Ibadhi.com

03:SEMA IMEKUJA HAKI - “NI MUHALI EWE MTOTO WANGU”

SEMA IMEKUJA HAKI


“NI MUHALI EWE MTOTO WANGU”


Mwanafunzi:

Namshukuru Allah mtukufu aliyenionyesha njia ya uhakika, Allah mtukufu akuongezee fadhila ewe sheikh wangu… Nimesikia baadhi ya watu wanamuomba Allah wakisema “Mola niruzuku ladha ya kutazama uso wako mtukufu”, Sheikh wangu niwekee wazi qauli hizi – Allah asininyime elimu yako – hivi kweli waja watamuona mola wao ?

Shiekh:

Aaah, Mwanangu wee, hakika mas ala haya ni makubwa, ufafanuzi wake ni mrefu, lakini nitakufupishia kwa haraka baadhi ya dalili zetu za akili na kunakili kuhusu KUTOJUZU KUMUONA ALLAH MTUKUFU
Katika dalili za kiakili, kuonekana hakutimii mpaka sharti zake zitimie kama: kinachoonekana kisiwe kidogo sana, wala chepesi sana, kisiwe mbali sana au karibu sana, kiwe na rangi chenyewe au kichukue rangi kutoka kwingine, na masharti haya hayawi ispokuwa kwa kitu chenye mwili, au kisichona mwili chenye kutegeea mwili, na Allah mtukufu hayuko hivyo.
Akili inahukumu kuwa hilo la kuonekana Allah mtukufu ni Muhali, kwa kuwa yenye kulazimika na kuonekana ni kuwa “lazima awe mwenye kupambanuka kwa rangi, mwenye umbile na namna, na yote hayo kwa Allah ni Muhali… na hapana budi mwenye kuonekana awe mwenye kugawika yaani mwenye vipande vipande mfano nyuma, mbele, viungo n.k. kwa kuwa mwenye kumtazama imma amuone wote, na kila chenye kuonekanwa chote kimegawika, au akione baadhi yake na hapo pia itadhihiri kugawika pia, na yote hayo kwa Allah mtukufu ni Muhali”
Amesema Imaam Alsaalimi R.A. kuhusu hili “wamejificha wasemao watamuona katika neno lao : tutamuona bila namna, wala umbile, wala hali tunayoweza kuiweka akilini… bila shaka huku ni kukimbia kumshabihisha Allah mtukufu wazi wazi pamoja na kwamba wao wamemshabihisha kwa maana, na hiyo ziada yao ya bil namna… haina dalili katika kitabu wala sunnah”
Amma dalili za kunakili: ni zile zilokuja katika kitabu cha Allah mtukufu aliposema:


“Havimdiriki yenye kuona, naye anavidiriki vyenye kuona, naye ni mpole mwenye khabari zote” An’aam:103


Basi vipi tutamdirki, kwani hilo linalazimisha awe ni mwili na awe ni sehemu ya kuelekewa – Ametakasika Allah mtukufu na hilo utakaso mkubwa – kwa hivyo kwetu sisi Allah mtukufu haonekani dunia wala Akhera.

Mwanafunzi: 

Lakini … hivi hawatolei dalili ya kutoonekana katika hii aya pia ?

Sheikh:

Ndio na wao huitolea dalili kwa kufasiri neno idraak kwa maana ya kukizunguka kitu, lakini uhakika ni kuwa isemwapo macho yamediriki haina maana ispokuwa kuona tu, hivyo ukisema “ nimemdiriki kwa macho” na ukisema “ nimemuona” maana ni moja, hakuna tofauti ispokuwa katika lafdhi, pia katika dalili zao ni Qauli ya Allah mtukufu : “Zipo nyuso siku hiyo zitao ng'ara, Zikiangalia kwa Mola wake Mlezi” Qiyama: 22-23

Mwanafunzi: lakini kutazama hapa kunaweza kuwa na maana nyingine au sivyo ewe sheikh wangu ?
Sheikh: ….


Khamis Yahya Alghammawi Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona. Ibadhi.com

Said Al Habsy

Website: https://www.ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment