Ibadhi.com

02. IBADHI BAINA YA KUNDI LA ALLY BIN ABII TALIB NA MUAWIYA BIN ABI SUFIANI

 

NURU ING’AAYO KATIKA NJIA YA UONGOFU

IBADHI BAINA YA KUNDI LA ALLY BIN ABII TALIB NA MUAWIYA BIN ABI SUFIANI


MJUKUU: Kwa hivyo Ibadhi wako wapi baina ya makundi haya mawili, Ewe babu yangu?

BABU: Jua – Allah mtukufu akuhifadhi- kuwa “Pale mambo yalipovurugika katika ukhalifa wa kiislamu, na ikawa hukmu inaelekea katika ufalme wa kurithishana, wa kutumia nguvu, uliokamtwa na Banii Umayya, Misimamo ya watu iligawanyika katika makundi mengi… wapo waliojifungamanisha na dola na kujisalimisha, wakijitahidi kujikurubisha na dola ili iwe ni njia ya kufikia ubwana mkubwa.

Na wapo waliojaribu kuifunga haki ya Ubwana kwa watu wa nyumba ya Mtume – Sallallaahu alayhi wasallam- kwa njia ya kurithishana au kuzusha kuwa kuna wasiyya unaofuatana kwao wao pasina wengine, na wapo waliokataa hili na lile na wakatoka katika dola hiyo kwa nguvu, na wakaweka njia ya kufikia hukmu ni kumchagua kiongozi kwa uhuru, kisha hawakumpa udhuru Yule aliyekhalifu rai hiyo.
Na wakati wa mgongano huu mkubwa baina ya makundi haya matatu wakati wa mwanzo wa dola ya Banii Umayya, lilitokea kundi lingine lilopita njia ya kati na kati baina ya makundi haya yenye kupinzana, halikuchukua njia ya kujisalimisha kwa ile hali iliyopo vyovyote itakavyokuwa, lakini pia haikuchukua ya kuwa wao ndio mfano kamili kiasi iwe lazima kwa watu wote kuwafuata wao, kwa njia hii wakawa wamekhalifu njia ya kundi la mwanzo kwa kujuzisha kwao kutoka dhidi ya utawala ikiwa kutoka huko kutaleta maslaha kwa ummah, wala haitoleta madhara zaidi na makubwa zaidi ya maslaha. Pia kundi hili limekhalifu njia yakundi la pili hivyo halikukubali utaratibu wa kurithishana utawala. Na pia kundi hili limekhalifu njia ya kundi la tatu kwa kuwa halikuwajibisha kutoka dhidi ya viongozi waovu katika hali zote, wala hawakulazimisha msingi wao kwa watu wote,na wakampa udhuru aliyewakhalifu wao, na hawa ndio IBADHI”1"

MJUKUU: Kweli, ufafanuzi wako ni wa kutosheleza na uko wazi ewe babu yangu…– Allah mtukufu akupe umri mrefu katika kumtii yeye – umetaja kuwa Ibadhi hawawajibishi kutoka dhidi ya viongozi waovu, Je hili linamaanisha kuwa wao wanawatii na kuzinyenyekea amri zao ?
BABU: Kuwa na hakika na amini kwa yaqini ewe mwanangu kuwa Ibadhi wanaona kuwa katika wajibu wa waislamu ni kusimamisha dola ya uadilifu, inayokwenda juu ya msingi wa sharia ya kiislamu, inatekeleza hukmu za Allah mtukufu, inasimamaisha huduud, inahifadhi haki, inarejesha dhulma, inahifadhi mipaka, na inapeleka daawa ya kiislamu katika miji ya kikafiri.
Amma ikiwa dola itakayosimama ni ovu, inajuzu kubaki chini ya hukmu yao, na inawajibika kuwatii katika yote yasiyokhalifu hukmu za uislamu, kama ambavyo inapaswa kwa waislamu wasilale tu, inatakiwa wajaribu kubadilisha hukmu zilizopo ikwa hilo halitoleta madhara makubwa kwa ummah na kusimamisha uadilifu, hii ni kwa kutazama vitendo, Amma kwa kutazama ukosoaji ((kuamrisha mema na kukataza mabaya)) basi haijuzu kwa muislamu mwenya pupa na uislamu wake kuacha au kukaa kimya kunako maovu.”2"

MJUKUU: Allah mtukufu anizidishie sehemu ya elimu yako ewe babu yangu na aninufaishe kwayo.. na ulikuwaje mwenendo wa Maibadhi katika kutekeleza sharia ya Allah mtukufu na kusimamia uadilifu katika ardhi wakati wa dola ya Amawiyya ? Njoo nasi katika makala ifuatayo…!

Khamis bin Yahya Alghammawi

Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.

__________________________________________________________________________________
1 - Muammar, Marejeo yaliyopita uk 185 – 187 (kwa mabadiliko kidogo)
2 - Marejeo yaliyopita uk 54-55 ((kwa mabadiliko kidogo))

 

Said Al Habsy

Website: https://www.ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment