea kutoka kwa huyu Abu Ubayda badala ya Dhumam huyu? Akasema: Mua'mmar na wengine miongoni mwa watu wa Basra.
Katuhadithia Abbas bin Muhammad kasema: katuhadithia Yahya bin Ma'iin kasema: katuhadithia Mua'utamir bin Suleiman kutoka kwa Abu Ubayda Al-Basari maarufu kwa jina la "RAZIIN" kutoka kwa Dhumam kutoka kwa Jabir bin Zayd kuhusu mwenye kuhirimia anaeuwa kiwindwa kimakosa, akasema: Je hasomi Qur-ani? Hakika hukumu ni ya mwenye kuuwa kwa makusudi, kasema Yahya: Mu'ammar kapokea kutoka kwa Dhumam, na akanipa khabari Abdallah bin Ahmad bin Hanbal akasema: Nilimwambia Yahya bin Ma'iin: Kuna Sheikh anahadithia Mu'utamir kutoka kwake anaitwa Abu Ubayda kutoka kwa Dhumam kutoka kwa Jair bin Zayd kwamba anachukia kula na hali kaegemea, je huyu Abu Ubayda ni nani? Akasema: ni mtu ambae Mu'utamir kapokea kutoka kwake naye hana matatizo (ليس به بأس) anaitwa Abdallah bin Al-Qassim, nikamuuliza: je ni nani kapokea mwengine asiekuwa huyu Mu'utamir? Akasema: watu wa Basra wamehadithia kutoka kwake, nikasema: je huyu Dhumam ambae Abu Ubayda kapokea kutoka kwake yeye ni nani? Akasema: ni Sheikh ambae kapokea kutoka kwa Jabir bin Zayd, na Abu Ubayda kapokea kutoka kwake (Dhumam), na akapokea Mu'ammar kutoka kwake, yaani kutoka kwa Dhumam vile vile.
Vile vile ukitupia macho katika "Ansaab Al-Ashraaf" cha Al-Balaadhiriy utaona kwamba anamtaja Imamu Abu Ubayda alipokuwa anazungumzia kuhusu barua aliyoituma Imamu Abdullahi bin Yahya Al-Kindiy (Taalib Al-Haqqi) ambapo alisema Al-Balaadhiriy:
((فكتب إلى أبي عبيدة مسلم كورين مولى بني تميم وإلى غيره من إباضية البصرة يشاورهم في الخروج فكتبوا إليه: "إن استطعت ألا تقيم يوما فافعل فإن المبادرة بالعلمل الصالح أفضل فإنك لا تدري متى يبلغ أجلك..."))
"Basi (Abdullahi bin Yahya Al-Kindiy) akamwandikia barua Abu Ubayda Muslim Kuuriin Maula wa Banii Tamim na wengine miongoni mwa Maibadhi wa Basra akiwashauri kuhusu kutoka (kujitenga) na wao wakamwandikia kwamba: "Ikiwa utaweza kutokukaa siku moja basi fanya, kwani hakika kukimbilia katika kufanya amali njema ni bora zaidi, kwasababu hujui lini itafika siku yako ya kufa [4]
 
-----------------------------------------------------------------------------------------------------
[2] - Katika chapa imeandikwa "Kuuriiz" nalo ni kosa, bali sahihi ni "Kuuriin"
[3] - Kusema kwamba jina lake ni "RAZIIN" huu ni upindishaji wa jina (Tas-hiif) Sahihi ni "KUURIIN" sio "RAZIIN" 
[4] - Al-Balaadhiriy alikuwa anataja uovu wa watawala wa Banii Umaiya alioukuta Imamu huyu wa Kiibadhi katika nchi ya Yemen, ambapo aliandika barua kumshauri Imam wake yaani Abu Ubayda
 

 
 
Hawa hapa Maulamaa wa Ahlu Sunna ewe Saad Aal Humayd wanamtaja Abu Ubayda Muslim bin Abi Karima, vyenginevyo tuonesheni ni Abu Ubayda gani aliyepokea kutoka kwa Maimamu hawa wa Kiibadhi kuanzia Jabir bin Zayd na Salih Al-Dahhan na Dhumam kama si huyu Abu Ubayda Muslim bin Abi Karima? Haya ndio waliyoyasema Maulamaa wa "Al-Jarhu wa Al-Ta'adiil" na mukhtasari wa haya ni kwamba:

⦁ Abu Ubayda ni mtu wa Basra, na ambae Mu'utamir kapokea kutoka kwake na watu wengine wa Basra vile vile wamepokea kutoka kwake (Abu Ubayda)
⦁ Abu Ubayda kapokea kutoka kwa Jabir bin Zayd
⦁ Abu Ubayda Kapokea kutoka kwa Dhumam kutoka kwa Jabir bin Zayd
⦁ Abu Ubayda kapokea kutoka kwa Ammara bin Hayyan kutoka kwa Jabir bin Zayd
⦁ Abu Ubayda kapokea kutoka kwa salih Al-Dahhan kutoka kwa Jabir bin Zayd
 
Na tumesema hapo kabla kwamba hawa watatu yaani Imamu Jabir bin Zayd na Salih Al-Dahhan na Dhumam ni masheikh wa Abu Ubayda, na wote hao ni Maibadhi. Ama kuhusu kuitwa huyu Abu Ubayda kwamba jina lake ni Abdallah bin Al-Qassim, huu ni uchanganyaji wa majina baina yake na baina ya Abu Ubayda Al-Saghiir, ambae ni mmoja wa wanaharakati wa Kiibadhi aliyefariki mwaka 170H. Naye ni katika wanafunzi wa huyu Imamu Abu Ubayda  Muslim bin Abi Karima tunaemzungumza, ama Abu Ubayda Al-Saghiir ambae ndio huyo Abdallah bin Al-Qassim yeye hakuwa mpokezi wa Hadithi kinyume na huyu Abu Ubayda Muslim ambae ni Faqiihi na ni Muhaddith.
Kwahivyo aliyemwita huyu Abu Ubayda Muslim kwa jina la Abdallah bin Al-Qassim, basi atakuwa kamjua Abu Ubayda kidhati na hakumjua kijina, na kwa hivyo itabaki kauli ya Ibnu Ma'iin aliposema kwamba:
((أبو عبيدة لم يسمع من جابر بن زيد، عن رجل عنه))
"Abu Ubayda hakusikia kwa mtu yoyote kutoka kwa Jabir bin Zayd"
 
Bila shaka huyu ni Abu Ubayda Al-Saghiir ambae yeye ndie aliyekuwa anaitwa Abdallah bin Al-Qassim, na kama tulivyotangulia kusema kwamba huyu hakuwa mpokezi wa Hadithi wala msimulizi kamwe,kwahivyo kuwa hakupokea au kusikia chochote kutoka kwa Jabir bin Zayd ni kauli sahihi.
Ama Abu Ubayda ambae ni Imamu wa pili wa Kiibadhi basi huyu kakaa pamoja na Sheikh wake ambae ni Jabir bin Zayd kwa muda mrefu sana, kwahivyo si kitu chenye mantiqi kusema kwamba huyu hakusikia chochote kutoka kwa Jabir bn Zayd, kwahivyo ni wazi kwamba kauli ya Ibnu Ma'iin kwamba Abu Ubayda hakusikia kitu kutoka kwa Jabir bin Zayd, makusudio ni Abu Ubayda Al-Saghiir kwani yeye ndiye ambae alikuwa anaitwa Abdallah Al-Qassim na ndie ambae hakusikia kutoka kwa Jabir bin Zayd.
Ama kuitwa huyu Abu Ubayda Imamu wa pili wa Kiibadhi kwa jina la KUURIIN, dhahiri ni kwamba (Laqabu hii) umaarufu wa jina hili la KUURIIN ni la baba yake ajulikanaye kwa jina la Abu Kariima, na haya yametajwa na hawa wafuatao:
 
1 Al-Jaahidh Al-Mu'utaziliy katika kitabu chake "AL-BAYAAN WA AL-TABYIIN" chapa ya mwanzo mwaka 1414H. 1993A.D – DAAR IHYAA AL-ULUUM – J. 1 UK. 523: Kasema: "Na miongoni mwa Makhawarij na maulamaa wao  na wapokezi wao, ni Muslim bin Kuuriin na umaarufu wake ni Abu Ubayda, na alikuwa ni Ibadhi  na alikuwa katika Maulamaa wa Sufriyya"
Na hii ni wazi kwamba Kuuriin ni jina la baba yake,  kwahivyo Abu Ubayda jina lake ni Muslim bin Kuuriin, ama kumzingatia kwake kwamba Abu Ubayda alikuwa ni katika Khawarij, hili si jambo jipya bali huu ni ushahidi tosha kwamba mtu huyu alikuwepo na alikuwa Ibadhi, kwani kama ilivyo maarufu kwamba jina hili wanaendelea kubandikwa nalo Maibadhi wa kale na wa sasa, na hili ni kosa walilokwisha kulizowea hata kufikia kwao kudhani kuwa kufanya hivyo ni katika dini wakiitakidi kwamba Mtume (s.a.w) kawaita Maibadhi kuwa ni Khawarij!!! na hali yakuwa mustalahi huu haukuwepo kabisa wakati wake wala hajalitamka neno hilo kamwe, kwa vyovyote vile maudhui ya Khawarij hapa si pahala pake, hebu turudi katika maudhui yetu ya asili.
Vile vile kauli yake huyu Al-Jaahidh Al-Mu'utaziliy kuhusu Abu Ubayda aliposema kwamba: ((وكان إباضيا، ومن علماء الصفرية)) "Alikuwa (Abu Ubayda) ni Ibadhi na katika Maulamaa wa Sufriyya" hii ni kauli ya ajabu kwani hakuna uhusiano wowote baina ya Ibadhi na Sufriyya, basi vipi 
adai hivyo ??!! Kwahivyo ni wazi kwamba hapa kachanganya baina ya mambo mawili, kama ambavyo wamechanganya Maulamaa wa "Al-Jarhu wa Al-Ta'adiil" pale walipomzingatia huyu  Abu Ubayda ambae ni mtu wa Basra, na ambae Mu'utamir kapokea kutoka kwake na watu wengine wa Basra vile vile wamepokea kutoka kwake, na akapokea kutoka kwa Jabir bin Zayd na kutoka kwa Dhumam na kutoka kwa Ammara bin Hayyan na kutoka kwa salih Al-Dahhan kwamba jina lake ni Abdallah bin al-Qassim, na hali ya kuwa jina lake ni Muslim bin Abi Karima, ama Abdallah bin Al-Qassim huyu ni mwanafunzi wa Abu Ubayda Muslim, ambae alijulikana mwanafunzi wake huyo kwa jina la umaarufu kwamba ni Abu Ubayda Al-Saghiir (Abu Ubayda mdogo).
Hivyo basi, tumesema kwamba, kuitwa huyu Abu Ubayda kwa jina la KUURIIN, dhahiri ni kwamba (Laqabu hii) au umaarufu wa jina hili ni la baba yake ajulikanaye kwa jina la Abu Kariima, kwahivyo kauli ya Al-Jaahidh huyu vile vile kuhusu Abu Ubayda aliposema kwamba jina lake ni Muslim bin Kuuriin, utaona kwamba kauli hii inaifasiri kauli yake nyengine aliposema katika mazungumzo kuhusu walioitwa Makhawarij kwamba: ((Na miongoni mwa Maulamaa wao ni: ((….Asghar bin Abdul Rahman na Abu Ubayda Kuuriin na jina lake ni Muslim naye ni Mawla)) Tazama: ((AL-BAYAAN WA AL-TABYIIN J.2 Uk. 907))
Inavyoonekana dhahiri ni kuwa limeanguka neno "bin" baina ya "Abu Ubayda" na "Kuuriin" katika chapa hiyo. Ama aliyoyataja Al-Dulabiy kutoka kwa Ibnu Ma'iin kwamba (laqab) umaarufu wake ni hili jina la "Raziin" badala ya "Kuuriin", ni wazi kwamba kumetokea upindishaji (Tas-hiif) wa jina na haya yanawatokea Maulamaa na wala si jambo geni.
Na miongoni mwa waliomtaja Abu Ubayda Muslim bin Abi Karima ni:
 
2) Imamu Al-Bukhari katika "At-Taarikh Al-Kabiir" (J. 7 UK. 271 No. 1144) kasema: "Muslim bin Abi Karima anataja kutoka kwa Ali"
 
3) Abdul Rahman bin Abi Hatim katika kitabu chake "Al-Jarhu wa At-Ta'adiil" (J. 8 UK. 193 NO. 1845) kasema: Muslim bin Abi Karima kapokea kutoka kwa Ali (r.a)….Nimemsikia Baba yangu akisema hivyo, na anasema kwamba hajulikani (Majhuul).
 
4) Ibnu Hibban katika kitabu chake "Al-Thiqaat" (J. 5 UK. 301) kasema: "Muslim bin Uqqal na Muslim bin Ammar na Muslim bin Abi Karima na Muslim bin Hurmuz na Muslim Mawla wa Ali, hao wote wamepokea kutoka kwa Ali bin Abi Talib, lakini mimi siwategemei, wala sipendezewi na kuwatolea hoja kwa kule kuwa kwao katika madhehebu dhalili" Na maneno haya ya Ibnu Hibban kayafasiri Ibnu Hajar katika Kitabu chake "Al-lisaan" (J. 6 UK. 37 NO. 1572/8357), na baada ya kunukuu kauli hiyo ya Ibnu Hibban alisema: "Anakusudia kwa ajili ya Ushia".
 
5) Ahmada bin Yahya Al-Naasir, mmoja wa Maulamaa wa Zaidiya aliyefariki mwaka 315H, vile vile kamtaja Abu Ubayda katika katabu chake kiitwacho "Al-Najaat" chapa ya mwaka 1405H sawa na 1985A.D. katika ukurasa 337[7]
 

 
 
Said Al Habsy

Website: https://www.ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment