Ibadhi.com

2.SAFINA YA UONGOFU - “KWA JINA LA ALLAH MTUKUFU, KWENDA KWAKE NA KUSIMAMA KWAKE”

SAFINA YA UONGOFU.

“KWA JINA LA ALLAH MTUKUFU, KWENDA KWAKE NA KUSIMAMA KWAKE”

Upepo wa fitna umeongezeka katika bahari ya maisha, mawimbi ya ujinga yameongezeka, na wengi katika watu wameangamia katika kiza cha matamanio na uasi, miaka inafuatana na kupishana, na hakuna hata mmoja anafikiria namna ya kujiokoa…!!!

Hukooo… katika fukwe ya bahari hii, amesimama kijana mtukufu, zinatoka nuru katika uso wake ulojaa unyenyekevu, lakini juu yake kuna mawingu ya huzuni, kwa anavyowaona watu wake wakibabishwa huku na huko na yale mawimbi makubwa, mawimbi ya ujinga na ushirikina, na zikiunguzwa nyuso zao na jua kali, jua kali la vita baina yao na dhulma. Kila siku…!! Kila leo…!!
Mara….!! Allah mtukufu anamchagua kijana huyu na kumleta karibu kwa kumpa utume, na anamtumia SAFINA YA UONGOFU ili avuke nayo katika bahari ilochafuka, na awaokoe kwa kadri awezavyo wale viumbe wanaopotea, kabla hawajafunikwa na kiza chake.

Naam …!!! Huyo ni MUHAMMAD, Mtume wa Allah mtukufu, Nahodha wa SAFINA YA UONGOFU, ambaye aliyaweka maisha yake katika hatari kwa ajili ya Laailaaha illallah..
SAFINA ikaendelea na safari ikiwa thabiti kwa aya za Allah mtukufu mbele ya upepo mkali wa Batili. Miaka inapita, wanaongezeka wanao okolewa, abiria wanakuwa wengi hali safari inaendelea kwa ulinzi wa Allah mtukufu, kisha kwa hikma na uwezo wa nahodha wake, kisha kwa ikhlaas na kujitolea kwa abiria wake ( masahaba ), ambao hawakuacha hata kwa kupwesa kuwatia adabu wavamizi wa baharini na wanyang’anyi – maadui wa haki -.
Muda wa mapigano ulirefuka…, lakini hali ya hewa ilitulia baadaye, na watu wakaneemeka kwa upepo mzuri wa Qur an, na wakaendelea na safari kwa muongozo wa Nahodha wao – Mtume Muhammad Rehma na Amani zimwendee -, katika bahari ile ilopanuka sana, yenye njia nyingi, lakini nahodha aliiweka SAFINA katika njia iliyonyooka, bila kupinda hata ukucha, wala kurudi nyuma.

Katika ufukwe wa amani, na nchi kavu iliyo salama, Nahodha alikhitariwa na Allah mtukufu, naam… imefikia wakati wa roho yake kupumzika, akawaacha akiwa kawatandikia njia ya uongofu, akiwacha kizazi alichokilea katika uongofu wa Qur an, na akawanywesha nuru ya kitabu hicho na utukufu wake.

Nini kilitokea baada ya Nahodha kufariki….. fuatilia makala ijayo

Ust. Abu Muslim

Website: www.ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment