Ibadhi.com

V. Makimbilio ya mwanaadamu wakati wa shida.

Subira na kuwa na msimamo thabiti ni jambo gumu sana, na hii ni asili ya maumbile ya mwanaadamu kwani kaumbwa na papara, akifikwa na shari basi hu-haha na kubabaika, na akifikwa na kheri hutakabari[1]. Hii ni tofauti na yule anaehifadhi Salaa yake, Mola anamhifadhi na tabia hizo, na anamuwezesha kuwa na msimamo imara katika kila hali inayomsibu.  Kasema Mola Mtukufu kuhusu tabia ya mwanaadamu katika Surat Al-Maa`rij aya ya 19 mpaka ya 23, ‘

﴿إِنَّ الإِنْسَانَ خُلِقَ هَلُوعًا﴾﴿إِذَا مَسَّهُ الشَّرُّ جَزُوعًا﴾﴿وَإِذَا مَسَّهُ الْخَيْرُ مَنُوعًا﴾﴿إِلَّا الْمُصَلِّينَ﴾﴿الَّذِينَ هُمْ عَلَى صَلاتِهِمْ دَائِمُونَ.

Maana yake, “Hakika mtu ameumbwa na papara. Inapo mgusa shari hupapatika. Na inapo mgusa kheri huizuilia. Isipokuwa wanao Sali. Ambao wanadumisha Salaa zao”. Mwanaadamu akiona milango yote ya faraja imefungika kwake naye yuko katika shida na dhiki, basi utamuona ana kimbilia kwa Mola Mtukufu kwa kunyenyekea na ibada, ingawa hili lilikuwa alifanye kwanza, na akipatikana na jambo basi azidishe ibada na kujisogeza karibu na Mola ili aweze kupata msaada, faraja, na kuthibitishwa. Mfano mzuri ni Mtume S.A.W. akipatwa na jambo la kumhuzunisha basi huwa akisali. Kasema Hudhaifa R.A.A.,[2]

كَانَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إِذَا حَزَبَهُ أَمْرٌ صَلَّى.

Maana yake, “Ilikuwa Mtume S.A.W. likimfika jambo zito husali”. Pia Miishari kasema, "Nimemsikia Mtume S.A.W akisema,[3]

يَا بِلالُ أَقِمْ الصَّلاةَ أَرِحْنَا بِهَا.

Maana yake, “Ewe Bilal kimu Salaa itutulize kwayo.”

 [1] Kuwa na majivuno na kiburi.

[2] Abu Daawud 4/88 (1124).

[3] Abu Daawud 13/165 (4333).

Said Al Habsy

Website: https://www.ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment