Ibadhi.com

09. FUNGA YA ARAFA BAINA YA MUANDAMO NA KISIMAMO

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Shukurani zote ni kwa Allah mtukufu, na rehma na amani ziwe kwa kipenzi chetu Mtume wa Allah Muhammad pamoja na wafuasi wake na masahaba wake mpaka siku ya malipo.

Asalamu alaykum wa rahmatullahi wa barakatuh.

Kwa hakika mvutano baina na haki na batili ndio hali inayowafikia waja katika ulimwengu huu, na katika kila zama na mitihani yake, na katika hayo ndio linapatikana lengo la uwepo wetu katika ulimwengu huu, amesema Allah mtukufu:

كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ ۗ وَنَبْلُوكُم بِالشَّرِّ وَالْخَيْرِ فِتْنَةً ۖ وَإِلَيْنَا تُرْجَعُونَ

((Kila nafsi itaonja mauti, na tunakujaribuni kwa shari na kheri kuwatahini, na kwetu sisi munarejeshwa.)) [Al-Anbiyaa 35].

Dini ya Uislamu imetimia tokea miaka 1429 iliyopita kama ilivoeleza Qurani tukufu, miaka yote hiyo Waislamu walifanyia kazi mafundisho yake, yako ambayo walikubaliana ndani yake na yako waliyotafautiana ndani yake, yaliyoingiwa na tafauti yalisababisha kupatikana madhehebu tafauti ili kudhibiti misimamo ya kila upande na wahusika wake katika kila zama, ni sawa katika Itikadi au Fiqhi au Siasa, na mapote yalizuka, ni hali isiyoweza kupingika wala kukatalika, na kila wahusika wa madhehebu walitokeza ndani yake wanavyuoni na watetezi, kwa mwenye kusoma kitabu cha Allah mtukufu anajua kuwa hiyo si hali ngeni; kwani imeelezwa kuwafikia waliopita kabla yetu.

Si tatizo kutafautiana, bali tatizo sugu ni kufanyiana uadui kwa sababu ya tafauti, kwa hiyo ni wajibu wa kila Muislamu kuheshimu tafauti iliyotokeza na inayotokeza na itayotokeza, kama ilivokua ni wajibu wa kila Muislamu kujiepusha na njia ya ubabe na uadui dhidi ya waliotafautiana naye kimadhehebu, na iwapo atajikuta kuwemo katika safu za fikra za kufanyia ubabe na uadui wengine kwa sababu ya kutafautiana kimadhehebu basi ajijue kuwa amekumbwa na maradhi mabaya yaliyoelezwa katika Quraani kuwapata waliopita kabla yetu, haraka sana airejee nafsi yake na ajue kuwa hapo alipo sipo; kwani yupo katika batili, kwa haya upendo utaenea, na jamii itaimarika, na umoja utapatikana, kwani mshikamano katika yenye makubaliano utaweza kuimarika, na heshima katika yaliyoingiwa na tafauti itaweza kupatikana, na kila wenye msimamo wataweza kueleza dalili zao katika jamii. Umoja kwamwe hauji kwa kulazimishana na kutetea wingi, kwani hakuna haki ya kuificha haki, na haki ni kwa dalili si kwa wingi.

Ibadhi kwa upande wetu ni tunda ya kujishika na haki kwa dalili katika kila lenye tafauti ndani yake, tunasema kwa wote: "Leteni dalili zenu ikiwa nyinyi ni wakweli mumepatia haki" tunajiongoza kwa Kitabu cha Allah na Sunna ya Mtume S.A.W. na yenye makubaliano ndani yake, hii ndiyo hali yetu tokea hapo mwanzo mpaka hivi leo.

Leo hii limekuja suala la funga ya siku ya arafa.

Jee! Kufunga siku ya arafa ni kwa kisimamo cha Mahujaji katika sehemu ya Arafa, au kwa Muandamo wa mwezi wa Dhul-Hijja (Mfunguo tatu)?

Kwa kweli inafahamika vizuri sana kuwa karne zote zilizopita Waislamu hawakua wakiijua siku ya arafa isipokua kwa kupitia muandamo wa mwezi wa Hija, na kuwa watu wa miji yote, kila mji waliijua siku hiyo ya arafa kupitia muandamo wa majira yao, na wanavyuoni wote waliijua siku ya kufunga arafah kuwa ni siku ya tisa ya mwezi wa Hijja (mfunguo tatu), kwa ufupi makubaliano ya wote ni kuwa siku ya arafa ni siku ya tisa ya mwezi wa Dhul-Hijja (mfunguo tatu), na kuwa siku hii ina ibada zinayoihusu, nazo ni mbili:

1. Ibada iliyofungamana na sehemu maalumu.

2. Ibada isiyofungamana na sehemu maalumu.

Zote ni ibada za siku ya arafa ambayo ni siku ya tisa ya mwezi wa Dhul-hijja.

Ama ibada iliyofungamana na sehemu maalumu hiyo ni ibada ya kusimama katika sehemu inayoitwa arafa iliyoko katika mji mtakatifu wa Makka, na ibada hii inawahusu Mahujaji peke yao nayo ni nguzo mama ya ibada ya Hijja.

Ama ibada isiyojifunga na sehemu maalumu hiyo ibada ni kufunga siku hii ya tisa ya mwezi wa Dhul-hijja nayo ndiyo inayojulikana kuwa ndiyo siku ya afara.

Kwa hiyo ni haki kuwa kila muislamu ajishike na majira ya mji wake katika kutekeleza ibada hii ya funga ya arafa kama vile anavyoanza mchana wake kwa aljfajiri ya mji wake na kumaliza kwa kuchwa jua katika magharibi ya mji wake basi vile vile afunge siku ya tisa kwa mujibu wa muandamo wa mji wake; kwa sababu hayo ndiyo majira aliyofungwa nayo katika ibada zake zote za wakati, kwa hakika sehemu iitwayo arafa ina majira yake nayo haindoki mpaka dunia itamalizika, kwa hiyo uhakika ni kuwa ibada ya siku ya arafa ni ya wakati wa majira ya sehemu ya mji husika na si kwa ibada ya Mahujaji mbayo pia imefungwa kwa majira ya mji wanaotekeleza ibada hiyo ndani yake, vipi Muislamu anakubali kuondoshwa katika asili na sababu ya ibada na kufungwa na jambo jengine?

Leo hii wamezuka watu na jambo jipya na geni, kwa hakika halikuwepo kwa miaka zaidi ya elfu moja iliyopita, watu hao hao utawasikia wakisema: Jichungeni sana na mambo mapya mapya, kwani kila jipya ni bidaa, na kila bidaa ni upotevu, na kila upotevu ni motoni".

Tunawambia: Ni yakini isiyokua na shaka yoyote kuwa Dini ya Uislamu imetimia tokea zama za Mtume S.A.W. na kuwa waislamu kwa miaka zaidi ya 1400 hawajui chengine katika ibada hizi isipokua kujifunga na tarehe ya muandamo kwa mujibu wa nyakati za majira yao tu, kama ilivokua hawasali wala hawafungi kwa mjira ya mji mtakatifu wa makka, basi vipi watafunga kwa ibada ya watu wa mji huo? Hakika ibada za walioko Makka zote zimefungwa kwa mujibu wa majira ya mji huo, kama ilivokua ibada zetu zote zimefungwa kwa majira ya miji yetu.

Mumepata wapi nyinyi sababu hiyo munayoidai hivi leo?

Vipi nyinyi leo munafanya kila pupa la kuwaondosha watu katika njia ya wema waliopita katika kila madhehebu na kuzua jambo jipya?

Ewe Allah hakika sisi tumeshabainisha.

Tunawatakia Waislamu wote siku kuu njema ya kheri na barka.

Amin.

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment