Ibadhi.com

IV. Nguo inayosihi kwa Salaa kwa wanawake.

Nguo inayosihi kwa Salaa kwa mwanamke ni ile inayomstiri mwanamke mwili mzima isipokuwa viganja na uso wake sitara ya kisheria. Kasema Mwenyezi Mungu S.W.T katika Surat AN-Nur aya ya 31, “

﴿وَلاَيُبدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلاَّمَاظَهَرَ مِنهاَ.

Maana yake, “Wala wasidhihirishe viungo vyao isipokuwa vinavyo dhihirika (navyo ni uso na vitanga/viganja vya mikono.)”

Kasema Bibi Aisha R.A.A.H., “Siku moja alikuja Asma Bint Abubakar akiwa amevaa nguo nyepesi ambazo hazikumsitiri vizuri. Alipoingia Mtume S.A.W., na kumkuta katika hali ile, aligeuza uso wake na akasema kumwambia,[1]

يَا أَسْمَاءُ إِنَّ الْمَرْأَةَ إِذَا بَلَغَتْ الْمَحِيضَ لَمْ تَصْلُحْ أَنْ يُرَى مِنْهَا إِلَّا هَذَا وَهَذَا وَأَشَارَ إِلَى وَجْهِهِ وَكَفَّيْهِ.

Maana yake, “Ewe Asmaa mwanamke akishavunja ungo, basi haifai kwake kuonyesha umbo lake isipokuwa hivi na hivi tu: na akaonyesha uso na vitanga vya mikono.”  Na pia imfunike miguu yake yote pamoja na nyayo zake. Kasema Abu Sa`id L-Khudry R.A.A., “Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. alipotaja kikoi (nguo ya mwananmume) akasema Bibi Ummu Salamah, “Na mwanamke, ewe Mjumbe wa Mola?” Akasema,[2]

تُرْخِي شِبْرًا.

Maana yake, “Iache ining`inie kiasi cha shubiri moja.” Akasema kuuliza, “Ikiwa itamfanya aonekane.” Akasema Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W., “

فَذِرَاعًا لا تَزِيدُ عَلَيْهِ.

Maana yake, “(Aiongezee) Dhiraa[3] na wala asizidishe kuliko hivyo.” Na wakati wa Salaa pia mwanamke afunike nyayo za miguu yake kwa mbele. Kasema Abdurahman bin Abdallah, "Bibi Umm Salamah R.A.A.H. alimuuliza Mtume S.A.W., “Jee mwanamke anaweza kusali amevaa deraya na mtandio.” Akajibu Mtume S.A.W. akasema, [4]

إِذَا كَانَ الدِّرْعُ سَابِغًا يُغَطِّي ظُهُورَ قَدَمَيْهَا.

 Maana yake, “Ikiwa dera ni kubwa na linafunika nyayo za miguu yake kwa mbele.”

 

UKUMBUSHO MUHIMU.

Hizo ni baadhi ya Hadithi zinazobainisha yale yanayotakiwa kwa kivazi cha mwanamke. Inasikitisha kuona mavazi yanayo valiwa sasa na wengi miongoni mwa dada zetu hayakidhi kusudio la vazi la kiisilamu, na badala yake imekuwa ndio njia ya mtu kuonyesha umbile nap ambo lake.

Kuufunika uso, na kuvaa nguo za kuufunika mwili mzima kunaweza kuwa hakukutosheleza kukidhi stara iliyo kusudiwa, ikiwa nguo zile zilizovaliwa hazikutimiza masharti ya nguo ya kisheria. Mfano: Ikiwa mtu atavaa nguo nyepesi kiasi ya kuonyesha rangi ya mwili wake, au atavaa nguo za kubana ambazo zitaonyesha maumbile ya mwili wake, kisheria atakuwa yuko uchi, na haya ni katika makosa na maasi makubwa. Kasema Ibn Umar R.A.A., “Nimemsikia Mtume S.A.W. akisema, “Watakuwepo baadae katika umma wangu,[5]

نِسَاؤُهُمْ كَاسِيَاتٌ عَارِيَاتٌ عَلَى رُءُوسِهِمْ كَأَسْنِمَةِ الْبُخْتِ الْعِجَافِ الْعَنُوهُنَّ فَإِنَّهُنَّ مَلْعُونَاتٌ.

Maana yake, “Wanawake wao watakuwa wamevaa nguo lakini watakuwa uchi[6], na juu ya vichwa vyao kama nundu za ngamia, walaanini kwani wamekwisha laanika.” Pia kasema Abu Huraira R.A.A., “Kasema Mtume S.A.W,[7]

صِنْفَانِ مِنْ أَهْلِ النَّارِ لَمْ أَرَهُمَا قَوْمٌ مَعَهُمْ سِيَاطٌ كَأَذْنَابِ الْبَقَرِ يَضْرِبُونَ بِهَا النَّاسَ وَنِسَاءٌ كَاسِيَاتٌ عَارِيَاتٌ مُمِيلَاتٌ مَائِلَاتٌ رُءُوسُهُنَّ كَأَسْنِمَةِ الْبُخْتِ الْمَائِلَةِ لَا يَدْخُلْنَ الْجَنَّةَ وَلَا يَجِدْنَ رِيحَهَا وَإِنَّ رِيحَهَا لَيُوجَدُ مِنْ مَسِيرَةِ كَذَا وَكَذَا.

Maana yake, “Aina mbili za watu wa motoni bado sijawaona: Watu ambao watakuwa na viboko kama mkia wa ng`ombe dume na watakuwa wakiwapigia watu. Na wanawake ambao watakuwa wamevaa nguo lakini watakuwa uchi[8]  wakienda kwa maringo[9].  Vichwa vyao vitakuwa kama nundu ya ngamia iliyoelekea upande mmoja[10]. Wanawake hao hawataingia peponi na wala hawataisikia harufu yake, na hakika harufu yake inasikika kwa masafa kama vile na vile.”

 [1] Abu Daawud 11/145 (3580).

[2] Al-Imamu Al-Rab`iu 1/86 (273), mfano wa Hadithi hii imetolewa na Abu Daawud 11/161 (3590), Nnasaai 16/146 (5242), Ahmad 10/462(4926).

[3] Urefu wa baina ya kiwiko cha mkono hadi kufika mwisho wa kidole kirefu cha mkono nchani inakadariwa karibu kiasi cha nchi kumi na nane hivi.

[4] Abu Daawud 2/273 (545).

[5] Ibn Haaban 13/64 (5753).

[6] Yaani nguo zao zitakuwa sio za stara na hazikusitiri nyuchi zao jinsi ilivyo kusudiwa katika uisilamu.

[7] Muslim 11/59 (3971), Ahmad 17/353 (8311).

[8] Hapa inaingia pia wanawake wanaovaa nguo nyepesi zinazoonyesha rangi ya miili yao, na wale wanaovaa nguo zinazobana zinazo onyesha umbile la maungo yao.

[9] Yaani mwendo wa kunata.

[10] Kwa mitindo ya kuchana nywele zao, na haya yamekwisha dhihiri.

Said Al Habsy

Website: https://www.ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment