Ibadhi.com

07. RAMADHANI NI MWEZI ADHIMU

Shukurani zote ni kwa Allah mtukufu na Rehma na Amani ziwe kwa Mtume wetu Muhammad pamoja na Aali zake na Masahaba wake na kila mwenye kuongoka katika njia yake mpaka siku ya malipo.

Kwa hakika mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao ni mwezi wa 9 katika kalenda ya Kiislamu ni mwezi adhimu aliohusisha Allah mtukufu kwa uteremsho wa Quraani tukufu, basi Allah mtukufu akauhusisha usiku wa uteremsho wa Quraani kwa cheo cha Lailatu Al-Qadri na kuupitishia hukumu ya ubora wake kuliko miezi elifu moja nao ni usiku katika misiku ya mwezi huu wa Ramadhani.

Mwezi huu Allah mtukufu ameupitishia hukumu ya ibada ya funga (siyaamu) kwa siku zake zote ima ziwe ni 29 au 30 kwa mujibu wa kuthibiti muandamo wa mwezi, pia Allah mtukufu akaifanya ibada hii ya kufunga (Siyaamu) mwezi huu wa Ramadhani ni moja kati ya nguzo tano za Uislamu, bali ameihusisha ibada hiyo kwa thawabu maalumu kutoka kwake, amesema Mtume S.A.W: ((Anasema Allah mtukufu: matendo yote ya mwana wa adamu ni yake isipokua funga hakika hiyo ni yangu na mimi ndiye mwenye kuilipia pepo, ameacha mja wangu mlo wake na kunywa kwake na matamanio yake kwa ajili yangu basi funga ni yangu)).

 Allah mtukufu ametueleza kuhusu Ibada ya funga kwa uwazi kabisa katika Kitabu chake kama ilivyo katika Sura ya pili (Al-Baqarah) kuanzia Aya ya 183 hadi 187, tunapoziangalia Aya hizi tunakutia kuwa Aya ya mwanzo ya 183 imetutajia lengo la ibada hii kuwa ni kuhakikisha Uchamungu na Aya ya mwisho 187 pia imetaja kuwa lengo la Ibada hii ni kuhakikisha sifa ya Uchamungu, basi tufahamu na tujue cheo cha Ibada hii ya funga ya mwezi huu mtukufu wa Ramadhani kuwa ni chuo cha kuielea nafsi ya mja katika uchamungu, nacho ni kituo alichokijaalia Allah mtukufu kila mwaka mara moja, basi ewe ndugu yangu muislamu fahamu kuwa kufika mwezi wa Ramdhani ni kheri kubwa kwako na iwe furaha katika moyo wako na uwe tayari kuingia ndani ya Ibada hii kikamilifu ili Allah mtukufu akupambe kwa nuru ya Uchamungu katika maisha yako ili uweze kufanikiwa kwa kupata maridhio ya Allah mtukufu na kuingia katika Pepo yake tukufu, anatuambia Allah mtukufu akiisifu Pepo yake:

 ((وَلَدَارُ الْآخِرَةِ خَيْرٌ وَلَنِعْمَ دَارُ الْمُتَّقِينَ * جَنَّاتُ عَدْنٍ يَدْخُلُونَهَا تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ لَهُمْ فِيهَا مَا يَشَاءُونَ كَذَلِكَ يَجْزِي اللَّهُ الْمُتَّقِينَ))

 ((Na kwa hakika nyumba ya Akhera ni bora, na ubora ulioje wa nyumba ya Wachamungu * Pepo za Adeni watakazoziingia inapita chini yake mito watapata humo wanayoyataka, namna hivo Allah anawalipa Wachamungu)) [Nahl 31-31]

Na amesema:

((تِلْكَ الْجَنَّةُ الَّتِي نُورِثُ مِنْ عِبَادِنَا مَنْ كَانَ تَقِيًّا)) 

((Hiyo Ndiyo Pepo ambayo tutamrithisha katika waja wetu yule aliye mchamungu)) [Maryam 63]

Anasema Imam Qutubu Al-Aimmah R.A.:

"نورث من كان تقيّاً من عبادنا ما لأهل النار من المساكن فى الجنة"

"Tutamrithisha alliyekua mchamungu katika waja wetu, hakuna kwa watu wa motoni makazi ndani ya Pepo" 

Basi tufahamu malengo ya funga ya Ramadhani kuwa sio kukaa na njaa na kiu, bali ni kujiepusha na yote yenye kuharibu funga ili kulinda usahihi wa ibada pia kulazimika na uchamungu ili kulinda kukubaliwa ibada kwani hakika Allah anawakubalia Wachamungu, basi tujiepushe na mabaya yote na tutubie kwa Mola wetu mlezi na tujihadhari na kila kitanzi cha asi na dhambi usiku na mchana tulazimike na mipaka ya Allah mtukufu.

 Tujue kuwa yanayoharibu ibada ya funga yako aina nne:

1. Kuingiza kitu tumboni kwa kukusudia kula au kunywa, ama aliyekula au kunywa kwa kusahau huyo hakuna lawama juu yake.

2. Kutoa kitu nje kwa kujitapisha kilichomo tumboni au kujitoa shahawa (manii) kwa kujichezea au kuamsha hisia za matamanio kwa njia ya kufikira au kutizama au kusikiliza au nyengine yoyote.

3. Kukutana kwa maingiliano ya kujamiiana zikikutana tupu mbili kwa kuvuuka mpaka wa jando basi funga imeharibika.

4. Madhambi makubwa yote kama vile kusengenya, kufitinisha, kusema uongo, kuacha kusali, kuangalia ya haramu yasiyofaa, kujichezea kimatamanio, kuvuta sigereti na mengineo.

Ramadhani ni chuo cha Uchamungu lazimika na Uchamungu ili ufanikiwe.

Asanteni.

Ndugu yenu: Abu Hamed Hafidh Al-Sawafi.

29/9/1438 HJ - 26/5/2017 A.D.

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment